Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Braille Ninawapongeza kwa ajili ya makala “Louis Braille—Kuwaangazia Nuru Wafungwa wa Giza.” (Septemba 8, 2000) Mwalimu mkuu wa shule ninayofanya kazi haoni vizuri. Alifurahi sana nilipomsomea makala hiyo. Nakala moja ya gazeti hilo iliwekwa kwenye maktaba ya shule.

M.A.S., Brazili

Kutafakari Ningependa kuwashukuru kwa ajili ya makala “Maoni ya Biblia: Kutafakari Ambako Hunufaisha.” (Septemba 8, 2000) Sasa nimejua kwamba kutafakari si kutunga tu taswira akilini. Kwa kutumia Wafilipi 4:8, sasa ninajua njia ifaayo ya kutafakari juu ya matatizo yangu. Asanteni sana!

W. P., Poland

Buku Nina umri wa miaka 15 na ningependa kushukuru kwa ajili ya makala “Mkataji-Miti wa Awali Angali Anafanya Kazi.” (Septemba 8, 2000) Mimi hufurahia kusoma juu ya wanyama na jinsi wanavyoishi. Lakini sijawahi kujua kwamba buku wanaweza kufanya mengi hivyo! Nafikiri inastaajabisha kuona jinsi wanavyojitunza pamoja na familia zao!

S. J., Marekani

Nina umri wa miaka kumi, na nilisoma makala hiyo nilipokuwa nimepiga kambi karibu na ghuba. Nilikuwa nikiwazia jinsi buku hao walivyokuwa wakifanya kazi bila kuacha. Mimi hufurahia makala zinazozungumza juu ya wanyama kwa sababu hunisaidia kuthamini uumbaji wote wa ajabu wa Yehova.

B. P., Marekani

Hesabu Isiyoeleweka? Ningependa kuwaonyesha kosa moja dogo kwenye makala “Jitihada ya Kutokeza Jamii Kamilifu.” (Septemba 22, 2000) Mlisema kwamba mtu atahitaji miaka 26 ili kusoma mabuku 200 yenye kurasa elfu moja. Kulingana na makadirio yangu, labda atahitaji miaka minne tu.

P. I., Rumania

Asante kwa maoni yako. Ingawa ni kweli kwamba yaweza kuchukua muda mfupi tu kusoma mabuku 200 ya hadithi yenye kurasa elfu moja, habari inayokusanywa na Mradi wa Kuchunguza Chembe za Urithi za Mwanadamu inahusu mifuatano ya DNA, ambayo yaweza kuchosha na kuchukua muda mrefu kusoma.—Mhariri.

Naamini kuwa mlifanya kosa linalofanywa mara nyingi, katika makala “Visivyoweza Kuonwa kwa Macho Matupu.” (Agosti 22, 2000) Katika makala hiyo mlisema kuhusu hadubini zinazoweza kukuza vitu zaidi ya mara milioni moja, “sawa na kukuza stempu ya posta iwe na ukubwa wa nchi ndogo.” Stempu milioni moja zaweza kutoshea zikipangwa katika umbo la mraba la stempu 1,000 kila upande. Tukikadiria kuwa stempu moja ina urefu wa sentimeta 2.5 kila upande, basi umbo hilo la mraba litakuwa na urefu wa meta 25 kila upande. Sifikiri kuna nchi ndogo hivyo!

R. C., Marekani

Badala ya kuwazia kwamba stempu moja yaweza kukuzwa kuwa kama umbo la mraba la stempu 1,000 kila upande, wazia juu ya mpangilio wa umbo la mraba wa stempu 1,000,000 kila upande, kwa sababu ukuzaji hukuza uso mmoja tu wa umbo. Hiyo itakuwa kama ukubwa wa nchi ndogo ya kisiwani.—Mhariri.

Usalama Unaposafiri kwa Ndege Ninawaandikia tu kuwashukuru kwa ajili ya makala “Kufanya Usafiri wa Ndege Uwe Salama Zaidi.” (Septemba 22, 2000) Ninapenda kusafiri kwa ndege, lakini baada ya kusoma makala hiyo, nimefahamu kuwa marubani huzoezwa kabisa, ili tusafiri salama.

E. P., Visiwa vya Virgin

Wembamba Mara tu nilipoona kichwa “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Mimi Ni Mwembamba Sana?” (Septemba 22, 2000), nilitokwa na machozi. Nina umri wa miaka 16 na nina uzani wa kilogramu 45. Kwa kuwa mimi ni mwembamba sana nilihisi kuwa nina sura mbaya na sivutii. Niliposoma makala hiyo, nilithamini sana madokezo yafaayo yaliyotolewa. Sehemu ya umalizio ndiyo iliyonigusa moyo zaidi kwa sababu ilinifanya nione kuwa Yehova huutazama moyo.

E. L., Italia