Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Akili Huathiri Moyo
Kulingana na kijarida cha Tufts University Health & Nutrition Letter, mkazo wa akili huongeza uwezekano wa kupatwa na mshtuko wa moyo mara ya pili, na “kuna uthibitisho wenye kuongezeka unaoonyesha kwamba akili pia huchangia kusitawi kwa maradhi ya moyo.” Uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba “watu wenye kukasirika upesi wako katika hatari ya kupatwa na mshtuko wa moyo mara tatu zaidi ya watu wengine au kufa kutokana na maradhi ya moyo” na kwamba “yaonekana athari ya hasira kwa moyo hujidhihirisha mapema maishani.” Mkazo huharibu misuli ya moyo na mishipa ya damu inayozunguka moyo na kuulisha. Kushuka moyo kwaweza kuongeza hatari ya mshtuko wa moyo au maradhi mengine ya moyo kwa asilimia 70. Hata hivyo, wachunguzi wanasema kwamba tegemezo zuri la kijamii—la washiriki wa familia na marafiki—laweza kupunguza athari ya mshukomoyo.
Papa Anayebishaniwa
Mnamo Septemba 2000, Papa John Paul wa Pili alimtangaza Pius wa Tisa (papa, 1846-1878) kuwa mtakatifu. Mwanahistoria Mfaransa René Rémond alisema katika gazeti la Kikatoliki la La Croix, kwamba Pius wa Tisa alifanya “uamuzi wenye kushtua wanadini—kama vile kuruhusu Waitalia wazalendo wahukumiwe kifo kwa kuwa walipinga mamlaka yake kama kiongozi wa Taifa.” Likimtaja kuwa “maliki wa mwisho mwenye uwezo wote huko Ulaya,” gazeti la Le Monde lilizungumzia ushupavu wa papa huyo ambaye pia alikuwa mfalme na hasa jinsi alivyopinga “uhuru wa kuchagua, haki za kibinadamu, na uhuru wa Wayahudi.” Gazeti hilo liliongeza kusema kwamba Pius wa Tisa “alipinga demokrasia, uhuru wa kidini, na kutenganishwa kwa mamlaka ya Kidini na ya Kitaifa” na pia “uhuru wa kuchapisha, uhuru wa kujieleza, na wa kukusanyika.” Ni mtu huyo, Pius wa Tisa aliyefungua mkutano wa kwanza wa baraza la Vatikani katika mwaka wa 1869 ambapo fundisho la ukamilifu wa papa katika mambo ya imani na maadili lilielezwa wazi.
Wachimbaji Wenye Bidii
Wakulima huko Chile wanasumbuliwa na panya mdogo mwenye manyoya mengi aitwaye coruro ambaye huchimba vijia katika udongo wa juu ambavyo hufikia urefu wa meta 600. Hivi karibuni, utafiti wenye kina wa mfumo tata wa vijia hivyo ulifanywa. Wanazuolojia wawili, mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Essen, Ujerumani, na mwenzake Mchile, walifukua kabisa makazi ya wanyama 26. Katika bohari ya chakula walipata viazi 5,000, ambavyo vimehifadhiwa vitumiwe wakati wa kiangazi. Mfumo huo wa vijia ulikuwa pia na vyumba vya kuzalia vilivyotandikwa nyasi na mifuko ya plastiki. Hata hivyo, ingawa wanyama hao weusi wenye meno ya mbele makubwa ni maridadi sana, wakulima huwaona kuwa wasumbufu. Ng’ombe huvunjika mguu wakanyagapo vijia hivyo na kuingia ndani.
Gugu la Ajabu —Dandelion
Gazeti la The News la Mexico City lasema kwamba gugu la dandelion ‘huonwa na wasimamizi wa nyanja za michezo ya gofu na watu wanaopenda nyanja zenye nyasi fupi kuwa adui mkubwa na pia gugu sugu.’ Hata hivyo, gugu la dandelion “ni mojawapo ya mimea yenye dutu nyingi za afya ulimwenguni” na linaweza kuchangia sana hali njema ya afya yako na lishe. Gugu hilo la dandelion lina Vitamini A na potasiamu nyingi na hivyo ni lenye lishe bora zaidi kuliko brokoli au spinachi. Sehemu zake zote zinalika. Majani yake machanga hutumika kama saladi au katika chakula chochote kinachohitaji spinachi, mizizi iliyokaushwa na kuchomwa hutumika kutengeneza kinywaji kinachofanana na kahawa na maua yake hutumika katika utengenezaji wa divai. Tangu zamani gugu la dandelion limetumika kutuliza na kusafisha ini, kusafisha na kuongeza damu mwilini na pia kama dawa hafifu ya kupambana na matatizo ya kukojoa. Gazeti la The News lasema kwamba gugu la dandelion “ni miongoni mwa dawa sita maarufu za mitishamba ya Wachina.” Watu wenye nyanja zenye nyasi fupi au wanaoishi karibu na malisho ya mifugo wanaweza kupata dandelion bila malipo.
Myeyuko wa Barafu Katika Milima ya Andes
Tangu miaka 67 iliyopita, eneo la barafuto katika Milima ya Andes huko Peru limepungua kwa meta 850 hadi meta 1,500, laripoti gazeti la El Comercio la Lima. Kulingana na uchunguzi uliofanywa na mtaalamu wa barafuto Mfaransa Antoine Erout, katika miaka 20 hivi, kuyeyuka kwa barafuto kumetokeza maziwa mapya 70—baadhi ya maziwa hayo yanatarajiwa
kufurika na kuvunja vizuizi vyake vya asili. Kuyeyuka kwa barafu na theluji, kunapunguza hifadhi ya maji safi yanayotumika katika mashamba, miradi ya kunyunyizia mashamba maji, na mitambo ya umeme inayoendeshwa na maji. Maji hayo ndio hutumika pia katika miji mikuu ya Amerika ya Latini: Lima, Peru; Quito, Ekuado; na La Paz, Bolivia. “Je, waweza kuwazia jinsi ambavyo hali ingekuwa ikiwa theluji na barafu yote hiyo ingeyeyuka?” lauliza gazeti hilo la El Comercio. Erout adokeza kwamba mabadiliko ya hali ya hewa yanayohusianishwa na El Niño ni miongoni mwa visababishi vikuu vya tatizo hilo.“Maradhi ya Utajiri wa Ghafula”
Gazeti la National Post la Kanada lasema kwamba “idadi ya mamilionea huko Marekani na Kanada imeongezeka kwa takriban asilimia 40 tangu mwaka wa 1997 kufikia watu milioni 2.5.” Gazeti hilo pia lilisema kwamba ulimwengu wa kitekinolojia umewafanya vijana wengi kuwa matajiri kupindukia. Hata hivyo, kulingana na mtaalamu wa afya ya akili Dakt. Stephen Goldbart wengi wa watu hao hawajui namna ya kukabiliana na utajiri huo wa ghafula. “Utajiri huo unaweza kusababisha familia yao kuvunjika na kuharibu maisha yao. Pesa hazitokezi amani na uradhi sikuzote,” akasema Goldbart. Kulingana na wataalamu fulani wa afya ya akili, ulimwengu wa kitekinolojia umetokeza “maradhi mapya—maradhi ya utajiri wa ghafula” ambayo dalili zake ni kushuka moyo sana, hofu ya ghafula, na kukosa usingizi. Kama ilivyotajwa katika gazeti la Post, “baadhi ya watu ambao wametajirika ghafula wanahisi wakiwa na hatia kwa sababu ya kuwa na pesa nyingi kupindukia na kwamba hawastahili kuwa nazo au kwamba utajiri huo si haki yao.” Wengine wamepatwa na wasiwasi na wanahofia kutumiwa vibaya na watu. Dakt. Goldbart adokeza kwamba watu hao matajiri wasio na furaha wajishughulishe na mambo ya kijamii badala ya kutoa tu msaada wa kifedha.
Kutumia Viuavijasumu Kupita Kiasi
“Maonyo ya mara kwa mara ya maofisa wa afya kuhusu kutumia viuavijasumu kupita kiasi hayazingatiwi kamwe,” lasema gazeti la New Scientist. “Uchunguzi uliofanywa kwa watu 10,000 katika majimbo tisa ya Marekani ulionyesha kwamba asilimia 32 bado wanaamini kwamba viuavijasumu vyaweza kutibu mafua, asilimia 27 wanaamini kwamba kutumia viuavijasumu wakiwa na mafua kutazuia kushikwa na magonjwa mabaya zaidi, na asilimia 48 wanatazamia kupewa viuavijasumu wanapomwona daktari kwa sababu ya mafua.” Hata hivyo, viuavijasumu havitibu maambukizo ya virusi kama vile mafua. Hutibu maambukizo ya bakteria pekee. Kutumia viuavijasumu kupita kiasi ni kisababishi kikubwa cha magonjwa sugu. (Ona Amkeni! la Desemba 22, 1998, ukurasa wa 28.) Brian Spratt wa Chuo Kikuu cha Oxford asema hivi: “Tunapaswa kupata njia nyingine nzuri zaidi ya kuelimisha watu juu ya tatizo hilo.”
Mdudu wa Ajabu wa Barafu
Gazeti la The Sunday Telegraph la London laripoti kwamba “picha za mwanzo-mwanzo kuchapishwa za ‘mdudu adimu wa barafu’ mwenye makao yake katika milima ya Rocky na katika sehemu za Urusi zitaonekana katika kitabu kilichoandikwa hivi karibuni cha Handbook of Insects.” Mdudu huyu mwenye kutambaa miambani anaishi juu ya milima mirefu na chakula chake ni wadudu wafu au viungo vya wadudu vilivyopeperushwa na upepo hadi mahali alipo. Mdudu huyo ana rangi ya hudhurungi na manjano na vipapasi virefu lakini hana mabawa, na wachanga wake hufanana na kiwavi cha mdudu aitwaye earwig. Ana urefu wa sentimeta tatu na ni baadhi ya wadudu waliogunduliwa muda usiozidi miaka 100 iliyopita. Gazeti hilo lasema kwamba “mdudu huyo amezoea mazingira hayo baridi hivi kwamba atakufa kwa mshtuko wa moyo kwa sababu ya joto akiwekwa kwenye kiganja cha mkono wa binadamu.” Mwandishi wa kitabu cha Handbook of Insects, Dakt. George McGavin wa Jumba la Makumbusho ya Mambo ya Asili katika Chuo Kikuu cha Oxford, asema kwamba katika jumla ya wadudu ulimwenguni ni takriban mdudu mmoja kati ya watano ambaye amewahi kugunduliwa.
Mbona Wanaongeza Kafeini Ndani ya Soda?
“Mbona kafeini iwe ndani ya soda iwapo si muhimu kwa ladha?” lauliza gazeti la New Scientist. “Wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins huko Baltimore waligundua kwamba kati ya watu wazima 25 ni 2 pekee ambao waliweza kutambua tofauti baina ya soda yenye kafeini na isiyo na kafeini.” Lakini, asilimia 70 ya soda bilioni 15 zilizotumiwa na Wamarekani katika mwaka wa 1998 zilikuwa na kafeini. Kwenye uchunguzi uliofanywa awali, mtaalamu wa dawa zinazoathiri akili, Roland Griffiths pamoja na wenzake “waligundua kwamba watoto walionyimwa kiwango chao cha kawaida cha soda walikumbwa na dalili zinazofanana na zile za kuacha dawa za kulevya.” Griffiths abisha hivi: “Wanaongeza dawa hafifu ya kulevya na hiyo ndiyo sababu soda zilizo na kafeini hutumiwa na watu wengi sana kuliko zile ambazo hazina kafeini.”