Uwongo na Ukweli Kuhusu Wazee
Uwongo na Ukweli Kuhusu Wazee
Kuna dhana nyingi zisizo za kweli juu ya uzee. Kichapo “Ageing—Exploding the Myths” (Uzee—Kufichua Uwongo), ambacho kimechapishwa na Programu ya Uzee na Afya ya Shirika la Afya Ulimwenguni, kinafichua baadhi ya dhana zisizo za kweli. Fikiria mifano kadhaa.
Uwongo: Wazee walio wengi wanaishi katika nchi zilizoendelea.
Ukweli: Asilimia 60 za wazee zaidi ya milioni 580 wanaishi katika nchi zinazoendelea. Watu wengi zaidi katika nchi hizo wanafikia umri wa uzee kwa sababu ya huduma bora ya afya na maendeleo kwa upande wa usafi, makao na lishe.
Uwongo: Wazee hawafaidi yeyote.
Ukweli: Wazee wanawasaidia wengine sana kwa kufanya kazi ambayo hawalipwi. Kwa mfano, imekadiriwa kwamba watoto milioni 2 hivi huko Marekani wanatunzwa na nyanya na babu zao, na milioni 1.2 kati yao wanaishi kwa nyanya au babu zao. Kwa hiyo, wazee wanawaandalia makao, chakula, elimu, na wanawafundisha wajukuu wao kanuni za jamii ili mama na baba waweze kufanya kazi ya kuajiriwa. Mashirika mengi ya wafanyakazi wa kujitolea katika nchi zilizoendelea hayangeweza kuendelea kuendesha shughuli zake bila msaada wa wazee. Wanatunza wengine pia. Katika nchi kadhaa zinazoendelea ambapo asilimia 30 za watu wazima wana ugonjwa wa UKIMWI, wazee hutunza watoto wao wazima walio wagonjwa, na watoto wao wanapokufa wanalea wajukuu wao walio maya- tima.
Uwongo: Wazee wanaacha kazi kwa sababu wameshindwa kufanya kazi.
Ukweli: Mara nyingi huacha kazi kwa sababu hawana elimu nzuri au hawajazoezwa kwa kufaa au kwa sababu ya ubaguzi dhidi ya wazee. Hawaachi kazi kwa sababu ya uzee.
Uwongo: Wazee hawataki kufanya kazi.
Ukweli: Mara nyingi wazee hufutwa kazi ya kuajiriwa ijapokuwa wanataka kuendelea kufanya kazi na wana uwezo wa kufanya hivyo. Hasa wakati wa ukosefu wa kazi, wengi huona kwamba wazee wanapaswa kuacha kazi ili kuwapa vijana fursa ya kupata kazi ya kuajiriwa. Hata hivyo, ijapokuwa wazee wanafutwa kazi haimaanishi kwamba vijana watapata kazi. Huenda kijana asiwe na ustadi unaohitajika kufanya kazi ambayo mzee alikuwa akifanya. Wafanyakazi wazee wenye uzoefu husaidia kudumisha uzalishaji nao ni wafanyakazi wenye kutegemeka.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lasema kwamba kwa kuzingatia mambo hayo, jumuiya kotekote duniani zapaswa kuwaona wazee kuwa chanzo cha utaalamu kinachoweza kuleta faida nyingi. Kwa hiyo, kiongozi wa kikundi cha Programu ya Uzee na Afya ya Shirika la Afya Ulimwenguni, Alexandre Kalache, asema hivi: “Nchi . . . zinapaswa kuona wazee kuwa suluhisho la matatizo mbalimbali wala si kuwaona kama tatizo.” Na huo ndio ukweli.