Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuna Tumaini Gani kwa Majiji?

Kuna Tumaini Gani kwa Majiji?

Kuna Tumaini Gani kwa Majiji?

“WAKATI wetu ujao unategemea majiji yetu.” Ndivyo alivyosema Ismail Serageldin wa Benki ya Dunia. Lakini kutokana na yale tuliyozungumzia, wakati wetu ujao hauonekani ukiwa mwangavu.

Jambo la kufurahisha ni kwamba jitihada madhubuti zinafanywa ili kuboresha maisha katika majiji mengi. Hivi majuzi New York City lilikamilisha ukarabati wa mtaa wa Times Square huko Manhattan. Hapo awali, mtaa huo ulikuwa maarufu kwa sababu ya majengo yaliyokuwa yakiendesha biashara za ponografia, ulanguzi wa madawa ya kulevya, na uhalifu. Sasa maduka mapya na kumbi mpya zimetapakaa mtaani na zinavutia maelfu ya watalii. Jiji la Naples, Italia, “jiji maridadi lenye majengo mengi ambalo pindi moja lilionwa kuwa la kiwango sawa na London na Paris,” kwa mujibu wa gazeti National Geographic, liliharibiwa wakati wa Vita ya Pili ya Ulimwengu. Jiji la Naples likawa kitovu cha uhalifu na vurugu. Hata hivyo, jiji hilo lilisitawi tena kufuatia kazi kubwa ya kukarabati eneo lake kuu la kibiashara baada ya kuteuliwa kuwa mahali pa kufanyia mkutano wa kisiasa mwaka wa 1994.

Bila shaka, jitihada zinahitajika ili kuwa na majiji salama na safi. Lazima kuwe na polisi wengi zaidi ili usalama zaidi uwepo. Huenda watu wakakosa faragha pia. Maeneo fulani ya umma huchunguzwa daima kwa kamera za televisheni kutia na polisi wanaovalia kiraia. Unapotembea bustanini na kupita mabubujiko ya maji, sanamu, au sehemu zenye maua, huenda ukapita vituo vya kulinda usalama pasipo kujua.

Nyakati nyingine maendeleo huathiri sana watu maskini. Fikiria hali inayoitwa gentrification—kugeuzwa kwa maeneo ya watu maskini yafae matajiri. Hali hiyo husababishwa na mabadiliko ya uchumi—“utoaji wa huduma unapositawi badala ya utengenezaji wa bidhaa, utumizi wa mashine badala ya kutegemea wafanyakazi wa viwandani.” (Kichapo Gentrification of the City, kilichohaririwa na Neil Smith na Peter Williams) Kazi za viwandani zinapokosekana na uhitaji wa wataalamu na wa mafundi-sanifu unapoongezeka, kunakuwa na uhitaji mkubwa wa nyumba nzuri za wastani. Badala ya kusafiri kila siku hadi vitongojini, wataalamu wengi wenye mishahara minono hupendelea kukarabati nyumba katika maeneo yaliyokuwa makazi ya watu maskini.

Bila shaka, hatua hiyo huboresha sana maeneo hayo. Lakini malipo ya nyumba hupanda sana maeneo yanapoboreshwa. Mara nyingi watu maskini hushindwa kumudu maisha kwenye maeneo ambako wameishi na kufanya kazi kwa miaka mingi!

Je, Majiji Yanadidimia?

Majiji yameanza tu kuathiriwa na mabadiliko yanayosababishwa na tekinolojia mpya. Kadiri watu wanavyozidi kutumia Internet kununua bidhaa na kuendesha biashara, ndivyo hali inavyobadilika sana. Tayari tekinolojia mpya imefanya iwe rahisi kwa biashara fulani kuhamia vitongojini—na wafanyakazi wengi wamehama pia.

Watu wengi wanaponunua bidhaa na kufanya kazi kupitia Internet, hawapendi tena kusafiri kwenye maeneo ya kibiashara yaliyosongamana watu. Kitabu Cities in Civilization chadokeza hivi: “Huenda tukaona wafanyakazi wengi wakifungua maofisi nyumbani au vitongojini tu, . . . na hivyo kupunguza msongamano.” Hali kadhalika, msanifu-ujenzi Moshe Safdie akisia hivi: “Katika mazingira haya mapya, huenda mamilioni ya vijiji vikasambaa ulimwenguni pote, ambamo wakazi watafurahia starehe katika miji midogo itakayofikiwa na mambo mengi ya kisasa kupitia kwa kompyuta na Internet kama majiji maarufu ya kihistoria.”

Kuna Tumaini Gani kwa Majiji?

Wachunguzi wengi wanaamini kwamba mbali na tekinolojia, majiji huandaa huduma na manufaa ambayo yataendelea kuvutia watu. Haidhuru hali ya wakati ujao, majiji ya leo yamo taabani sasa! Na hakuna tumaini la kusuluhisha matatizo makubwa ya ukosefu wa nyumba na kuondoa uchafu katika mitaa ya mabanda majijini. Wala hakuna yeyote aliyepata njia muafaka ya kukomesha uhalifu, uharibifu wa mazingira, au uchafuzi wa majiji.

Huenda wengine wakawa na maoni kwamba serikali zapasa kutumia fedha zaidi kutunza majiji yake. Lakini tuzingatiapo historia ya serikali nyingi ya kutunza mali zake, je, ni jambo la busara kufikiri kwamba ni rahisi sana kusuluhisha matatizo yanayokabili majiji mradi kuna fedha? Miongo mingi iliyopita kitabu The Death and Life of Great American Cities kilisema hivi: “Kuna kauli yenye kosa ya kwamba kama tungekuwa na fedha za kutosha . . . , tungeondolea mbali mitaa yetu yote ya mabanda . . . Lakini fikiria matokeo ya kutumia mabilioni kadhaa ya kwanza ya fedha ili kuboresha vitongoji: Makazi yasiyoleta faida ambayo yamejaa uhalifu, uharibifu wa mali na matatizo mengine mengi ya kijamii ambayo yalitarajiwa kutokomea baada ya mitaa ya mabanda kubomolewa.” Maneno hayo yangali kweli.

Basi ikiwa fedha hazitasuluhisha matatizo hayo, yatasuluhishwaje? Ni sharti tukumbuke kwamba majiji hufanyizwa na watu, si majengo tu wala barabara. Kwa hivyo, watu hawana budi kubadilika iwapo maisha ya majijini yatakuwa bora. “Ufanisi bora wa jiji ni utunzaji na uelimishaji wa watu,” asema Lewis Mumford katika kitabu The City in History. Ili kukomesha matumizi mabaya ya dawa za kulevya, ukahaba, uchafuzi, uharibifu wa mazingira, tofauti za kijamii, uharibifu wa mali, michoro ya ukutani, na mambo kama hayo, haitoshi tu kuongeza idadi ya askari au kupaka upya majengo rangi. Ni lazima watu wasaidiwe kubadili kabisa fikira zao na tabia zao.

Mabadiliko Katika Usimamizi

Ni wazi kwamba wanadamu hawana uwezo wa kubadili mambo. Kwa hiyo jitihada za kusuluhisha matatizo ya majiji ya leo—hata ziwe na madhumuni bora kama nini—hazitafaulu mwishowe. Hata hivyo, wanafunzi wa Biblia hawakati tamaa kwa sababu wanaona matatizo yanayokumba majiji leo kuwa mfano mmoja wa kushindwa kwa mwanadamu kusimamia sayari yetu ifaavyo. Majiji ya leo makubwa na yenye vurugu, huthibitisha waziwazi maneno ya Biblia kwenye Yeremia 10:23: “Njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” Jitihada za mwanadamu za kujitawala zimesababisha matatizo mengi sana—matatizo ambayo yameenea sana katika majiji yetu.

Wakazi wa majijini kotekote ulimwenguni wanaweza kufarijiwa na ahadi ya Biblia iliyorekodiwa kwenye Ufunuo 11:18, kwamba Mungu ‘atawaleta kwenye uangamizi wale wanaoiangamiza dunia.’ Badala ya kuashiria mabaya, ahadi hiyo yatoa tumaini zuri la wakati ujao kwa wanadamu. Yaahidi kwamba Mungu atasimamia sayari yetu kupitia kwa serikali, au Ufalme. (Danieli 2:44) Mamilioni ya watu hawataishi tena wakiwa maskini hohehahe, kwenye makao yasiyofaa na machafu, hawatadhalilishwa tena, wala kuishi bila tumaini. Chini ya utawala wa serikali ya Mungu, watu watafurahia ufanisi wa kimwili, afya nzuri, na nyumba nzuri.—Isaya 33:24; 65:21-23.

Ulimwengu huo mpya ndio tumaini halisi na la pekee la kusuluhisha matatizo yanayokumba majiji ya leo.

[Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Jitihada madhubuti zinafanywa ili kuboresha maisha katika majiji mengi

Naples, Italia

New York City, Marekani

Sydney, Australia

[Hisani]

SuperStock

[Picha katika ukurasa wa 10]

Ulimwengu mpya wa Mungu utasuluhisha matatizo ya wakazi wa majijini leo