Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Majiji Yanafurika Watu”

“Majiji Yanafurika Watu”

“Majiji Yanafurika Watu”

“Wanadamu wanahama sana kuliko wakati mwingineo wote, na wengi wanaotoka nyumbani huelekea kwenye majiji ili kutafuta maisha bora.”

NDIVYO kilivyosema kichapo Foreign Affairs katika utangulizi wa makala yenye kichwa “Majiji ya Nchi Zinazositawi Yanafurika Watu.” Kwa mujibu wa makala hiyo, watu wengi “wameshawishiwa na maisha ya kuvutia, au wamelazimika kuhama mashambani kwa sababu ya misukosuko ya kisiasa na ya kiuchumi, mikazo ya ongezeko la idadi ya watu, na kuharibika kwa ekolojia.”

Majiji yanakua kasi kadiri gani? Watu fulani hukadiria kwamba idadi ya watu wanaofurika majijini ni zaidi ya milioni moja kila juma! Zaidi ya majiji 200 katika nchi zinazositawi sasa yana watu zaidi ya milioni moja. Idadi ya watu katika majiji yapatayo 20 imefikia milioni kumi! Na watu wangali wanaongezeka. Kwa mfano, fikiria jiji la Lagos, Nigeria. Ripoti moja ya Taasisi ya Worldwatch inasema kwamba “kufikia mwaka wa 2015, huenda Lagos likawa na wakazi wapatao milioni 25, na kuwa ya tatu kutoka nambari kumi na tatu katika orodha ya majiji yenye wakazi wengi.”

Wataalamu wengi wanahisi kwamba hiyo ni dalili mbaya ya wakati ujao. Federico Mayor, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, aonya kwamba kufikia mwaka wa 2035, “watu milioni elfu tatu watakuwa wakiishi katika majiji yaliyopo leo.” Ili idadi hiyo kubwa ya watu ipate makao, “tutalazimika kujenga majiji elfu moja yenye wakazi milioni tatu kwa muda wa miaka arobaini ijayo, majiji ishirini na matano kila mwaka.”

Wataalamu wanasema pia kwamba idadi ya watu inayoongezeka kasi katika majiji inaathiri sana majiji ulimwenguni pote. Kutia ndani majiji ya nchi zilizositawi kiviwanda. Majiji yanakabili matatizo yapi, na matatizo hayo yanaweza kukuathirije? Je, yatasuluhishwa? Makala zifuatazo zinachanganua masuala hayo muhimu.