Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Misiba Mingi Mwaka wa 2000

Kulingana na kampuni ya bima iitwayo Munich Re, misiba mingi ya maumbile ilikumba dunia katika mwaka wa 2000 kuliko mwaka wowote mwingine. Zaidi ya misiba 850 iliripotiwa. Watu 10,000 walikufa kutokana nayo, na ilisababisha hasara ya zaidi ya dola bilioni 30 za Marekani. Hata hivyo, ijapokuwa idadi ya misiba iliongezeka, hasara ya kifedha ilikuwa ndogo na watu wachache walikufa mwaka huo kuliko mwaka uliotangulia. Hiyo ni kwa sababu misiba mingi ilikumba maeneo yasiyo na watu wengi, kampuni hiyo inasema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari. Asilimia 73 za hasara zilisababishwa na dhoruba, na asilimia 23 zilisababishwa na gharika. Ripoti hiyo yasema kwamba “bila shaka hasara zinazosababishwa na misiba ya kimaumbile zitaendelea kuongezeka wakati ujao,” kwa kuwa idadi ya watu na thamani ya mali huzidi kuongezeka.

Bahasha Zinazoonyesha Kilichomo Ndani

Gazeti la New Scientist laripoti kwamba kampuni moja ya Marekani imetengeneza dawa ya kupuliza ambayo “hufanya bahasha zisizofunguliwa ziweze kuonekana kilichomo ndani,” bila kuacha alama yoyote. Bob Schlagel, ambaye ni msemaji kwa niaba ya kampuni hiyo, anasema kwamba dawa hiyo ya kupuliza “ni umajimaji ambao hauna sumu, haudhuru mazingira, na haupitishi chochote,” nayo inatumika kwa kufanya bahasha za rangi zote zionyeshe kilichomo. Schlagel anaongeza kusema kwamba mbali na harufu inayosikika kwa dakika 10 au 15 hivi “dawa hiyo haiharibu maandishi ya bahasha au barua, haiachi alama ya maji, wala alama nyinginezo zozote.” Dawa hiyo ilivumbuliwa ili kuyasaidia mashirika kama ya polisi, kugundua makombora yanayotiwa katika barua na vilevile vifurushi vingine hatari. Hata hivyo, dawa hiyo inaweza kutumiwa pia ili kusoma barua zisizofunguliwa, kwa hiyo ofisa mmoja anayetetea haki za binadamu anasema kwamba dawa hiyo haifai kiadili.

Safari za Nyuki

Uwezo wa nyuki kusafiri kutoka mzinga wao hadi maua na kurudi mzingani unajulikana wazi. Lakini makundi ya nyuki wanaohama kutoka Assam, katika sehemu ya kaskazini mwa India, wanasafiri mamia ya kilometa, na kurudi, si kwenye mti uleule tu bali pia kwenye tawi lilelile ambapo nyuki wenzao walijenga tundu miaka miwili mapema! Jambo ambalo linashangaza ni kwamba nyuki-kibarua anaishi tu kwa muda usiozidi miezi mitatu. Kwa hiyo, nyuki wanaorudi si nyuki waliojenga tundu la awali, kwa kuwa vizazi vingi vya nyuki vimepita tangu tundu hilo lijengwe. Haijulikani jinsi wanavyojua njia ya kurudi. Gazeti la The Sydney Morning Herald laripoti kwamba huenda wakatumia uwezo wa kunusa. Au huenda ikawa nyuki-malkia aliyekuwapo awali anawaelekezea nyuki-wapelelezi njia ya kusafiri kwa kucheza dansi.

Lugha na Ubongo

Gazeti la Science News laripoti kwamba sehemu mbili za ubongo zinazotumiwa na watu wanaosikia na kuongea lugha fulani zinatumiwa pia na viziwi wanapotumia lugha ya ishara. Ripoti hiyo inasema kwamba uchunguzi wa ubongo unaonyesha kwamba “sehemu hizo zenye neva hufanya kazi wakati viziwi wanapoongea kwa kutumia lugha ya ishara.” Kulingana na Laura-Ann Petitto wa Chuo Kikuu cha McGill huko Montreal, aliyesimamia uchunguzi huo, matokeo hayo yanaonyesha kwamba sehemu hizo za ubongo huongoza “mambo ya msingi ya lugha mtu anaposema na pia anapotumia lugha ya ishara.” Uchunguzi zaidi unahitajika ili kuelewa uwezo wa ubongo wa mwanadamu wa kuelewa lugha. Gazeti hilo la Science News lasema hivi: “Sehemu kubwa za ubongo zinazohusika mtu anaposema hutumika vilevile mtu anapotumia lugha ya ishara.”

Ukahaba Waanza Kukubalika?

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linaripoti kwamba mahakama ya Ujerumani imeamua kwamba ukahaba “si jambo ovu,” mradi mtu hajalazimishwa kuutenda. Mahakama ya utawala ya Berlin iliamua kwamba mkahawa mmoja huko Berlin-Wilmersdorf unaweza kuendelea kuendesha shughuli zake, ijapokuwa makahaba wanatafuta wateja wao humo na baadaye kukodi vyumba katika eneo hilo. Mahakimu walisema kwamba uamuzi wao ulionyesha maoni yaliyobadilika ya watu juu ya ukahaba. Uchunguzi uliohusisha watu 1,002 ulionyesha kwamba asilimia 62 ya watu hao walihisi kwamba ukahaba unapaswa kuonwa kuwa kazi ya kawaida. Kulingana na mahakimu, uchunguzi mwingine ulionyesha kwamba wengi wa wale walioulizwa walihisi kwamba “ukahaba umekuwa njia ya kujiruzuku” huko Ujerumani kwa muda mrefu.

Usingizi na Kumbukumbu

Gazeti The Independent la London lasema kwamba watafiti wanaochunguza usingizi wamegundua kwamba kulala mapema na kupata usingizi vya kutosha, “ni kwa lazima mtu akitaka kukumbuka yale atakayojifunza katika majuma yanayofuata.” Profesa Robert Stickgold wa Shule ya Tiba ya Harvard alichunguza watu 24 waliojitolea. Nusu kati yao waliruhusiwa kulala usiku baada ya kujifunza somo fulani, huku wale wengine walikaa macho usiku kucha. Kisha wote waliruhusiwa kulala usingizi kama kawaida siku mbili zilizofuata ili wale wasiolala wasiwe wachovu sana. Jaribio la kumbukumbu lilionyesha kwamba wale waliolala usiku wa kwanza “walikuwa na matokeo mazuri zaidi katika jaribio hilo, huku wale wasiolala usiku wa kwanza hawakufanya maendeleo yoyote, japo waliweza kulala vizuri baadaye.” Inaonekana kwamba usingizi husaidia kuimarisha kumbukumbu, kwa hiyo matokeo ya uchunguzi huo yanaonyesha kwamba ni heri kulala usingizi mapema kuliko kusoma usiku kucha.

Madhara ya Chernobyl

Gazeti la The Independent la London lasema hivi: “Mimea inayokua karibu na mtambo wa nyuklia ulioharibika huko Chernobyl nchini Ukrainia ina mabadiliko katika chembe za urithi mara sita zaidi kuliko mimea mingine.” Watafiti wa Uswisi, Uingereza, na Ukrainia walipanda ngano katika mashamba mawili—shamba moja lilikuwa na ardhi iliyochafuliwa kwa mnururisho wa Chernobyl na lile lingine lilikuwa kwa umbali wa kilometa 30 lenye ardhi sawa lakini isiyochafuliwa. Kisha walitumia mbegu za mazao hayo na kuzipanda tena katika mashamba yale mawili. Ijapokuwa kiwango cha mnururisho kwenye shamba lililoko karibu na mtambo kilikuwa chini, bado ngano kwenye shamba hilo ilikuwa na mabadiliko mengi katika chembe zake za urithi. Wanasayansi wenye wasiwasi wanasema kwamba athari za mnururisho huo kwa wale wanaoishi katika sehemu hizo hazijulikani kwa wakati huu. Matokeo hayo yanasababisha wasiwasi juu ya vizazi vya siku zijazo vya mimea, wanyama, na wanadamu vitakavyoathiriwa na mnururisho wa Chernobyl.

Wanaume Hawasikilizi Sawa na Wanawake

Shirika la habari la Discovery.com News laripoti kwamba watafiti wamegundua kwamba wanawake hutumia pande zote mbili za ubongo wanaposikiliza, lakini wanaume hutumia upande mmoja tu. Katika uchunguzi mmoja, ubongo wa wanaume 20 na wanawake 20 ulichunguzwa waliposikiliza kitabu kilichosomwa kwenye utepe uliorekodiwa. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba wanaume wanasikiliza hasa na sehemu ya kushoto ya ubongo inayohusishwa hasa na kusikiliza na kusema. Wanawake kwa upande mwingine walisikiliza na pande zote mbili za ubongo. Dakt. Joseph T. Lurito, aliye profesa msaidizi wa tiba ya mnururisho kwenye Shule ya Chuo Kikuu ya Tiba huko Indiana, anasema hivi: “Uchunguzi wetu huonyesha kwamba wanaume hawasikilizi sawa na wanawake, hata hivyo haimaanishi kwamba uwezo wa kusikiliza ni tofauti.” Uchunguzi mbalimbali huonyesha pia kwamba wanawake “wanaweza kusikiliza mazungumzo mawili kwa wakati mmoja,” Dakt. Lurito asema.

Kubuni Dini Yako Mwenyewe

Dini si muhimu tena kwa Wafaransa. Uamuzi huo ulifikiwa na uchunguzi uliogharimiwa na gazeti la Katoliki la habari La Vie. Walipoombwa kuchagua kati ya mambo muhimu 14 kwenye orodha fulani, asilimia 7 pekee za waliohusika katika uchunguzi huo walichagua “mambo ya kiroho,” kuwa jambo muhimu kwao. Yaliyotangulizwa mbele ya mambo ya kiroho yalitia ndani mambo kama wakati wa kustarehe, mafanikio kazini, uhuru wa binafsi, sanaa, ngono, na mafanikio ya kifedha. Kulingana na Pierre Bréchon na Gérard Mermet, wanaochunguza jamii na jumuiya, uchunguzi huo unaonyesha kwamba kila mtu anataka kufanya dini imfae yeye mwenyewe. Kwa njia gani? Watu “huchanganya” itikadi mbalimbali wakichagua “zile ambazo zinalingana na maisha yao na maoni yao,” Bréchon anasema.

Je, Kile Kinachoitwa Mauaji ya Huruma Yahalalishwe?

Gazeti la NRC Handelsblad la Rotterdam laripoti kwamba, Uholanzi ikawa nchi ya kwanza kuhalalisha mauaji ya huruma mwezi wa Aprili mwaka uliopita. Bunge la Uholanzi lilipitisha pendekezo la kuhalalisha mauaji ya huruma kwa kura 46 dhidi ya 28. Sheria hiyo inaruhusu madaktari kusaidia wagonjwa wenye ugonjwa usiotibika au wenye maumivu yasiyoweza kupunguzwa na yasiyovumilika wajiue. Kulingana na wanasheria wa Uholanzi wagonjwa wanaotaka kujiua lazima watimize matakwa fulani makali: Lazima mgonjwa mwenyewe awe ameomba jambo hilo kwa hiari. Lazima daktari na mgonjwa wakubaliane kwamba hakuna suluhisho lingine ambalo mgonjwa aweza kukubali. Lazima angalau daktari mmoja mwingine amchunguze mgonjwa. Lazima mauaji hayo ya huruma yafanywe kwa njia inayokubalika na sayansi ya tiba.