Kukabiliana na Tisho la Ugaidi
Kukabiliana na Tisho la Ugaidi
MWISHONI mwa miaka ya 1980, ilionekana kana kwamba ugaidi ulikuwa ukididimia. Hata hivyo, mbinu mpya za ugaidi zimeibuka. Tatizo lililopo la ugaidi linasababishwa hasa na watu wenye siasa kali ambao wanapata pesa kutokana na ulanguzi wa dawa za kulevya, biashara za kibinafsi, matajiri, misaada, na wadhamini wengine. Magaidi wangali wakatili.
Kumekuwa na visa chungu nzima vya ugaidi vyenye kusikitisha katika miaka ya karibuni. Jengo la World Trade Center huko New York City lililipuliwa kwa bomu, watu 6 wakauawa na 1,000 kujeruhiwa. Washiriki wa madhehebu fulani walisambaza gesi ya sarin inayodhuru neva kwenye magari ya moshi ya chini ya ardhi huko Tokyo, watu 12 waliuawa na zaidi ya 5,000 kujeruhiwa. Jengo la serikali huko Oklahoma City liliporomoka baada ya kulipuliwa kwa bomu lililotegwa katika lori na gaidi mmoja. Watu 168 waliuawa na mamia kujeruhiwa. Kama chati iliyo kwenye ukurasa wa 4 na 5 inavyoonyesha, visa vya kigaidi vya kila namna vimeendelea kutukia hadi leo.
Kwa ujumla, yaonekana siku hizi magaidi wanatenda kwa ukatili zaidi kuliko awali. Gaidi aliyeshtakiwa kwa kulipua jengo la serikali la Oklahoma City mnamo mwaka wa 1995, alinukuliwa akisema kwamba alihitaji kuua watu wengi zaidi ili madai yake yatimizwe. Kiongozi wa kikundi kilichohusika na ulipuaji wa jengo la World Trade Center huko New York City mwaka wa 1993, alitaka kulipua majengo yote mawili na kuua kila mtu aliyekuwamo.
Leo magaidi wanaweza kupata silaha mbalimbali pia. Louis R. Mizell, Jr., mpelelezi stadi wa ugaidi, alisema hivi: “Twaishi katika enzi iliyo na silaha nyingi hatari zinazoweza kuangamiza watu wengi sana: silaha za nyuklia, kemikali, na zenye viini.” Watu wenye siasa kali wanaotaka kushtua ulimwengu wanatumia silaha hatari zaidi za kisasa.
Mashambulizi ya Kigaidi Kupitia kwa Kompyuta
Ugaidi wa Internet (cyber-terrorism) hutumia teknolojia ya kisasa kama vile kompyuta. Mojawapo ya vitu wanavyotumia ni programu hatari za kompyuta (computer virus) ambazo zinaharibu habari zilizohifadhiwa au kutatanisha mifumo ya kompyuta. Pia kuna programu nyingine hatari zinazoitwa kwa Kiingereza “logic bombs” ambazo huvuruga kompyuta. Kompyuta hujaribu kufanya kazi isiyowezekana halafu inakwama. Watu wengi wanahisi kwamba umma unakabili hatari ya ugaidi wa aina hiyo kwa sababu uchumi na usalama wa nchi nyingi unategemea sana mifumo ya kompyuta. Na ijapokuwa majeshi mengi yana mifumo ya mawasiliano inayoweza kustahimili vita ya nyuklia, huduma za umma kama vile usambazaji wa umeme, usafiri, na masoko ya fedha yanaweza kuvamiwa kwa urahisi sana.
Miaka michache iliyopita, gaidi angeweza kukata umeme, tuseme katika jiji la Berlin, labda kwa kuomba kazi kwenye kampuni ya umeme akiwa na kusudi la kuharibu mfumo wa umeme. Lakini sasa, watu fulani wanasema kwamba mtaalamu wa kompyuta anaweza kukata umeme jijini akiwa nyumbani mwake katika kijiji kilicho upande mwingine wa dunia.
Hivi majuzi mtaalamu mmoja wa kompyuta wa Sweden alivamia mfumo wa kompyuta huko Florida na kuvuruga huduma za dharura kwa muda wa saa moja. Polisi, wazima-moto, na magari ya wagonjwa hayangeweza kuitikia mwito wa dharura.
“Ni kana kwamba tumetokeza jumuiya ya ulimwenguni pote isiyo na idara ya polisi,” akasema Frank J. Cilluffo, mkurugenzi wa Kikundi Kinachopambana na Ugaidi wa Kompyuta kilicho kwenye kituo cha Center for Strategic and International Studies (CSIS). Naye Robert Kupperman, mshauri mkuu wa kituo cha CSIS, alisema mnamo mwaka wa 1997 kwamba “hakuna shirika lolote la serikali linaloweza kukabiliana na mashambulizi ya magaidi” endapo magaidi wataamua kutumia teknolojia ya kisasa.
Wachunguzi fulani wanaamini kwamba magaidi
wanaotumia kompyuta wana ustadi wa kitekinolojia unaoweza kuwasaidia kuepuka kunaswa na vifaa vyovyote vinavyobuniwa na vikosi vya ulinzi. George Tenet, mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), alisema kwamba “adui mwenye ujuzi wa kuweka programu hatari kwenye mfumo wa kompyuta au anayeweza kufikia kompyuta ifaayo kwenye mtandao anaweza kusababisha hasara kubwa sana.”Magaidi Wanaotumia Kemikali au Viini
Wengi wanahofia pia matumizi ya silaha za kemikali na zenye viini hatari. Watu wengi ulimwenguni walishtuka mapema mwaka wa 1995 waliposikia kwamba magaidi walishambulia magari ya moshi ya chini ya ardhi huko Tokyo kwa kutumia gesi ya sumu. Madhehebu yanayotabiri mwisho wa ulimwengu ndiyo yaliyolaumiwa kwa tukio hilo.
“Kuna mbinu mpya za ugaidi,” asema Brad Roberts wa Institute for Defense Analyses. “Magaidi wa kale walitaka mikataba ya kisiasa. Lakini sasa makundi fulani ya kigaidi yanasema kwamba lengo lao kuu ni kuua watu wengi. Ndiyo sababu magaidi wanapendelea silaha zenye viini hatari.” Je, ni vigumu kupata silaha hizo? Gazeti Scientific American lasema hivi: “Mtu anaweza kukuza matrilioni ya bakteria kwa kutumia kifaa sahili cha kuchachusha pombe na mkorogo maalumu wa protini. Aweza kujikinga pia kutokana na gesi na viini kwa kuvalia kinyago usoni, na vazi refu la plastiki.” Baada tu ya kukuza viini hivyo, vinaweza kusafirishwa kwa urahisi sana. Watu hugundua siku moja au mbili baadaye kwamba wameshambuliwa kwa silaha ya viini. Na huwa tayari wameathiriwa mno.
Yasemekana kwamba silaha yenye viini vya maradhi ya wanyama yanayoambukiza wanadamu (anthrax) hupendwa sana. Jina la maradhi hayo latokana na neno la Kigiriki la makaa ya mawe. Jina hilo larejezea upele mweusi unaoibuka kwenye ngozi ya wale wanaogusa wanyama wenye maradhi hayo. Wataalamu wa vikosi vya ulinzi wanahofia zaidi maambukizo ya mapafu yanayotokana na kupumua viini vya maradhi hayo. Wanadamu wengi wanaoambukizwa maradhi hayo hufa.
Kwa nini silaha yenye viini vya maradhi ya wanyama yanayoambukiza wanadamu huwa hatari? Viini hivyo hukuzwa kwa urahisi na hustahimili hali mbalimbali. Siku chache baada ya kuambukizwa, mtu hupata dalili za kwanza za maradhi hayo. Yeye hujihisi akiwa mchovu kana kwamba ana mafua. Kisha hukohoa na kuhisi maumivu kifuani. Muda si muda yeye hushindwa kabisa kupumua, anakuwa mahututi, halafu anakufa baada ya saa chache tu.
Je, Magaidi Wana Silaha za Nyuklia?
Baada ya kuporomoka kwa Muungano wa Sovieti, baadhi ya watu walihofu kwamba huenda silaha ya nyuklia ikaibiwa na kuuzwa kwa njia haramu. Hata hivyo, wataalamu wengi hawadhani jambo hilo litapata kutukia. Robert Kupperman, aliyenukuliwa awali, asema kwamba “hakuna ushuhuda unaoonyesha kwamba kikundi chochote cha magaidi kimejaribu kununua silaha za nyuklia.”
Silaha inayohofiwa zaidi ni silaha ya mnururisho ambayo ni hatari kama bomu ya nyuklia. Silaha hiyo haijulikani sana. Hailipuki. Haina sauti wala moto. Badala yake, inatokeza mnururisho unaoangamiza chembe mwilini. Chembe zinazoangamizwa zaidi ni chembe za uboho wa mifupa. Chembe hizo zinapokufa matatizo mbalimbali yanatokea, kutia ndani kuvuja damu na kuharibika kwa mfumo wa kinga. Tofauti na silaha za kemikali, ambazo hufifia mara tu zinapochanganyika na oksijeni na unyevu, mnururisho huendelea kudhuru kwa miaka mingi.
Msiba uliotokea Goiânia, jiji lililo kusini ya kati ya Brazili, waonyesha hatari ya mnururisho. Mnamo mwaka wa 1987 mwanamume fulani alifunua pasipo kujua mkebe wa madini ya risasi uliokuwa kwenye mashine ya kitiba iliyotupwa. Mkebe huo ulikuwa na madini ya cesium-137. Alivutiwa mno na madini hayo yenye mng’ao mwangavu wa buluu kiasi cha kwamba alienda kuwaonyesha rafiki zake. Baada ya juma moja kupita, watu walioathiriwa na mnururisho walianza kumiminika kwenye hospitali moja ya karibu. Maelfu walichunguzwa ili kuona iwapo waliathiriwa na mnururisho huo. Wakazi wapatao 100 wakawa wagonjwa. Wakazi 50 wakalazwa hospitalini, na wanne wakafa. Wataalamu wanaopambana na ugaidi hushtuka sana wafikiripo kile kinachoweza kutukia iwapo kemikali hiyo ya cesium itasambazwa kimakusudi.
Matokeo Mabaya ya Ugaidi
Matokeo yaliyo wazi ya ugaidi ni vifo vya kusikitisha vya wanadamu. Lakini kuna matokeo zaidi. Ugaidi unaweza kuharibu au kuzorotesha jitihada za kuleta amani katika maeneo yenye vita duniani. Ugaidi huzidisha mapambano na jeuri.
Ugaidi unaweza pia kuathiri uchumi wa nchi. Serikali nyingi zimelazimika kutumia wakati mwingi na mali ili kukabiliana nao. Kwa mfano, nchi ya Marekani peke yake ilitenga zaidi ya dola bilioni kumi katika mwaka wa 2000 ili kukabiliana na ugaidi.
Ugaidi hutuathiri sote iwe twajua hivyo au la. Huathiri jinsi tunavyosafiri na maamuzi tunayofanya tunaposafiri. Nchi nyingi ulimwenguni hulazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha za kodi ili kulinda watu mashuhuri, vifaa au majengo muhimu, na kulinda raia kutokana na ugaidi.
Basi swali linalobaki ni hili, Je, tatizo la ugaidi litatatuliwa kabisa? Makala ifuatayo itazungumzia swali hilo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Magaidi Wanaodai Wanahifadhi Mazingira
Gazeti la Oregonian laripoti kwamba kuna magaidi wapya “wanaochoma mali kimakusudi, kulipua mabomu na kujeruhi watu wakidai eti wanahifadhi mazingira na viumbe.” Matendo hayo ya kihuni yameitwa ugaidi wa kimazingira (ecoterrorism). Angalau visa vibaya 100 vya aina hiyo vimetukia magharibi mwa Marekani tangu mwaka wa 1980. Vimesababisha hasara ya jumla ya dola milioni 42.8 za Marekani. Kwa kawaida uhalifu huo unakusudiwa kuzuia ukataji wa miti, kuwazuia watu kufanyia tafrija mbugani, au kuzuia watu kutumia wanyama kwa utafiti, kula nyama yao, au kutumia manyoya yao.
Matukio hayo huonwa kuwa vitendo vya kigaidi kwa kuwa ujeuri hutumiwa ili kuwalazimisha watu na mashirika kubadili mtazamo, au kubadili sera za kijamii. Magaidi wa kimazingira huwavunja moyo wachunguzi wa mazingira kwa kushambulia vifaa muhimu. Kwa kawaida wanashambulia vifaa hivyo na kuviharibu kabisa wakati wa usiku. Ni hivi karibuni tu ndipo uhalifu unaofanywa kwa madai ya kuhifadhi mazingira ulipoanza kuenea na kushtua watu wengi. Lakini kuna vifaa vingi vinavyoweza kushambuliwa na magaidi siku hizi. Mpelelezi maalumu James N. Damitio, ambaye amekuwa mtafiti wa Idara ya Misitu ya Marekani kwa muda mrefu, alisema hivi: “Kusudi lao ni kuwafanya watu watambue harakati zao za kuleta mabadiliko. Wanapoona kwamba watu hawajali maoni yao, wanajaribu mbinu nyingine.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]
Ugaidi na Vyombo vya Habari
“Magaidi wanaowadhulumu watu wasio na hatia hupenda sana kutangazwa kote ili kutimiza malengo yao ya kisiasa au kubabaisha watu tu,” asema Terry Anderson, mwandishi wa habari ambaye alitekwa na magaidi nchini Lebanon kwa miaka saba hivi. “Magaidi huhisi wamefaulu hasa inapotangazwa kwamba mtu ametekwa nyara kwa sababu za kisiasa, au ameuawa au watu wamelipuliwa kwa bomu. Habari hizo zisiposambazwa ulimwenguni pote, magaidi wanahisi kwamba matendo yao ya kikatili hayakuwa na maana yoyote.”
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
1. Bomu lalipuliwa na gaidi aliyejitolea kufa, huko Jerusalem, Israel
2. Magaidi wa kikabila walipua benki kwa bomu huko Colombo, Sri Lanka
3. Bomu lililotegwa katika gari lalipuka Nairobi, Kenya
4. Familia za watu waliouawa kwa mlipuko wa bomu huko Moscow, Urusi
[Hisani]
Heidi Levine/Sipa Press
A. Lokuhapuarachchi/Sipa Press
AP Photo/Sayyid Azim
Izvestia/Sipa Press