Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mnara wa Crest

Mnara wa Crest

Mnara wa Crest

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA

MINARA ya kale ina umbo na ukubwa mbalimbali na ilitumika kwa makusudi mengi. Minara kadhaa ilikuwa makao ya walinzi ilhali mingine ilitumika kama magereza, hata hivyo minara mingi leo hutembelewa na watalii. Mnara mkubwa katika mji mdogo wa Crest ulio kando ya Mto Drôme kusini-mashariki mwa Ufaransa umetumika kwa njia zote tatu.

Mnara wa Crest waweza kuonekana kutoka mbali kwa sababu ya ukubwa wake wa ajabu. Upande wake wa kaskazini-mashariki wenye urefu wa meta 52 hufanya uwe mojawapo ya minara mirefu zaidi katika Ufaransa. Mtu akiwa kwenye kilele chake aweza kuona mandhari yenye kuvutia sana ya vilima vya Vercors, milima ya Ardèche na bonde la Rhone.

Haijulikani ulijengwa lini ingawa mwanzoni ulikuwa ngome. Katika karne ya 13, wakati wa ile krusedi ya Waalbi, majeshi ya Wakatoliki yakiwa chini ya Simon de Montfort yalitwaa mnara huo yakisaidiwa na maaskofu Wakatoliki. Tangu wakati huo ulitumika ukiwa makao makuu ya wanajeshi waliokuwa wakipigana dhidi ya Waalbi.

Wakati wa Vita vya Kidini (1562-1598), mnara huo ulishambuliwa mara kadhaa na majeshi ya Waprotestanti lakini haukutwaliwa. Nusura mnara huo ubomolewe kabisa mwaka wa 1633, Mfalme Louis wa 13 alipoagiza uharibiwe. Sehemu yake iliyo imara sana ndiyo iliyosalia. Kutoka wakati huo na kuendelea ulitumika ukiwa gereza la wahalifu wa kawaida na wapinzani wa mfalme kutia ndani Wahuguenoti. Waprotestanti hao Wafaransa walifungwa wakati ile Amri ya Nantes ambayo ilikuwa imeruhusu kuwapo kwa dini nyingi huko Ufaransa ilipokuwa ikipuuzwa. Kuta za gereza hilo bado zina maandishi yaliyoandikwa na wafungwa hao wa kidini.

Mnara wa Crest sasa ni kumbukumbu la kihistoria lenye kutembelewa na takriban watalii 30,000 kila mwaka. Katika mwaka wa 1998 mnara huo ulitiwa ndani katika sherehe za kuadhimisha miaka 400 tangu kutiwa sahihi kwa Amri ya Nantes. Kuta zake ni ukumbusho wenye kuogofya wa matokeo ya kutovumiliana kidini.