Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kongoti Ndege Anayeeleweka Vibaya

Kongoti Ndege Anayeeleweka Vibaya

Kongoti Ndege Anayeeleweka Vibaya

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KENYA

‘Sijawahi kumwona ndege anayeashiria mabaya zaidi ya kongoti.’ The World’s Wild Places —Africa’s Rift Valley.

KATI ya ndege wengi wanaopatikana Afrika, ni wachache tu ambao wamechambuliwa vikali kama kongoti. Kwa kawaida ndege huyo husemwa kuwa mkatili, mwenye sura mbaya, na kwamba yeye huleta mabaya. Kwa wazi, kongoti hapendwi.

Je, wewe huvutiwa na ndege maridadi na wenye sauti tamu? La, kongoti hana sifa hizo. Kwa kuwa ana kichwa na shingo la rangi ya waridi lisilo na manyoya, ndege huyo huonekana kuwa mwenye huzuni na mnyonge. Kongoti waliokomaa huwa na kifuko chekundu kinachoning’inia kwenye koo zao. Kifuko hicho chaweza kufura kinapojazwa hewa nacho hufanana na tai kubwa. Watu wengi huonelea kwamba kifuko hicho hakimrembeshi kiumbe huyo kwa vyovyote. Hata hivyo, Dakt. Leon Benun, mkuu wa Idara ya Maarifa ya Ndege kwenye Majumba ya Ukumbusho ya Kitaifa ya Kenya, atukumbusha hivi: “Ikiwa kifuko hicho hakituvutii haimaanishi kwamba kongoti havutiwi nacho.” Hata hivyo, kufikia sasa, hakuna ajuaye kazi ya kifuko hicho mwilini mwake.

Pia, ulaji wa ndege huyo haupendezi. Sababu moja ni kwamba yeye hula mizoga. Mizoga isipopatikana, yeye huwaua ndege wengine ili kutosheleza hamu yake nyingi ya kula. Si ajabu kwamba watu wengi humchukia sana.

Hata hivyo, japo sura na tabia za kongoti hazivutii, ana sifa nzuri zenye kupendeza. Jiunge nasi tunapojifunza zaidi kuhusu ndege huyo aliyepachikwa sifa nyingi mbaya.

Jitu Kati ya Ndege

Yamkini kongoti ndiye ndege mkubwa zaidi katika jamii ya korongo. Kongoti wa kiume aliyekomaa anaweza kuwa na kimo cha sentimeta 150 na uzito wa zaidi ya kilogramu nane. Kongoti wa kike ni wadogo kidogo. Mdomo wake mzito wenye umbo la kabari, waweza kukua kufikia urefu wa zaidi ya sentimeta 30. Mdomo wake ni chombo chenye nguvu cha kunyafua nyama kutoka kwenye mizoga.

Japo korongo huyu ni mkubwa sana, yeye ni mrukaji stadi. Akiwa na mabawa yenye upana wa meta 2.5 kutoka ncha hadi ncha, kongoti anaweza kuruka kama ndege wengine stadi. Yeye huruka kwa madaha, akiwa amerudisha kichwa chake ndani kidogo mabegani na kunyosha miguu yake mirefu nyuma ya mwili wake. Kongoti anajua kutumia mikondo ya hewa yenye joto, na anaweza kuruka juu sana hivi kwamba nyakati nyingine huwezi kumwona kutoka chini! Naam, kongoti wameonekana wakiruka juu kufikia kimo cha meta 4,000!

Wazazi Wanaotegemeka

Hata hivyo, jambo lenye kupendeza hasa ni jinsi kongoti anavyotimiza daraka lake kama mzazi. Kuwa mzazi ni kazi ngumu inayoanza kwa kujenga kiota. Baada ya kuchagua sehemu inayofaa, kongoti wa kiume huanza ujenzi. Baadaye yeye huungwa mkono na kongoti wa kike. Kiota, ambacho nyakati nyingine hujengwa meta 30 juu ya ardhi, hakina madoido. Kiota hicho chenye upana wa meta moja ni jengo sahili lililoinuliwa ambalo hujengwa kwa vijiti vikavu, matawi, na majani. Kwa kweli, nyakati nyingine ndege anayetaga aweza kuingia ndani ya kiota kilichojengwa zamani na kukiboresha kwa kuongeza matawi na vifaa vingine. Aina fulani za kongoti zinajulikana kwa kudumisha kiota kwa miaka 50.

Ujenzi wa kiota unapoendelea, kongoti wa kiume huanza kutafuta mwenzi. Tofauti na jamii nyingi za ndege, kongoti wa kiume husubiri kongoti wa kike amfikie. Kongoti kadhaa wa kike hujitokeza wakiwa na matumaini ya kumvutia kongoti wa kiume. Mara nyingi wanakataliwa. Lakini mvumilivu hula mbivu, na mwishowe kongoti mmoja wa kike hukubaliwa. Wanapochumbiana, ndege wa kiume na wa kike hutoa sauti za kuwafukuza ndege wengine huku vifuko vyao vya shingoni vikiwa vimefura kabisa. Sauti hizo zimefafanuliwa kuwa kama mlio wa ng’ombe, mlio wa mbwa mwoga, na mbinja. Hizo ndizo sauti za kongoti zinazojulikana, ijapokuwa mara kwa mara wao hutoa sauti kwa kugonganisha midomo yao mikubwa. Urafiki mkubwa husitawi, na huimarishwa kwa salamu ya kawaida inayoitwa eti salamu ya “juu-chini.” Wao husalimiana hivyo wakati mwenzi aliyekuwa ameondoka anaporudi kwenye kiota. Salamu hiyo huhusisha kurudisha kichwa nyuma, kuinamisha kichwa, na kisha kugonganisha midomo kwa muda mrefu.

Wenzi hao wawili humaliza kujenga kiota pamoja. Wote wawili watashiriki kuyaatamia mayai. Baada ya kuyaatamia mayai kwa mwezi mmoja, mayai mawili au matatu meupe yataanguliwa na kutokeza vifaranga wadogo wa rangi ya waridi wenye manyoya machache, ambao watashughulikiwa sana na wazazi wote wawili. Kongoti hao wachanga hutunzwa vizuri sana. Wao huanza kulishwa sana vyakula vyenye lishe bora vinavyotia ndani samaki. Kwenye maeneo yenye umajimaji ambapo kongoti huenda mara nyingi, wazazi hupata vyura wengi. Ndege huyo hula vyura sana. Vifaranga hula vipande vya vyakula ambavyo wazazi wao hutapika kwenye kiota. Vifaranga hao hukua polepole. Wao huanza kujitegemea baada ya miezi minne, wakati ambapo wanaweza kuruka nje ya kiota.

Wao Husafisha

Ingawa kongoti ameshutumiwa mara nyingi kwa kula mizoga, yeye huandaa huduma bora. Wanyama wawindaji huacha mizoga inayooza ikitapakaa kwenye nyanda za Afrika. Mizoga hiyo isipoondolewa, yaweza kueneza ugonjwa kwa urahisi na kuwadhuru wanadamu na wanyama. Hata hivyo, kongoti huandaa huduma bora ya kuzoa takataka. Wao pamoja na tumbusi huruka juu ya nyanda wakitafuta mizoga ya wanyama waliouawa. Tumbusi ni ndege wanaokula mizoga nao hula sana. Wanapopata mzoga, kongoti husubiri tumbusi wenye nguvu waupasue mzoga kwa midomo yao yenye nguvu iliyojipinda. Fursa inapotokea, kongoti huurukia huo mzoga upesi akiwa ameutayarisha mdomo wake mrefu kama kisu cha upasuaji, na kukamata kipande cha nyama. Kisha yeye hurudi kando na kungojea fursa nyingine. Tumbusi wanaposhiba, kongoti hupigania minofu iliyosalia. Kongoti hula kila kitu, ila tu mifupa. Wao humeza vipande vya nyama vyenye uzito wa gramu 600 kwa urahisi sana.

Katika miaka ya karibuni, kongoti amekuwa akisafisha maeneo mengine mbali na makao yake ya asili. Ndege huyo haogopi tena wanadamu na mara nyingi yeye huenda kwenye takataka za majiji na vijiji. Matokeo huwa nini? Mazingira huwa safi zaidi. Kongoti hata huchakura-chakura takataka za machinjioni akitafuta vipande vidogo vya nyama vilivyosalia. Mfano ufuatao waonyesha jinsi ndege huyo alivyo sugu. Kongoti mmoja alikuwa akichakura-chakura vyakula vilivyosalia penye machinjio huko magharibi mwa Kenya. Katika harakati hizo, alimeza kisu cha bucha. Siku chache baadaye, kisu hicho kilipatikana palepale kikiwa safi na kimeng’ara huku kongoti aliyekitapika akiendelea na shughuli zake kama kawaida, salama salimini!

Wakati Ujao wa Kongoti

Huku idadi ya korongo wenzake wa Asia inapopungua, kongoti wa Afrika wanaongezeka. Hana maadui katika makao yake ya asili. Zamani, mwanadamu alikuwa adui mkuu wa kongoti. Korongo huyo mkubwa alikuwa akifyatuliwa risasi, na manyoya yake laini ya nyuma yalitumiwa kurembesha kofia za wanawake. Kitabu Storks, Ibises and Spoonbills of the World chasema hivi: “Haiaminiki kwamba manyoya laini na maridadi kama hayo, yanayorembesha feni au kitu chochote kinachopendwa sana na mwanamke, yametoka kwa ndege huyo mkubwa mla-mizoga, aliyekonda sana na asiyevutia.” Ni jambo zuri kwamba, uharibifu huo umepungua kadiri miaka inavyopita, na idadi ya ndege hao inaongezeka. Hapana shaka kwamba uchunguzi wetu mfupi wa kongoti umefunua kwamba hastahili kamwe kudharauliwa wala kupachikwa sifa mbaya. Uhodari wake na bidii yake ya kusafisha mazingira hutunufaisha sana. Ingawa yeye si ndege maridadi sana, bado yeye humletea Muumba wake sifa kwa njia fulani.—Zaburi 148:7, 10.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mdomo wake mzito wenye umbo la kabari, waweza kukua kufikia urefu wa zaidi ya sentimeta 30

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kongoti ana mabawa yenye upana wa meta 2.5 kutoka ncha hadi ncha

[Hisani]

© Joe McDonald

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kongoti wachanga hutunzwa vizuri sana

[Hisani]

© M.P. Kahl/VIREO

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kazi ya kifuko cha kongoti mwilini mwake haijulikani bado

[Picha katika ukurasa wa 19]

Nyakati nyingine kiota hujengwa meta 40 juu ya ardhi