Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Waingereza Wanabadili Dini

Gazeti The Sunday Telegraph laripoti kwamba sasa Waingereza wanabadili dini sana. Kila juma Waingereza 1,000 hivi wanabadili dini. “Waanglikana wanageuka kuwa Wakatoliki, Wakatoliki kuwa Waanglikana, Wayahudi kuwa Wabudha, Waislamu kuwa Waanglikana, na Wakatoliki kuwa Wayahudi.” Watu wengi sana wanaobadili imani yao wanajiunga na Uislamu, Ubudha, harakati za Muhula Mpya, na upagani. Dakt. Ahmed Andrews wa Chuo Kikuu cha Derby huko Uingereza, ambaye pia alibadili dini, asema: “Katika nchi hii, Wazungu 5,000 hadi 10,000 hivi wamegeuka kuwa Waislamu na walio wengi kati yao walikuwa Wakatoliki.” Asilimia 10 hadi 30 ya watu waliobadili dini yao kuwa Wabudha, ni Wayahudi. Kanisa la Anglikana lilipowaweka wanawake kuwa wahudumu, Waanglikana wengi sana walibadili dini wakawa Wakatoliki. Kulingana na Rabi Jonathan Romain, “watu huhisi njaa ya kiroho, basi wanatafuta dini tofauti.”

Mtindo wa Maisha na Kansa

Gazeti la The Guardian la London laripoti kwamba “uchunguzi uliofanyiwa mapacha 90,000 umeonyesha kwamba kansa haisababishwi hasa na maumbile yako bali husababishwa hasa na mahala ulipo, yale unayofanya na yale yanayotukia maishani mwako.” Dakt. Paul Lichtenstein wa Taasisi ya Karolinska huko Sweden, ndiye aliyesimamia uchunguzi huo. Yeye asema: “Mazingira ni ya maana zaidi kuliko hali ya chembe za urithi.” Wanasayansi huamini kwamba uvutaji wa sigareti husababisha asilimia 35 ya visa vya kansa ilhali yaonekana asilimia 30 huhusiana na lishe. Chembe za urithi husababisha hasa kansa ya kibofu, ya koloni na puru, na ya matiti lakini Dakt. Tim Key wa Hazina ya Kiserikali ya Utafiti wa Kansa huko Oxford, Uingereza, ashauri hivi: “Hata kama . . . kuna watu katika familia yenu [waliokuwa na kansa], mambo unayofanya maishani ndiyo ya maana zaidi. Hupaswi kuvuta sigareti, unapaswa kuwa na lishe bora. Mambo hayo hupunguza uwezekano wa kupata kansa.”

Utumie Ubongo Wako

“Uwezo wa ubongo waweza kudumu katika maisha yetu yote, maadamu tunaendelea kuutumia,” lasema gazeti la Vancouver Sun. “Soma, soma, soma,” ndivyo anavyosema Dakt. Amir Soas wa Shule ya Kitiba ya Chuo Kikuu cha Case Western Reserve huko Ohio, Marekani. Ili kudumisha uwezo wa akili unapoendelea kuzeeka, fanya mambo yanayochemsha bongo, jifunze lugha mpya, jifunze kucheza ala ya muziki, au ushiriki katika mazungumzo yanayochangamsha. “Fanya chochote kinachochemsha bongo,” asema Dakt. Soas. Pia, anawashauri watu wasitazame televisheni sana. Yeye asema, “unapotazama televisheni, ubongo hulala.” Gazeti la Sun laongezea kusema kwamba ubongo wenye afya huhitaji oksijeni inayopitia kwenye mishipa yenye afya. Kwa hiyo, mazoezi na lishe bora husaidia ubongo kama vile yanavyosaidia kuzuia ugonjwa wa moyo na ugonjwa wa sukari.

Tembo “Hawasahau Rafiki Zao”

“Tembo hawasahau kamwe—au angalau, hawasahau rafiki zao,” laripoti gazeti New Scientist. Dakt. Karen McComb wa Chuo Kikuu cha Sussex, Uingereza, alirekodi “milio ya kuwasiliana” ya tembo jike wa Kiafrika katika Mbuga ya Wanyama ya Amboseli nchini Kenya na akagundua wale tembo waliokutana mara nyingi na wale wasiojuana. Kisha akachezea familia 27 za tembo kanda hiyo ili kuchunguza itikio lao. Ikiwa tembo hao walimjua vizuri tembo aliyekuwa akilia, wao waliitikia mara moja. Ikiwa walimjua kidogo tu, walisikiliza lakini hawakuitikia. Na waliposikia mlio wa tembo wasiyemjua walikasirika na kutaka kushambulia. Makala hiyo ilisema kuwa “waliwatambua tembo wa familia 14 nyingine kupitia milio yao, ikionyesha kwamba kila tembo anaweza kukumbuka tembo 100 wengine wakubwa.” Vilevile, tembo wanaweza kuwakumbuka wanadamu. Baada ya kufanya kazi na tembo mmoja wa Asia kwa miaka 18, John Partridge, anayesimamia wanyama kwenye Bustani ya Wanyama ya Bristol nchini Uingereza, asema kwamba tembo huyo alimkumbuka aliporudi kwenye sehemu hiyo baada ya miaka mitatu.

Walanguzi Stadi wa Dawa za Kulevya

Siku zilizopita, walanguzi wa dawa za kulevya nchini Kolombia walificha dawa hizo katika ndege za abiria au merikebu. Hata hivyo, hivi karibuni wenye mamlaka walishangaa walipogundua kwamba walanguzi hao walikuwa wakitengeneza nyambizi ya hali ya juu. Nyambizi hiyo ilikuwa na kipenyo cha meta tatu, na ingeweza kubeba tani 200 za kokeini. Wakazi wenye shaka waliokaa karibu na mahala hapo waliwapeleka polisi kwenye “ghala moja nje ya Bogotá, lililokuwa meta 2,300 juu ya milima ya Andes na kilometa 300 kutoka bandarini,” lasema gazeti la The New York Times. “Chombo hicho kilichokuwa na urefu wa meta 30 kingeweza kuvuka bahari na kupita kwenye ufuo wa Miami au majiji mengine ya pwani na kupakuliwa shehena hiyo ya dawa za kulevya kisirisiri.” Ijapokuwa hakuna aliyekuwa kwenye ghala hilo au aliyekamatwa na polisi, washukiwa wanatia ndani wahalifu wa Urusi na Marekani, pamoja na mhandisi mmoja stadi wa nyambizi. Maafisa walisema kwamba huenda matrela yalibeba nyambizi hiyo ikiwa imetenganishwa katika sehemu tatu hadi pwani. Walistaajabia namna walanguzi hao wa dawa za kulevya walivyotumia ustadi na jitihada nyingi ili kusafirisha bidhaa zao kwenye nchi za nje.

Wanyama Wasitawi Katika Eneo Lisilo na Majeshi

“Tangu eneo lisilo na majeshi lilipoanzishwa baada ya Vita ya Korea kumalizika mwaka wa 1953, hatua za usalama zilizochukuliwa zimefanya mazingira ya eneo hilo kuwa na utulivu,” lasema gazeti la The Wall Street Journal. “Ardhi inapoendelea kuharibiwa kwingineko kwa sababu ya ustawi wa kiuchumi katika nchi mbili za Korea, wanyama wengi wanakimbilia eneo la mpakani.” Ndege na wanyama wasiopatikana kwa urahisi au wanaohatarishwa huishi huko. Pia, yadaiwa kwamba simbamarara na chui wanapatikana huko. Wanamazingira wanaogopa kwamba juhudi za kutafuta amani kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini zitaharibu makao ya wanyama. Kwa hiyo, wanaomba kuwe na “‘mbuga ya wanyama ya amani’ mpakani” ili kuwahifadhi na kuwaruhusu wanyama kutoka nchi zote mbili wajamiiane. Gazeti la Journal laendelea kusema: “Wanamazingira wanatiwa moyo wanapowaza kwamba amani yaweza kuwaunganisha tena wanyama hao, sawa na jinsi washiriki wa familia waliotengana kwa muda mrefu walivyounganishwa kupitia maelewano.”

Mapumziko ya Adhuhuri Yanayopoteza Wakati

“Waingereza wanaopenda kufanya kazi sana hukiona chakula cha mchana kuwa cha magoigoi, huku wakisusia chakula hicho na kula tu sandwichi ofisini mwao,” laripoti Financial Times la London. Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi waonyesha kwamba Mwingereza wa kawaida sasa hutumia dakika 36 tu kwa mapumziko ya chakula cha mchana. Wataalamu wa kitiba wanasema kwamba mapumziko ya adhuhuri hupunguza mfadhaiko. Lakini waajiri fulani hupangia mikutano wakati wa adhuhuri, wakiwanyima wafanya-kazi pumziko. Shirika la Datamonitor, lililotayarisha ripoti hiyo, lasema hivi: “Kwa kuwa wanaishi katika jamii inayotaka wafanya-kazi watimize mengi mno, watu wengi huyaona mapumziko ya adhuhuri kuwa ni kupoteza wakati.” Sarah Nunny, mchanganuzi wa Datamonitor aongezea hivi: “Twashindana na mashirika mengine ya kimataifa. Hatuwezi kusema ‘Nitafanya kazi hii baadaye.’ Ni lazima ifanywe sasa.”

Uraibu wa Tumbaku Nchini Mexico

Katika mradi wa hivi majuzi wa kuzuia uraibu wa tumbaku nchini Mexico, José Antonio González Fernández, aliyekuwa Katibu Mkuu wa kitaifa wa afya wakati huo, alisema kwamba asilimia 27.7 ya wenyeji wa Mexico huvuta sigareti. Jambo linalosababisha wasiwasi ni kwamba karibu wavutaji-sigareti milioni moja wana umri wa kati ya miaka 12 hadi 17. Bw. Gonzalez alisema kwamba vifo 122 hivi kila siku nchini Mexico husababishwa na uraibu huo wa tumbaku. Alihuzunishwa na jinsi “jambo hilo linavyoleta hasara kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi ya taifa hilo, maisha yanayopotea, . . . na madhara tunayopata kutoka kwa wale wanaovuta sigareti miongoni mwetu.”

Je, Ni Kutosheleza Uhitaji wa Kiroho?

Washauri wanaozidi kuwa maarufu kwa kuwatia watu moyo kujiamini, kuwa na mtazamo unaofaa, na kuwa na mafanikio ‘wanawaondoa watu kutoka kwenye dini,’ lasema gazeti la Globe and Mail la Kanada. “Watu wangali wanapenda sana mambo ya kiroho, lakini upendezi wao katika desturi za kidini unafifia.” Uchunguzi waonyesha kwamba ingawa asilimia 80 ya Wakanada husema kwamba wanamwamini Mungu, asilimia 22 ya wale wanaodai kuwa Wakristo hupendelea kuamini mambo yao wenyewe kuliko yale ya dini yoyote ile. Ripoti hiyo ya gazeti la Globe yasema kuwa ushauri wa kiroho unaotolewa na washauri hao ni “kitu cha kukutia nguvu tu ili uendelee na shughuli zitakazokufanikisha.”