Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Taiwan Yatoa Msamaha

Gazeti la The China Post linaripoti kwamba ‘Rais Chen Shui-bian [wa Taiwan] alitoa msamaha kwa wafungwa 21 . . . , kutia ndani wafungwa 19 waliokataa kuandikishwa jeshini. Msamaha huo uliotolewa Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu [Desemba 10, 2000], utawaondolea mashtaka Mashahidi wa Yehova 19, waliofungwa kwa sababu ya kukataa kuandikishwa jeshini kwa sababu za kidini.’ Mashahidi 14 kati ya wale 19 tayari walikuwa wameachiliwa kwa masharti. Msamaha huo wa pekee ulikuwa wa kwanza kutolewa katika muda wa miaka kumi. Kampuni ya Wakili Nigel Li ilitetea Mashahidi, naye alisema hivi: “Niliguswa na Mashahidi na ujumbe wao wa amani. . . . Msimamo wao upande wa amani unaonyesha maadili bora. Inatupasa kuwapa heshima ya pekee.”

“Je, Kuna Watu ‘Wengi Mno’ Duniani?”

Gazeti la Vitality linasema hivi: “Jambo la kushangaza ni kwamba jimbo la Texas huko Marekani linaweza kutoshea watu wote duniani.” Kulingana na gazeti hilo, shirika la Umoja wa Mataifa linakadiria kwamba idadi ya watu duniani imefikia bilioni sita, na jimbo la Texas lina eneo la kilometa 680,000 za mraba. Kila mtu duniani angekuwa na makao yenye eneo la meta 22 hivi za mraba. Gazeti hilo lasema: “Familia yenye watu 5 ingekuwa na makao yenye eneo la meta 113 za mraba. Hiyo ni nyumba kubwa sana hata ikilinganishwa na nyumba za kawaida huko Texas. Na maeneo mengine yote ya dunia yangeweza kutumiwa kwa kilimo, kutengeneza bidhaa mbalimbali, elimu, na burudani!”

Je, Mmea wa Nopal Unafaidi Wanaougua Ugonjwa wa Kisukari?

Watu wengi hufikiri kwamba nopal ni mmea wa kawaida tu wa jangwani. Hata hivyo, gazeti la The News la Mexico City, liliripoti kwamba mmea huo wenye matumizi mengi huenda ukafaa hasa watu wenye ugonjwa wa kisukari. Kwa nini? Wanasayansi wamegundua kwamba kiwango cha sukari katika damu ya watu walio na ugonjwa wa kisukari hakiongezeki wanapokula vyakula vilivyotengenezwa kwa unga wa mmea huo uliokaushwa. Yaonekana kwamba mmea wa nopal unapoimarisha ini na kongesho, unazidisha uwezo wa mwili wa kutumia insulini.

Uchafuzi wa Hewa Juu ya Bahari ya Hindi

Gazeti la MorgenWelt Nachrichten linaripoti kwamba kuna kiwango kikubwa cha uchafuzi wa hewa katika maeneo makubwa ya sehemu ya kaskazini mwa Bahari ya Hindi. Wachunguzi kutoka nchi sita walipata kwamba pepo za msimu wa baridi hupeleka masizi, majivu na moshi, mavumbi ya asilia na yasiyo ya asilia, chumvi na salfa mbalimbali, kutoka sehemu za kusini na kusini-mashariki mwa Asia hadi Bahari ya Hindi. Kuanzia Januari hadi Machi mwaka wa 1999, tabaka la ukungu lenye unene wa karibu kilometa tatu lilifunika eneo la karibu kilometa milioni kumi za mraba. Eneo hilo ni kubwa kuliko nchi ya Kanada. Gazeti hilo likasema hivi: “Kulingana na wanasayansi, ongezeko la uchafuzi wa hewa huko Asia linafanya hewa iharibike kwa kiwango kikubwa sana, na hilo linaathiri hewa ya sehemu hiyo na pia duniani pote.”

Je, Chokoleti Ni Yenye Manufaa kwa Afya?

Gazeti la Japani la Nihon Keizai Shimbun linasema kwamba baadhi ya watu wanaona chokoleti kuwa yenye manufaa kwa afya. Kwa nini? Kwa kuwa chokoleti ina kakao iitwayo polyphenol, ambayo inakinga dhidi ya ugonjwa wa mishipa ya damu na kansa. Isitoshe, inasemekana kwamba chokoleti husaidia kinga ya mwili kufanya kazi ifaavyo na hutuliza mwili baada ya kupatwa na mashinikizo mbalimbali. Profesa Hiroshige Itakura wa Chuo Kikuu cha Kikristo cha Ibaraki anasema hivi: “Chokoleti bora yenye kakao nyingi na sukari kidogo na mafuta kidogo ni yenye manufaa zaidi.” Hata hivyo, profesa huyo alisisitiza kwamba ni muhimu kula “mboga zenye rangi ya kijani-kibichi na manjano na protini zenye aina tofauti-tofauti za polyphenol,” ambazo mwili huhitaji.

Urefu wa Maisha

Ijapokuwa watafiti fulani wanatumaini kwamba watu kwa ujumla wataweza kutarajia kuishi kwa muda wa miaka 100 wakati ujao, bado ni vigumu sana kufanya urefu wa maisha uzidi miaka 80. Kulingana na gazeti la The Globe and Mail la Kanada, wataalamu wanasema “hatuwezi kutarajia kwamba maisha yetu yataweza kurefushwa sana kwa ghafula isipokuwa wanasayansi wa tiba wakigundua matibabu ya bei nafuu yanayoweza kubadili hali ya kuzeeka. Hadi wakati huo, tuwe tunaboresha maisha yetu kadiri gani au tunameza vidonge vingi vya vitamini au homoni kadiri gani, bado urefu wa maisha yetu hautabadilika sana.” Kwa habari ya urefu wa maisha, Kanada ilikuwa namba 12 kwenye orodha yenye nchi 191 iliyotayarishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni mwaka uliopita. Huko Kanada, wanaume wanatarajiwa kuishi miaka 70 na wanawake miaka 74 wakiwa na afya nzuri. Ripoti hiyo ikasema kwamba Wajapani wanaonwa kuwa wenye afya bora ulimwenguni, kwa kuwa wanatarajiwa kuishi miaka 75 wakiwa na afya nzuri.

Kaburi la Chaza Wakubwa

Gazeti la El Comercio linaripoti kwamba zaidi ya visukuku vya chaza 500 wakubwa, baadhi yake vikiwa na mzingo wa meta 3.5 na uzito wa kilogramu 300, vilipatikana huko Acostambo, Peru, kwenye mwinuko wa meta 3,750. Mwanasayansi Arturo Vildozola aligundua kaburi hilo la chaza lililokuwa umbali wa meta chache tu kutoka kwa barabara ya katikati ya mji wa Pampas na Colcabamba. Chaza hao hawakuwa wamegunduliwa ijapokuwa walikuwapo kwa miaka mingi. Ugunduzi huo unathibitisha kwamba zamani za kale bahari ilifunika safu ya milima ya Andes.

Harufu ya “Gari Jipya”

Usemi “nyumba zinazosababisha ugonjwa” unatumiwa mara kwa mara huko Japani kurejezea nyumba mpya zenye vifaa vinavyotoa kemikali zinazodhuru afya. Lakini gazeti la The Daily Yomiuri linasema kwamba vifaa vya magari mapya vilevile vinatoa kiasi kikubwa cha kemikali zenye sumu. Watafiti kwenye Taasisi Kuu ya Afya ya Umma ya Osaka walipata kwamba kiwango cha kemikali zinazodhuru afya katika gari moja jipya kilizidi kiwango kinachoruhusiwa katika nyumba mara 34. Shirika la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ndilo linaloweka viwango hivyo. Hata baada ya kutumia gari kwa mwaka mmoja, kiwango cha kemikali kilizidi kiwango kinachoruhusiwa baada ya muda kupita. Iwao Uchiyama wa Taasisi ya Afya ya Umma ya Taifa anasema hivi: “Uwe mwangalifu unapokaa katika gari kwa muda mrefu.” Vipi? Akasema: “Ikiwa hewa inaingizwa garini, kemikali hizo zinaweza kwisha haraka zaidi garini kuliko katika nyumba.”

Vijana Wanaopata Mimba Marekani

Gazeti la U.S.News & World Report linasema kwamba “vijana wengi zaidi wanapata mimba huko Marekani kuliko katika nchi nyingine zilizoendelea.” Inakadiriwa kwamba, vijana milioni moja, wenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 19, wanapata mimba kila mwaka kule Marekani. Asilimia 25 ya vijana hao watazaa mtoto mwingine kabla ya miaka miwili kwisha baada ya kuzaa mtoto wa kwanza. Tarakimu za mwaka wa 1997 zinaonyesha kwamba asilimia 20 ya watoto waliozaliwa huko Mississippi walizaliwa na mama vijana, na jimbo la Massachusetts lilikuwa na kiwango cha chini zaidi (asilimia 7.2). Sehemu yenye vijana wengi zaidi waliopata mimba ilikuwa sehemu inayoitwa Bible Belt (Kanda ya Biblia), sehemu ya kusini mwa Marekani.

Wazee Wanatendwa kwa Ukatili Nyumbani

Gazeti la O Estado de S. Paulo linaripoti hivi: “Wazee hutendwa kwa ukatili mara nyingi kwa sababu ya mabishano juu ya mali.” Uchunguzi wa malalamiko yaliyopelekwa kwa polisi huko São Paulo, Brazili, kati ya mwaka wa 1991 na 1998 ulionyesha kwamba watu wa ukoo—watoto, wajukuu na wenzi wao, na wengine—walihusika katika asilimia 47 ya kesi hizo. “Kwa kawaida, mzee huumizwa kimwili na kiakili wengine wanapojaribu kumlazimisha kuwagawia watu wa ukoo mali yake akiwa hai,” akasema profesa João Estêvão da Silva ambaye ni mwendesha-mashtaka. Nyakati nyingine wazee huachwa bila huruma kwenye hospitali za Serikali na makao ya wazee ili kuokoa fedha. “Wazee wanakuwa mzigo kwa sababu ya umaskini, na hilo linatokeza uhasama,” akaeleza Silva.