Wimbo wa Mapenzi wa Nyenje
Wimbo wa Mapenzi wa Nyenje
HUKU akiwa na urefu wa milimeta 50 hivi, nyenje haonekani kuwa mdudu anayevutia. Hata hivyo, wimbo wa nyenje huwavutia mamilioni ya watu ulimwenguni. Mdudu huyo huimbaje, na kwa nini yeye huimba?
Kwa kupendeza, kati ya jamii 2,400 hivi za nyenje, ni nyenje wa kiume tu huimba au hulia. Badala ya kuimba kwa kutumia koo zao, nyenje wa kiume hutumia mabawa yao. Ensaiklopidia moja hueleza kwamba nyenje wa kiume hulia kwa kusugua sehemu moja ya bawa lao la mbele kwenye michomozo 50 hadi 250 iliyo kwenye bawa la mbele la upande ule mwingine. Frikwensi ya milio yao hutegemea idadi ya michomozo iliyosuguliwa kwa sekunde moja. Mitetemo husambaa na kutokeza wimbo wa kipekee wa nyenje.
Lakini nyenje wa kiume haimbi tu ili kuwatumbuiza wanadamu! La hasha! Nyenje wa kiume humwimbia nyenje wa kike. Kitabu Exploring the Secrets of Nature chaeleza hivi: “Katika harakati zake za kutafuta mwenzi, nyenje wa kiume, mwasiliani stadi, huimba nyimbo tatu tofauti: wa kujitangaza, wa kuvutia, na wa kuwafukuza nyenje wengine wa kiume.” Nyenje wengine huendelea kuimba ili kujitangaza hadi nyenje wa kike anapovutiwa. Nyenje wa kike anaposikia wimbo huo kupitia “masikio” yaliyo kwenye miguu yake ya mbele, haendelei kukaa mbali. Anapokaribia mahala ambapo mlio huo unatoka, nyenje wa kiume huanza kuimba kwa kuendelea na kutetemesha sauti yake. Huo ndio wimbo wa mapenzi. Wimbo huo wa mapenzi, humvutia nyenje wa kike kwa mpenzi wake. Kisha nyenje hao hujamiiana.
Katika Asia Mashariki, watu wengine hufuga nyenje wa kiume kwa sababu wao huburudishwa na wimbo wao. Wengine hufurahia kusikiliza muziki wa nyenje kwenye makao yao ya asili. Popote uimbwapo, wimbo wa nyenje huwafurahisha wanadamu ulimwenguni kote naye humletea Mbuni wake sifa.