Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Familia za Korea Zilizoungana Je, Huo Ni Mwanzo Mpya?

Familia za Korea Zilizoungana Je, Huo Ni Mwanzo Mpya?

Familia za Korea Zilizoungana Je, Huo Ni Mwanzo Mpya?

Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Korea

TUKIO hilo lilikuwa lenye kusisimua. Waandishi 1,300 kutoka Korea na waandishi 400 kutoka nchi za kigeni waliwasili ili watoe ripoti juu ya tukio hilo. Katika pindi hiyo, familia mbalimbali kutoka sehemu za kaskazini mwa Korea na kusini mwa Korea ambazo zimetenganishwa kwa miaka 50 hivi ziliungana tena.

Kwa muda wa miaka 50, Wakorea wengi hawakuwa wamewasiliana na watu wa ukoo—wala kupitia barua, faksi, wala simu. Eneo linalogawanya nchi hiyo, ambamo utendaji wa kijeshi hauruhusiwi, limetenganisha familia mbalimbali. Ni nini kilichowawezesha kuungana? *

Muungano Wenye Maana Zaidi

Ndege moja yenye bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea ilitua kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Kimpo wa Jamhuri ya Korea Agosti 15, 2000. Ndege hiyo ilibeba watu wa kaskazini mwa Korea ambao walikuwa wamepata uthibitisho kupitia shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu kwamba bado baadhi ya watu wa ukoo wao walikuwa hai huko kusini mwa Korea. Baadaye ndege iyo hiyo ilisafirisha Wakorea 100 kutoka kusini mwa Korea hadi kaskazini mwa Korea na kuwapa fursa ya kukutana na watu wao wa ukoo. Wazia jinsi ambavyo ungehisi kama ungekuwa na ndugu, dada, mama, baba, mwana, au binti, au mwenzi wa ndoa ambaye hujamwona kwa muda wa miaka 50! Wengi waliokuja ili waungane na familia zao walikuwa katika miaka yao ya 60 na 70, na hawakuwa wamewaona watu wao wa ukoo tangu walipokuwa vijana!

Ziara hizo zilipangwa ziendelee kwa muda wa siku nne tu, na baadaye wote wangerudi kwenye nchi zao. Bila shaka ndiyo sababu wengi walioungana na watu wa familia yao waliongea mfululizo karibu muda huo wote! Madaktari na wauguzi walikuwapo na pia magari ya kubeba wagonjwa, kwa sababu ya uwezekano wa wengine kuvurugika akili na kushtuka. Si ajabu kwamba magari hayo na pia huduma za madaktari zilihitajika.

Wale walioungana walikuwa wachache tu kati ya watu wote ambao wametenganishwa na familia zao. Inakadiriwa kwamba bado kuna watu 690,000 wenye umri wa zaidi ya miaka 60 na watu 260,000 wenye umri wa zaidi ya miaka 70, ambao wametenganishwa na wapendwa wao. Hata hivyo, kati ya watu 76,000 wa Jamhuri ya Korea waliotimiza matakwa fulani na kupeleka ombi la kutembelea watu wao wa ukoo huko kaskazini mwa Korea, watu 100 tu ndio waliochaguliwa.

Yang Jin-yeul, aliye na umri wa miaka 82 alikuwa mmoja wao. Alipata habari kupitia Msalaba Mwekundu kwamba Yang Won-yeul, ndugu yake mwenye umri wa miaka 70 huko kaskazini mwa Korea, alikuwa anawatafuta watu wake wa ukoo wanaoishi kule kusini mwa Korea. Ndugu huyo mdogo wa Yang Jin-yeul alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Seoul katika mwaka wa 1950 alipopotea wakati wa Vita ya Korea. Hakuna habari yoyote kutoka kwake tangu wakati huo. Wote wawili pamoja na dada zao wawili waliungana baada ya kutenganishwa kwa miaka 50!

Lee Pok-yon, aliye na umri wa miaka 73, aliungana na mke wake mwenye umri wa miaka 70, na wana wawili. Mmoja wa wana wake alikuwa na umri wa miaka mitano na yule mwingine miaka miwili tu alipowaona mara ya mwisho. Wakati wa vita alitoka nyumbani siku moja kwa kusudi la kwenda kununua baiskeli. Akapotea na watu wa familia yake hawakuwa wamepata habari yoyote kutoka kwake tangu siku hiyo. Kwenye muungano wao wenye kufurahisha hatimaye mke wake, aliye na ugonjwa wa kupooza na vilevile ugonjwa wa sukari, aliweza kuuliza swali alilokuwa amejiuliza kwa miaka mingi: Kwa nini ilichukua muda mrefu hivi kununua hiyo baiskeli?

Lee Chong-pil, aliye na umri wa miaka 69, alikuwa mwanafunzi wa shule ya msingi alipotenganishwa na familia yake katika mwaka wa 1950, akaorodheshwa miongoni mwa watu waliopotea. Aliungana na Cho Won-ho, mama yake mwenye umri wa miaka 99, ndugu zake wawili, na dada zake wawili kutoka kusini mwa Korea. Kwa kusikitisha, mama yake mzee hakumtambua.

Watu hao ni wachache tu kati ya wale waliofurahia sana kuungana na watu wao wa ukoo. Tukio hilo lilionyeshwa moja kwa moja kwenye vipindi kadhaa vya televisheni ya Korea na katika nchi za ng’ambo. Watazamaji walitokwa na machozi ya furaha walipoangalia vipindi hivyo! Wengi walijiuliza ikiwa sasa wengi zaidi wangepata fursa ya kuungana na watu wao wa ukoo. Hata hivyo, siku hizo zilipita haraka, na watu hao walihisi uchungu kuachana kama vile walivyohisi walipotenganishwa awali. Wapendwa hao hawakujua ikiwa wangepata fursa ya kuonana tena, au ni wakati gani wangeweza kufanya hivyo.

Je, Kutengana kwa Miaka 50 Kwakaribia Kwisha?

Korea ilipata uhuru kutokana na ukandamizaji wa miaka 36 wa utawala wa Wajapani Agosti 15, 1945. Hata hivyo, Korea ilielekea kugawanyika kwa sababu ya siasa ya siku hizo. Wajapani walipofukuzwa kutoka katika rasi ya Korea, jeshi la Marekani lilitwaa eneo la kusini na jeshi la Sovieti likatwaa eneo la kaskazini la nchi hiyo. Vita iliyozuka baada ya muda mfupi haikusuluhisha tatizo hilo. Sasa kulikuwa na serikali mbili nchini Korea. Kuanzia mwaka wa 1945 na kuendelea na kwa muda wote wa Vita ya Korea, maelfu ya watu walitenganishwa na familia zao. Vita ilipokwisha hatimaye, mwaka wa 1953, sasa nchi hiyo iligawanywa kati kwa eneo ambalo utendaji wa kijeshi hauruhusiwi lililojaa mabomu ya ardhini.

Kwa miaka mingi, hakukuwa na dalili zozote za kuungana. Hata hivyo, Juni 13, 2000, ndege iliyobeba rais wa Jamhuri ya Korea, Kim Dae-jung, ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Sunan, jijini Pyongyang. Mkuu wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, Kim Jong-il, alimngojea hapo ili amsalimu. Kukawa na tumaini bila kutazamiwa. Viongozi hao wawili hawakuwa wamekutana mbeleni. Lakini katika pindi hiyo walitenda kana kwamba walikuwa ndugu ambao hawajaonana kwa muda mrefu. Katika mkutano mkuu wa siku tatu uliofuata viongozi hao wawili waliahidi kujitahidi kukomesha chuki ambayo imeendelea kwa muda wa miaka 50 na kujaribu kufikia upatano. Kuungana kwa familia zilizotenganishwa kulikuwa matokeo ya kwanza-kwanza ya mkutano huo. Punde, mambo mengine yalifuata.

Viongozi hao wawili walikubaliana kuunganisha tena reli kati ya kaskazini mwa Korea na kusini mwa Korea. Reli hiyo ina urefu wa kilometa 12 upande wa Korea Kusini na kilometa 8 upande wa kaskazini mwa Korea nayo itarekebishwa kufikia mwezi wa Septemba 2001. Itavuka lile eneo linalogawanya kaskazini mwa Korea na kusini mwa Korea, na kuunganisha tena sehemu hizo mbili za Korea. Na reli hiyo, inayoanzia Korea, itapita China na kuendelea hadi Ulaya itakapounganishwa hatimaye na reli ya Trans Chinese Railroad. Rais Kim Dae-jung alisema kwamba hiyo itakuwa ‘barabara mpya ya kuunganisha China na Ulaya.’ Baadaye reli nyingine itapita katikati ya eneo linalogawanya Korea nayo itaunganishwa na reli ya Urusi ya Trans-Siberian Railroad.

Haijulikani bado ikiwa matokeo hayo ni dalili za mwanzo mpya. Kwa sasa, jitihada za kuunganisha familia zapaswa kusifiwa. Hata hivyo, ni wazi kwamba wanadamu wanahitaji utawala wa ulimwenguni pote wa Ufalme wa Mungu. (Mathayo 6:9, 10) Mashahidi wa Yehova walianza kueneza ujumbe huo wenye tumaini huko Mashariki mwaka wa 1912. Wengi huko kaskazini mwa Korea walipata kuusikia na watu kadhaa waliukubali. Hata hivyo, wengi wao walifungwa gerezani wakati wa utawala wa Wajapani kwa sababu walikataa kwenda vitani.

Baada ya mwisho wa Vita ya Pili ya Ulimwengu, Wakristo hao walio Mashahidi wa Yehova waliachiliwa, na wakaanza kukutanika pamoja. Wengi wao walihamia kusini mwa Korea ambako waliweza kuabudu kwa uhuru. Kutaniko la kwanza huko Seoul lilianzishwa Juni 1949, na Mashahidi watendaji wameongezeka hivi kwamba leo kuna Mashahidi zaidi ya 87,000 huko Jamhuri ya Korea. Miongoni mwao pia kuna maelfu ambao wametenganishwa na watu wao wa ukoo huko kaskazini mwa Korea.

Huenda ikawa hali itabadilika ili familia zote zilizotenganishwa huko Korea ziweze kuungana tena. La maana zaidi, ikiwa kugawanyika huko kwaweza kukomeshwa huenda wale wakazi milioni 22 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea watapata fursa ya kusikia ujumbe wa Biblia.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Kulikuwa na mpango wa kuunganisha familia mwaka wa 1985 vilevile.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Mume na mke (juu) na mama na mwana (chini) wanaungana

[Picha katika ukurasa wa 14]

Mwanamume anamwabudu mzazi akiinama mbele ya picha ya babake, aliyekufa kabla hawajaungana

[Picha katika ukurasa wa 15]

Yang Jin-yeul (kushoto kabisa), ameungana na ndugu yake (katikati) kutoka Korea Kaskazini

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

Picha kwenye ukurasa wa 13-15: The Korea Press Photojournalists Association