Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Useremala wa Kipekee wa Japani

Useremala wa Kipekee wa Japani

Useremala wa Kipekee wa Japani

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI JAPANI

KUNA msitu mnene kwenye milima ya Hakone karibu na Mlima Fuji nchini Japani. Tunasafiri kwenye barabara nyembamba iliyopindapinda, ambayo haitumiki sana, na kuwasili kwenye kijiji chenye kupendeza kinachoitwa Hatajuku. Yosegi ilianzishwa katika kijiji hiki kitulivu.

Maana halisi ya neno Yosegi ni “mpangilio wa vipande vya mbao.” Yosegi hutambulishwa kwa mapambo ya mraba kwenye sehemu ya juu ya vyombo vya mbao ambayo yametengenezwa kwa mikono, kuanzia vitu vidogo kama ishara zinazowekwa ndani ya kitabu hadi masanduku yenye mtoto telezi wa meza. Kuna mapambo yenye maumbo na rangi mbalimbali. Tunavutiwa na yosegi hata zaidi tunapotambua kwamba mapambo hayo hayajachorwa, lakini yametokezwa kwa kuunganisha kwa gundi mbao zenye rangi mbalimbali.

Useremala huo wa kipekee ulianzaje? Katika miaka ya 1800, seremala anayeitwa Nihei Ishikawa alivumbua njia hiyo ya kuunganisha kwa gundi mbao zenye rangi mbalimbali. Halafu, alikata kwa msumeno mbao hizo zilizounganishwa kwa gundi ili apate vipande vyembamba vya mbao vya kutengenezea masanduku na vitu vingine ambavyo vingekuwa na mapambo yenye rangi mbalimbali.

Baadaye, njia rahisi ya kutengeneza yosegi ilibuniwa. Njia hiyo ilitia ndani kutengeneza mbao nyembamba kwa kuranda mbao ambazo zilikuwa zimeunganishwa kwa gundi, na kuziunganisha kwa gundi mbao hizo nyembamba (vinia) kwenye mbao nyingine nene. Kwa njia hiyo vitu vya makumbusho vya bei nafuu viliweza kutengenezwa kwa ajili ya watalii ambao huzuru chemchemi zenye maji ya moto za Hakone.

Mbao za aina nyingi hutumiwa kutengeneza yosegi. Kwa mfano, mbao za rangi nyeupe hutokana na miti aina ya spindle, na dogwood; mbao za manjano hutokana na mti aina ya lacquer na mti uitwao wax wa Japani; mbao za kahawia hafifu hutokana na miti aina ya cherry na zelkova; na mbao nyeusi hutokana na mti aina ya katsura.

Unapozuru Hakone, huenda ukafurahi kununua mikeka midogo yenye mapambo ya yosegi au ishara ambazo zinawekwa ndani ya kitabu. Vitu hivyo ni vya bei nafuu kiasi. Hata vitu hivyo vidogo vitakukumbusha safari ya kwenda Hakone karibu na Mlima Fuji ulio maarufu. Vitakukumbusha pia juu ya useremala wa kipekee ulioanzishwa zaidi ya miaka 150 iliyopita.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 19]

KUTENGENEZA YOSEGI

Seremala wa Yosegi huranda mbao zenye rangi mbalimbali ziwe zenye unene unaotakikana. Halafu huziunganisha kwa gundi mbao hizo. Kwa njia hiyo mapambo yenye rangi mbalimbali hutokezwa kwenye kipande cha mbao hicho kilichounganishwa kwa gundi. Kisha seremala hukata kwa msumeno kipande hicho ili apate vipande vyembamba vyenye tabaka nyingi. Hivyo huwekwa katika kibanio cha aina fulani. (1) Baada ya kuviranda, yeye huvitoa katika kibanio, huviunganisha kwa gundi ili kufanyiza mapambo, kisha huvifunga kwa kamba za pamba. Yosegi hutengenezwa kwa vipande hivyo vyembamba vya mbao.

Halafu seremala huunganisha kwa gundi vipande kadhaa ili kutengeneza kipande kikubwa zaidi. (2) Kisha hukata kwa msumeno kipande hicho kikubwa vipandevipande. (3) Halafu huvipanga vipande hivyo na kuviunganisha kwa gundi, kwa njia hiyo hutokeza kielelezi kikubwa zaidi. Seremala huendelea kuunganisha kwa gundi vipande vya mbao pamoja hadi awe ametengeneza kipande kikubwa cha mbao, ambacho kinaitwa kwa Kijapani tanegi.

Seremala ametokeza vinia yenye mapambo kwa ajili ya vyombo ambavyo ametengeneza. (4) Anaranda tanegi kwa kutumia randa ya kipekee, ili kutokeza mbao nyembamba kama karatasi, ziitwazo zuku. (5) Baada ya kuzipiga pasi mbao hizo nyembamba, seremala yuko tayari kurembesha vyombo ambavyo ametengeneza kwa kuvitia vinia hiyo ya zuku.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mapambo ya “yosegi” hayajachorwa bali yanatokezwa kwa kuunganisha kwa gundi mbao zenye rangi mbalimbali