Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vyanzo vya Chuki

Vyanzo vya Chuki

Vyanzo vya Chuki

CHUKI ilianza mapema katika historia ya mwanadamu. Simulizi la Biblia kwenye Mwanzo 4:8 lasema hivi: “Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua.” “Na ni kwa ajili ya nini yeye alimchinja?” aliuliza Yohana mwandikaji wa Biblia. “Kwa sababu kazi zake mwenyewe zilikuwa mbovu, lakini zile za ndugu yake zilikuwa za uadilifu.” (1 Yohana 3:12) Habili aliuawa kwa sababu ya chanzo kimoja cha chuki, yaani, wivu. “Wivu ni ghadhabu ya mtu,” yasema Mithali 6:34. Leo, watu huchukiana kwa sababu ya kuoneana wivu kwa sababu ya cheo, utajiri, kazi, na mafanikio mengine.

Kutojua Mambo Fulani na Woga

Lakini kuna vyanzo vingine vingi vya chuki licha ya wivu. Mara nyingi, chuki husababishwa na kutojua mambo fulani na woga. “Kabla sijajifunza kamwe kuchukia, nilijifunza kuogopa,” asema kijana mmoja aliye mshiriki wa kikundi kijeuri cha ubaguzi wa rangi. Woga huo husababishwa na kutojua mambo fulani. Kwa mujibu wa kichapo The World Book Encyclopedia, watu wenye ubaguzi huwa na mwelekeo wa kushikilia maoni ‘yasiyotegemea uthibitisho uliopo. . . . Watu wenye ubaguzi hugeuza, hupotosha, huelewa kimakosa, au hata hupuuza mambo ya hakika yasiyopatana na maoni yao.’

Maoni hayo hutoka wapi? Ripoti moja ya habari ya Internet yasema hivi: “Historia huchangia maoni mengi ya kitamaduni yasiyobadilika, lakini pia historia yetu binafsi huchangia mambo mengi tunayobagua.”

Kwa mfano, nchini Marekani biashara ya watumwa ilizusha migogoro inayoendelea hadi leo kati ya Wazungu wengi na watu wa asili ya Kiafrika. Mara nyingi, wazazi huwapitishia watoto wao maoni mabaya kuhusu jamii fulani. Mzungu mmoja aliyejitambulisha waziwazi kuwa mbaguzi alikubali kwamba alisitawisha maoni mabaya ya ubaguzi “bila kushirikiana hata kidogo na watu weusi.”

Pia kuna watu wanaowadharau tu watu walio tofauti. Huenda wakawa na maoni kama hayo baada ya kuchukizwa mara moja tu na mtu wa jamii au utamaduni tofauti. Kutokana na hayo, wao hukata kauli mara moja kwamba kila mtu wa jamii au utamaduni huo ana tabia zisizopendeza.

Mtu mwenye ubaguzi huudhi, lakini ubaguzi unapoenea katika taifa au jamii nzima, waweza kusababisha maafa. Mtu anapoamini kwamba taifa lake, rangi yake ya ngozi, utamaduni wake, au lugha yake humfanya awe bora kuliko wengine hilo laweza kumfanya ashikilie sana maoni ya ubaguzi au kudharau mtu yeyote au kitu chochote kigeni. Katika karne ya 20, mara nyingi ubaguzi wa aina hiyo ulisababisha jeuri.

Si lazima chuki au ubaguzi uwe wa rangi ya ngozi au wa kitaifa tu. Mchunguzi Clark McCauley wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania aliandika kwamba ‘kuwagawanya watu tu katika vikundi viwili, kwaweza kuwafanya wapendelee vikundi vyao.’ Katika majaribio maarufu kuhusu jambo hilo, mwalimu mmoja wa darasa la tatu alionyesha hilo alipowagawanya wanafunzi wake katika vikundi viwili—kikundi cha watoto wenye macho ya bluu na kikundi cha watoto wenye macho ya kahawia. Baada ya muda mfupi, uadui ulisitawi kati ya vikundi hivyo viwili. Hata vikundi vinavyofanyizwa kwa sababu ya mambo madogo kama kupendelea timu fulani ya michezo vyaweza kusababisha mapambano ya kijeuri.

Kwa Nini Kuna Ujeuri Mwingi Sana?

Lakini ni kwa nini uadui huo huonyeshwa kwa njia za kijeuri? Wachunguzi wamechunguza masuala hayo kwa undani lakini bado wanatoa makisio tu. Clark McCauley alitayarisha orodha ndefu ya utafiti kuhusu ujeuri na ugomvi wa wanadamu. Yeye anukuu uchunguzi mmoja uliochapishwa unaosema kwamba “uhalifu wa kijeuri hutokea wakati wa vita na baada ya ushindi.” Wachunguzi hao waligundua kwamba “mataifa yaliyoshiriki katika Vita ya Kwanza ya Ulimwengu na Vita ya Pili ya Ulimwengu, hasa mataifa yaliyoshinda, yamekuwa na visa vingi vya mauaji baada ya vita hivyo.” Kulingana na Biblia, twaishi katika kipindi cha vita. (Mathayo 24:6) Je, yawezekana kwamba vita hivyo vimechangia kwa njia fulani ongezeko la ujeuri wa aina nyingine?

Wachunguzi wengine wanatafuta sababu ya kibiolojia inayosababisha ugomvi wa wanadamu. Uchunguzi mmoja uliofanywa ulidokeza kwamba ugomvi mwingine husababishwa na “viwango vidogo vya kemikali ya serotonin katika ubongo.” Dokezo jingine linalojulikana sana ni kwamba ugomvi u katika chembe zetu za urithi. Mtaalamu mmoja wa siasa alisema kwamba “huenda sehemu kubwa ya [chuki] ni ile tuliyorithi.”

Biblia yenyewe yasema kwamba wanadamu wasiokamilika wamezaliwa wakiwa na tabia mbaya na kasoro. (Mwanzo 6:5; Kumbukumbu la Torati 32:5) Kwa wazi, maneno hayo yanawahusu wanadamu wote. Lakini si wanadamu wote wanaochukia wengine isivyofaa. Watu hujifunza kuchukiana. Hivyo, mwanasaikolojia maarufu, Gordon W. Allport, alitambua kwamba vitoto vichanga ‘havina mwelekeo mkubwa wa kuharibu vitu. . . . Mtoto huwa na maoni mazuri, naye hukaribia kila kitu kinachompendeza na kila mtu.’ Mambo kama hayo yaonyesha kwamba ugomvi, ubaguzi, na chuki ni tabia ambazo watu hujifunza! Uwezo huo wa kujifunza chuki hutumiwa kwa urahisi na watu wanaoeneza chuki.

Kufisidi Akili

Wanaofanya hivyo hasa ni viongozi wa magenge mbalimbali yanayoeneza chuki, kama vile genge linalofuata sera za Nazi linalonyoa kipara na genge la Ku Klux Klan. Magenge hayo huwachochea hasa vijana wanaovutiwa na mambo kwa urahisi ambao wanatoka kwenye familia zenye matatizo ili wajiunge nao. Huenda vijana wasiojiamini na wanaohisi kuwa hawafai wakaona kwamba magenge ya kueneza chuki yanawafanya wapendwe.

Njia moja ambayo imetumiwa na watu fulani kueneza chuki sana kwa matokeo ni Internet. Kwa mujibu wa hesabu iliyochukuliwa hivi karibuni, kuna vituo 1,000 kwenye Internet vya kueneza chuki. Gazeti la The Economist lilimnukuu mmiliki mmoja wa kituo cha Internet cha kueneza chuki akijigamba hivi: “Internet imetupa fursa ya kuwasilisha maoni yetu kwa mamia ya maelfu ya watu.” Kituo chake cha Internet kina “Sehemu ya Watoto.”

Matineja wanapotafuta muziki kwenye Internet, wanaweza kupata vituo vinavyosambaza muziki unaoeneza chuki. Muziki wa aina hiyo huchezwa kwa sauti kubwa na ni wa kijeuri, ukiwa na maneno yanayopitisha ujumbe mkali wa kubagua jamii fulani. Vituo hivyo vya Internet huunganisha watu na vikundi vinavyozungumzia habari, sehemu za kupigia gumzo, au vituo vingine vinavyoeneza chuki.

Vituo fulani vya Internet vya kueneza chuki huwa na sehemu maalum kwa ajili ya michezo na mambo mengine ya vijana. Kituo kimoja cha Internet cha genge linalofuata sera za Nazi hujaribu kutumia Biblia ili kutetea ubaguzi wa kijamii na wa Wayahudi. Vilevile, genge hilo limefungua kituo cha Internet chenye mafumbo ya kujaza maneno yaliyo na maelezo ya ubaguzi wa kijamii. Lengo ni nini? “Ili kuwasaidia vijana Wazungu wafahamu mambo tunayopigania.”

Lakini, watu wengine wanaoeneza chuki si washiriki wa magenge yanayoshikilia maoni ya ubaguzi. Mwanasosiolojia mmoja aliyeandika kuhusu mapambano yaliyotokea hivi karibuni katika nchi za Balkani alisema hivi kuhusu waandishi fulani wanaoheshimiwa na pia watu fulani wenye uvutano katika jamii: “Nilishangaa ku[wa]ona wakiandika kwa njia inayowapendeza wananchi wenzao wenye maadili yaliyopotoka, njia inayochochea chuki yao kali, inayovuruga kufikiri kwao kwa kuwahimiza wasione kuwa kitu chochote kimekatazwa . . . , na kupotosha ukweli.”

Kwa habari hii, hatupaswi kusahau fungu la makasisi. Katika kitabu chake Holy Hatred: Religious Conflicts of the ‘90’s, mwandishi James A. Haught asema jambo hili linaloshtua: “Jambo la kushangaza katika miaka ya 1990 ni kwamba dini—inayopaswa kuwa yenye fadhili na kuwahangaikia wanadamu—imekuwa chanzo kikuu cha chuki, vita, na ugaidi.”

Basi, vyanzo vya chuki ni vingi na vyahusisha mambo mengi. Je, hiyo yamaanisha kwamba wanadamu hawana njia ya kuacha upumbavu wa kuchukiana ambao umekuwepo sana katika historia yao? Je, kuna jambo lolote linaloweza kufanywa na watu mmoja-mmoja na vilevile watu wote ulimwenguni ili kujitahidi kukomesha kutoelewana, kutojua, na woga unaosababisha chuki?

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Ubaguzi na chuki ni tabia ambazo watu hujifunza!

[Picha katika ukurasa wa 4, 5]

Hatukuzaliwa na . . .

. . . hisia za chuki na ubaguzi

[Picha katika ukurasa wa 7]

Vikundi vinavyoeneza chuki vinatumia Internet ili kuwavutia vijana wajiunge nao

[Picha katika ukurasa wa 7]

Mara nyingi, dini imechochea mapambano

[Hisani]

AP Photo