Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hali ya Pekee ya Jua Letu

Hali ya Pekee ya Jua Letu

Hali ya Pekee ya Jua Letu

UNAPOSOMA makala hii, huenda jua limechomoza au huenda unajua litachomoza baada ya muda mfupi. Je, hilo ni jambo muhimu? Naam, kwa sababu pasipo nuru ya jua, matrilioni ya viumbe walio duniani—kutia na wewe—hawangekuwapo. Mamilioni ya viumbe mbalimbali, kuanzia kwa bakteria wenye chembe moja hadi nyangumi wakubwa mno wangeangamia wote.

Ni kweli kwamba ni takriban nusu tu ya sehemu moja kwa bilioni ya nishati ya jua inayofikia sayari yetu. Lakini, hata “kiasi hicho kidogo sana” cha “nuru” ya jua chatosha kulisha na kutegemeza uhai duniani. Isitoshe, endapo kiasi hicho kidogo sana cha nuru kinachotufikia kinaweza kutumiwa ifaavyo, kinaweza kutosheleza mahitaji ya nishati ya jamii yetu ya kisasa kwa urahisi, na bado kuwe na nishati ya ziada.

Vitabu vingi vya astronomia vinasema kwamba jua letu ni nyota ya kawaida, “ni kitu cha kawaida tu angani.” Lakini je, kweli jua ni “kitu cha kawaida tu angani”? Guillermo Gonzalez, mwastronomia katika Chuo Kikuu cha Washington huko Seattle, amedokeza kwamba jua letu ni la pekee. Je, hilo lapasa kuathiri jitihada za kutafuta kuwapo kwa uhai katika sayari nyingine? Gonzalez ajibu: “Tofauti na watu wanavyodhani, ni nyota chache sana zinazoweza kutegemeza uhai wa viumbe wenye akili.” Aongezea hivi: “Waastronomia wasipochunguza kwa makini sana nyota za pekee kama vile Jua, wanapoteza wakati wao.”

Ni hali zipi zinazofanya jua letu liweze kutegemeza uhai? Tunapochunguza hali hizo, tukumbuke kwamba taarifa nyingi kuhusu fizikia ya ulimwengu ni za kinadharia.

Hali Zenye Kustaajabisha

● Nyota iliyo peke yake: Waastronomia hukadiria kwamba asilimia 85 ya nyota katika ujirani wa jua ziko katika makundi ya nyota mbili au zaidi, na kila nyota huzunguka nyingine. Nyota hizo huunganishwa na nguvu za uvutano.

Hata hivyo, jua liko peke yake. “Yaonekana hali ya jua kuwa peke yake ni jambo lisilo la kawaida,” aandika mwastronomia Kenneth J. H. Phillips katika kitabu chake Guide to the Sun. Gonzalez asema kwamba hali ya jua kuwa peke yake huwezesha dunia izunguke kwa uthabiti zaidi, na hilo, hudumisha hali zinazositawisha uhai duniani.

● Nyota kubwa sana: Hali nyingine ya pekee sana ya jua, kulingana na Gonzalez, ni kwamba “liko miongoni mwa asilimia 10 ya nyota kubwa sana katika ujirani wake,” laripoti gazeti la New Scientist. Phillips asema: “Jua hufanyiza asilimia 99.87 ya mfumo wake. Nalo hudhibiti sayari nyingine zote katika mfumo huo kwa nguvu zake za uvutano.”

Hali hiyo huiruhusu dunia kuwa umbali wa kiasi kutoka kwa jua—kilometa milioni 150—na bado haiwezi kuondoka mahali pake. Umbali huo mkubwa kwa wastani, hulinda viumbe duniani wasiangamizwe na jua.

● Elementi nzito: Gonzalez asema kwamba jua lina elementi nzito—kaboni, nitrojeni, oksijeni, magnesi, silikoni, na chuma—zinazozidi kwa asilimia 50 zile zilizo katika nyota nyingine yoyote iliyodumu kama jua na inayofanana nalo. Jua letu halina kifani kwa habari hii. “Elementi nyingi nzito zilizo juani si nyingi kupita kiasi,” asema Phillips, “lakini nyota nyingine . . . zina elementi chache zaidi nzito.” Kwa hakika, nyota zenye elementi nyingi nzito kama jua huwa katika kundi hususa la nyota linaloitwa Population I.

Hilo lahusianaje na kuwapo kwa uhai duniani? Kwa wazi, elementi nzito ni muhimu katika kutegemeza uhai. Lakini ni adimu sana, ukubwa wake hauzidi asilimia 1 ya ulimwengu. Hata hivyo, dunia yetu karibu yote hufanyizwa na elementi nzito. Kwa nini? Kwa sababu waastronomia wanasema kwamba dunia huzunguka nyota ya msingi isiyo ya kawaida—jua letu.

● Mzunguko ulio nusura duara: Kuna faida nyingine ya jua kuwa nyota aina ya Population I. “Kwa kawaida nyota za kundi la Population I huzunguka katikati ya galaksi kwa mzunguko ulio nusura duara,” chasema kitabu Guide to the Sun. Mzunguko wa jua ni nusura duara tofauti na nyota nyingine zilizodumu kama jua na zinazofanana nalo. Mbona hilo liathiri kuwapo kwa uhai duniani? Kwa sababu umbo la duara la mzunguko wa jua huzuia jua kutumbukia kwenye galaksi ya ndani, ambayo huwa na milipuko mingi ya nyota (supernova).

● Kubadilika kwa mng’ao: Hili ni jambo jingine lenye kupendeza kuhusu nyota ya mfumo wetu wa jua. Mng’ao wa jua haubadiliki-badiliki kama mng’ao wa nyota nyingine zinazofanana na jua. Yaani, jua hung’aa daima bila kubadilika-badilika.

Mng’ao huo madhubuti wa nuru ni muhimu sana katika kutegemeza uhai duniani. “Kuwa kwetu duniani,” asema mwanahistoria wa sayansi Karl Hufbauer, “huthibitisha kwamba mng’ao wa jua ni mojawapo ya hali za mazingira zisizobadilika.”

● Mwinamo wa mzunguko: Mzunguko wa jua umeinama kidogo tu kuelekea uso wa galaksi ya Kilimia. Hilo lamaanisha kwamba pembe iliyopo kati ya uso wa mzunguko wa jua na uso wa galaksi yetu ni ndogo sana. Hilo hutegemezaje masilahi ya viumbe duniani?

Sehemu za mbali za mfumo wetu wa jua zimezingirwa na nyotamkia nyingi sana zenye umbo la tufe, ambazo huitwa wingu la Oort. * Tuseme mwinamo wa mzunguko wa jua kuelekea uso wa galaksi yetu ungekuwa mkubwa zaidi. Basi jua lingevuka uso wa galaksi yetu ghafula, na hivyo kutibua wingu la Oort. Matokeo yangekuwa nini? Waastronomia wanasema kwamba nyotamkia nyingi zingedondoka duniani na kusababisha maafa.

Kupatwa kwa Jua Kwafunua Nini?

Mfumo wetu wa jua una angalau miezi 60. Miezi hiyo huzunguka sayari saba kati ya sayari tisa zilizo kwenye mfumo huo. Hata hivyo, yaonekana dunia ndiyo sayari pekee ya mfumo wa jua ambamo kupatwa kwa jua kunakovutia hutukia. Kwa nini?

Jua hupatwa wakati mwezi unapokuwa katikati ya jua na dunia. Ili mwezi ufunike jua kikamili, ni lazima mwezi uwe karibu unalingana na jua. Na ndivyo inavyotukia! Ijapokuwa kipenyo cha jua ni mara 400 zaidi ya kipenyo cha mwezi, umbali kati ya jua na dunia ni mara 400 hivi ya umbali kati ya dunia na mwezi.

Lakini umbali wa dunia kutoka kwa jua—na hivyo ukubwa wa jua—hauchangii tu kupatwa kwa jua. Ni muhimu pia kwa uhai duniani. “Kama tungekuwa karibu zaidi au mbali zaidi na Jua,” Gonzales asema, “Dunia ingekuwa moto sana au baridi sana kiasi cha kutokalika.”

Kuna mengi zaidi. Mwezi ulio mkubwa isivyo kawaida hutegemeza uhai kwenye sayari hii kwa sababu nguvu zake za uvutano huzuia dunia kuyumbayumba sana kwenye mhimili wake. Kuyumbayumba huko kungeweza kusababisha mabadiliko makubwa yaliyo hatari ya hali ya hewa. Kwa hiyo ili uhai uwepo duniani, kinachohitajiwa ni kipimo barabara cha umbali kati ya jua na dunia na vilevile mwezi wenye ukubwa unaofaa—pamoja na hali nyinginezo zote zinazohusiana na hali ya jua. Je, yawezekana kwamba yote hayo yalitokea kwa sadfa?

Je, Yalitokea kwa Sadfa?

Tuseme unapeleka gari lako kwa fundi stadi aliyezoezwa ili alirekebishe. Ajitahidi kumaliza kazi hiyo, nawe wapata gari likiwa sawa kabisa. Unafikiri atahisije iwapo utasisitiza baadaye kwamba marekebisho sahihi ya gari lako yalitukia kwa aksidenti tu au yalitukia kwa nasibu tu?

Twaweza kuuliza swali hilohilo kuhusiana na hali ya pekee ya jua letu. Baadhi ya wanasayansi wanataka uamini kwamba hali ya jua letu, mzunguko wake, na umbali wake kutoka kwa dunia, na hali zake nyingine zote zilitukia kwa sadfa tu. Je, hilo lasadikisha? Je, wafikiri ni mkataa wa kiakili?

Kama vile tu gari lililorekebishwa kwa njia bora linavyodhihirisha uzoefu na ustadi wa fundi, ndivyo na jua letu—na nyota nyingine za kimbingu—linavyodhihirisha jambo fulani. Hali za pekee za nyota yetu ya karibu inayotegemeza uhai duniani huwasilisha ujumbe dhahiri wa kwamba nyota hiyo ni kazi ya mikono ya Mbuni na Muumba mwenye akili na nguvu nyingi. Mtume Paulo alieleza hivi: “Sifa zake zisizoonekana zaonwa waziwazi tangu uumbaji wa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zafahamiwa kwa vitu vilivyofanywa, hata nguvu zake za milele na Uungu.”—Waroma 1:20.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 17 Kwa habari zaidi kuhusu wingu la Oort, ona Amkeni! la Julai 22, 1999, ukurasa wa 26.

[Blabu katika ukurasa wa 17]

Ni takriban nusu tu ya sehemu moja ya bilioni ya nishati ya jua inayofikia sayari yetu

[Picha katika ukurasa wa 16]

Joto kali la jua kama hili halijahatarisha viumbe duniani

[Hisani]

Ukurasa wa 2, 15, na 16: NASA photo

[Picha katika ukurasa wa 17]

Je, yalitokea kwa sadfa? Ulinganisho wa ukubwa wa jua na mwezi husababisha kupatwa kwa jua kunakovutia

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kama mzunguko wa jua ungebadilika, nyotamkia nyingi zingedondoka duniani na kusababisha maafa