Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Uthibitisho wa Uumbaji Kwa miaka mingi nilipokuwa nikifanya kazi miongoni mwa wanasayansi, nilikerwa mara nyingi niliposikia wakidai kwamba imani katika uumbaji ni sahili mno. Jibu mwafaka kwa madai hayo lapatikana katika mfululizo wa makala “Kuona Visivyoonekana kwa Macho Matupu.” (Agosti 22, 2000) Kwenye kurasa chache tu mliweza kuandaa uthibitisho wenye kusadikisha wa uumbaji. Gazeti la Amkeni! lastahili pongezi kwa sababu ya ubora wa yaliyomo na utafiti wake.

B. E., New Zealand

Najifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova, na pasina shaka imani yangu katika Mungu ilitiwa nguvu nilipojifunza kuhusu atomu, chembe, na DNA.

T. K., Japani

Sasa naweza kueleza jinsi upinde-mvua unavyofanyizwa, kwa nini nyasi zina rangi ya kijani kibichi, na atomu ni nini! Ijapokuwa Amkeni! si gazeti la kisayansi linachapisha habari ya kisayansi yenye kuunga mkono imani katika Muumba.

M. F., Marekani

Kupona Bila Kutiwa Damu Niliguswa sana na ile makala “Inategemea Dhamiri.” (Agosti 22, 2000) Nilijikuta katika hali kama hiyo ilipobainishwa kuwa nina kansa hatari sana iitwayo promyelocytic leukemia. Mambo yaliyonipata baada ya hapo yafanana sana na yale ya Darlene. Nilielezwa ningekufa baada ya siku chache tu. Hiyo ilikuwa miaka mitatu iliyopita.

A. B., Ujerumani

Kusumbuliwa Kingono Nataka kuwashukuru kwa ajili ya makala “Vijana Huuliza . . . Naweza Kupambanaje na Kusumbuliwa Kingono?” (Agosti 22, 2000) Shuleni wanafunzi walinibandika majina mengi kwa sababu nilikataa ukosefu wa adili. Nilipomaliza shule ya sekondari nilifikiri tabia hiyo ingekoma, lakini bado wasichana fulani wamenitongoza kwa maneno. Kujulisha waziwazi imani yangu ya Kikristo kumenilinda na utongozi huo. Asanteni kwa kutuandalia chakula hicho cha kiroho.

H. C., Zambia

Makala hiyo ilifaa sana. Mvulana fulani katika darasa letu la kidato cha tatu hachoki kunitazama. Sasa najua jinsi ya kukabili hali hiyo.

H. K., Marekani

Makala hiyo ilikuja wakati ufaao! Ninasumbuliwa kingono kazini. Nimekuwa nikisumbuka sana moyoni. Nilipokuwa nimelemewa kabisa, makala hiyo ikatokea. Sasa najua namna ya kushughulika na wafanyakazi hao.

L. T., Marekani

Jiji la Urusi Kwa sababu kampuni ninayofanyia kazi ni ya kimataifa, mimi hufurahia kusoma makala kuhusu nchi mbalimbali. Mwana wa mfanyakazi mwenzetu anaishi Urusi, kwa hiyo nikamweleza juu ya makala “Kuzuru ‘Jiji la Kale Zaidi la Urusi.’” (Agosti 22, 2000) Alifurahi alipoipokea na baada ya kuisoma akaagiza nakala nyingine ya Amkeni! Nilimpa toleo la Mei 22, 2000, lenye makala “Saa ya Pekee Huko Prague.” Toleo hilo lilimchochea akubali kuandikisha Amkeni! Asanteni kwa kuchapisha habari muhimu jinsi hiyo.

S. O., Marekani

Mchuzi Wenye Maji Mengi Mno Niliamua kupika mchuzi wa Hungaria kwa kutumia mapishi katika makala “Kiungo Kilichotoka Sehemu za Mbali Sana za Dunia.” (Septemba 8, 2000) Upishi uliendelea vyema hadi nilipotia maji lita mbili kama ilivyoshauriwa. Mchuzi wangu ulikuwa majimaji badala ya kuwa mzito kama unavyoonekana kwenye picha. Je, labda sikuelewa mapishi hayo?

L. P., Kanada

La, tulirejezea kimakosa mlo huo kuwa mchuzi ilhali wapasa kuwa supu ya Hungaria. Vitabu vingine vya mapishi hudokeza kutumia kiasi kidogo cha maji kuliko tulivyopendekeza. Hata hivyo, baadhi ya wasomaji walipika mlo huo wakitumia madokezo hayo na wametuandikia kutuarifu jinsi walivyofurahia!—Mhariri.