Mbona Watu Hutumia Dawa za Kulevya?
Mbona Watu Hutumia Dawa za Kulevya?
“NILIPOKUWA na umri wa miaka 13, dada ya rafiki yangu mkubwa alitualika nyumbani kwao jioni moja. Kila mtu akaanza kuvuta bangi. Mwanzoni, nilikataa, lakini mwishowe nilionja baada ya kusihiwa mara kadhaa nijaribu.” Hivyo ndivyo, Michael, kutoka Afrika Kusini alivyosimulia jinsi alivyoanza kutumia dawa za kulevya.
“Familia yetu ilizingatia mno desturi za kale. Tulipenda kucheza muziki bora wa kale. Nilikuwa mshiriki wa bendi moja ya muziki, na mwanamuziki fulani alizoea kuvuta bangi wakati wa mapumziko. Alinisihi sana kwa miezi mingi nijaribu kuvuta bangi. Hatimaye, nilijaribu halafu nikaanza kuivuta kwa ukawaida.” Hivyo ndivyo Darren, mkazi wa Kanada, alivyoanza kutumia dawa za kulevya.
Watu hao wawili walianza kutumia dawa nyingine za kulevya, kama vile LSD, kasumba, na dawa zinazochochea utendaji wa mwili. Waliacha kutumia dawa hizo, lakini wanapokumbuka mambo yaliyotukia, wanakubali kwamba walianza kutumia dawa za kulevya kwa sababu ya msongo wa marafiki. Michael asema hivi: “Sikudhani kamwe kwamba ningeanza kutumia dawa za kulevya, lakini sikuwa na marafiki wengine ila hao, na ni jambo la kawaida tu kwa mtu kuiga marafiki wake.”
Vitumbuizo
Msongo wa marafiki ni mojawapo ya sababu zinazowafanya wengi waanze kutumia dawa za kulevya, hasa vijana. Isitoshe, wanaiga watumbuizaji ambao huvutia mashabiki wao wachanga na kuathiri maoni na mwenendo wao.
Dawa za kulevya hutumiwa sana katika vitumbuizo. Mara nyingi wanamuziki maarufu hutumia dawa kali za kulevya pindi fulani-fulani. Waigizaji wengi maarufu wa sinema ni waraibu wa dawa za kulevya.
Watumbuizaji wanaweza kutukuza na kusifu sana dawa za kulevya kiasi cha kwamba vijana wanashawishiwa kuzitumia. Gazeti la Newsweek liliripoti hivi mnamo mwaka wa 1996: “Barabara za Seattle zimejaa vijana wanaokuja kutumia heroini, eti kwa sababu Cobain [mwimbaji wa muziki wa roki] alitumia heroini.”
Utumizi wa dawa za kulevya unatukuzwa na magazeti, sinema, na televisheni. Wabuni maarufu wa mitindo ya mavazi hupendelea wanamitindo walio wembamba, na dhaifu kama waraibu wa dawa za kulevya.
Kwa Nini Watu Fulani Huanza Kutumia Dawa za Kulevya?
Kuna sababu nyingi zinazochangia ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya. Baadhi ya sababu hizo ni kutamauka sana, kushuka moyo, na kukosa kusudi maishani. Matatizo ya kifedha, ukosefu wa kazi, na mifano mibaya ya wazazi huchangia pia tatizo hilo.
Watu fulani wanaoshindwa kushughulika na wengine hutumia dawa za kulevya ili kukabiliana na hali hiyo. Wanaamini kwamba dawa za kulevya huwasaidia kuwa na ujasiri, zinawafanya wawe wacheshi na wahisi wanapendwa. Wengine huona ni rahisi kutumia dawa za kulevya badala ya kujifunza jinsi ya kukabiliana na maisha.
Pia vijana hutumia dawa za kulevya kwa sababu hawana la kufanya. Kitabu The Romance of Risk—Why Teenagers Do the Things They Do chasema hivi kuhusu kutokuwa na la kufanya na kutopata mwelekezo wa wazazi: “Wavulana na wasichana wanaporejea kutoka shuleni hawamkuti yeyote nyumbani. Ndiyo sababu wanahisi upweke na hawataki kuwa peke yao. Wanatembelewa na marafiki lakini bado wanahisi uchoshi wakiwa pamoja. Wanatazama televisheni na video za muziki kwa muda mrefu au kutafuta mambo yenye kusisimua kwenye Internet. Muda si muda, huenda
wakaanza kuvuta sigareti, kutumia dawa za kulevya na kunywa pombe.”Michael, aliyetajwa awali, alisema kuwa yeye hakupata mwelekezo wa wazazi wake nyumbani: “Familia yetu ilikuwa na furaha. Tulikuwa na uhusiano wa karibu sana. Hata hivyo, wazazi wangu walifanya kazi ya kuajiriwa na sikuwaona mchana kutwa. Isitoshe, wazazi wetu walitupatia uhuru mkubwa sana. Hawakutuadhibu. Wazazi wangu hawakujua kamwe kwamba nilikuwa nikitumia dawa za kulevya.”
Mara tu baada ya kuanza kutumia dawa za kulevya, vijana wengi huendelea kuzitumia kwa sababu moja tu: Wanafurahia kufanya hivyo. Michael, aliyetumia dawa za kulevya kila siku, alitaja athari zake: “Nilipumbaa akili. Niliweza kusahau mikazo yoyote niliyokuwa nayo. Sikuhofu kamwe. Hali ilionekana kuwa sawa kabisa.”
Dick, mwenyeji wa Afrika Kusini, aliyetumia dawa za kulevya awali asema jinsi bangi ilivyomwathiri tangu alipoanza kuivuta akiwa na umri wa miaka 13: “Nilicheka ovyoovyo. Kila jambo lilinichekesha.”
Yaonekana vijana hata hawatishwi na maonyo yanayotolewa kuhusu madhara ya dawa za kulevya. Wao hudhani kwamba ‘hawawezi kupatwa na madhara hayo.’ Kitabu Talking With Your Teenager chaeleza kwa nini vijana hupuuza maonyo kuhusu madhara ya dawa za kulevya kwa afya: “Wana afya nzuri na nguvu nyingi hivi kwamba wanafikiri afya yao haiwezi kuathiriwa. Kwa kawaida vijana wengi wanaobalehe hudhani kwamba hawawezi ‘kuumizwa.’ Matineja huona kansa ya mapafu, ulevi, uraibu wa dawa kali za kulevya, kuwa mambo yanayowapata watu wenye umri mkubwa, na hayawezi kuwapata.” Kwa kweli wengi hawajui hatari zilizopo, kama inavyothibitishwa na idadi inayoongezeka ya vijana wanaotumia dawa ya kulevya iitwayo ecstasy. Ecstasy ni nini?
Dawa ya Kulevya ya Ecstasy na Dansi za Usiku Kucha
Dawa ya kulevya ya MDMA inayotokana na kemikali ya amphetamine, hutumiwa sana kwenye tafrija za dansi za usiku kucha zinazoitwa kwa Kiingereza rave. Dawa hiyo huitwa ecstasy. Wauzaji wa dawa hiyo husema kwamba dawa ya kulevya ya ecstasy ni salama na humsisimua mtu na kumtia nguvu zaidi ili acheze dansi usiku kucha. Dawa hiyo huwasaidia wachezaji-dansi waendelee kucheza dansi kwa saa nyingi sana hadi wanapofikia ile hali iliyotajwa na mwandishi mmoja kuwa ‘hali ya kupumbaa kiakili’ au kuwa hoi kabisa. Kijana mmoja alisema kile kinachofanya ecstasy ivutie: ‘Msisimuko huanza miguuni, moyo wako hupiga-piga kasi, halijoto ya mwili wako hupanda na msukumo wa damu kuongezeka.’
Uchunguzi wa ubongo wa watumiaji wa ecstasy umethibitisha kwamba dawa hiyo ni hatari sana tofauti na madai ya wauzaji.
Kwa wazi, ecstasy huharibu nyuzi za neva ubongoni na kupunguza vipimo vya homoni ya serotonin. Yaelekea madhara hayo ni ya kudumu. Baada ya muda, hilo laweza kusababisha matatizo kama vile kushuka moyo na kuzorota kwa kumbukumbu. Imeripotiwa kwamba baadhi ya watumiaji wa ecstasy wamekufa. Na walanguzi kadhaa wa dawa za kulevya huchanganya ecstasy na heroini ili kuwafanya wateja wao wawe waraibu.Je, Ni Rahisi Kupata Dawa za Kulevya?
Bei ya dawa za kulevya imeshuka katika nchi nyingi kwa sababu idadi ya wauzaji imeongezeka. Mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi yamechangia hali hiyo. Mfano mmoja ni nchi ya Afrika Kusini. Mabadiliko ya kisiasa nchini humo yameboresha biashara na mawasiliano kati yake na nchi nyingine. Mbali na hayo, kutokuwapo kwa sheria kali za kuzuia watu kuvuka mipaka kumesitawisha biashara ya dawa za kulevya. Maelfu ya watu hutegemea ulanguzi haramu wa dawa za kulevya ili kupata riziki kwa sababu ya ukosefu mkubwa wa kazi ya kuajiriwa. Kwa kawaida uhalifu wenye jeuri unahusiana sana na biashara ya dawa za kulevya. Gazeti moja liliripoti kwamba watoto wa shule katika jimbo la Gauteng, Afrika Kusini—baadhi yao wakiwa na umri wa miaka 13 tu—wanapelelezwa na polisi kwa sababu ya kuhusika na biashara ya dawa za kulevya. Shule kadhaa katika jimbo hilo zimekuwa zikiwapima wanafunzi kuona iwapo wanatumia dawa za kulevya.
Ni Nini Kiini cha Tatizo Hilo?
Bila shaka kuna sababu nyingi zinazowafanya watu watumie dawa za kulevya. Lakini sababu hizo zote ni dalili tu za kiini cha tatizo hilo. Mwandishi Ben Whitaker alitaja kiini hicho aliposema hivi: “Kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya leo ni ishara hatari ya kwamba jamii yetu ina kasoro, licha ya kwamba watu ni wapweke na wamevunjika moyo. Ikiwa hilo si kweli, kwa nini watu wengi wenye vipawa na fursa nzuri maishani watumie dawa za kulevya badala ya kukabiliana na maisha ya leo?”
Hilo ni swali lenye kuchochea fikira sana, linalotusaidia tuelewe kwamba jamii yetu inayokazia mno ufuatiaji wa mali na umashuhuri, imeshindwa kutimiza mahitaji yetu ya kihisia-moyo na ya kiroho. Hata dini nyingi hazijafaulu kutimiza mahitaji hayo kwa sababu zimepuuza kiini cha matatizo ya wanadamu.
Ni lazima tutambue na kukabiliana na kiini kabla hatujapata suluhisho la kudumu kwa tatizo la dawa za kulevya. Habari hiyo itazungumziwa kwenye makala inayofuata.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Nyakati nyingine watu mashuhuri hutukuza matumizi ya dawa za kulevya
[Picha katika ukurasa wa 7]
Muziki wa kisasa unakazia sana matumizi ya dawa za kulevya
[Picha katika ukurasa wa 8]
Dawa ya kulevya ya “ecstasy” hupatikana sana kwenye dansi za usiku kucha
[Hisani]
AP Photo/Greg Smith
Gerald Nino/U.S. Customs