Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Meteora Miamba Mirefu Sana

Meteora Miamba Mirefu Sana

Meteora Miamba Mirefu Sana

“Kati ya mambo yote niliyopata kuona, hakuna kilichonistaajabisha zaidi kama eneo hili lenye kuvutia. Katika . . . maeneo mengine yenye milima ambayo nimetembelea, hakuna kitu kinachoweza kulinganishwa na vilele hivi vya ajabu.”—Robert Curzon, mtalii Mwingereza, 1849.

HATUTARAJII kabisa kupata mandhari yenye kustaajabisha ambayo tunaona tunapokaribia mji wa Kalabáka na kijiji kilicho karibu cha Kastráki, kwenye uwanda wa Thessaly, nchini Ugiriki. Kuna mawe mengi yanayofanyiza zaidi ya nguzo 20 kubwa za miamba. Miamba hiyo imekaa shaghalabaghala na imetengana. Ina miinuko mikali na ina urefu wa mamia ya meta. Vilele vyake vina makao makubwa ya watawa yenye madari yaliyotiwa nakshi yanayotegemezwa na safu za mbao.

Hiyo ndiyo Meteora ya Ugiriki, ambapo miamba isiyo na kifani imeunganishwa kupitia shughuli za ajabu za wanadamu. Jina “Meteora” latokana na neno la Kigiriki linalomaanisha “kuinuliwa juu ya ardhi” nalo hurejelea kikundi hiki cha nguzo zilizotenganishwa za miamba na yale makao ya watawa yanayozidi 30 yaliyojengwa juu yake. Kwa wastani, miamba hiyo ina urefu wa meta 300, mwamba mrefu zaidi ukiwa na urefu wa meta 550 kutoka chini.

Tunapokaribia miamba hiyo, vivuli vya miamba hiyo mirefu sana vinarefuka. Mandhari ya eneo hilo hubadilika-badilika jua linapotokeza vivuli mbalimbali katikati ya miamba. Katika majira ya baridi kali, miamba hiyo mikubwa huonekana waziwazi ikiwa imeinuka katika eneo lililofunikwa kabisa kwa theluji.

Jinsi Ilivyofanyizwa

Watu wamekisia sana jinsi miamba ya Meteora ilivyofanyizwa. Wengi huamini kwamba miaka mingi sana iliyopita, uwanda wa Meteora ulifunikwa na ziwa kubwa sana. Kulingana na nadharia moja, utendaji mkubwa sana wa miamba ulifanya miamba iinuke kwa njia fulani. Gazeti la Experiment laeleza kuwa wanajiolojia wengine huamini kwamba “miamba hii ilipata umbo lake kati ya mwaka wa 2000 na 1000 K.W.K.”

Robert Curzon, aliyenukuliwa mwanzoni, aliandika hivi kuhusu Meteora: “Yamkini ncha ya safu ya vilima vyenye miamba ilivunjwa na tetemeko la ardhi au ikafagiliwa mbali na ile Gharika, na kuacha tu . . . miamba mirefu, myembamba, laini, iliyochongoka.” Kwa kupendeza, hekaya za kale za Ugiriki zaonyesha kwamba milima ya Thessaly ilifanyizwa kupitia furiko, au gharika, lililosababishwa na miungu.—Mwanzo 6:1–8:22.

Makao ya Watawa Angani

Haidhuru ufafanuzi wa asili ya Meteora, tangu karne ya tisa W.K., miamba hiyo imewavutia watu. Wapanda-milima wa siku hizi, wanaopanda Meteora wakiwa na vifaa maalum vya kupanda milima, waweza kutambua ustadi wa watawa wa kale waliokaa ndani ya mapango na nyufa za miamba hiyo. Mjadala juu ya jinsi makao hayo ya watawa yalivyojengwa juu ya miamba isiyoweza kufikiwa kwa urahisi ungali waendelea.

Watu hao wa kale walitumia njia gani kupanda na kushuka kutoka kwenye makao yao yenye fahari? Naam, kama vile kitabu Meteora—The Rock Monasteries of Thessaly kinavyosema ‘huenda walipanda kwa ngazi za mbao ambazo zilishushwa kutoka juu ya majabali au wangevutwa wakiwa ndani ya neti ambayo iliteremshwa kwa kutumia chombo cha kuinua vitu kilichokuwa juu kwenye makao yao. Vyovyote vile, mgeni alihitaji tu kutumaini nia njema na ubuni huo usioaminika wa watawa wa kiume.’ Mtu mmoja aliyekuwa mkuu wa watawa alipoulizwa ni mara ngapi ile kamba iliyovuta neti ilibadilishwa, alisema hivi: ‘Inapokatika tu.’ Mwaka wa 1925 sehemu za kukanyagia zilichongwa kwenye mwamba ili iwe rahisi kupanda miamba hiyo.

Watawa wa kwanza kupanda nguzo hizo walikuwa Varnavas, kati ya mwaka wa 950 W. K. na 965 W. K., na Andronikos kutoka Krete, mnamo mwaka wa 1020. Watawa wengine wa kiume kutoka sehemu zote za Byzantium walifuata, wakifanya idadi ya makao ya watawa yaliyo juu ya miamba yaongezeke kufikia 33. Kufikia karne ya 16 na 17, jamii hizo zilikuwa zimefikia upeo wao, lakini tangu wakati huo zimedidimia.

“Tutazame tulivyo sasa!” akaomboleza mkuu mmoja wa makao ya watawa. “Ah, . . . vijana hawatutaki tena!” Kwa hakika, ni makao sita tu ya watawa yanayotumiwa kwa sasa. Makao mawili hukaliwa na watawa wa kike. Waweza kupata makao ya watawa yaliyoachwa ukiwa kwenye miamba kadhaa ya Meteora.

Mandhari Yenye Utamaduni Mwingi

Leo makao ya watawa yaliyo miambani ni mojawapo ya sehemu za kitamaduni zenye kuvutia zaidi za Ugiriki. Kwa mujibu wa Shirika la Elimu, Sayansi, na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, makao hayo ni sehemu ya kitamaduni yenye thamani sana. Hivi karibuni Serikali ya Ugiriki ilihangaikia sana kuhifadhiwa kwa utamaduni wa Meteora. Majengo yaliyorekebishwa na majumba ya makumbusho yamefunguliwa kwa ajili ya wageni. Yana nini?

Licha ya mambo kama sanamu zinazobebeka, mavazi rasmi ya kanisa, na vitabu vya muziki, majumba hayo yana hati za Biblia zisizopatikana kwa urahisi. Kati ya hati hizo kuna hati ya ngozi ya Kodeksi 591, ya mwaka wa 861 W. K.-862 W. K., ambayo ina habari zinazofasiri kitabu cha Biblia cha Mathayo.

Kwelikweli, nguvu nyingi za asili zimetokeza mandhari isiyo na kifani. Iwapo utatembelea Ugiriki, mbona usitembelee pia eneo la Meteora? Na uhakikishe una filamu nyingi kwa kuwa utataka kupiga picha nyingi.—Imechangwa.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Makao ya watawa ya Mt. Nicholas Anapausas

Makao ya watawa ya Rousanou

[Hisani]

M. Thonig/H. Armstrong Roberts

[Picha katika ukurasa wa 17]

Makao ya watawa ya Utatu Mtakatifu

Makao ya watawa ya Great Meteoron

[Hisani]

R. Kord/H. Armstrong Roberts

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Mandhari ya nyuma: Y. Yannelos/Greek National Tourist Organization