Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Silaha Zitaweza Kudhibitiwa?

Je, Silaha Zitaweza Kudhibitiwa?

Je, Silaha Zitaweza Kudhibitiwa?

KATIKA miaka ya hivi karibuni serikali kote ulimwenguni zimezungumzia mbinu za kupambana na biashara haramu ya silaha ndogondogo. Suala hilo limezungumziwa pia na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Ripoti zimetayarishwa, madokezo yametolewa na maazimio kupitishwa. Hata hivyo, wachambuzi wanasema kwamba kukazia uangalifu soko la magendo pekee kwamaanisha kwamba wale wauzaji wakubwa wa silaha—serikali zenyewe—hawatachunguzwa.

Kwa kweli, si rahisi kubainisha biashara haramu na biashara halali ya silaha. Silaha nyingi haramu ziliuzwa kihalali wakati mmoja. Mara nyingi, silaha ambazo zimeuzwa kwa idara za kijeshi au za polisi huibwa na kuuzwa kimagendo. Isitoshe, ni kawaida kwa mtu aliyenunua silaha kumwuzia mtu mwingine bila mwuzaji wa kwanza kujua au kutoa idhini. Makala moja katika jarida la Arms Control Today yasema hivi: “Zaidi ya kutegemeza juhudi za kupambana na biashara haramu ya silaha nyepesi, serikali za kitaifa hazina budi kuchunguza utendaji wake katika biashara ya wakati huu ya silaha halali.” Ingawa watu wengi wanatumaini kwamba serikali zitachukua hatua kali dhidi ya biashara ya silaha ndogondogo, mwandishi mmoja wa habari alisema hivi: “Labda hatupaswi kuwa na matumaini makubwa kwa sababu washiriki watano wa kudumu wa baraza [la usalama la Umoja wa Mataifa] peke yake, wanamiliki asilimia 80 ya biashara ya silaha ulimwenguni.”

Urahisi wa kutokeza silaha nyepesi umetatiza jitihada za kudhibiti ongezeko la silaha hizo. Ingawa ni nchi 12 hivi zinazotengeneza silaha tata kama vile, vifaru, ndege, na manowari, makampuni zaidi ya 300 katika nchi 50 sasa yanatengeneza silaha nyepesi. Idadi kubwa na inayoongezeka ya watengenezaji wa silaha hawaongezi tu mabohari ya silaha ya kitaifa bali pia hutoa fursa nyingi kwa wanamgambo, vikundi vya waasi na mashirika ya wahalifu kupata silaha.

Masuala Yenye Kubishaniwa Sana

Kufikia hapo, tumezungumzia jinsi silaha ndogondogo zinavyotumika katika nchi zilizokumbwa na mapigano. Hata hivyo, masuala ya uuzaji wa bunduki hubishaniwa zaidi katika nchi ambazo ni shwari bila mapigano. Wale wanaounga mkono sheria kali za uuzaji wa bunduki wanasema kwamba ongezeko la bunduki huongeza idadi ya mauaji. Wanasababu kwamba katika Marekani, ambako sheria za uuzaji wa bunduki ni hafifu na bunduki ni nyingi, kuna kiwango kikubwa cha mauaji, lakini katika Uingereza ambako kuna sheria kali za uuzaji wa bunduki, kiwango cha mauaji ni cha chini. Wanaopinga sheria hizo, husema upesi kwamba nchi ya Uswisi ambayo imeruhusu watu kupata bunduki kwa urahisi ina kiwango cha chini sana cha mauaji.

Jambo la kutatanisha hata zaidi ni kwamba uchunguzi waonyesha kwamba Marekani ina kiwango kikubwa zaidi cha mauaji yasiyohusisha bunduki kuliko jumla ya mauaji yote katika nchi nyingi za Ulaya. Na bado kuna nchi nyingine zenye mauaji yasiyohusisha bunduki yanayozidi jumla ya mauaji yote katika Marekani.

Ni kawaida kutumia—au kughushi takwimu ili kutetea maoni fulani. Na katika suala la uuzaji wa bunduki, inaonekana kwamba kwa kila hoja yenye kuunga mkono kuna hoja nyingine kinyume yenye kukubalika. Masuala hayo ni magumu. Hata hivyo, wataalamu wanakubaliana kwa ujumla kwamba zaidi ya watu kuwa na bunduki, kuna sababu nyinginezo zinazoathiri kiwango cha mauaji na uhalifu.

Shirika la Kitaifa la Bunduki huko Marekani ambalo lina uwezo mkubwa limesema hivi mara nyingi: “Bunduki haziui watu; watu ndio huua.” Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ingawa bunduki imetengenezwa kwa kusudi la kufisha, yenyewe haiui. Lazima mtu fulani afyatue bunduki, kimakusudi au kwa aksidenti. Bila shaka, watu fulani hubisha kwamba bunduki hufanya iwe rahisi kwa watu kuua watu.

Kufua Panga Ziwe Majembe

Kulingana na Biblia, tatizo la watu kuuana halitasuluhishwa kwa kuwanyanganya bunduki watu wenye nia ya kuua. Uhalifu si tatizo linalosababishwa na watu kuwa na silaha, bali ni tatizo la kijamii. Suluhisho la kweli ni kubadili mielekeo na tabia ya watu wenyewe. Nabii Isaya alipuliziwa kuandika hivi: “Naye [Mungu] atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.”—Isaya 2:4.

Hilo si jambo lisilowezekana kama wengine wanavyoweza kudhani. Unabii wa Isaya sasa unatimizwa kote ulimwenguni miongoni mwa Wakristo wa kweli. Kugeuza kwao kitamathali silaha za vita kuwa vyombo vya amani hudhihirisha tamaa yao yenye kina ya kumpendeza Mungu na kuishi kwa amani na watu wengine. Wakati ujao, chini ya Ufalme wa Mungu, kila mtu duniani ataishi kwa amani kamilifu na usalama. (Mika 4:3, 4) Bunduki hazitaua watu. Watu hawatawaua watu. Vifaa vya kufisha havitakuwapo tena.

[Picha katika ukurasa wa 10]

“Watafua panga zao ziwe majembe”