Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutambua Vyanzo

Kutambua Vyanzo

Kutambua Vyanzo

“Kwa kawaida, kushuka moyo kwa matineja hakusababishwi tu na jambo moja bali husababishwa na mikazo mingi.” —Dakt. Kathleen McCoy.

NI NINI huwafanya matineja washuke moyo? Mambo mengi yahusika. Kwanza kabisa, mabadiliko ya kimwili na ya kihisia-moyo yanayotokea vijana wanapobalehe yaweza kuwafanya wababaike na kuogopa sana, na kuwafanya watazamie mabaya. Vilevile, mara nyingi ni rahisi matineja kuhisi vibaya wanapoona kwamba wamekataliwa na rafiki zao au mtu waliyempenda kimahaba. Pia, kama ilivyoonyeshwa katika makala yetu ya kwanza, matineja wa sasa wanakua katika ulimwengu unaoweza kusababisha mshuko wa moyo. Kwa hakika, twaishi katika “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.”—2 Timotheo 3:1.

Isitoshe, vijana wanapata misongo ya maisha kwa mara ya kwanza kabisa, na hawana stadi wala ujuzi kama watu wazima. Hivyo, mara nyingi matineja huwa kama watalii wanaotafuta njia kwenye eneo wasilofahamiana nalo—wanafadhaishwa na hali hiyo na, kama inavyokuwa mara nyingi, hawataki kuomba msaada. Hali hizo zaweza kusababisha mshuko wa moyo.

Lakini kuna sababu nyingine kadhaa zinazoweza kuwafanya matineja washuke moyo. Acheni tuchunguze baadhi ya sababu hizo.

Mshuko wa Moyo na Hasara

Nyakati nyingine mshuko wa moyo hutokea baada ya kupata hasara kubwa—labda kifo cha mpendwa au kutenganishwa na mzazi kupitia talaka. Katika nchi fulani, hata kifo cha mnyama aliyependwa chaweza kumfadhaisha sana tineja.

Kuna hasara nyingine zisizotambuliwa wazi. Kwa mfano, mtu anapohamia eneo lingine yeye huacha mazingira aliyokuwa amezoea na rafiki wapendwa. Hata mtu anapofikia mradi ambao alitazamia kwa muda mrefu—kama vile kumaliza shule—aweza kuhisi kwamba amepata hasara. Kwani, anapoanza maisha mapya yeye hupoteza starehe na usalama aliofurahia hapo zamani. Kisha, kuna vijana wanaovumilia ugonjwa fulani wa kudumu. Katika hali kama hiyo, tineja anapofadhaika kwa sababu ya kuwa tofauti na rafikize—labda hata kupuuzwa nao—aweza kuhisi kwamba yeye si timamu.

Ni kweli kwamba vijana wengi hupata hasara kama hizo bila kufadhaika sana. Wao huhuzunika, hulia, husikitika, na kuomboleza—lakini baada ya muda wanazoea hali hiyo. Hata hivyo, mbona matineja wengine hushuka moyo, ilhali wengi hukabiliana na mikazo ya maisha kwa urahisi? Jibu kwa swali hilo lahusisha mambo mengi, kwa kuwa mshuko wa moyo ni ugonjwa tata. Lakini vijana wengine waweza kuathiriwa kwa urahisi zaidi.

Uhusiano na Utendaji wa Kemikali Mwilini

Wataalamu wengi wa masuala ya akili huamini kwamba kuvurugika kwa utendaji wa kemikali ubongoni huchangia sana mshuko wa moyo. * Mvurugo huo waweza kupitishwa katika chembe za urithi, kwa kuwa wachunguzi wamegundua kwamba kuna uwezekano mkubwa kuwa matineja walio na mzazi aliyeshuka moyo watapatwa na hali hiyo. “Mara nyingi watoto walioshuka moyo huwa na angalau mzazi mmoja aliyeshuka moyo,” chasema kitabu Lonely, Sad and Angry.

Jambo hilo lazusha swali hili, Je, kweli watoto hurithi mshuko wa moyo, au wao hujifunza kushuka moyo wanapoishi na mzazi mwenye ugonjwa huo? Ni vigumu kujibu swali hilo, kwani ubongo ni tata sana. Ndivyo ilivyo pia kuhusu mambo mengine ambayo yanaweza kuwafanya matineja washuke moyo.

Mshuko wa Moyo na Mazingira ya Familia

Kwa kufaa, mshuko wa moyo umetajwa kuwa suala la kifamilia. Kama ilivyokwisha kutajwa, kuna kitu fulani katika chembe za urithi ambacho hupitisha uwezekano wa kushuka moyo kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Lakini mazingira ya familia huchangia pia. “Watoto wanaotendwa vibaya na wazazi wao wanaelekea zaidi kushuka moyo,” aandika Dakt. Mark S. Gold. “Ndivyo ilivyo pia kwa watoto ambao wazazi wao huwachambua kupita kiasi na kukazia kasoro zao.” Kushuka moyo kwaweza kutokea wazazi wanapomchunga na kumzuia mtoto kupita kiasi. Hata hivyo, kwa kustaajabisha, mchunguzi mmoja aligundua kwamba watoto hushuka moyo zaidi wanapopuuzwa tu na wazazi.

Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba matineja wote walioshuka moyo wamepata ugonjwa huo kwa sababu ya malezi mabaya. Kukata shauri hivyo kungekuwa kupuuza mambo mengineyo yanayoweza kuchangia tatizo hilo. Hata hivyo, katika visa fulani mazingira ya familia ni sababu kubwa inayochangia hali hiyo. “Watoto wanaoishi katika nyumba ambazo wazazi huzozana kila mara wanaelekea zaidi kushuka moyo kuliko watoto walio katika mazingira matulivu,” aandika Dakt. David G. Fassler. “Sababu moja ni kwamba wazazi wanaozozana hujihusisha sana katika migogoro yao hivi kwamba wanapuuza mahitaji ya watoto wao. Sababu nyingine ni kwamba wazazi hao hugombana kuhusu watoto wao, jambo linaloweza kuwafanya vijana wajilaumu, wakasirike, na kuudhika.”

Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayoweza kusababisha matineja washuke moyo. Kuna mengine. Kwa mfano, wataalamu fulani wasema kwamba sababu za kimazingira (kama kukosa lishe bora, vichafuzi vyenye sumu, na utumiaji wa dawa za kulevya) zaweza kusababisha mshuko wa moyo. Wengine wadokeza kwamba dawa fulani (kama dawa fulani za kupunguza kemikali ya histamini na za kutuliza wasiwasi) zaweza pia kusababisha mshuko wa moyo. Pia, yaonekana kwamba watoto wenye kasoro za kujifunza wanaweza kushuka moyo kwa urahisi, labda kwa sababu pole kwa pole wanaacha kujiamini wanapotambua kwamba hawawezi kuwa sawa na wanadarasa wenzao.

Hata hivyo, haidhuru sababu ya kushuka moyo, ni muhimu kufikiria swali hili, Matineja walioshuka moyo waweza kusaidiwaje?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Wengine hufikiri kwamba japo watu fulani walioshuka moyo huzaliwa na mvurugo huo wa kikemikali, wengine huzaliwa wakiwa na afya njema kisha jambo la kufadhaisha hubadili utendaji wa kemikali ubongoni na kufanya iwe rahisi kwao kushuka moyo.

[Picha katika ukurasa wa 8]

Mara nyingi mizozo ya familia huchangia sana mshuko wa moyo