Cherrapunji-Mojawapo ya Sehemu Zenye Mvua Nyingi Zaidi Duniani
Cherrapunji-Mojawapo ya Sehemu Zenye Mvua Nyingi Zaidi Duniani
Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini India
ETI mojawapo ya sehemu zenye mvua nyingi zaidi duniani? Yawezekanaje? Ni jambo la kawaida kukosa maji hapa India, na mara nyingi hutahitaji kubeba mwavuli! Basi mahala hapo pa ajabu ni wapi? Ni Cherrapunji—mji ulio katika jimbo la Meghalaya, kaskazini-magharibi mwa India. Mji huo unapakana na Bangladesh. Meghalaya ni sehemu maridadi sana hivi kwamba imeitwa “Scotland ya Mashariki.” Jina lake humaanisha “makao ya mawingu.” Lakini, ni kwa nini mji wa Cherrapunji umejulikana kuwa mojawapo ya sehemu zenye mvua nyingi zaidi duniani? Acheni tufunge safari fupi kuelekea sehemu hiyo yenye kupendeza. *
Twaanza safari yetu Shillong, jiji kuu la jimbo la Meghalaya. Twapanda basi la watalii na kusafiri kuelekea upande wa kusini. Tunapopita vilima na kanda za mbuga, twaona mawingu mbele yetu, nasi twakumbuka mara moja kwamba jina Meghalaya lafaa.
Barabara inapanda na kupinda kuzunguka ncha kali ya bonde lililofunikwa na miti mingi. Maji yaporomoka kutoka juu sana na kuingia kwenye mto unaotiririka kwa nguvu bondeni. Basi letu linaposimama Mawkdok, twaona mawingu yakijikusanya katikati ya vilima. Punde si punde mawingu yanafunika sehemu fulani ya ile mandhari kisha yaanza kuonekana mawingu yanaposonga. Kwa muda mfupi, hata sisi twafunikwa gubigubi na mawingu bila kuona chochote. Kisha, mawingu yanatoweka na jua laangaza mandhari hiyo yenye kuvutia.
Mji wa Cherrapunji uko meta 1,300 juu ya usawa wa bahari. Tunapofika mjini, hatuoni hata wingu moja, na hakuna aliyebeba mwavuli. Ni sisi wageni tu tuliojitayarisha kwa ajili ya mvua kubwa! Basi mvua hunyesha lini?
Maeneo ya tropiki hupata mvua kubwa wakati jua linapovukiza maji mengi kutoka kwenye sehemu zenye joto za bahari. Wakati upepo wenye mvuke kutoka kwenye Bahari ya Hindi unapogonga upande wa kusini wa Milima ya Himalaya na hivyo kuinuliwa, mvua kubwa hunyesha. Uwanda wa juu wa Meghalaya hupata
mvua nyingi. Isitoshe, kwa kuwa eneo hilo hupata jua kali la tropiki wakati wa mchana, yaonekana kwamba mawingu huinuka na kuelea juu ya uwanda huo mpaka hewa inapokuwa baridi saa za jioni. Huenda ndiyo sababu mara nyingi mvua hunyesha usiku.Mnamo mwezi wa Julai 1861, mji wa Cherrapunji ulipata sentimeta 930 za mvua! Na katika kipindi cha miezi 12, kuanzia Agosti 1, 1860 hadi Julai 31, 1861 mji huo ulipata sentimeta 2,646 za mvua. Kwa wastani, siku hizi mji wa Cherrapunji hupata mvua siku 180 kwa mwaka. Mvua nyingi sana hunyesha kati ya Juni na Septemba. Kwa kuwa mara nyingi mvua hunyesha usiku, wageni wanaweza kufurahia matembezi yao bila kulowa.
Ni vigumu kuamini kwamba eneo hilo hukumbwa na uhaba wa maji ilhali mvua hunyesha sana hivyo. Lakini, hivyo ndivyo inavyokuwa katika ile miezi ya baridi kali. Basi yale maji ya mvua huenda wapi? Kwa sababu ya uharibifu wa misitu katika maeneo yaliyo nje ya Cherrapunji, maji ya mvua hutiririka kutoka kwenye uwanda ulioinuka na kuingia kwenye mito iliyo kwenye sehemu tambarare. Mito hiyo hutiririka hadi Bangladesh. Kuna miradi ya kuzuia maji ya vijito na mpango wa ujenzi wa mabwawa. Lakini kulingana na mfalme wa kikabila wa Mawsynram, G. S. Malngiang, hakujawa “jitihada zozote za pekee za kulitatua tatizo la uhaba wa maji.”
Bila shaka, safari ya kwenda Cherrapunji imekuwa yenye kusisimua na yenye kuelimisha. Mandhari yenyewe inavutia kama nini! Hata kuna maua maridadi sana, kutia ndani jamii 300 za okidi na jamii ya kipekee ya ule mmea ulao wadudu unaoitwa pitcher. Isitoshe, kuna wanyama wengi wa pori, mapango ya chokaa unayoweza kuzuru, na vilevile majabali. Mashamba mengi ya michungwa katika eneo hilo huzaa tunda hilo lenye umajimaji ambalo hutumiwa kutengenezea asali tamu ya machungwa. Wageni wanaozuru Meghalaya, yale “makao ya mawingu,” wanaweza kuyaona yote hayo. Naam, hata wale wanaozuru Cherrapunji, mojawapo ya sehemu zenye mvua nyingi zaidi duniani.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Mlima Waialeale ulio kwenye kisiwa cha Kauai huko Hawaii na Mawsynram—kijiji kilicho kilometa 16 hivi kutoka Cherrapunji—zimerekodi mvua nyingi zaidi ya Cherrapunji wakati mwingine.
[Ramani katika ukurasa wa 22]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
INDIA
Cherrapunji
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Maporomoko ya maji huingia ndani ya mto unaotiririka kwa nguvu bondeni
[Picha katika ukurasa wa 23]
Jamii hii ya ule mmea ulao wadudu unaoitwa “pitcher” hupatikana hasa katika sehemu hiyo
[Hisani]
Photograph by Matthew Miller