Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Tunaweza Kuhifadhi Mti wa Candelabra?

Je, Tunaweza Kuhifadhi Mti wa Candelabra?

Je, Tunaweza Kuhifadhi Mti wa Candelabra?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI

ZAMANI kulikuwako misitu ya misindano kotekote nchini Brazili. Mojawapo ya miti hiyo ulipata jina la “candelabra tree,” katika lugha ya Kiingereza, kwa sababu hufanana na kinara cha mishumaa chenye matawi mengi. Pia, unajulikana kama msindano wa Paraná na msindano wa Brazili.

Matunda yenye mbegu yanayoning’inia kwenye matawi ya mti wa candelabra ni makubwa kushinda balungi. Baadhi ya matunda hayo yana uzito wa kilogramu tano. Tunda moja linaweza kuwa na mbegu 150, ambazo zinaitwa pinhões katika lugha ya Kireno. Baada ya tunda hilo kuiva hupasuka kwa mshindo mkubwa na mbegu huanguka chini.

Wanadamu, ndege, na wanyama hula mbegu hizo. Zamani mbegu hizo za pinhões,—zenye protini nyingi na kalisiamu—zilikuwa chakula kikuu cha baadhi ya makabila yanayoishi sehemu ya kusini mwa Brazili. Mbegu hizo huliwa hata leo. Kwa mfano, katika Jimbo la Santa Catarina nchini Brazili, hutumiwa kutengeneza vyakula vya kienyeji kama vile paçoca de pinhão (pinhões zilizopondwa).

Mti wa candelabra ulikabili hatari ya kutoweka wakati wakazi Wazungu walipoanza kugundua, katika miaka ya 1700, kwamba mti huo uliweza kutumiwa kwa mbao. Miti hiyo ilikatwa ili kujenga nyumba au kutengeneza mashamba ya mahindi na ya mizabibu. Miti mingi iliendelea kukatwa kuliko iliyopandwa. Wakati huu, kuna misitu midogo huko na huko tu. Kwa hiyo, bei ya mti huo imepanda sana. “Msindano, si chanzo cha mbao tu siku hizi, bali ni dhahabu,” akasema mwanamume ambaye amekuwa akitengeneza mbao za mti wa candelabra kwa muda wa miaka 50.

Watafiti husema kwamba ndege waitwao azure jay (jamii ya kunguru) wamezuia mti huo usitoweke kabisa. Ndege huyo mwenye kurukaruka kila mahali hula mbegu za mti huo, naye huficha nyingine katika kuvumwani na vilevile katikati ya mimea ya kangaga kwenye miti iliyokauka. Mbegu kadhaa humea baadaye. Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba ndege huyo ni mpanzi mwenye bidii wa mti huo! Kwa masikitiko, idadi ya ndege hao imepungua kwa sababu ya uharibifu wa misitu ya misindano.

Kwa sasa kampuni fulani zimeanza kuhifadhi misitu midogo ya mti huo na pia kuupanda upya sehemu ya kusini mwa Brazili. Huenda jambo hilo likamaanisha kwamba mti huo hautatoweka kabisa.

[Picha katika ukurasa wa 11]

Kila tunda lina mbegu 150 hivi za “pinhões”

[Hisani]

Mti na matunda yenye mbegu: Marcos Castelani