Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Makanisa Makuu Yamejengwa kwa Sifa ya Mungu au ya Wanadamu?

Je, Makanisa Makuu Yamejengwa kwa Sifa ya Mungu au ya Wanadamu?

Je, Makanisa Makuu Yamejengwa kwa Sifa ya Mungu au ya Wanadamu?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA

JIJINI Moscow, jambo fulani la ajabu limetukia. Kanisa Kuu la Mwokozi Kristo, ambalo lilibomolewa na Stalin katika mwaka wa 1931, limejengwa upya. Kuba zake za dhahabu zinang’ara huko Urusi. Wajenzi wamemaliza kujenga Kanisa Kuu jijini Évry, lililoko karibu na Paris. Hilo ni kanisa kuu pekee ambalo lilijengwa nchini Ufaransa katika karne ya 20. Ujenzi huo ulimalizika miaka michache tu baada ya kuzinduliwa kwa kanisa kuu la Almudena huko Madrid. Hatupaswi kusahau kanisa kuu la New York City ambalo linaitwa Mtakatifu Yohana wa Mungu (St. John the Divine). Mara nyingi kanisa hilo limeitwa Mtakatifu Yohana Lisilomalizika kwa kuwa limeendelea kujengwa kwa muda wa zaidi ya miaka 100. Hata hivyo, hilo ni miongoni mwa makanisa makubwa zaidi ulimwenguni. Lina ukubwa wa zaidi ya meta 11,000 za mraba.

Kotekote katika Jumuiya ya Wakristo kuna makanisa makuu katika majiji mengi. Waumini huyaona makanisa hayo kuwa ukumbusho wa imani ya wajenzi. Hata watu wasioamini wanayathamini na kuyaona kuwa kazi ya sanaa au vielelezo vya usanifu bora wa ujenzi. Hata hivyo, nyumba hizo za ibada zenye fahari na za gharama kubwa zinazusha maswali muhimu: Kwa nini zilijengwa? Na zilijengwaje? Zina kusudi gani?

Kanisa Kuu Ni Nini?

Baada ya kifo cha Kristo, wanafunzi wake walijipanga katika makutaniko, na wengi wao walikutanika katika nyumba binafsi za watu. (Filemoni 2) Makutaniko hayo yalitunzwa na “wazee” wa kiroho kwa miaka mingi sana. (Matendo 20:17, 28; Waebrania 13:17) Hata hivyo, baada ya mitume kufa, uasi-imani ulianza. (Matendo 20:29, 30) Muda si muda, wazee kadhaa walijitukuza juu ya wale wengine, nao walikuja kuonwa kuwa maaskofu ambao walisimamia makutaniko kadhaa. Yesu alikuwa ameonya wafuasi wake wasijitukuze juu ya ndugu zao. (Mathayo 23:9-12) Kisha, neno “kanisa,” ambalo awali lilitumiwa kuhusu Wakristo wenyewe, likaja kutumiwa vilevile kuhusu mahali walipokutanikia—yaani, jengo lenyewe. Punde si punde, baadhi ya maaskofu walitaka kuwa na makanisa ambayo yalifaa cheo chao. Ili kufafanua kanisa la askofu, neno jipya lilitungwa. Katika lugha ya Kiingereza neno hilo ni cathedral ambalo hutafsiriwa “kanisa kuu” katika Kiswahili.

Neno hilo latokana na neno la Kigiriki kathedra, ambalo lamaanisha “kiti.” Kwa hiyo kanisa kuu lilikuwa kiti cha enzi cha askofu, mfano wa mamlaka yake ya kidunia. Askofu aliongoza dayosisi yake kutoka kanisa lake kuu.

“Enzi ya Makanisa Makuu”

Baraza la Nisea lilikubali kirasmi mpango wa maaskofu wa majiji katika mwaka wa 325 W.K. Mara kwa mara maaskofu walipokea zawadi za mashamba kutoka kwa Serikali ya Roma kwa kuwa iliwaunga mkono wakati huo. Walichukua pia majengo yaliyotumiwa kwa ibada ya kipagani. Wakati Milki ya Roma ilipoporomoka, mpango wa maaskofu wa miji ulidumu, nao ulikuja kuwa wenye nguvu katika Enzi za Kati. Kulingana na mwanahistoria Mfaransa Georges Duby, pindi hiyo ilikuja kuitwa “Enzi ya Makanisa Makuu.”

Idadi ya watu wa Ulaya iliongezeka mara tatu kuanzia karne ya 7 hadi karne ya 14. Ongezeko hilo kubwa la watu lilinufaisha hasa majiji ambayo yalikuwa na utajiri mwingi. Kwa hiyo, makanisa makuu yalijengwa hasa katika majiji hayo. Kwa nini? Kwa sababu ujenzi wa majengo hayo makubwa uliweza kufanikiwa tu palipokuwapo na fedha nyingi!

Ujenzi wa makanisa makuu ulichochewa pia na ibada ya Bikira Maria na ya vitu vitakatifu vilivyohusishwa na watakatifu. Ibada hiyo ilipendwa na wengi, nayo ilisitawi sana katika karne ya 11 na 12. Maaskofu waliendeleza ibada hiyo, na hivyo wakafanya makanisa makuu yao yapendwe zaidi. Jina Notre-Dame (Bikira Maria) lilianza kutumiwa kuhusu makanisa makuu huko Ufaransa siku hizo. Kichapo Théo cha Kikatoliki kinasema hivi: “Hakuna mji ambao haukuweka wakfu kanisa na hata kanisa kuu kwa Bikira Maria.” Kwa hiyo, kanisa kuu la Paris la Saint-Étienne liliwekwa wakfu kwa Notre-Dame. Kanisa kuu la Notre-Dame mjini Chartres, Ufaransa, likawa mojawapo ya mahali patakatifu sana huko Ulaya. Kitabu cha The Horizon Book of Great Cathedrals kinasema kwamba “hakuna mtu yeyote—hata Kristo Mwenyewe—ambaye ametawala mawazo ya wajenzi wa makanisa makuu kadiri ambavyo Bikira Maria aliyatawala.”

“Tutajenga Kanisa Kubwa Hivi . . .”

Kwa nini makanisa hayo yalikuwa makubwa hivyo? Mapema katika karne ya nne, makanisa makuu ya Trier, Ujerumani na Geneva, Uswisi, yalikuwa makubwa sana, ingawa waabudu walikuwa wachache. Katika karne ya 11, kanisa kuu la mji wa Speyer, Ujerumani, lilitoshea wakazi wote wa mji huo, na bado kulikuwa na nafasi ya wengine. Kwa hiyo, kitabu cha The Horizon Book of Great Cathedrals kinasema kwamba “[makanisa makuu] yalikuwa makubwa na yenye fahari sana kwa sababu kadhaa ambazo hazikuwa za kidini.” Mojawapo ilikuwa “kiburi cha askofu au mkuu wa watawa ambaye aligharimia ujenzi huo.”

Katika karne ya 12 na 13, makanisa makuu yalikuwa na urefu wa wastani wa meta 100, nayo yalikusudiwa kuwa na upana sawa na urefu. Kanisa kuu la Winchester huko Uingereza lenye upana wa meta 169, na lile liitwalo Duomo la Milan huko Italia lenye upana wa meta 145 ni makubwa sana. Ofisa Mhispania wa kanisa huko Seville alisema hivi katika mwaka wa 1402: “Tutajenga kanisa kubwa hivi kwamba wale watakaoliona watafikiri hatuna akili timamu.” Kanisa kuu la Seville linasemekana kuwa la pili kwa ukubwa duniani. Lina kuba yenye urefu wa meta 56. Mnara wa kanisa kuu la Strasbourg huko Ufaransa, wenye urefu wa meta 142, ni mrefu kama jengo lenye orofa 40. Kanisa kuu liitwalo Gothic Münster lilijengwa huko Ulm nchini Ujerumani katika karne ya 19. Mnara wake wenye urefu wa meta 161, ndio mnara mrefu kushinda minara yote iliyojengwa kwa mawe ulimwenguni. Mwanahistoria Pierre du Colombier anasisitiza kwamba “hakuna ibada yoyote inayohitaji majengo makubwa hivyo.”

Katika karne ya 12 na 13, walioendeleza ujenzi wa makanisa makuu walichochewa na sababu nyingine ‘isiyo ya kidini’—uzalendo. Kichapo Encyclopædia Britannica kinasema hivi: “Miji ilishindana kujenga kanisa kuu refu zaidi.” Wakuu wa miji, wakazi wa miji, na mashirika ya mafundi walitaka makanisa makuu yaletee miji yao sifa.

Gharama Kubwa

Mwandikaji mmoja anasema kwamba ujenzi wa makanisa makuu ni miradi inayogharimu kiasi kikubwa sana cha fedha. Kwa hiyo, majengo hayo—yanayodumishwa kwa fedha nyingi sana leo—yaligharimiwaje zamani? Mara nyingine, maaskofu wenyewe waligharimia ujenzi. Askofu mmoja aliyefanya hivyo alikuwa Maurice de Sully wa Paris. Mara nyingine, watawala wa serikali, kama Mfalme James wa Kwanza wa Aragon, walitoa fedha kuyajenga. Hata hivyo, kwa kawaida ujenzi wa makanisa makuu uligharimiwa kwa mapato ya dayosisi. Fedha hizo zilitokana na kodi ambazo watu walilazimishwa kulipa na uzalishaji wa mashamba makubwa. Askofu wa Bologna huko Italia alikuwa na mashamba makubwa 2,000! Zaidi ya hayo, mapato yalitokana pia na mambo yaliyohusiana na dini kama vile sadaka, malipo ya rehema, na malipo kwa sababu ya dhambi. Wale ambao walijinunulia haki ya kula chakula kinachotokana na maziwa wakati Wakatoliki wanapofunga, waligharimia kile kinachoitwa Mnara wa Siagi wa kanisa kuu la Rouen, Ufaransa.

Baadhi ya wachangaji walikuwa wakarimu sana, nao waliheshimiwa kwa kuwa na picha zao katika madirisha ya kanisa yenye rangi na sanamu zilichongwa kwa mfano wao. Yaelekea walikuwa wamesahau kwamba Mkristo anapaswa kutoa bila kutangaza utoaji wake. (Mathayo 6:2) Fedha zilihitajika daima kwa kuwa mara nyingi gharama ilizidi kiasi kilichokadiriwa. Kwa hiyo haishangazi kwamba jitihada za kutafuta fedha mara nyingi zilisababisha udanganyifu na utozaji wa fedha kwa nguvu. Kwa mfano, mara nyingi mtu aliyeshtakiwa kuwa mwasi-imani alinyang’anywa mali zake. Kwa hiyo, wale Wakathari waliodaiwa kuwa waasi-imani walinyang’anywa mali zao, na mali hizo zilitumiwa kugharimia ujenzi wa makanisa kadhaa. *

Bila shaka kanisa lilihitaji kuendelea daima kutafuta fedha. Baadhi ya wanahistoria wamedai kwamba watu walijenga majengo hayo kwa hiari. Lakini hilo si kweli. Mwanahistoria Henry Kraus anasema hivi: “Ingawa watu walioishi katika Enzi ya Kati walishikilia dini sana, hata hivyo kujenga makanisa hakukuwa jambo ambalo walitaka kutanguliza maishani.” Kwa hiyo, wanahistoria wengi wanachambua kanisa kwa utumizi huo wa fedha wa kupita kiasi. Kitabu cha The Horizon Book of Great Cathedrals kinasema hivi: “Fedha zilizotumiwa kujenga makanisa zingaliweza kutumiwa kulisha wenye njaa . . . au kudumisha hospitali na shule mbalimbali. Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba ujenzi wa makanisa makuu ulisababisha vifo vya maelfu ya watu.”

Jinsi Yalivyojengwa

Makanisa makuu ni uthibitisho wa ubunifu wa wanadamu. Ni jambo la ajabu kwamba majengo hayo makubwa yalijengwa kwa kutumia tekinolojia ya kale. Kwanza, ramani ya ujenzi ilichorwa. Kwenye machimbo ya mawe violezo vilitumiwa kuhakikisha kwamba mapambo ya mawe yalifanana na kwamba mawe yote yalikuwa na ukubwa uliotakikana. Mawe yalitiwa alama kwa usahihi kuonyesha mahali pake hususa katika jengo. Usafirishaji ulikuwa wa polepole sana na wenye gharama ya juu, hata hivyo, kulingana na mwanahistoria Mfaransa aitwaye Jean Gimpel, ‘mawe mengi yalichimbwa huko Ufaransa kati ya miaka 1050 na 1350 kuliko yalivyochimbwa katika Misri ya kale.’

Kwenye mahali pa ujenzi penyewe, wafanyikazi walifanya kazi ya ajabu kwa kutumia mashine za kale za kuinua uzani, kama vile kapi iliyoendeshwa kwa gurudumu lililokanyagwa kwa miguu. Hesabu ambazo hutumiwa na wahandisi wa leo hazikujulikana wakati huo. Wajenzi walitegemea vipawa na uzoefu. Si ajabu kwamba visa vingi vibaya vilitukia. Kwa mfano, kuba za kanisa kuu la Beauvais, Ufaransa, ziliporomoka katika mwaka wa 1284 kwa sababu zilikuwa kubwa mno. Hata hivyo, vitu kama nguzo zinazoshikilia ukuta, mgongo wa kuba, viminara, na mihimili vilibuniwa na wajenzi walifaulu kujenga majengo marefu zaidi.

Kanisa kuu lililojengwa kwa muda mfupi kushinda yote lilijengwa kwa muda wa miaka 40 (Salisbury, Uingereza), lakini mengine yalimalizika baada ya mamia ya miaka. Mengine, kama vile makanisa makuu ya Beauvais na Strasbourg, Ufaransa, hayajamalizika kufikia leo.

‘Watanguliza Mambo Yasiyofaa’

Papa Honorius wa Tatu alisema kwamba ‘majengo [hayo] yenye fahari yaliyogharimu fedha nyingi,’ yalisababisha ubishi tangu mwanzoni. Baadhi ya makasisi walipinga ujenzi huo na utumizi wa fedha nyingi sana. Kasisi Pierre le Chantre wa Notre-Dame de Paris, aliyeishi katika karne ya 13, alisema hivi: “Ni dhambi kujenga makanisa vile tunavyofanya siku hizi.”

Hata leo ujenzi wa makanisa makuu unachambuliwa, kama vile ujenzi wa kanisa kuu la Évry. Gazeti Le Monde la Ufaransa liliripoti kwamba watu wengi huona makanisa makuu kuwa “utangulizaji wa mambo yasiyofaa,” na kwamba dini “zinapasa kujishughulisha na watu na kuhubiri habari njema badala ya kushughulikia mawe na mapambo.”

Bila shaka wengi waliosaidia kujenga majengo hayo makubwa walikuwa watu waliompenda Mungu kwa moyo mweupe. Walikuwa na “bidii kwa ajili ya Mungu,” lakini bidii hiyo haikuwa “kulingana na ujuzi sahihi.” (Waroma 10:2) Yesu Kristo hakupendekeza kamwe wafuasi wake wajenge majengo makubwa yenye madoido kwa ajili ya ibada. Aliwasihi waabudu wa kweli “waabudu kwa roho na kweli.” (Yohana 4:21-24) Licha ya fahari yake, makanisa makuu ya Jumuiya ya Wakristo yanapinga kanuni hiyo. Huenda makanisa makuu yakawa ukumbusho kwa wanadamu ambao waliyajenga, lakini hayamletei Mungu sifa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 18 Soma makala ya “Wakathari—Je, Walikuwa Wakristo Wafia-Imani?” katika toleo la Septemba 1, 1995 la Mnara wa Mlinzi, linalochapishwa na Mashahidi wa Yehova, ukurasa wa 27-30.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Kanisa Kuu la Santiago de Compostela, Hispania

[Picha katika ukurasa wa 15]

Juu kabisa: Dirisha lenye picha ya waridi, la kanisa kuu la Notre-Dame, Chartres, Ufaransa

Juu: Sehemu ya picha ya mchongaji-mawe, Notre Dame, Paris

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kanisa kuu la Notre-Dame, Paris, lililojengwa katika karne ya 12

[Picha katika ukurasa wa 15]

Ndani ya kanisa kuu la Notre-Dame, Amiens. Ndilo jengo kubwa zaidi la kidini nchini Ufaransa. Kuba zake ni zenye urefu wa meta 43