Maswali Mengi Yamezuka Kuhusu Kaburi la Newgrange
Maswali Mengi Yamezuka Kuhusu Kaburi la Newgrange
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI IRELAND
FASIHI za kale za watu wa Ireland zinaliita eneo hili Brú na Bóinne. Jina hilo lamaanisha kihalisi “Nyumba au Jumba la Boyne.” Makaburi yanayofukuliwa katika eneo hilo lenye mafumbo, ni baadhi ya makaburi ya kale zaidi duniani. Eneo hilo liko umbali wa kilometa 50 kaskazini ya Dublin, mahali ambapo mto Boyne unapinda. Mojawapo ya makaburi hayo linaitwa Newgrange. Wakati hususa wa ujenzi haujulikani, ijapokuwa baadhi ya watu hudhani lilijengwa kabla ya piramidi kubwa ya Giza huko Misri. Kila mwaka, katika siku iliyo na kipindi kifupi zaidi cha nuru ya mchana kuliko siku zote mwakani, watalii humiminika Newgrange ili kujionea uthibitisho wa ajabu wa uwezo wa watu wa kale.
Kwa Nini Lilijengwa?
Bila shaka, jengo hilo la ukumbusho ambalo halijaeleweka vizuri lilikuwa muhimu sana kwa wajenzi wake. (Soma sanduku kwenye ukurasa 24.) Kwa nini walitumia wakati, jitihada na mali nyingi hivyo kulijenga? Kwa nini walijenga kaburi hilo la ajabu?
Yaelekea kwamba, mbali na kuwa kaburi takatifu, Brú na Bóinne, au Brugh na Boinne, palikuwa pia mahali pa ibada ya kidesturi. Profesa Michael O’Kelly aliyefukua eneo hilo alisema hivi: “Kaburi la Brú lilihusishwa na Dagda, Mungu Mwema; mke wake Boann; na mwana wao Oengus; ambao wote walikuwa watu wa Tuatha Dé. Yasemekana watu hao waliishi Ireland kabla ya Waselti kuhamia huko. Baadaye watu hao walihamia kwenye makaburi na ngome za Ireland zenye mashetani. Hao . . . walionwa kuwa viumbe walio na nguvu kufanya vitendo ambavyo wanadamu hawana nguvu ya kuvifanya.”—Newgrange—Archaeology, Art and Legend.
Mto Boyne ulipewa jina la Boann aliyekuwa mungu wa kike katika hadithi za kubuniwa za kale. Kwa sababu eneo hilo lilikuwa na mto katika pande tatu, huenda wajenzi waliamini kwamba Boann angelinda kaburi hilo. Kulingana na mtafiti Martin Brennan huenda waliamini pia kwamba baadhi ya miungu waliishi katika kaburi hilo. Kwa kweli, asema kwamba hadithi za kale zaidi kuhusu makaburi hayo zinasema kwamba “yalionwa kuwa makao ya miungu hai, ambao walitungwa mimba na kuzaliwa hapo.”—The Stars and the Stones.
Hata hivyo, kaburi la Newgrange halikuwa tu kaburi la kuzikia wafu wala kao la miungu. Ni mojawapo ya majengo ya ukumbusho ya kale ambayo yalijengwa ili yapatane na nyota. Kwa usahihi kabisa, wasanifu wa ujenzi walipatanisha ujia mrefu na chumba cha kaburi na mahali ambapo jua huchomoza katika siku iliyo na kipindi kifupi zaidi cha nuru ya mchana kuliko siku zote mwakani. Halafu walitengeneza tundu la kipekee juu ya mlango wa kaburi. Tundu hilo liliruhusu miali ya jua kufika sehemu ya ndani kabisa ya kaburi.
Hata leo, watalii huja Newgrange kila mwaka katika siku ya katikati ya majira ya baridi wakati miali ya jua inapofika katika chumba cha ndani kwa muda wa dakika 15 hivi. Msimamizi wa kituo cha watalii cha Brú na Bóinne aitwaye Clare Tuffy alisema hivi: “Baadhi ya watu huamini kwamba miali ya jua
inayofika ndani ya kaburi iliwakilisha ndoa kati ya mungu wa kike wa dunia na mungu wa jua. Watu wa kale waliamini kwamba ndoa hiyo ingeleta mazao.”Fumbo la Michoro ya Mawe
Hakuna maandishi yanayojulikana yaliyoandikwa na wajenzi hao wa kaburi wasioeleweka vizuri. Lakini ni kana kwamba walitia sahihi yao kwa kuchora katika mawe michoro mbalimbali ya ajabu. Walichora michoro yenye maumbo ya mizunguko, michoro inayofanana na herufi V, ya miraba, ya pembetatu, duara, mipindo na maumbo mengineyo. Na yaelekea vyombo vyao vya ujenzi vilikuwa tu sehemu za jiwe gumu aina ya shondo au jiwe linginelo. Na nyundo zao zilikuwa za mawe. Brennan anasema kwamba waliwaachia watu wa Ireland “mkusanyo mkubwa wa sanaa kuliko yote duniani uliochorwa kwenye mawe.”
Baadhi ya watu hudhani kwamba maandishi hayo ya mafumbo yaweza kufasiriwa, na kwamba yana maelezo sahihi kuhusu mambo ya nyota. Brennan huamini kwamba yanaonyesha jinsi ambavyo jua na mwezi huzunguka. Yeye anasema hivi: ‘Yaelekea kwamba . . . makaburi na pia michoro ilionwa kuwa vitu vilivyowekwa wakfu
kwa jua na mwezi. Tukikubali kwamba makaburi na michoro vilikuwa vitu vitakatifu tunasaidiwa kuelewa sababu za kuvitengeneza.’ Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wanakubaliana na Michael O’Kelly, aliyenukuliwa mapema, ambaye aliandika kwamba michoro hiyo “bila shaka ilikuwa na maana kwa wale walioiona, lakini yaelekea sisi hatutajua kamwe maana yake. Michoro hiyo itabaki kuwa fumbo kama vile kaburi la Brú au jumba la miungu wa kale litakavyobaki kuwa fumbo.”“Watu Wenye Akili Nyingi”
Yaonekana kwamba maswali mengi huzuka kuhusu kaburi la Newgrange na hakuna jibu la hata swali moja. Kufikia leo mambo mengi kuhusu wajenzi wa kaburi lenye ujia la Brú na Bóinne hayajaeleweka. Lakini jambo moja ni wazi, wajenzi hawakuwa watu wasiostaarabika. O’Kelly alisema kwamba wasanifu wa ujenzi wa kaburi la Newgrange, wasanii wake, na mafundi wake “bila shaka walikuwa watu wa utamaduni wa hali ya juu.” Mwandishi Peter Harbison anasema kwamba wajenzi “hawakuwa watu walioishi pangoni kama vile watu wengi walivyoamini . . . Walikuwa watu wenye akili nyingi.”
Wajenzi wa kaburi la Newgrange kwenye Brú na Bóinne hawajulikani. Hata hivyo, kaburi hilo huonyesha kwamba wasanifu wa ujenzi na wajenzi wake walikuwa watu wa kale ambao walikuwa stadi na wenye akili nyingi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]
Wajenzi na Ujenzi
Tunajua nini kuhusu wajenzi wa kaburi la Newgrange? Clare Tuffy, msimamizi wa kituo cha wageni cha Brú na Bóinne, anasema hivi: ‘Hatujui mengi, lakini tumejifunza mambo kadhaa. Tunajua kwamba walikuwa wakulima. Walikuwa matajiri, la sivyo hawangekuwa na mali ya kutosha kujenga kaburi hilo la fahari. Na walikuwa na vifaa vya ujenzi vya mawe tu.’
Wajenzi walijenga ujia wenye urefu wa meta 19, wenye kimo cha meta 2, na upana kwa kutoshea mwanamume bila shida. Mawe makubwa yenye uzito wa kilogramu 10,000 yalitumiwa kwa ujenzi huo. Ujia huelekeza kwenye chumba cha kaburi chenye upana wa meta sita. Chumba hicho kina vyumba vidogo vitatu vinavyoshikamana nacho. Ujia na chumba vina umbo la msalaba mrefu.
Juu ya chumba hicho cha kaburi, wajenzi hao stadi walijenga kwa mawe mengine makubwa, bila ya kutumia saruji, paa lenye umbo la kuba lenye kimo cha meta sita. Kisha walitengeneza tuta kubwa juu ya kaburi hilo lenye kipenyo cha meta 80 na kimo cha meta 12. Pia walijenga ukuta wa kushikilia kwa mawe makubwa na kuufunika kwa mawe madogo aina ya shondo. Waliweka mawe makubwa 97 kwenye ukingo wa kaburi. Kila moja la mawe hayo lina uzito wa kilogramu 2,000 kufikia 5,000. Mawe hayo ya ukingoni na mlango wa kaburi vilifunikwa kwa ardhi zamani. Kisha katika mwaka wa 1699 mfanyikazi ambaye alikuwa akitafuta mawe aligundua mlango huo, na kaburi hilo lenye ujia likapatikana tena.
[Picha]
Mlango wa ujia wa kaburi la Newgrange
[Ramani katika ukurasa wa 22]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Newgrange
DUBLIN
[Picha katika ukurasa wa 23]
Juu: Miali ya jua hufika katika chumba cha ndani kwa muda wa dakika 15 kila mwaka katika siku yenye kipindi kifupi cha nuru ya mchana kuliko zote mwakani
Chini: Sehemu ya ndani kabisa ya chumba cha kaburi; ona michoro ya mzunguko yenye sehemu tatu
[Hisani]
Picha zote kwenye ukurasa wa 22-23 isipokuwa ramani: Dúchas, The Heritage Service, Ireland
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kaburi lililojengwa kwa mawe makubwa
[Hisani]
Dúchas, The Heritage Service, Ireland