Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Je, Historia ya Kidini Ifundishwe?

Kulingana na kura ya maoni iliyofanywa hivi majuzi na magazeti ya Le Monde na Notre Histoire, ni asilimia 57 tu ya Wafaransa waliokubali kuwe na mitaala ya historia ya kidini katika shule za Serikali. “Idadi ya wanaopinga wazo hilo inaongezeka sana,” lasema gazeti Notre Histoire. “Hiyo yaonyesha wanashuku kwamba wanafunzi watashawishiwa kugeuza imani yao au kwamba hawataki kabisa dini ifundishwe shuleni.” Jambo la kushangaza ni kwamba watu wengi sana wanaamini kuwa mitaala hiyo itawafanya wanafunzi waheshimu imani za wenzao. Kwa mujibu wa kura hiyo ya maoni, dini ya Uislamu yenye wafuasi milioni nne, sasa inafuata dini ya Kikatoliki ambayo ndiyo dini kubwa zaidi nchini Ufaransa. Katika nchi hiyo yenye “dini mbalimbali,” kuna Waprotestanti, Wayahudi, Wakristo-Waothodoksi, na pia Mashahidi wa Yehova.

Kueneza Magonjwa

“Magonjwa ya kuambukiza yanaweza kupitishwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa urahisi kama vile kufungua mfereji wa maji au kwa kutumia simu,” lasema gazeti The Guardian la London. Wanasayansi kwenye Chuo Kikuu cha Arizona huko Tucson, Marekani, waliripoti kwamba mtu aliye na mafua makali akipenga kamasi kisha afungue mfereji anaweza kuacha “virusi zaidi ya 1,000 hapo kwenye mfereji.” Mtu atakayetumia mfereji huo baada yake, aweza kuambukizwa virusi hivyo hasa ikiwa atashika mdomo, pua, au macho yake. Majaribio ya bakteria mbalimbali yalionyesha kwamba “vipokezi vya simu vilipitisha asilimia 39 ya bakteria na asilimia 66 ya virusi, ilhali mifereji ilipitisha asilimia 28 ya bakteria na asilimia 34ya virusi.” Mtu akigusa mdomo wake wa chini kwa kutumia kidole kilichoambukizwa, aweza kupata zaidi ya theluthi moja ya viini hivyo. Magonjwa yanayosababishwa na virusi na kuharisha kunakosababishwa na bakteria, kwaweza kuenezwa kwa urahisi kupitia njia hiyo mtu asiponawa mikono.

Utatuzi wa Baa la Nzige

“Bata na kuku 700,000 waliozoezwa, wameandaliwa ili kulimaliza baa kubwa zaidi la nzige lililopata kuikumba China katika muda wa miaka 25,” laripoti gazeti The Daily Telegraph la London. Katika majira ya kiangazi ya mwaka wa 2000, makundi ya nzige yaliharibu ekari milioni 4.1 za mazao kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo, na ekari milioni 9.6 za kanda za mbuga magharibi mwa Xinjiang. Bata na kuku hao wamezoezwa kuwafuata na kuwala wadudu hao mara tu wanaposikia mlio wa filimbi. Zhao Xinchun, makamu wa mkurugenzi kwenye Shirika la Kupambana na Nzige na Panya huko Xinjiang, ambako bata na kuku hao huzoezwa aeleza hivi: “Wakulima walijua kwamba kuku wanapenda sana kula nzige, basi tukafanya majaribio [na] kupata kwamba bata wanaweza kula zaidi ya kuku [kila mmoja anaweza kula nzige 400 kwa siku], wanaweza kustahimili hali mbaya ya hewa na hawaliwi sana na tai au vicheche. . . . Twawaachilia kwenye kanda za mbuga, twapuliza filimbi, kisha wanakula nzige.” Bata na kuku hao wanatumiwa katika mradi unaohusisha kumwaga dawa ya unga kwenye mazao kwa kutumia ndege na pia kutumia vijidudu vinavyowaua nzige.

Ni Muhimu Kulala

“Angalau robo ya wenyeji wa Afrika Kusini hawafanyi yote wawezayo kwa sababu ya kutolala au kutolala vya kutosha,” lasema gazeti la Afrika Kusini la The Natal Witness. Dakt. James Maas, mchunguzi wa usingizi, anasema kwamba kulala huuwezesha ubongo kuongeza vipitisha-habari muhimu. Basi kulala vya kutosha ni muhimu ili kukumbuka mambo vizuri, kuwa mbunifu, kutatua matatizo, na kuweza kujifunza. Matokeo ya kutolala vya kutosha yanatia ndani kushuka moyo, kukasirika upesi, wasiwasi, kutokuwa mcheshi na kutotaka kuchangamana na wengine, kutoweza kukaza fikira kwa muda mrefu na kukumbuka mambo, kushindwa kuwasiliana ifaavyo na kufanya maamuzi, kujihatarisha zaidi, kushindwa kufanya kazi ifaavyo na kuzorota kwa hali ya maisha. Watu wanaolala kwa muda wa saa tano tu, huambukizwa virusi kwa urahisi. Maas asema, “Ili tutimize yote tuwezayo, yatupasa kutumia theluthi moja ya maisha yetu kulala, yaani, muda wa saa nane kila usiku.”

Tumbawe Chini ya Bahari

“Katika vilindi vya Ulaya Magharibi, miamba ya tumbawe imegunduliwa. Miamba hiyo ina viumbe mbalimbali wa baharini sawa na miamba ya maeneo ya kitropiki,” laripoti gazeti National Post la Kanada. Matumbawe hayo hutegemeza jamii mbalimbali kama vile sifongo, marijani-tanzu, na “jamii nyingi za minyoo ya baharini, ambazo wanasayansi hawajawahi kuzifafanua.” Wanyama wengi wadogo walipatikana kwenye matope yaliyotolewa chini ya bahari. ‘Nusu yao hawajawahi kugunduliwa na wanasayansi,’ asema Alex Rogers wa Kituo cha Sayansi ya Bahari kwenye Chuo Kikuu cha Southampton huko Uingereza. “Twahitaji kuilinda miamba hiyo, si kwa sababu ya matumbawe hasa—ambayo hupatikana kwingineko—bali kwa sababu ni makao ya viumbe wengine wanaoishi humo.” Anakadiria kwamba kuna jamii 900 zinazoishi kati ya matumbawe hayo. Yamkini matumbawe hayo ni makao ya “baadhi ya samaki wachanga wa kuuzwa,” lasema gazeti hilo.

Kuvunjika kwa Familia Uingereza

Uingereza ndiyo nchi yenye kiwango cha juu cha talaka katika Ulaya na kiwango cha juu hata zaidi cha kuvunjika kwa uhusiano kati ya watu wanaoishi pamoja bila ya kuoana. Ripoti ya uchunguzi ulioidhinishwa na serikali yenye kichwa, “Matokeo ya Kuvunjika kwa Familia,” yaonya hivi: “Sababu kuu ya kuzorota kwa ustawi wa mtoto ni kuvunjika kwa familia—hasa kuvunjika kwa ule muungano kati ya baba na mama.” Matokeo yaliyo wazi ni kwamba raia wa Uingereza atalipa kodi ya dola 15 za Marekani kwa wastani kila wiki ilhali matokeo yasiyo wazi yanatia ndani uhitaji wa nyumba nyingi kwa ajili ya familia zilizogawanyika na pia uharibifu wa mazingira. Ingawa ripoti hiyo haikuandikwa ili kuboresha maadili, ilisema hivi: “Twaamini kwamba sikuzote ndoa imekuwa msingi imara wa jamii thabiti na wa kulea watoto.”

Tembo Wachanga Waasi

Tangu mwaka wa 1991, tembo wachanga wa kiume wamewaua vifaru 36 kwenye Mbuga za Wanyama za Hluhluwe na Umfolozi huko Afrika Kusini, yasema ripoti moja ya African Wildlife yenye kichwa ‘Mchelea Mwana Kulia Mwisho Hulia Mwenyewe.’ Tembo hao wachanga wajeuri ni mayatima waliotolewa kwenye Mbuga ya Wanyama ya Kruger baada ya idadi ya tembo kupunguzwa. Ijapokuwa wana umri mdogo, tayari wana msisimko wa kufanya ngono. Wachunguzi wanasema kwamba ujeuri wao unasababishwa na kukosa kuwa katika jamii ya kawaida ya tembo. Basi ndiyo sababu tembo kumi wa kiume wameletwa kutoka kwenye Mbuga ya Wanyama ya Kruger ili kuwarekebisha tembo hao wachanga wajeuri. Tangu mradi huo uanzishwe mwaka wa 1998 katika mbuga nyingine, hakujaripotiwa vifo vingine vya vifaru.

Jeshi la Sanamu za Udongo za China Lashambuliwa

“Mojawapo ya sehemu zinazowavutia watalii nchini China, yaani, lile jeshi la sanamu za udongo ambalo limekuwako kwa miaka 2,200, linashambuliwa na adui mwingine,” laripoti The Guardian la London. Aina 40 za kuvu zimeharibu zaidi ya sanamu 1,400 kati ya sanamu zipatazo 8,000 za askari, watupa-mishale, na farasi. Sanamu hizo zilichimbuliwa karibu na kaburi la kifalme la maliki wa China Qin Shihuang nje ya Xi’an, jiji kuu la zamani la nchi hiyo. Mkusanyo huo wa sanamu zenye kuvutia, uliogunduliwa mwaka wa 1974 na ambao sasa umewekwa ndani ya chumba kilicho chini ya ardhi, unahatarishwa pia kwa sababu “pumzi na joto la mwili la wageni wapatao 4,300 kila siku linachakaza sanamu hizo,” lasema gazeti The Times la London. Ili kuzuia kuvu zisisambae kwenye sanamu nyingine, wasimamizi wa jiji la Xi’an wameipa kampuni moja ya Ubelgiji kazi ya kuondoa kuvu.

Majira ya Baridi Kali —Wakati Mzuri au Mbaya?

Jarida la habari za afya la Ujerumani, Apotheken Umschau, laripoti kwamba si lazima hali ya hewa ya mvua au baridi idhuru afya yako. Badala yake, kulingana na mtaalamu wa tiba ya hali ya hewa Dakt. Angela Schuh, kutembea kwa ukawaida wakati wa baridi kali kwaweza kusaidia moyo na mzunguko wako wa damu na pia kuimarisha mwili wote. Huenda kujifungia tu ndani ya nyumba zinazopashwa joto kukapunguza uwezo wa mwili wa kubadilika ili ufaane na hali mbalimbali za joto. Labda hilo laweza kufanya iwe rahisi kuambukizwa magonjwa, kuchoka na kuumwa na kichwa. Lakini mwili ulioimarishwa kupitia mazoezi wakati wa hali “mbaya” ya hewa hautahisi baridi wala kuchoka upesi.