Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kufanya Bara Kame Litoe Mazao

Kufanya Bara Kame Litoe Mazao

Kufanya Bara Kame Litoe Mazao

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI INDIA

Inawezekanaje kulifanya bara kame la Ladakh, wilaya moja iliyoko kaskazini mwa India, litoe mazao zaidi? Swali hilo lilikuwa akilini mwa Tsewang Norphel, mhandisi-ujenzi aliyestaafu. Maji ya barafu yenye kuyeyuka kutoka Milima ya Himalaya huanza kutiririka mwezi wa Juni, wala sio mwezi wa Aprili kunapokuwa na ukame na wakulima wanapohitaji kunyunyizia mashamba yao maji. Norphel alibuni mpango mwafaka: kuanzisha barafu isiyo ya asili katika sehemu za chini za mlima, ambapo barafu inaweza kuyeyuka mapema zaidi mwakani.

Kwa mujibu wa gazeti la habari la India The Week, Norphel pamoja na kikundi chake alianza kwa kuelekeza maji ya kijito kimoja cha mlimani kwenye mtaro wenye urefu wa meta 200 uliochimbwa na watu uliounganishwa na mifereji midogo 70 ya kutolea maji. Kupitia mifereji hiyo, maji yalitarajiwa kutiririka kwa utaratibu wenye kudhibitiwa na kuwa barafu kabla ya kufika kwenye kuta za kuyazuilia zilizojengwa sehemu ya chini ya mlima. Barafu ilitarajiwa kuongezeka na kufunika kuta hizo. Kwa sababu sehemu yenye barafu iko upande wa mlima usioelekea upepo, barafu hiyo ilitarajiwa kuyeyuka tu mwezi wa Aprili, wakati ambapo hali ya joto huongezeka, na kwa njia hiyo kuwapa wakulima maji yanayohitajika sana kunyunyizia mashamba.

Je, mpango huo wa kujenga barafu isiyo ya asili ulifua dafu? Mradi wa Norphel ulifanikiwa sana hivi kwamba miradi mingine kumi ya barafu kama huo imekamilishwa huko Ladakh, na miradi mingine zaidi inaendelea kujengwa. Mojawapo ya miradi hiyo uliojengwa kwenye kimo cha meta 1,400 hutokeza maji lita milioni 34. Uligharimu pesa ngapi? “Kujenga mradi wa barafu isiyo ya asili hukamilishwa kwa miezi miwili hivi na hugharimu dola 1,860 za Marekani, kiasi kikubwa cha pesa hizo hutumiwa kulipa mishahara ya wafanyakazi,” lasema gazeti la The Week.

Maarifa ya mwanadamu yanapotumiwa ifaavyo, bila shaka yanaweza kuleta faida. Ebu wazia yale wanadamu wataweza kutimiza chini ya mwelekezo wa Ufalme wa Mungu wa kimbingu! Biblia yaahidi hivi: “Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. . . . Katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani.” (Isaya 35:1, 6) Itakuwa furaha iliyoje kushiriki kazi ya kuigeuza dunia yetu kuwa paradiso!

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

Arvind Jain, The Week Magazine