Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Pambano Langu na Ugonjwa wa Mfumo wa Kinga

Pambano Langu na Ugonjwa wa Mfumo wa Kinga

Pambano Langu na Ugonjwa wa Mfumo wa Kinga

KAMA ILIVYOSIMULIWA NA MARC HOLLAND

MIAKA mitano iliyopita familia yangu ilikuwa na shughuli nyingi katika huduma ya Kikristo. Maisha yalikuwa mazuri.

Kisha, Aprili 1996, mimi na mke wangu, Lisa, tukashikwa na mafua. Lisa alianza kupona polepole, lakini mimi sikupata nafuu. Homa yangu ya mafua ilisababisha ugonjwa wa nimonia (mchochota wa mapafu), ulioendelea kwa muda wa majuma kumi. Baadaye mikono yangu na nyayo zangu zilianza kuuma na kufura. Nilipotembea ilikuwa kana kwamba nilitembea juu ya mawe. Miezi michache mapema tu nilikuwa na afya nzuri sana—nilikuwa na umri wa miaka 45 na uzito wangu ulikuwa kilogramu 75. Matokeo yote ya uchunguzi wa afya wa kila mwaka yalikuwa mazuri. Sasa madaktari walitatanishwa na dalili zangu. Maumivu ya viungo na misuli yangu yalizidi, na kufikia mwezi wa Julai ngozi yangu ilianza kuwa ngumu. Nilisikia baridi sikuzote, na sikuweza kuvumilia kukaa karibu na chombo cha kupooza hewa.

Mara moja tulianza kufanya utafiti ili kujua ni ugonjwa gani ambao una dalili hizo zisizo za kawaida. Daktari wa familia yangu alipanga nimwone mtaalamu wa magonjwa ya yabisi baridi Julai 1996. Nilisikia baridi sana nilipongoja katika ofisi ya daktari, na alipoingia mikono na nyayo zangu zilikuwa zimebadilika rangi kabisa. Baada ya kunichunguza, daktari aliniambia matokeo yenye kushusha moyo. Nilikuwa na ugonjwa wa mfumo wa kinga wa mwili wa diffuse scleroderma (SD).—Soma sanduku “Scleroderma—Mwili Unapojishambulia Wenyewe.”

Daktari alieleza kwamba ugonjwa huo hauna tiba na kwamba unaweza kusababisha kifo. Ugonjwa huo husababisha maumivu makali kama vile magonjwa mengine ya mfumo wa kinga kama lupus na yabisi baridi. Huenda watu wengine hawaelewi matatizo ya yule mgonjwa kwa sababu dalili nyingine za ugonjwa huu hazionekani kwa macho—kama vile maumivu na uchovu.

Magumu Mapya

Sikuzote familia yangu ilishirikiana katika utumishi wa Yehova. Kwa mfano, tulikuwa tumehamia mahali palipokuwa na uhitaji mkubwa wa walimu wa Biblia. Tulikuwa tumekuwa na fursa yenye kufurahisha ya kujitolea kufanya kazi kwenye ujenzi mbalimbali wa Majumba ya Ufalme huku Marekani na nchi za ng’ambo. Hata tulikuwa tumeshiriki katika kazi ya kutoa misaada wakati wa dharura katika nchi ya kigeni. Kabla tu ya kushikwa na mafua, tulikuwa tumepanga kuhamia Mexico ili tusaidie vikundi vya Kiingereza vya Mashahidi wa Yehova na pia kusaidia katika kazi ya ujenzi. Sasa ilielekea kwamba maisha yetu ya utumishi yangebadilika sana.

Kuanzia wakati huo, ilimbidi Lisa kufanya maamuzi muhimu na kushughulikia madaraka mazito. Nyakati nyingine alilemewa na hali iliyobadilika haraka sana hivi kwamba aliweza tu kumwambia Yehova, “Tusaidie kufanya maamuzi yenye hekima leo.”

Kile kinachosababisha ugonjwa wa SD hakijulikani, na ugonjwa wenyewe hauna tiba. Badala yake, dawa hutumiwa kutuliza dalili zake. Uchunguzi mbalimbali ulionyesha kwamba mapafu yangu yalifanya kazi kwa asilimia 60 na baadaye asilimia 40 tu. Mapafu yangu yalizidi kuwa magumu, na madaktari walipendekeza tiba ya kemikali ili kupunguza utendaji wa mfumo wa kinga au kuukomesha kabisa. Matibabu hayo yangefanya niwe mgonjwa hata zaidi, na ijapokuwa yamkini yangezuia ugonjwa kwa muda mfupi, hakuna uhakika kwamba ningepata nafuu ya kudumu. Tuliamua kukataa matibabu hayo, kwa kuwa sikutaka kuzidisha ugonjwa wangu. Familia yangu walipanga mazishi yangu kwa mara ya kwanza wakati huo, na walipata kufanya hivyo mara nne nilipokuwa mgonjwa sana.

Athari Mbalimbali za Ugonjwa wa SD

Baadhi ya madaktari walisema kwamba hawakuwa wameona kisa kibaya kama changu mbeleni. Ugonjwa wangu ulizidi kuwa mbaya hivi kwamba mwishoni mwa Septemba 1996, ngozi yangu ilikuwa imekuwa ngumu kuanzia kichwa changu, kiwiliwili chote, hadi katikati ya mapaja, na kuanzia nyayo hadi nyuma ya magoti. Nilipoinua kidevu changu nilihisi jinsi ngozi kwenye mapaja yangu ilivyosogea. Nilizidi kukonda, na maumivu yalikuwa makali sana. Wakati huo madaktari walisema kwamba singeweza kuishi zaidi ya mwaka mmoja.

Wakati ulipita polepole sana. Baada ya miezi sita tangu nishikwe na mafua, nilikuwa nimekuwa mlemavu aliyelala kitandani kwa muda wa saa 24 kwa siku. Nilikuwa nimepoteza karibu thuluthi moja ya uzito wangu. Sikuweza kujivalisha mavazi. Nilikata tamaa kwa sababu sikuweza kujilisha kwa njia inayofaa, niliangusha chakula kingi kwenye nguo na kitandani. Mikono yangu ilianza kujikunja kana kwamba nilikuwa nikishikilia mpira mdogo, na sikuweza kukunja viwiko vyangu. Kumeza kulianza kunitatiza, kwa sababu umio langu lilizidi kukosa unyumbufu. Nilihitaji mtu kunisaidia kuoga na vilevile nilipokwenda chooni. Maumivu yalikuwa makali na ya daima. Nililala sana, nyakati nyingine nililala kwa muda wa saa 18 hadi 20 kila siku.

Lisa alipofanya utafiti juu ya ugonjwa wa SD alisoma juu ya uchunguzi mmoja ambao katika huo viuavijasumu vilitumiwa kutibu ugonjwa huu. * Tuliwasiliana na wagonjwa wengi ambao walikuwa wametibiwa kwa njia hiyo, nao waliona kwamba matibabu hayo yaliwasaidia. Tulinakili habari zote ambazo tulipata na tukampelekea daktari wangu, na kumwomba azisome. Daktari alihisi kwamba matibabu hayo hayangeweza kunidhuru kwa hiyo aliagiza nitumie viuavijasumu hivyo. Vilinisaidia kwa muda.

Sikupuuza Utendaji wa Kiroho

Nilijitahidi kuhudhuria mikutano ya Kikristo. Ili niweze kuhudhuria mikutano tulinunua gari kubwa zaidi, kwa sababu sikuweza kuinama ili niingie katika gari la kawaida. Mara nyingi nilikuwa nikibeba bakuli kwa sababu safari ya gari ilifanya nipatwe na kichefuchefu. Nilibeba pia mablanketi na mablanketi yanayopashwa moto kwa umeme ili nijikinge na baridi. Ili nitoe hotuba zangu, niliburutwa jukwaani na kuwekwa katika kiti, kwa sababu sikuweza kusogeza miguu yangu.

Sikuweza kushiriki tena katika kazi ya kuhubiri nyumba hadi nyumba—kazi ambayo nilipenda sana ambayo nilikuwa nimeitanguliza maishani mwangu. Hata hivyo, niliweza kuwahubiria wauguzi na madaktari. Niliweza pia kuwapigia simu watu ambao walikuwa wamejifunza Biblia mbeleni. Nilishuka moyo wakati utendaji wetu wote katika utumishi wa Mungu ulipokuwa karibu kukoma. Hatukuweza kwenda katika huduma ya nyumba hadi nyumba pamoja na mwana wetu Ryan katika pindi hiyo, kwa kuwa mke wangu alihitaji kuniangalia wakati wote. Hata hivyo, baadhi ya mapainia, waeneza-Injili wa wakati wote, katika kutaniko letu walijitolea kutusaidia na jambo hilo.

Hata hivyo, nilipopata nafuu kidogo, tulianza kufikiria zaidi huduma yetu ya Kikristo. Tuliuza nyumba yetu na kuhamia karibu na binti yetu Traci na mume wake, Seth, ili waweze kutusaidia na mambo mbalimbali na pia kututia moyo.

Mtendaji Nijapokuwa Mlemavu

Sikuweza tena kufanya kazi ya kuajiriwa kwa kuwa ama nililazwa kitandani ama nilikaa katika kiti cha magurudumu. Hata hivyo, ndugu katika kutaniko letu jipya walinipa madaraka fulani. Nilikubali kwa furaha kazi ya kupanga wasemaji kwa ajili ya hotuba ya watu wote kwenye Jumba la Ufalme. Hatua kwa hatua niliweza kusaidia kazi nyingine pia katika kutaniko letu. Ijapokuwa nimepata nafuu kidogo na sina matatizo sana ya kutembea, bado nina tatizo la kusimama. Kwa hiyo, ninatoa hotuba zangu nikiwa nimeketi.

Tuliombwa kusaidia na miradi ya kujenga Majumba ya Ufalme kwa kuwa tulikuwa tumezoea kazi ya ujenzi. Kwa hiyo, mimi na Lisa tunasaidia kununua bidhaa kwa ajili ya miradi hiyo. Ninafanya kazi hiyo nikiwa kitandani. Kazi hiyo hufanya mimi na Lisa tuwe wenye shughuli zenye kufurahisha kwa muda wa saa chache kila siku.

Mwana wetu, Ryan, amesaidia sana kunitunza, ijapokuwa alikuwa na umri wa miaka 13 tu nilipoanza kuugua ugonjwa huu. Nimefurahishwa sana kuona jinsi amekuwa mtu wa kiroho. Muda mfupi baada ya kuhamia kutaniko jipya, alianza kutumikia kama painia.

Kutia Moyo Wengine

Tumejifunza mengi juu ya jinsi ya kutia moyo wale wanaougua ugonjwa wa kudumu au ugonjwa mbaya. Dalili za ugonjwa wa SD za maumivu na uchovu hazionekani kwa macho, hata hivyo, zinaathiri mtu sana kiafya na kihisia. Nyakati nyingine, nimeshuka moyo. Vidondamalazi na ulemavu na vilevile kupoteza uwezo wa kutumia mikono zimenikatisha tamaa.

Hata hivyo, barua na simu kutoka kwa marafiki zimenitia moyo. Tumethamini hasa marafiki ambao wametuhakikishia kwamba wanatukumbuka katika sala zao. Kwa upande wetu tumetafuta na kutembelea wengine walio na ugonjwa huu ili kutiana moyo. Kwa njia hiyo tumepata marafiki wapya wa karibu.

Maisha yetu si rahisi. Nyakati nyingine hali si nzuri, na hatujui jinsi mambo yatakavyokuwa wakati ujao. Lakini licha ya kuzuiwa kufanya yale ambayo tulikuwa tumepanga, bila shaka tunaweza kuwa wenye furaha. Furaha yetu hutokana hasa na uhusiano wa karibu pamoja na Yehova. Tumeona pia kwamba, licha ya hali yetu ngumu, tunaweza kudumisha furaha kadiri fulani tukiwa na shughuli nyingi za Kikristo. Kisa chetu huthibitisha wazi kwamba Yehova hutupa fursa nyingi za kumtumikia, naye anatoa kwa ukarimu “nguvu ipitayo iliyo ya kawaida.” (2 Wakorintho 4:7) Tunaimarishwa kwa kuweka moyoni ahadi ya Mungu kwamba hivi karibuni “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.”—Isaya 33:24.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 14 Viuavijasumu hivyo vilitia ndani minocycline (Minocin) na tetracycline. Gazeti la Amkeni! halipendekezi matibabu yoyote hususa. Maamuzi kuhusu matibabu na dawa ni ya mtu binafsi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Scleroderma Mwili Unapojishambulia Wenyewe

Neno “scleroderma” (SD) latokana na neno la Kigiriki linalomaanisha “ngozi ngumu.” Lakini mbali na ngozi, ugonjwa huo huathiri pia tishu-unganishi nyingine zote. Ugonjwa huo ni ugonjwa wenye kudumu wa mfumo wa kinga wa mwili, na hasa wanawake wanashikwa na ugonjwa huo. Kuongezeka kwa unene wa ngozi kusiko kwa kawaida ni dalili kuu ya ugonjwa huo. Mara nyingi ugonjwa huo hautambuliwi labda hata kwa miaka mingi, kwa sababu dalili za wagonjwa hutofautiana kwa kadiri fulani.

Kile kinachosababisha ugonjwa huo hakijulikani. Wanasayansi wanakubaliana kwamba mwili wa mgonjwa hutokeza kupita kiasi protini yenye nyuzinyuzi inayoitwa kolagini. Kisha protini hiyo hushambulia tishu za mwili zisizo na ugonjwa. Kwa hiyo, mara nyingi inasemekana ugonjwa huo unaitwa ugonjwa ambao hufanya mwili ujishambulie wenyewe.

Kuna aina mbili za kawaida za ugonjwa wa SD, na vilevile aina nyingine zisizo za kawaida sana. Ugonjwa wa diffuse scleroderma (unaoenea) au systemic scleroderma (unaoathiri mwili kwa ujumla) ndio hatari zaidi nao unafanya ngozi kuwa nene upesi sana, kuanzia mikono na uso na kuenea hadi sehemu ya juu ya mikono na kiwiliwili. Watu walio na ugonjwa wa SD unaoenea wamo hatarini kupata matatizo ya viungo vya ndani vya mwili katika hatua za kwanza za ugonjwa huo. Aina nyingine ya ugonjwa huo unaitwa limited SD (usioenea).

Katika SD unaoenea, ngozi huwa nene kotekote mwilini na kwenye pande zote mbili za mwili. Dalili za ugonjwa huo hutia ndani pia uvimbe wa misuli, na kufura kwa vidole, mikono, na nyayo. Machafuko ya tumbo na matumbo ni ya kawaida, lakini hali inakuwa hatari zaidi ugonjwa huo unapoathiri mapafu, moyo na figo.

Mishipa ya damu pia huathiriwa. Hiyo husababisha ugonjwa wa Raynaud, ambao hufanya vidole vya mikono na miguu kukosa kusambazwa damu, kwa hiyo katika hali ya baridi vinauma na vinakuwa vyeupe, vyekundu, na samawati.

Kwa sasa hakuna matibabu yanayofanya kazi au tiba zozote kwa magonjwa aina yoyote ya SD.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

Kuelewa Wale Wanaougua Ugonjwa wa Scleroderma

Ili kuwasaidia na kuwatia moyo walio na ugonjwa wa scleroderma (SD), mtu anahitaji kuwaelewa vizuri. Kwa sababu ugonjwa huo hautambuliwi kwa urahisi, mtu anaweza kuwa na ugonjwa huo kwa miaka mingi bila kujua anaugua ugonjwa gani. Katika hatua za kwanza za ugonjwa huo, huenda akapimwa na kuchunguzwa mara nyingi. Ugonjwa usipotambuliwa, huenda akahisi ameshindwa, mpweke, na kuwa na wasiwasi kwa sababu ya mabadiliko ya mwili wake yasiyoeleweka.

Maisha ya mgonjwa hubadilika kwa njia nyingi, na vizuizi vingi humzuia asifanye yale aliyokuwa amezoea kufanya. Ikiwa ugonjwa unamlemea kadiri ya kuhitaji matibabu na kutunzwa, huenda hataweza kujitegemea mwenyewe. Huenda mahusiano na wapendwa yakabadilika kwa sababu wengine watachukua madaraka yake katika familia. Huenda mgonjwa asiweze kushirikiana na marafiki au kushiriki tafrija mbalimbali. Huenda atahitaji kubadilisha kazi au kuacha kazi kabisa.

Mara nyingi mabadiliko kama hayo, hufanya mgonjwa asijistahi mwenyewe tena. Ni muhimu kwa mgonjwa kukumbuka kwamba hisia kama hizo ni za kawaida kwa mtu aliye na ugonjwa huo.

Kwa upande mwingine, wengi wenye ugonjwa huo wameona kwamba upendo, furaha, na tumaini zimeongezeka katika maisha yao kwa sababu watu wa familia yao na wengine wanajitahidi kuwasaidia. Hata ingawa mgonjwa na wapendwa wake wanakabili magumu makubwa, wanaweza kudumisha tumaini na kuepuka kuvunjika moyo. Hisia za kukata tamaa ni za kawaida, lakini mgonjwa hapaswi kulemewa nazo.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Binti yetu Trisha na mume wake Matthew wanatumikia huko Betheli

[Picha katika ukurasa wa 25]

Naweza kusaidia kwenye miradi ya ujenzi hata nikiwa kitandani

[Picha katika ukurasa wa 25]

Binti yetu Traci na mume wake, mwana wetu Ryan, na mke wangu, Lisa