Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Eneo Lenye Maua ya Pekee

Eneo Lenye Maua ya Pekee

Eneo Lenye Maua ya Pekee

Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Afrika Kusini

BAADA ya kuchunguza furushi la maua kutoka Afrika, mtaalamu wa mimea wa karne ya 18, Carolus Linnaeus alisema kwamba yalitoka katika ‘paradiso iliyo duniani, eneo la Cape of Good Hope. Muumba Mkarimu alirembesha eneo hilo kwa mimea maridadi ajabu.’

Mimea hiyo maridadi ajabu inakua kwenye eneo lililo kwenye ncha ya kusini ya Afrika. Walowezi Waholanzi waliiita mimea mingi iliyokuwa kwenye eneo hilo fijnbosch, yaani “vichaka maridadi” au “pori maridadi.” Neno fijn lamaanisha “-dogo,” kwa hiyo huenda hilo lilirejezea majani na mimea midogo na vilevile miti myembamba iliyomea kwenye eneo hilo. Muda si muda, neno fijnbosch likawa “fynbos.” Majani ya mimea katika eneo la fynbos yaweza kuwa madogo na magumu, lakini maua yake huwa na ukubwa, rangi, na maumbo mbalimbali yenye kupendeza.

Jimbo la Fynbos liko kwenye eneo ambalo ni tofauti sana na maeneo mengine yanayokuza maua ulimwenguni—Eneo la Maua la Cape of Good Hope. * Ijapokuwa eneo hilo si kubwa sana, lina jamii nyingi sana za mimea—kichapo kimoja chasema lina zaidi ya jamii 8,550. Theluthi mbili ya jamii hizo hazipatikani penginepo ulimwenguni.

Jamii 1,470 za mimea zimepatikana kwenye Mlima wa Table peke yake! Gazeti la New Scientist lasema kwamba “jamii hizo ni zaidi ya jamii zilizo kwenye Visiwa vyote vya Uingereza.” Jimbo la Fynbos pia limeathiri sehemu nyinginezo za ulimwengu. Jinsi gani?

Jamii Nyingi Sana za Maua

Iwapo una ua la jeraniamu nyumbani mwako, basi yaelekea unatunza ua la jamii ya mmea uliotoka jimbo la Fynbos. Zaidi ya theluthi mbili ya jamii 250 za maua yanayokua kiasili duniani yako katika jimbo la Fynbos.

Isitoshe, theluthi moja ya maua 1,800 ya jamii ya Iridaceae, pamoja na zaidi ya jamii 72 za maua ya mzambarausime yasiyopatikana sehemu nyinginezo ulimwenguni, hukua kwenye eneo hilo. Kuna jamii 1,646 za maua ya daisy na vygies katika ncha ya kusini ya Afrika. * Jamii hizo zinatia ndani maua yaitwayo everlasting, ambayo huwa maangavu sana na hutumiwa katika mapambo ya maua makavu yanayodumu kwa miaka mingi.

Hata hivyo, maua yenye kustaajabisha zaidi katika jimbo la Fynbos ni maua yaitwayo erica au heath. Amini usiamini, jimbo la Fynbos lina jamii 625 kati ya jamii 740 za maua ya erica zilizopo ulimwenguni pote!

Maua ya Sugar-Bush na Ndege wa Sugarbird

Linnaeus alichunguza kikundi kimoja cha maua ya Fynbos yenye maumbo mbalimbali ya ajabu. Aliyaita maua hayo Protea (maua ya jamii ya Proteaceae), jina la mungu wa Ugiriki Proteus. Iliaminika kwamba mungu huyo aliweza kubadili-badili mwili wake. Kwa ujumla, jamii 328 za maua ya proteas hukuzwa katika jimbo la Fynbos. Inasisimua kama nini kupanda milima ya Cape na kuona ghafula ua kubwa sana la protea! Nyakati nyingine ua hilo maridadi huwa kubwa kushinda uso wa mwanadamu.

Mmea mwingine wa kawaida wa jamii ya protea ni sugar-bush. Maua ya mmea huo yanafanana na vikombe, nayo huwa na mbochi nyingi sana. Walowezi wa kale walitikisa maua hayo ili kukusanya mbochi yake kwenye bakuli. Kisha walichemsha mbochi hiyo na kutengeneza umajimaji wa sukari.

Ndege aitwaye sugarbird—anayeishi tu kwenye jimbo la Fynbos, katika jiji la Cape—pia anapenda sana mbochi ya maua ya protea. Ndege huyo hufyonza mbochi ya mmea huo kwa mdomo wake mrefu na ulimi wake mrefu. Halafu anasaidia kuchavusha maua hayo kwa kubeba chavua kutoka kwenye ua moja hadi jingine. Isitoshe, ndege wa sugarbird hula wadudu wanaovutiwa na maua hayo makubwa. Kwa hiyo ndege huyo hutegemezana na ua hilo.

Uhusiano Mwingine Muhimu Sana

Maua fulani ya protea hutambaa ardhini na kufichwa na mimea mingine. Panya huvutiwa na harufu kama ya chachu inayotokezwa na maua hayo ya protea. Panya hao hutumbukiza vichwa vyao uani na kunywa mbochi kutoka kwa ua moja hadi jingine. Kisha manyoya yao ya uso hubeba chavua na kuihamisha kwa maua mengine. Ndivyo panya wa porini wanavyotegemeana na maua ya protea ili kuishi.

Vivyo hivyo, maua ya erica hutegemeana na ndege wa Fynbos aitwaye sunbird mwenye kidari chenye rangi ya machungwa. Mdomo wa ndege huyo unafaana kabisa na ua hilo kwa sababu ua hilo lina umbo la mabomba yaliyopindika. Ndege huyo anapotumbukiza mdomo wake uani ili kufyonza mbochi, kichwa chake hukusanya chavua. Kwa mwaka wote maua ya erica yanayochanua humwandalia chakula sunbird, na mimea hiyo hunufaika kutokana na uchavushaji wa ndege huyo. Inapendeza kama nini kutembea milimani na kuona ushirikiano huo wenye kustaajabisha!

Jimbo la Fynbos lina viumbe wengine muhimu sana. Kwa mfano, kipepeo anayeitwa Table Mountain beauty huchavusha jamii 15 za maua mekundu akiwa peke yake. Mojawapo ya maua hayo ni ua maarufu la disa, linaloremba Mlima wa Table.

Halafu kuna fuko fulani wanaokula mizizi yenye umbo la vitunguu ya mimea ya jamii ya okidi, yungiyungi, na iris. Fuko wa Cape husafirisha na kuhifadhi vipande vya mizizi kwenye mashimo yao. Visehemu vya mizizi hiyo huanguka njiani au kubaki mashimoni bila kuliwa, na mara nyingi vipande hivyo huota mizizi na kukua.

Mamia ya mimea ya Fynbos huwa na nyama yenye mafuta kwenye mbegu zake. Nyama hiyo husambaza harufu inayovutia chungu sana. Chungu hushika nyama hiyo na kuburuta mbegu hizo hadi ardhini. Kisha, chungu hula nyama hiyo laini na kuacha mbegu zilizokauka. Hivyo basi, mbegu zilizofukiwa ardhini zinaweza kuchipuka baadaye bila kuliwa na ndege wala panya.

Kisha kuna inzi wenye mrija mrefu wa mdomoni. Inzi hao ni wachavushaji stadi wa mimea ya Fynbos yenye maua yenye shingo ndefu. Inzi mmoja ana mrija wenye urefu wa sentimeta 8 hivi. Kwa kweli, ni lazima viumbe wa Fynbos wategemeane ili kuishi!

Uhusiano Usio Thabiti

Mwanamazingira T.F.J. van Rensburg asema katika kitabu An Introduction to Fynbos, kwamba “inasikitisha kuwa Mwanadamu, ambaye amepewa wajibu wa kutunza Uumbaji, mara nyingi anaharibu maeneo fulani ya asili.” Kwa kweli, uharibifu mkubwa umetukia katika muda mfupi tu, kama anavyoeleza Dakt. Piet van Wyk: “Miaka 300 hivi iliyopita tangu kuwapo kwa ukoloni, mbuga tambarare ya fynbos imegawanywa na kuharibiwa sana na mwanadamu hivi kwamba ni asilimia 31 tu ya mimea ya asili . . . ya fynbos ndiyo inayosalia. Tayari jamii 39 za mimea ya fynbos zimetoweka, ilhali jamii nyingine 1,033 zimekuwa adimu sana.”

Matendo ya mwanadamu yanatisha pia uhusiano muhimu uliopo baina ya wanyama na mimea ya Fynbos. Kitabu Table Mountain—A Natural Wonder kinasema kwamba “wataalamu wa viumbe na mimea wameanza tu kuelewa uhusiano muhimu uliopo kati ya wanyama na mimea katika jimbo la fynbos. Mmea unapotoweka, je, mchavushaji wake (mnyama-mgugunaji, vipepeo au mbawakavu) atatoweka pia?” Vipi kuhusu ndege wa Fynbos? Mwanabiolojia mmoja wa Afrika Kusini C. J. Skead, asema kwamba ndege wa sugarbird wamo hatarini kwa sababu ya “uhusiano wao wa karibu na mimea ya Protea.”

Ripoti hizo zenye kutisha kuhusu jimbo la Fynbos zinahangaisha. Hata hivyo, wale wanaomwamini “Muumba Mkarimu” kama Linnaeus, wanaweza kuwa na tumaini. Tunaweza kuwa na hakika kwamba Yehova Mungu atakapotimiza ahadi yake ya ‘kufanya vitu vyote kuwa vipya,’ dunia itasitawi na kuchanua maua kuliko wakati mwingine wowote.—Ufunuo 21:5.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Kuna maeneo sita yanayokuza maua ya pekee ulimwenguni. Wataalamu wa mimea hutambua maeneo hayo kwa sababu yana mimea ya pekee sana. Jimbo la Cape nchini Afrika Kusini ni mojawapo ya maeneo hayo sita.

^ fu. 9 Maua ya daisy ni ya jamii iitwayo Asteraceae, na maua ya vygies ni ya jamii ya Mesembryanthemum.

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Jimbo la Fynbos (lenye rangi ya kijani-kibichi)

Mlima wa Table

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Ua la “painted lady,” ni mojawapo ya jamii 72 za mzambarausime zisizopatikana penginepo duniani

[Hisani]

Una Coetzee (www.agulhasfynbos.co.za)

[Picha katika ukurasa wa 16]

Maua fulani ya “protea” ni makubwa kushinda uso wa mwanadamu

[Hisani]

Nigel Dennis

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mojawapo ya jamii nyingi za maua ya “daisy” yaliyo katika Fynbos

[Hisani]

Kirstenbosch, Cape Town

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ua la “Strawberry everlasting”

[Hisani]

Nigel Dennis

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kipepeo wa “Table Mountain beauty” ndiye pekee anayechavusha jamii 15 za maua mekundu

[Hisani]

Colin Paterson-Jones

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kwenye Mlima wa Table peke yake, jamii 1,470 za mimea zimerekodiwa

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ua la “Pincushion protea”

[Hisani]

National Parks Board of South Africa

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kuna uhusiano wa pekee kati ya maua ya “erica” na “sunbird”

[Hisani]

Colin Paterson-Jones

[Picha katika ukurasa wa 18]

Maua ya “protea” na ndege aitwaye “sugarbird” wa eneo la Cape wana uhusiano wa pekee

[Hisani]

Kirstenbosch, Cape Town

[Picha katika ukurasa wa 18]

Ua la “Watsonia”

[Picha katika ukurasa wa]

Kirstenbosch, Cape Town

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

National Parks Board of South Africa