Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mabomu ya Ardhini Yafafanuliwa Upya

Tayari nchi zaidi ya 135 zimetia sahihi Mkataba wa Ottawa uliopiga marufuku mabomu ya ardhini. Marekani imepangiwa kutia sahihi mwaka wa 2006. “Lakini kuna mwelekeo unaohangaisha wa kupenda vifaa vya kitekinolojia vinavyoundwa ili kubadili ufafanuzi wa bomu la ardhini lililopigwa marufuku,” lasema New Scientist. “Japani . . . yaamini kwamba vitu vinavyolipuka vinavyosambaa ufuoni si mabomu ya ardhini maadamu vinaendeshwa kutoka mbali. . . . Badala ya kuliita bomu la ardhini, linaitwa ‘kifaa kinachotupa na kusambaza.’” Kwa sasa, Marekani inatumia mabomu ya ardhini ili kulinda mabomu ya kuharibu vifaru. Kwa hiyo, Marekani inaunda mabomu ya kuharibu vifaru yanayoweza kuruka ili kuzuia majaribio ya kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini. Mabomu yanapoondolewa au kuharibiwa ili kufanyiza njia kwenye sehemu zilizotegwa, mabomu yaliyosalia “yatagundua kuwa kuna mabomu yasiyokuwepo na kuruka hadi yatakapojipanga kwa njia maalumu tena,” gazeti hilo laripoti. Mabomu hayo yanayojipanga upya ‘yatakuwa na kifaa kinachoongozwa kwa pistoni kwenye vitako vyao ambacho kitayarusha kwa zaidi ya meta 10 angani.’

Matarajio ya Muda wa Kuishi Yaongezeka

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa juu ya ustawi wa mwanadamu, matarajio ya muda wa kuishi katika Peru yaliongezeka kwa miaka 12.8 katika kipindi cha miaka 25 iliyopita. Matarajio ya muda wa kuishi kati ya mwaka wa 1970 na 1975 yalikuwa miaka 55.5, lakini kati ya mwaka wa 1995 na 2000 yaliongezeka na kuwa miaka 68.3. Gazeti la El Peruano lasema kuwa ongezeko hilo la matarajio ya muda wa kuishi limesababishwa na hali ya afya iliyoboreshwa. Hiyo pia imepunguza idadi ya vifo vya watoto waliotoka tu kuzaliwa kutoka vifo 115 kati ya watoto 1,000 hadi vifo 43 kati ya watoto 1,000, na vya watoto walio chini ya miaka mitano kutoka vifo 178 kati ya watoto 1,000 hadi vifo 54 kati ya watoto 1,000 katika kipindi hichohicho. Inakadiriwa kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, “asilimia 23 ya idadi ya watu wataishi kwa miaka 60,” lasema gazeti El Peruano.

Vitamini Yenye Manufaa

Tunapofanya kazi kwa kutumia kompyuta, macho yetu huathiriwa kwa miangaza inayotokea kwenye skrini, lasema gazeti la afya la Kipolishi la Zdrowie. Kadiri miangaza inavyokuwa mikali zaidi, ndivyo macho yetu yanavyotumia rodopsini zaidi. Rodopsini ni rangi inayoharibiwa na mwanga na hutuwezesha kuona. Vitamini A huchangia sana kufanyizwa kwa rodopsini. Kwa mujibu wa gazeti la Zdrowie, vyakula vyenye vitamini A vyatia ndani maini na mafuta ya chewa. Watu wanaohitaji kupunguza utumizi wa mafuta na kolesteroli wanaweza kula vyakula vyenye kemikali zenye rangi zinazoitwa beta-carotene, ambazo mwili hubadilisha kuwa vitamini A kwa kutumia mwangaza wa jua. Kemikali ya beta-carotene hupatikana kwenye mboga za manjano, za rangi ya manjano iliyoiva, za rangi nyekundu, na za kijani kibichi na matunda kama embe ulaya, pichi, plamu kavu, tikiti maji, na maembe.

Aksidenti Zinazosababishwa na Simu za Mkononi

Simu za mkononi hazisababishi aksidenti babarani tu. Maofisa wa stesheni za treni katika Japani husema kwamba abiria wanaosubiri mahala palipoinuka kando ya njia ya reli huongea sana kwa simu za mkononi na kusahau walipo. Kati ya aksidenti zilizoripotiwa na gazeti la Asahi Evening News kuna moja iliyohusisha kijana aliyekuwa akiegemea kwenye ncha ya mahala palipoinuka kando ya njia ya reli huku akizungumza kwa kutumia simu yake. Alipokuwa akimwinamia mtu aliyekuwa akizungumza naye bila kujua, kichwa chake kilikwaruzwa na treni iliyokuwa ikiingia. Jambo zuri ni kwamba ‘alikatwa tu juu ya jicho lake la kulia.’ Hata hivyo, katika kisa kingine, “mwanafunzi wa shule ya sekondari aliyekuwa akiongea kwa kutumia simu ya mkononi, aliegemea kwenye ncha ya mahala palipoinuka kando ya reli na akagongwa na kuuawa na treni ya kubeba mizigo.” Wafanyakazi wa stesheni za treni huripoti kuwa nyakati nyingine watu huangusha simu zao kwenye reli. Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 26 aliyeruka chini ili kuokota simu yake “alikufa kwa kupondwa” na treni. Maofisa wa stesheni za reli huwaomba watu “wakumbuke kwamba mahala palipoinuka kandokando ya reli ni sehemu hatari sana.”

Aksidenti za Ndege Zinazosababishwa na Mitazamo

Makala moja katika gazeti la Singapore la The Straits Times yataja mawasiliano kwenye chumba cha rubani kuwa mojawapo ya visababishi vya aksidenti za ndege. Ripoti hiyo yasema kuwa “katika Asia, mawasiliano kwenye chumba cha rubani kati ya rubani mkuu na rubani msaidizi huathiriwa sana na cheo. Rubani mkuu hawezi kupingwa, hivi kwamba rubani msaidizi anapotambua kasoro fulani huenda atasita kusema akiogopa kuwa atapinga mamlaka ya rubani mkuu.” Kwa mujibu wa gazeti hilo, watu wanaweza kutambua tatizo litakalotokea lakini wajizuie kusema “kwa sababu huenda watachukiwa.” Au huenda wakahisi kuwa uaminifu wao utatiliwa shaka kwa sababu ya “cheo chao.” Katika chumba cha rubani, rubani msaidizi asipotaka kusema waziwazi, hiyo yaweza kuongeza uwezekano wa kupata aksidenti.

Matumbawe Yako Hatarini Sana

Gazeti la The Economist lasema kwamba matumbawe katika Bahari ya Hindi kutoka Afrika Kusini hadi India yanakabili hatari kubwa sana. Hivi karibuni, wanabiolojia wa viumbe wa baharini walifanya ugunduzi wenye kushtua. Waligundua kwamba “asilimia 50 hadi 95 ya matumbawe baharini yamekufa katika muda wa miaka miwili iliyopita.” Sababu ni kwamba matumbawe hayo hayawezi kustahimili wakati halijoto baharini inapoongezeka kwa digrii 1 au 2 Selsiasi kwa zaidi ya majuma machache. Ripoti hiyo yasema, “katika 1998, kwa majuma kadhaa halijoto karibu na Seychelles ilikuwa digrii 3 Selsiasi zaidi ya halijoto ya kawaida.” Wachunguzi wanaamini kuwa hiyo huandaa “uthibitisho ulio wazi kwamba kuna ongezeko la joto ulimwenguni.” Katika miaka ya 1998 na 1999, Visiwa vya Maldive vilipoteza dola milioni 63 za Marekani kwa sababu ya kufa kwa matumbawe. Gazeti la The Economist lasema watalii wanaotarajia kuona matumbawe yanayopendeza “huondoka wakiwa wametamauka kwa kuona marundo ya vifusi visivyopendeza vya rangi ya kijivu.” Olof Linden, mhariri-mshiriki wa ripoti hiyo, alisema kuwa “sehemu kubwa ya mfumo wa ekolojia wa dunia umevurugwa.” Kwa kuwa viumbe wa baharini hukulia kwenye matumbawe, baa hilo linaonyesha kuwa wakazi wa maeneo ya pwani wanaotegemea uvuvi watapata matatizo.

Talaka ya Watu Waliostaafu

Katika Ufaransa “idadi ya wenzi wenye umri wa zaidi ya miaka 55 wanaotalikiana imeongezeka kwa asilimia 52 katika kipindi cha miaka minne,” laripoti gazeti la Le Figaro. Katika kipindi hichohicho, kiwango cha talaka za wenzi walio na zaidi ya umri wa miaka 70 kimeongezeka zaidi ya maradufu huku wanawake wengi zaidi wakiomba talaka. Kisababishi kimoja ni magumu ya kuzoea maisha baada ya kustaafu. Mara nyingi, matatizo yaliyotatuliwa kwa urahisi mwenzi mmoja alipokuwa kazini, hayavumiliki sasa wenzi wote wanapokuwa nyumbani. Kwa kuongezea, kuna ongezeko la idadi ya wanawake wenye umri wa miaka zaidi ya 50 wanaoweza kujitegemea kiuchumi. Tofauti na wanawake wa vizazi vilivyopita, wanawake hao wanaweza kuwataliki kwa urahisi waume wasio waaminifu. Ingawa mara nyingi wanaume waliostaafu hupata mwenzi aliye kijana, idadi inayoongezeka ya wanawake walio katika miaka ya 60 na 70 ambao si wajane hubaki peke yao.

Ukarimu wa Wafaransa

Wanawake ni wakarimu zaidi ya wanaume, na wazee ni wakarimu zaidi ya vijana. Hiyo ni mikataa miwili iliyofikiwa baada ya kura ya maoni ya mwaka mmoja iliyoagizwa na shirika la ufadhili liitwalo Fondation de France. Matokeo yaonyesha kuwa nusu ya idadi ya Wafaransa huwa wakarimu. Asilimia 28 ya Wafaransa hutoa zawadi mara kadhaa kwa mwaka, iwe ni pesa, muda, au kwa njia nyingine. Ripoti hiyo ilionyesha kwamba “kujihusisha katika dini na kuwa katika shirika fulani” huchangia ukarimu. Kwa kutumia uchunguzi huo, gazeti la Paris la Le Monde lilimfafanua mtu mchoyo kuwa kijana mseja mwanamume asiyekwenda kanisani, ambaye labda anaishi kwenye Pwani ya Mediterania au mashambani.

UKIMWI Waenea Sana

Katika mwaka wa 2000, zaidi ya watu milioni tano waliambukizwa virusi vya UKIMWI, yasema ripoti ya Programu ya Pamoja ya Shirika Linalopambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa (UNAIDS) na Shirika la Afya Ulimwenguni. Hiyo yafikisha idadi ya watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI kuwa zaidi ya milioni 36. Hiyo ni asilimia 50 zaidi ya makadirio yaliyofanywa mwaka wa 1991. Ugonjwa huo umeenea sana katika Ulaya Mashariki, ambako idadi ya watu walioambukizwa—hasa watumiaji wa dawa za kulevya kwa kujidunga sindano—karibu iongezeke maradufu katika mwaka mmoja. Ripoti hiyo pia yasema kuwa jitihada za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika nchi tajiri ulimwenguni zimesimama huku UKIMWI ukienea hasa miongoni mwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa kujidunga sindano na miongoni mwa wagoni-jinsia-moja. Kwa upande mwingine, idadi ya walioambukizwa katika eneo lililo kusini mwa jangwa la Sahara katika Afrika yaonekana imebaki hivyohivyo kwa mara ya kwanza, ambako kuna watu milioni 25.3 walioambukizwa. Tangu ugonjwa huo ulipotokea, zaidi ya watu milioni 21 wamekufa kutokana na ugonjwa huo.