Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Viumbe wa Dunia Wanaweza Kuhifadhiwa?

Je, Viumbe wa Dunia Wanaweza Kuhifadhiwa?

Je, Viumbe wa Dunia Wanaweza Kuhifadhiwa?

“WANADAMU wanaendelea kuhatarisha nyani, alibatrosi, kereng’ende na viumbe wengine na kwa kufanya hivyo tunajihatarisha sisi wenyewe,” lasema gazeti The Globe and Mail la Kanada. Gazeti hilo lilirejezea kichapo cha 2000 IUCN Red List of Threatened Species (orodha ya mimea na wanyama waliomo hatarini), ambacho kimechapishwa na Shirika la Kuhifadhi Viumbe Ulimwenguni (IUCN) la Geneva, Uswisi. Kichapo hicho kinaonya kwamba zaidi ya jamii 11,000 za mimea na wanyama zimo hatarini. Wanyama wanaonyonyesha watoto wao wameathiriwa zaidi kuliko wengine. Gazeti hilo la Globe linasema: “Karibu robo ya jamii za wanyama hao wanaoishi Duniani leo—au asilimia 24—wamo hatarini.”

Hali hiyo hatari imesababishwa na nini? Wanasayansi wanaeleza kwamba kinachosababisha jamii za wanyama kutoweka haraka kuliko mbeleni hutia ndani biashara ya kimataifa ya wanyama-vipenzi, kuvua samaki wengi kwa kutumia njia za kisasa, na wanyama kupoteza makao yanayofaa. Isitoshe, barabara nyingi zinajengwa katika misitu ambayo haikuwa imevamiwa na watu, na hivyo, sasa “watu wanaweza kuwinda wanyama ambao hawakufikiwa hapo awali. Kisha wanawaua na kuwala. Wakifanya hivyo kupita kiasi, jamii za wanyama hutoweka.”

Wanasayansi huonya kwamba hali hiyo huhatarisha wanadamu pia. David Brackett, ambaye ni mwenyekiti wa tume ya kuhifadhi jamii ya mimea na wanyama ya Shirika la Kuhifadhi Viumbe Ulimwenguni, anasema hivi: “Tunachezea mfumo unaotegemeza uhai wetu tunaposababisha jamii za wanyama zitoweke. . . . Dunia haitaokoka ikiwa jamii zote za wanyama zitapatikana katika bustani za wanyama tu.”

Ripoti hiyo ya IUCN inawasihi watu wote wajitahidi kutatua tatizo hilo. “Wafanyakazi na hata fedha zinahitajika mara 10 hadi mara 100 zaidi ya kiwango kinachotumiwa wakati huu ili tatizo hilo litatuliwe. Hata hivyo, mara nyingi pupa huzuia jitihada za kuhifadhi vitu na viumbe wanaotegemeza uhai duniani.”

Je, jamii za mimea na wanyama zinaweza kuhifadhiwa? Wanadamu wa kwanza na watoto wao walipewa kazi ya kutunza uhai wote duniani. Biblia inasema hivi: “BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.” (Mwanzo 2:15) Ijapokuwa wanadamu wameshindwa kutimiza daraka hilo, kusudi la Mungu kwa dunia halijabadilika. Yeye hujali dunia, na hataruhusu iharibiwe kwa sababu ya uzembe wala ubinafsi. (Ufunuo 11:18) Neno lake linaahidi hivi: “Wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele.”—Zaburi 37:29.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]

U.S. Fish & Wildlife Service, Washington, D.C./J.D. Pittillo