Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Wasalimika Kiajabu
Ijapokuwa misitu ya Ufaransa iliharibiwa vibaya sana na dhoruba katika Desemba 1999, uchunguzi uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kwamba wanyama wakubwa hawakuumia kama ilivyokuwa imetarajiwa, laripoti gazeti la Le Monde la Paris. Mizoga ya wanyama 20 tu—paa-dume 10, kulungu 5, na nguruwe-pori 5—ilipatikana kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 25,000 katika misitu iliyoharibiwa, mashariki mwa Ufaransa. Wanyama hao walisalimika kwa kutumia “mbinu zisizojulikana,” labda kwa kujificha chini ya miti iliyoanguka au kwa kukusanyika pamoja mahala pasipokuwa na miti. Jean-Paul Widmer wa Ofisi ya Misitu ya Kitaifa ya Ufaransa asema hivi: ‘Twajua mambo mengi kuhusu [tabia] za simba na wanyama-pori wengine wanaokaa mbali kuliko tujuavyo kuhusu paa-dume na nguruwe-pori.’
Ugonjwa wa Abiria wa Daraja la Kawaida la Ndege
Katika kipindi cha miaka minane iliyopita, abiria 25 waliowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Narita huko Japani “walikufa kwa sababu ya ugonjwa unaoitwa eti ugonjwa wa abiria wanaosafiri kwenye daraja la kawaida la ndege,” laripoti gazeti la The Daily Yomiuri. Abiria wanaosafiri kwenye daraja la kwanza wanaweza kupata ugonjwa huo pia. Kuketi kwa saa kadhaa kwaweza kuzuia mzunguko wa damu miguuni na kusababisha damu kuganda. Damu iliyoganda ikiingia mapafuni, yaweza kusababisha matatizo ya kupumua na hata kifo. Kila mwaka, kati ya wasafiri 100 na 150 wanaowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Narita huathiriwa kwa njia fulani na tatizo hilo, asema Toshiro Makino, msimamizi wa zahanati ya Shule ya Kitiba ya Nippon iliyo kwenye Uwanja Mpya wa Ndege wa Kimataifa wa Tokyo. Yeye adokeza mambo haya: “Abiria wanaosafiri kwa ndege kwa saa saba au nane mfululizo wapaswa kunywa maji mengi kuliko kawaida na kuepuka hali hiyo kwa kukunja na kukunjua miguu yao.”
Halijoto ya Tokyo Yaongezeka
Gazeti la The Daily Yomiuri laripoti kwamba “kwa wastani, idadi ya siku za mwaka ambazo halijoto katika Tokyo ilikuwa chini ya kiwango cha mgando ilipungua kwa asilimia 95 katika karne ya 20.” Kwa wastani, katika miaka ya 1990, halijoto katika Tokyo ilikuwa chini ya kiwango cha mgando kwa siku 3.2 kwa mwaka tofauti na siku 61.7 kwa mwaka katika miaka kumi ya kwanza ya karne hiyo. Mtaalamu mmoja wa hali ya hewa kwenye Shirika la Hali ya Hewa la Japani alisema kwamba ongezeko la joto la dunia limefanya halijoto isipungue kama ilivyokuwa awali, na akaeleza wasiwasi wake kuwa siku moja Tokyo haitakuwa na “majira ya baridi kali sana.” Kwa mujibu wa shirika hilo, iwapo joto litaongezeka kama ilivyo sasa, inatabiriwa kwamba halijoto ulimwenguni pote itaongezeka kwa digrii 1.0 hadi digrii 3.5 Selsiasi katika karne ya 21. Ongezeko la digrii 3.5 Selsiasi katika Japani litafanya jiji la Tokyo liwe na joto kama la Nairobi.
Ugonjwa wa Kaswende Umeibuka Tena
Ugonjwa wa kaswende ulikuwa ni kama umetokomea kabisa nchini Ufaransa kwa miongo mingi. Hata hivyo, mwaka jana madaktari waligundua ugonjwa huo unaoambukizwa kingono ukienea hasa miongoni mwa wagoni-jinsia moja, laripoti gazeti la Ufaransa la Le Figaro. Katika mwaka wa 2000, ugonjwa huo wa kaswende ulitokea pia huko Uingereza na Ireland. Kaswende ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria na hufanyiza vidonda na upele ngozini na usipotibiwa unaweza kudhuru mfumo wa neva na mishipa ya damu ya moyo. Kutokea tena kwa ugonjwa wa kaswende kunahangaisha kwani “madaktari waliohitimu karibuni hawaujui kwa kuwa hawakuuchunguza kamwe katika mafunzo yao ya kitiba,” lasema gazeti la Le Figaro. Basi, huenda madaktari wakautibu kama ugonjwa mwingine na kutoa matibabu yasiyofaa. Wataalamu wa magonjwa wanashuku mazoea hatari ya ngono kuwa kisababishi cha kutokea tena kwa kaswende. Hivyo, wanahofu kwamba huenda hilo linaonyesha kwamba “ugonjwa wa UKIMWI utaenea sana.”
Onyo kwa Watalii Wazee
Idadi ya wazee wanaosafiri kwenye nchi zinazositawi ulimwenguni inaongezeka, na wengi huwa wagonjwa kwa sababu ya kula chakula au kunywa maji yenye bakteria, lasema jarida la Tufts University Health & Nutrition Letter. Mambo hayo husababisha ‘watalii kuharisha’ ambako kwaweza kusababisha matatizo mabaya sana ya kiafya kwa watu wenye umri wa miaka 60 au zaidi. Isipokuwa uwe unakula kwenye hoteli au mkahawa wa hali ya juu kwenye jiji kubwa la kisasa, jarida hilo la Health & Nutrition Letter laonya hivi:
□ Usinywe maji ya mfereji wala usiyatumie kupiga meno mswaki. Tumia tu maji yanayouzwa kwa chupa, yaliyochemshwa, au yaliyosafishwa. Usitie barafu ndani ya vinywaji isipokuwa iwe imetengenezwa kwa maji safi.
□ Usile samaki wala nyama isipokuwa iwe imepikwa vizuri kabisa.
□ Usile vyakula vilivyotengenezwa kwa maziwa yasiyoondolewa vijidudu au mboga ambazo hazijapikwa.
□ Usile matunda isipokuwa wewe mwenyewe uyamenye baada ya kuyaosha kwa maji safi. Baada ya kuyamenya, nawa mikono kabla ya kula.
□ Usile vyakula vinavyouzwa barabarani, hata ikiwa vinauzwa vikiwa moto.
Wengi Wanakimbilia Sehemu Nyingine za Nchi Yao
“Idadi yao ni sawa na ile ya watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI, ni maradufu ya idadi ya wakimbizi. Jumuiya ya kimataifa ya kuandaa msaada huwataja kuwa ‘watu wanaokimbilia sehemu nyingine za nchi yao,’” laripoti gazeti la The Independent la London. Ingawa wanalazimika kutoroka nyumbani kwa sababu ya vita, wao hubaki katika nchi zao. Shirika la UM lakadiria kwamba kuna watu milioni 25 hadi milioni 30 wasio na makao ulimwenguni pote. Wengi huishi pamoja na familia nyingine au barabarani, wala si katika kambi za wakimbizi. Dennis McNamara, msimamizi maalum wa UM wa kushughulikia tatizo hilo, asema kwamba badala ya kukimbilia nchi nyingine, “wengi hujaribu kukaa karibu iwezekanavyo na kwao: mashamba yao yako huko.” Nyakati nyingine, mashirika ya kuandaa msaada hayaruhusiwi kuwafikia watu hao. Asilimia 90 ya watu hao ni wanawake na watoto. “Ni wanaume wanaopigana vitani,” aongeza McNamara. “Wanawake na watoto ndio wanaoathiriwa. Wanawake wakimbizi wanakabili hatari ya kubakwa na majeshi yanayowanyanyasa.”
Ulimi Ulio Kama Mpira Unaofyonza
Kinyonga huwanasaje mijusi wengine na hata ndege walio na uzito wa asilimia 10 ya uzito wake? Kwa muda mrefu, iliaminika kuwa viumbe hao walikuwa wakikwama kwenye ulimi unaokwaruza na unaonata wa kinyonga. Lakini hilo halikueleza jinsi kiumbe huyo anavyowanasa viumbe wazito. Ili kuchunguza hilo, wanasayansi huko Antwerp, Ubelgiji, walirekodi video zinazoonyesha namna ulimi wa kinyonga husonga haraka sana anaponasa viumbe, laripoti shirika la habari za sayansi la Ujerumani la Bild der Wissenschaft-Online. Wanasayansi hao waligundua kwamba kinyonga anapouchomoa ulimi wake, ulimi huo hufanyiza mpira kwenye ncha yake. Kabla ya kulenga, misuli miwili kwenye ulimi hukazika kisha ncha ya ulimi huwa kama mpira wa kufyonza unaonata mawindo.
Jangwa Linaloenea
‘Jangwa la Sahara limeenea kufikia nchi zilizo kaskazini mwa Mediterania huku udongo unaokosa rutuba na badiliko la halihewa likigeuza sehemu fulani zilizo kusini mwa Ulaya kuwa jangwa,’ laripoti gazeti The Guardian la London. Kwenye mkutano mmoja wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na kuenea kwa majangwa, uliofanywa Desemba 2000, mtaalamu mmoja alisema kwamba uuzaji wa mazao ulimwenguni pote unahusika kwa kuwa umewazuia wakulima wanaofanya kilimo cha kiwango kidogo wasiuze mazao yao. Basi, wakulima huacha mashamba yaliyokuwa yamelimwa na kumwagiliwa maji kwa miaka mingi, na hatimaye udongo hubebwa na maji ya mvua. Hali hiyo imezidi kusini mwa Italia, Hispania, na Ugiriki. Bulgaria, Hungaria, Rumania, Moldova, Urusi, na China zinakabili pia kuenea kwa majangwa. Klaus Töpfer, msimamizi mkuu wa Programu ya Mazingira ya UM, alisema hivi: “Udongo ni mali-asili ya maana kwa mwanadamu na kwa mazingira kama vile maji safi na hewa safi.”
Chimbuko la Mto Amazon Latambuliwa
Kikosi cha wachunguzi 22 kimegundua “chimbuko la mto mkubwa zaidi ulimwenguni, na kukomesha makisio na habari za muda mrefu zinazotiliwa shaka,” laripoti gazeti The Times la London. Mto Amazon huanza kama kijito kwenye kilele kinachoitwa Nevado Mismi, kusini mwa Mlima Andes huko Peru. Kilele hicho kina urefu wa meta 5,000. Kutoka hapo, mto huo hujipinda kupitia bonde lenye nyasi na kuvu-mwani ambapo unaungana na vijito na mito mingine kabla ya kutiririka tena kwa kilometa 6,000 hadi kwenye Bahari ya Atlantiki. Andrew Pietowski, kiongozi wa kikosi hicho, alisema hivi kuhusu chimbuko hilo: “Ni sehemu inayopendeza. Unasimama kwenye bonde lenye mimea ya kijani-kibichi, chini ya jabali kubwa jeusi hivi lenye kuvutia lililo na urefu wa meta 40. Kumenyamaza sana na kuna utulivu.”