Maji Yanapokuwa Mekundu
Maji Yanapokuwa Mekundu
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFILIPINO
Hebu wazia wavuvi wakitembea ufuoni, wakiwa tayari kabisa kuendelea na shughuli yao ya kawaida ya kutayarisha mashua na nyavu zao asubuhi na mapema. Kama kawaida, wanatarajia kuvua samaki wengi. Lakini, ingawa wana usingizi wanashangazwa na wanachoona. Maelfu ya samaki waliokufa wamebebwa na maji hadi ufuoni. Ni nini kilichowaua samaki wengi hivyo? MAJI MEKUNDU BAHARINI!
SEHEMU mbalimbali za ulimwengu zimekumbwa na maji mekundu baharini. Maji ya aina hiyo yameonekana kwenye pwani za Bahari ya Atlantiki na ya Pasifiki huko Marekani na Kanada. Maji hayo yameonekana pia huko Australia, Brunei, kaskazini-magharibi mwa Ulaya, Japani, Malasia, Papua New Guinea, Ufilipino na sehemu nyinginezo. Ingawa watu wengi hawajasikia kuhusu maji mekundu baharini, hilo si jambo geni.
Huko Ufilipino, maji mekundu baharini yalionekana kwa mara ya kwanza kwenye mkoa wa Bataan mnamo mwaka wa 1908. Mwaka wa 1983, maji mekundu yenye sumu yaliwaathiri samaki na chaza katika Bahari ya Samar, Ghuba ya Maqueda, na Ghuba ya Villareal. Tangu wakati huo, maji mekundu yameonekana kwenye sehemu nyingine za pwani. Zenaida Abuso mshiriki wa Kikosi cha Kitaifa cha Kupambana na Maji Mekundu Baharini cha Ufilipino, alimwambia mwandishi wa Amkeni! kwamba “licha ya samaki waliokufa, Idara ya Shughuli za Uvuvi na Bahari ya Ufilipino imerekodi visa 1,926 vya watu waliopooza kutokana na kula viumbe wa baharini wenye sumu ya maji mekundu.” * Lakini, hayo maji mekundu baharini yenye sumu, ni nini hasa?
Hayo Maji Mekundu Ni Nini?
Usemi “maji mekundu baharini” humaanisha kule kugeuka kwa rangi ya maji ambako hutukia katika sehemu fulani za bahari. Ingawa kwa kawaida rangi ya maji hubadilika kuwa nyekundu, yaweza pia kuwa kahawia au manjano. Kichapo The World Book Encyclopedia chasema kuwa “sehemu zinazobadilika rangi huwa na ukubwa wa yadi au meta kadhaa za mraba kufikia maili 1,000 za mraba (kilometa 2,600 za mraba).”
Ni nini kinachofanya rangi ya maji ibadilike? Maji mekundu baharini husababishwa na jamii mbalimbali za mwani wenye chembe moja au protozoa zinazoitwa dinoflagellates zilizo ndogo sana. Viumbe hao wadogo wana sehemu zenye nyuzinyuzi zilizojitokeza zinazoitwa flagella. Sehemu hizo huwa kama kamba za mijeledi na viumbe hao huzitumia kusonga majini. Kuna aina 2,000 za dinoflagellates. Kati ya aina hizo, 30 huwa na sumu. Viumbe hao wadogo hukaa katika maji yenye joto na chumvi nyingi.
Maji huwa mekundu baharini wakati viumbe hao wanapoongezeka ghafula na kwa haraka
sana. Idadi ya viumbe hao yaweza kuongezeka kufikia viumbe 50,000,000 katika kila lita moja ya maji! Ingawa wanasayansi hawafahamu sana ni kwa nini hilo hutukia, wanajua kwamba viumbe hao huongezeka wakati hali fulani zinapoyaathiri maji kwa wakati mmoja. Hali hizo zatia ndani halihewa isiyo ya kawaida, halijoto za juu kabisa, virutubisho tele majini, jua kali, na mikondo ya maji inayofaa kwa ukuzi. Mvua kubwa inaponyesha, madini na virutubisho vingine husukumwa kutoka kwenye nchi kavu hadi kwenye maji ya pwani. Virutubisho hivyo vyaweza kusababisha ongezeko la viumbe hao. Tokeo ni nini? Maji mekundu baharini!Kwa kusikitisha, yamkini nyakati nyingine wanadamu huzidisha hali hiyo. Kinyesi cha binadamu na takataka za viwanda zinapotupwa majini, zaweza kuongeza virutubisho fulani kupita kiasi. Hiyo yaweza kuongeza ukuzi wa viumbe hao. Punde si punde, hewa huisha majini na samaki wengi hufa.
Kwa kawaida, maji huwa mekundu kwenye bahari zenye joto na maji matulivu ya pwani, mwishoni mwa miezi yenye joto na mwanzoni mwa majira ya mvua. Maji yaweza kuwa mekundu kwa muda wa saa chache au kwa miezi kadhaa, ikitegemea hali za sehemu hiyo.
Wanaoathiriwa
Kwa kawaida maji mekundu baharini hayasababishi madhara. Hata hivyo, mengine husababisha hasara kubwa. Jamii fulani za dinoflagellates huyatia maji sumu na kuwafanya samaki na viumbe wengine wa baharini wapooze au wafe. Maji fulani mekundu yamewaua samaki, chaza, ngisi, kivaaute, kome, kamba, na kaa wengi wanaokula dinoflagellates. Kunapokuwa na maji mekundu baharini yanayodhuru, waweza kuona samaki wengi waliokufa wakielea juu ya maji na wanaweza kurundamana ufuoni kwa kilometa nyingi.
Hata wanadamu wameathiriwa sana. Katika sehemu ambazo watu hufanya kazi ya uvuvi, maji mekundu yamewaharibia wavuvi pato lao, yaani riziki yao. Jambo la kusikitisha hata zaidi ni kwamba maji mekundu yamewaua wanadamu wengi.
Sumu ya Maji Mekundu
Aina moja ya sumu inayopatikana kwenye jamii fulani za dinoflagellates inaitwa saxitoxin. Hiyo ni aina ya chumvi inayoyeyuka majini nayo huudhuru mfumo wa neva wa mwanadamu. Hivyo, inaorodheshwa kati ya sumu zinazodhuru mfumo wa neva. Kichapo The New Encyclopædia Britannica huripoti kwamba “sumu iliyo kwenye maji hayo huathiri mfumo wa kupumua.” Hoteli zilizo ufuoni zimehitaji kufungwa mawimbi yanaporusha sumu ya maji mekundu hewani.
Je, unapenda kula chaza au viumbe wengine wa baharini? Maji mekundu yaweza kuwatia sumu chaza wanaokula dinoflagellates. Gazeti la Infomapper lasema kwamba ‘viumbe wa baharini wenye koa mbili na aina nyingine za chaza kama kome na kivaaute waweza kusababisha hatari kubwa kwa kuwa wao huyachuja maji ili kupata chakula, na hunywa sumu nyingi kuliko samaki.’ Hata hivyo, “samaki, ngisi, kamba, na kaa . . . bado wanaweza kuliwa na watu, bila kusababisha hatari yoyote.” Kwa nini? Sumu ya maji mekundu hukusanyika kwenye matumbo ya viumbe hao, na kwa kawaida matumbo hayo huondolewa kabla ya kupika.
Hata hivyo, ni lazima mtu awe mwangalifu anapokula viumbe wa baharini—hasa “chaza—wanaotolewa kwenye sehemu zinazojulikana kuwa na maji mekundu. Maji hayo yaweza kusababisha hali ya kupooza (paralytic shellfish poisoning au PSP). Iwapo sumu ya maji mekundu imeingia mwilini, utahisi dalili baada ya dakika 30. Baadhi ya dalili hizo zimeorodheshwa kwenye chati unayoona. Hali hiyo ya kupooza isipotibiwa upesi yaweza kufanya mfumo wa kupumua usifanye kazi, na kusababisha kifo.
Dawa ya kuponya madhara ya sumu ya maji mekundu haijapatikana kufikia sasa. Hata hivyo, hatua fulani zinazochukuliwa wakati wa dharura zimesaidia kwa kiasi fulani. Sumu ya maji mekundu yaweza kuondolewa kwenye tumbo la mgonjwa kwa kumfanya atapike. Mrija unaoingizwa tumboni umetumiwa pia kusafisha tumbo na kuondoa sumu. Katika hali fulani, ni lazima mashine za kusaidia kupumua zitumiwe. Nchini Ufilipino, wengine huamini kwamba kunywa maji ya dafu pamoja na sukari yenye rangi ya kahawia huwasaidia walioathiriwa kupona haraka.
Utatuzi
Kwa sasa, tatizo la maji mekundu halijatatuliwa. Lakini wengi wanaamini kuwa tatizo hilo litapungua iwapo mbolea zenye kemikali na dawa za kuwaua wadudu hazitatumiwa sana. Hiyo itazuia dawa hizo zisibebwe na maji ya mvua hadi baharini. Pia, kupiga marufuku utupaji wa takataka za viwanda na kinyesi cha binadamu majini kutasaidia. Njia nyingine ni kuondoa kutoka kwenye pwani vitu vyenye virutubisho vinavyochangia kuongezeka kwa dinoflagellates.
Kwa sasa, serikali fulani zinachunguza hali hiyo kwa uangalifu. Kwa mfano, nchini Ufilipino, shirika moja la kiserikali huchunguza chaza ili kuhakikisha kwamba hawatasababisha madhara wanapouzwa katika nchi hiyo na katika mataifa mengine. Hata hivyo, ni Muumba tu anayeweza kuondoa madhara yote yanayowapata wanadamu wakati maji yanapokuwa mekundu.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Ingawa huko Ufilipino maji mekundu yamesababisha watu wapooze, wataalamu fulani wanasema haijawa hivyo katika nchi zote ambazo zimekumbwa na maji hayo.
[Sanduku katika ukurasa wa 24]
Dalili za Madhara ya Sumu ya Maji Mekundu
1. Kuhisi mwasho au mchomo kwenye midomo, fizi, na ulimi
2. Hali ya kufa ganzi na mwasho wa uso, ambayo huenea kotekote mwilini
3. Kuumwa na kichwa na kizunguzungu
4. Kuhisi kiu sana na kutoa mate mengi
5. Kichefuchefu, kutapika, na kuendesha
6. Kutoweza kupumua, kuongea, na kumeza kwa urahisi
7. Maumivu ya maungo na kizunguzungu
8. Mpigo wa haraka wa moyo
9. Kulegea kwa misuli na kutokuwa na usawaziko wa maungo
10. Kupooza mwili
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Viumbe vinavyosababisha maji mekundu
“Pyrodinium bahamense”
“Gymnodinium catenatum”
“Gambierdiscus toxicus”
[Hisani]
Courtesy of Dr. Rhodora V. Azanza, University of the Philippines
Courtesy of Dr. Haruyoshi Takayama
ASEAN-Canada Cooperative Programme on Marine Science
[Picha katika ukurasa wa 25]
Athari za maji mekundu
[Hisani]
Grant Pitcher/Courtesy WHOI
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
Peter J. S. Franks, Scripps Institution of Oceanography
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Scripps Institution of Oceanography