Safarini Huko Ghana
Safarini Huko Ghana
Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Ghana
HUKU kukipambazuka na ukungu ukipungua, twasafiri taratibu umbali wa kilometa 80 kwenye barabara isiyo na lami kuelekea kwenye Mbuga ya Wanyama ya Mole, katika Mkoa wa Kaskazini wa Ghana. Eneo hilo lina nyasi, vichaka, na miti mifupi. Mara moja-moja, twapita vijiji vyenye vibanda vilivyotengenezwa kwa udongo na kuezekwa majani makavu.
Lakini twaona tofauti kubwa sana tunapofika Damongo, mji wa mashambani ulio na maduka, barabara zilizo na lami, na msongamano wa magari. Watoto waliovalia yunifomu za rangi ya mchanga na kahawia wanaelekea shuleni. Wanawake waliovalia nguo maridadi wanabeba mizigo ya kila aina kichwani kama vile kuni, vyakula, na mitungi yenye maji. Magari na matrekta yapiga honi, na waendesha baiskeli wanapita. Tungali na safari ya kilometa 20.
Kwenye Mbuga ya Wanyama ya Mole
Hatimaye twafika kwenye mbuga. Zechariah, ambaye anatuongoza, anatuambia kuwa Mbuga ya Wanyama ya Mole iliyo kwenye eneo la kilometa 4,840 za mraba, ilianzishwa mwaka wa 1971. Kumekuwa na jamii 93 za mamalia, jamii 9 za amfibia, na jamii 33 za wanyama watambaazi kwenye mbuga hiyo. Wanyama hao watia ndani simba, chui, fisi wenye madoadoa, fungo, ndovu, swara, nyati, ngiri, kuro, funo, kala, kongoni, nguchiro, nyani, tumbili wa aina mbalimbali, korongo, nungunungu, mamba, na nyoka, kutia ndani chatu. Kwa kuongezea, zaidi ya jamii 300 za ndege zimeonekana huko.
Tunapotembea kwenye nyasi ndefu na kuwaondoa wadudu wanaopuruka mbele yetu, twakaribia kundi la paa. Mwanzoni inakuwa vigumu kuwaona, kwani rangi yao yafanana na mazingira yao. Tunapowatazama, wao pia wanatukodolea macho, ni kana
kwamba hata wao wanafurahi kutuona. Tunapopiga picha, tunashtuliwa na mngurumo unaotoka upande wa kulia. Akikasirika kwa sababu tumekatisha starehe yake, kuro mmoja dume akimbia kwenye kichaka kilicho mbele yetu.Kisha twaona ndovu wanne wakubwa chini ya mti mkubwa. Wanatumia mikonga yao kuyashusha matawi kisha wanatafuna majani yaliyo laini. Tunasonga karibu, na tunapokuwa meta kumi tu karibu nao, Zechariah anatuambia tupige picha. Anapopiga kitako cha bunduki yake, ndovu hao wanashtuliwa na kelele hiyo na wanatoka chini ya mti. Basi, tunapata nafasi ya kupiga picha nzuri. Ndovu hao wafika kwenye dimbwi la matope lililo karibu na kugaagaa ndani ya dimbwi hilo. Zechariah aeleza kwamba rangi ya ndovu hao hubadilika—kuwa nyekundu au kahawia badala ya kuwa nyeusi kama kawaida—ikitegemea rangi ya matope.
Twasonga mbele zaidi na kuona mandhari kamili ya mbuga hiyo. Kati ya mimea mingineyo, kuna migunga na miti aina ya shea. Tunaporudi, twapitia njia ileile ambayo ndovu wamepitia. Wangali meta kadhaa mbele yetu. Lakini yule ndovu
mkubwa zaidi kati yao anainua masikio yake, anaonekana ni kama anataka kushambulia, kisha anaanza kuja tuliko. Je, atashambulia?Zechariah anatuambia tusibabaike huku akichukua bunduki iliyo begani na kutuongoza kando ya njia ambayo ndovu wamepitia. Twaendelea kutembea, huku kiongozi wetu akishika bunduki yake nasi tukiwa na kamera zetu mkononi tayari kuzitumia. Punde si punde, hatuwaoni tena wale ndovu.
Zechariah anatueleza kwamba ndovu hao wamewazoea watu na kwamba hata wengine huwakaribia watu. Ndovu wakionekana mara nyingi, viongozi wa mbuga huwapa majina. Walimwita ndovu mmoja Uvimbe kwa sababu alikuwa na uvimbe mkubwa ngozini. Naye ndovu mwingine wakamwita Machachari kwa sababu alizoea kuwatisha watalii.
Kisha tunawaona nyani. Tunawatazama nyani wakirukaruka kwenye miti na kukimbia huku na huku. Kiongozi wetu anatuonyesha nyani mmoja anayebeba watoto wake wawili, mmoja mgongoni, mwingine kifuani. Anatuambia kwamba ni mapacha.
Leo tumeona wanyama wengi kwelikweli. Zechariah anatuambia kwamba wakati wa kiangazi—kati ya Aprili na Juni—unahitaji tu kungoja kwenye vidimbwi vya maji ili uwaone wanyama kwani wanakuja makundi-makundi ili kukata kiu. Pia, anatuambia kwamba ukizuru mbuga hiyo kwa gari, unaweza kuwaona wanyama wengi zaidi, kutia ndani nyati na simba.
Sasa ni wakati wa chakula cha mchana. Tunapokula, nyani mmoja mkubwa anapanda nyuma ya gari lililoegeshwa karibu na gari letu naye anakikodolea macho chakula changu. Nyani wengine wanapita huku wakifuatwa na paa wachache na ngiri mmoja. Mwishowe ndovu wanne wanatokea juu ya kilima kilicho karibu. Labda huo ndio wakati mzuri wa kuwapiga picha wanyama hao.
Sokoni
Tunakaa kwa muda mfupi tu kwenye Mbuga ya Wanyama ya Mole, lakini sasa tunasafiri muda wa saa mbili hivi kwenye barabara zisizo na lami tukielekea Sawla, mji wa mashambani unaokaliwa na Walobi, kabila
la wakulima. Wanawake wa kabila hilo wana desturi isiyo ya kawaida ya kupanua ukubwa wa midomo yao. Ijapokuwa utamaduni huo unafifia huku wasichana wakistaarabika, wanawake wengi bado hujivunia ukubwa wa midomo yao. Kwa kweli, kumwambia mwanamke Mlobi kwamba ana midomo midogo kama ya mwanamume, ni kumtukana.Twafika kwenye kijiji kimoja na kuingia sokoni. Vibanda vimetengenezwa kwa matawi ya miti na kuezekwa kwa nyasi. Kuna mzungu mmoja aliyesimama pale sokoni kati ya Waafrika wengi. Tunamkaribia na kugundua kwamba alikuja hivi majuzi ili kuitafsiri Biblia katika lugha ya Kilobi. Anakaa kwenye kijiji jirani cha Walobi ili ajifunze kuzungumza lugha yao vyema. Hiyo yanikumbusha Robert Moffat. Katika karne ya 19, alianzisha misheni miongoni mwa Watswana, wanaokaa kusini mwa Afrika, na akaitafsiri Biblia katika lugha yao.
Mwanamke mzee Mlobi mwenye midomo iliyopanuliwa, amekalia benchi ndani ya kibanda kimoja. Visahani vyeupe vidogo, vimeingizwa kwenye yale mashimo yaliyo midomoni. Ningependa kumpiga picha, lakini mara tu ninapoinua kamera yangu, anageuka. Mtalii mwenzangu ananieleza kwamba Walobi wazee huamini kwamba wakipigwa picha nafsi zao zitapata madhara.
Tunaporudi Sawla, mahali ambapo tutakaa usiku huu, ninafikiria juu ya hekima na mambo tofauti tuliyoona katika uumbaji wa Mungu. Aliwaumba wanyama na wanadamu kwa ustadi. Ni kama vile mtunga-zaburi alivyotangaza: “Ee BWANA, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako.”—Zaburi 104:24.
[Ramani katika ukurasa wa 14, 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
GHANA
[Picha katika ukurasa wa 14]
Ngiri
[Picha katika ukurasa wa 14]
Fisi mwenye madoadoa
[Picha katika ukurasa wa 15]
Kundi la paa
[Picha katika ukurasa wa 15]
Ndovu
[Picha katika ukurasa wa 15]
Viboko
[Picha katika ukurasa wa 16]
Nyani akibeba watoto wake wawili
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kongoni
[Picha katika ukurasa wa 17]
Soko