Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

“Watoto Wasumbufu”

Maeneo ya maduka huko Uingereza “yamevamiwa na kizazi kipya cha watoto wenye kutumia pesa ovyo, na wenye kupenda mitindo mipya,” laripoti gazeti la The Times la London. Gazeti hilo laongeza kusema kwamba “wakiwa na umri wa miaka kati ya 10 na 13, wanaweza kujiamulia wanachotaka kununua lakini ni ‘watoto wasumbufu’ wanapotaka kupata pesa kutoka kwa wazazi wao za kulipia vitu vya bei ghali wanavyotaka.” Piers Berezai wa kampuni ya Datamonitor ya utafiti wa hali ya ununuzi, asema hivi: “Talaka zenye kuongezeka zimefanya wanawake wengi wazazi wafanye kazi na kuwapa watoto wao pesa ili kutuliza dhamiri zao zenye kuwashutumu kwa sababu hawatumii wakati pamoja nao. Watoto wamegundua kwamba kusumbua ni njia mwafaka ya kupata kile wanachotaka. Wazazi wanaokuwa mbali na watoto wao kwa muda mrefu huwa na haraka ya kukubali madai yao na kuwaendekeza.”

Wanakula Chakula cha Watoto

Shirika la habari la Ujerumani dpa-Basisdienst laripoti kwamba kiasi kikubwa cha chakula cha watoto wachanga huliwa na watu wazima. Asilimia kumi ya chakula cha watoto kinachotayarishwa na kampuni moja kubwa huko Ujerumani huuzwa kwenye nyumba zisizo na watoto. Watu wa kila umri na wa namna zote hupenda chakula cha maziwa kilicho na matunda cha watoto. Kwa kuwa mlo mmoja huenda ukawa na kalori 100 tu watu wengi wenye kuhofia kunenepa hupendelea mlo mwepesi wa watoto. Ili kuchochea tabia hiyo, makampuni hutangaza bidhaa zao kuwa zinafaa “wakubwa kwa wadogo” na hutoa maelezo ya upishi yanayotia ndani bidhaa zao. Hata hivyo, shirika la lishe la German Nutrition Society limehuzunishwa na tabia hiyo. Kulingana na msemaji wake, Anette Braun, watu wazima hawapaswi kula chakula kilichotayarishwa kwa njia hiyo ya kipekee isipokuwa tu wawe wagonjwa. Wanapasa kutafuna chakula chao. “Meno ni ya kusudi hilo,” asema Braun.

Uraibu wa Sigareti Huanza Upesi

Shirika la habari la Associated Press laripoti kwamba, watafiti katika Chuo Kikuu cha Massachusetts wamethibitisha kwamba dalili za uraibu huonekana “siku chache baada tu ya mtu kuanza kuvuta sigareti.” Watafiti hao walichunguza kwa mwaka mmoja tabia ya vijana 681 wenye umri wa kati ya miaka 12 na 13 wanaovuta sigareti na kurekodi dalili za uraibu. “Imekisiwa kwamba watu huwa waraibu upesi sana,” asema Dakt. Richard Hurt, “lakini huu ndio ushuhuda halisi wa kwanza wenye kuthibitisha jambo hilo.” Mkurugenzi wa kundi hilo la watafiti Dakt. Joseph DiFranza alisema hivi: “Jambo muhimu liwezalo kutimizwa na utafiti huu ni kuwaonya vijana kwamba hawapaswi kuona kuvuta sigareti kuwa jambo la mzaha wala hawawezi kutazamia kuanza kuvuta sigareti na kuacha tabia hiyo baada ya majuma machache.”

Makanisa Yakiri Kutumikisha Watu

Hivi karibuni wenyeji wa Ujerumani walishangaa waliposikia kwamba kanisa Katoliki na makanisa ya Kievanjeli yalitumikisha watu wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili. Kulingana na msemaji wa Kongamano la Maaskofu Wakatoliki huko Ujerumani, “watu walifanya kazi ya sulubu kwenye mashamba yenye kumilikiwa na kanisa—kwenye bustani za watawa, mashamba ya mizabibu na katika mahospitali,” laripoti gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung. Gazeti la Süddeutsche Zeitung lasema kwamba “watu walitumikishwa [katika mashirika makubwa ya kutoa misaada na ya kijamii ya Makanisa ya Kievanjeli] muda wote wa Vita ya Ulimwengu ya Pili.” Kanisa Katoliki na makanisa ya Kievanjeli yametenga milioni kadhaa za maki za Ujerumani kufidi watu waliotumikishwa, wengi wao ni wenyeji wa nchi za Ulaya Mashariki.

Je, Peremende za Zinki Zaweza Kutuliza Mafua?

Uwezo wa madini ya zinki wa kutuliza mafua umejadiliwa na watafiti kwa miaka mingi. Katika uchunguzi wa hivi karibuni ilipatikana kwamba “kwa wastani mafua hutulia kwa muda mfupi peremende za zinki zitumiwapo kila baada ya saa chache,” laripoti gazeti la Science News. Isitoshe, watu waliomumunya peremende hizo kila baada ya saa mbili au tatu kwa siku nne au tano “walipata kwamba kukohoa na kufuta kamasi kulipungua sana kuliko wale waliopokea dawa bandia.” Hata hivyo, baadhi ya watu waliomumunya peremende hizo walipatwa na tatizo la kufunga choo na kukauka mdomo, lasema gazeti hilo.

Kuleta Makasisi Kutoka Nchi Nyingine

Kanisa Katoliki limeanza kuleta makasisi kutoka nchi za kigeni ili kutatua tatizo la uhaba wa makasisi katika nchi zilizoendelea, laripoti gazeti la L’Espresso la Italia. Seminari katika Italia, Ulaya na Amerika Kaskazini hazitokezi tena makasisi na kwa sababu hiyo dayosisi zimeshindwa kujaza nafasi za makasisi,” lasema gazeti hilo. Makasisi wameletwa kutoka Brazili, India, na Filipino ili kujaza nafasi hizo. Gazeti hilo la L’Espresso, laripoti kwamba “Huu ni mwanzo tu lakini jambo hilo limebadili kanisa. . . . Tayari kuna makasisi 1,131 katika Italia wasio wenyeji wa Muungano wa Ulaya, wao ni asilimia 3 ya makasisi wote wanaolipwa na Kongamano la Maaskofu.” Kwa sababu hiyo Italia imekuwa ‘eneo la kimishonari,’ lasema gazeti hilo.

Chakula Kikavu cha Wanyama Chaweza Kufanya Uwe Mgonjwa

“Chakula kikavu cha wanyama kinachotayarishwa kwa kutumia masikio, kwato, mapafu, na mifupa ya nguruwe na ng’ombe kimewaletea watu ugonjwa mbaya wa tumbo unaosababishwa na kiini cha Salmonella,” laripoti gazeti la FDA Consumer. Kulingana na madaktari huko Kanada, kwa muda uzidio mwaka mmoja, zaidi ya Wakanada 35 wamekuwa wagonjwa na kutibiwa baada ya kugusa masikio ya nguruwe yaliyokaushwa. Mkurugenzi wa shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa za Mifugo, Gloria Dunnavan adokeza kwamba watu wawe waangalifu sana wanaposhughulika na chakula kikavu cha wanyama. “Yaani, nawa mikono kwa sabuni na maji moto baada ya kugusa chakula hicho, usiweke chakula hicho palipo chakula cha binadamu (kama vile jikoni) na kuzuia watoto kuweka mikono yao mdomoni baada ya kugusa chakula hicho,” lasema gazeti hilo.

Vidonge Vinavyoona

Kampuni moja ya Israeli imebuni kidonge chenye uwezo wa kuona na kukagua maradhi yaliyoko kwenye utumbo mwembamba baada ya kumezwa, laripoti gazeti la Excelsior la Mexico. Kidonge hicho chenye kamera hupeleka habari kwenye mshipi maalumu ulio nyongani mwa mgonjwa. Kisha habari hiyo huchanganuliwa na kompyuta na kusomwa na wataalamu. Kidonge hicho hutoka mwilini pamoja na kinyesi. Kulingana na Dakt. Blair Lewis, njia hii ya kuchunguza magonjwa inafaa kwa sababu haisababishi maumivu. Mmoja wa watu waliobuni kidonge hicho, Profesa Paul Swain, asema kwamba “itawezekana kukagua sehemu ya chini ya utumbo mwembamba bila upasuaji au unusukaputi hata mgonjwa anapotembea.” Shirika la Marekani la Usimamizi wa Chakula na Dawa limetoa idhini vidonge hivyo vifanyiwe majaribio kwa wagonjwa 20 huko New York na London.

Kushuka Moyo Kazini Kwaongezeka

“Mkazo, mahangaiko na kushuka moyo kunakosababishwa na kazi huathiri mtu mmoja kati ya 10 kote ulimwenguni,” laripoti gazeti la kila siku la International Herald Tribune la Paris. Uchunguzi mmoja uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wafanyakazi ulipata kwamba mkazo unaosababishwa na kazi unagharimu Ulaya na Marekani zaidi ya dola bilioni 120 kila mwaka. Mkazo huo umesababishwa kwa sehemu na tekinolojia ambayo imetokeza mkazo zaidi kwa wafanyakazi. Gazeti la Tribune liliripoti kwamba katika Marekani, “wafanyakazi hushindwa kufika kazini siku zipatazo milioni 200 kila mwaka kwa sababu ya maradhi ya akili” na katika Finland zaidi ya nusu ya wafanyakazi huugua maradhi yanayosababishwa na mkazo. Zaidi ya hayo, asilimia 30 ya wafanyakazi katika Uingereza wameripotiwa kuwa na maradhi ya akili na asilimia 5 wamekumbwa na mshuko-moyo mkali sana.

Watu Mchanganyiko Hekaluni

Hekalu moja la kale la Kibudha nchini Japani linatembelewa na wageni ambao si waabudu. Tangu hekalu hilo liliporekebishwa mwaka wa 1955, ndege waitwao vigogota wamekuwa wakizuru humo. Mashimo ambayo ndege hao wametoboa katika hekalu hilo “ni mengi hivi kwamba watalii wamefikiri ni sehemu ya ujenzi—unaoruhusu mwangaza wa jua kupenya,” lasema gazeti la Asahi Evening News. Kasisi mkuu amelalamika kwamba jitihada ya kuwafukuza ndege hao imeambulia patupu. Hekalu hilo liitwalo Daizenji Temple lililo kwenye Mkoa wa Yamanashi lilijengwa mwaka wa 1286 na jumba lake kuu huonwa kuwa mali ya Kitaifa.