Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jamii Mbalimbali—Hutegemeza Uhai

Jamii Mbalimbali—Hutegemeza Uhai

Jamii Mbalimbali—Hutegemeza Uhai

KATIKA miaka ya 1840, idadi ya wakazi wa Ireland ilizidi milioni nane, na hivyo ikawa nchi yenye watu wengi zaidi huko Ulaya. Chakula kikuu nchini humo kilikuwa viazi, na viazi vya jamii ya lumpers ndivyo vilivyokuzwa kwa wingi sana.

Mnamo mwaka wa 1845 wakulima walipanda viazi hivyo kama kawaida, lakini ugonjwa unaosababishwa na kuvu uliharibu karibu viazi vyote vilivyopandwa. “Wakazi wengi wa Ireland waliokoka mwaka huo wenye shida,” akaandika Paul Raeburn katika kitabu chake The Last Harvest—The Genetic Gamble That Threatens to Destroy American Agriculture. “Tatizo hilo lilizuka tena mwaka uliofuata. Wakulima hawakuwa na la kufanya ila kupanda viazi hivyo tena. Hawakuwa na aina nyingine za viazi. Ugonjwa huo ulizuka tena, lakini ulisababisha uharibifu mkubwa hata zaidi pindi hii. Watu waliteseka sana.” Wanahistoria wanakadiria kwamba watu wapatao milioni moja walikufa njaa, ilhali watu milioni 1.5 walihama, wengi wao wakaenda Marekani. Waliobaki walikuwa maskini hohehahe.

Katika Andes huko Amerika Kusini, wakulima walipanda viazi vya aina mbalimbali, na ni aina chache tu zilizoathiriwa na ugonjwa wa kuvu. Kwa hiyo, ugonjwa huo haukusambaa. Ni wazi kwamba ukuzaji wa jamii na aina mbalimbali za mimea ni ulinzi. Ukuzaji wa aina moja tu ya mimea unakiuka mbinu hii ya kuhifadhi mimea. Na hivyo mimea huwa katika hatari ya kushambuliwa na magonjwa au wadudu ambao wanaweza kuharibu kabisa mavuno yote. Ndiyo sababu wakulima wengi hutumia sana dawa za kuua wadudu-waharibifu, dawa za kuangamiza magugu na kuvu, hata ingawa mara nyingi dawa hizo huwa hatari sana kwa mazingira.

Basi kwa nini wakulima hukuza zao moja tu badala ya mimea mbalimbali ya kienyeji waliyo nayo? Kwa kawaida, wanafanya hivyo kwa sababu ya mikazo ya kiuchumi. Kupanda zao la aina moja hurahisisha kazi ya uvunaji, huboresha bidhaa, huzuia mimea kuharibika, na huongeza uzalishaji. Kilimo hicho kilianza kuenea sana katika miaka ya 1960 kupitia zile zilizojulikana kama harakati za kuboresha uzalishaji.

Harakati za Kuboresha Uzalishaji

Kupitia kampeni kubwa za serikali na mashirika, wakulima katika nchi zinazokumbwa na njaa walisihiwa wakuze nafaka za aina moja zinazozaa sana, hasa mpunga na ngano badala ya mimea mbalimbali. Nafaka hizo zinazozaa sana zilisifiwa kuwa suluhisho la njaa duniani. Lakini zilikuwa ghali sana—bei yake ilikuwa mara tatu zaidi ya bei ya mbegu za kawaida. Mavuno yalitegemea sana kemikali zilizotumiwa, kutia ndani mbolea, pamoja na vifaa vyenye gharama ya juu sana kama vile trekta. Hata hivyo, harakati za kuboresha uzalishaji zilipamba moto kwa msaada wa fedha kutoka kwa serikali. “Ingawa harakati hizo zimeokoa mamilioni wasife njaa,” asema Raeburn, “[sasa] zinahatarisha hifadhi ya chakula ulimwenguni.”

Kwa kweli, ni kana kwamba harakati hizo zilileta faida ya muda na kusababisha hasara ya kudumu. Ukuzaji wa mazao ya aina moja ukaenea upesi katika mabara yote—ingawa utumiaji wa mbolea nyingi ulifanya magugu yasitawi sana, na dawa za kuua wadudu-waharibifu ziliangamiza wadudu na wanyama muhimu pia. Katika mashamba ya mpunga, kemikali zenye sumu ziliua samaki, uduvi, kaa, vyura, mitishamba na mimea-mwitu, vingi vikiwa ni vyakula muhimu vya ziada. Baadhi ya wakulima waliathiriwa na sumu ya kemikali walizokuwa wakitumia.

Mwalimu mmoja katika Idara ya Biolojia ya Chuo Kikuu cha Open katika Muungano wa Uingereza, Dakt. Mae-Wan Ho, aliandika hivi: “Sasa ni wazi kabisa kwamba ukuzaji wa mimea ya aina moja ulioanzishwa katika ‘Harakati za Kuboresha Uzalishaji,’ umeathiri sana ukuzaji wa mimea ya aina mbalimbali na hifadhi ya chakula ulimwenguni pote.” Kulingana na Shirika la UM la Chakula na Kilimo, asilimia 75 ya chembe mbalimbali za urithi katika mimea iliyopandwa karne moja iliyopita sasa zimetoweka, hasa kwa sababu ya mbinu za kilimo cha mashamba makubwa.

Kichapo kimoja kinachochapishwa na Taasisi ya Worldwatch kinaonya kwamba “kukuza mimea ya aina moja kunasababisha hatari kubwa sana ya kiikolojia.” Tunaweza kupunguzaje hatari hizo? Wakulima wanahitaji msaada wa kifedha, msaada wa wataalamu wa kilimo, na wanahitaji pia kemikali zenye nguvu. Lakini bado hakuna tumaini. Ukuzaji wa mimea ya aina moja ulichangia sana ugonjwa wa kuvu ulioharibu mahindi nchini Marekani na mashamba ya mpunga yenye ukubwa wa ekari nusu milioni nchini Indonesia. Hata hivyo, harakati mpya ya kilimo imebuniwa katika miaka ya karibuni. Inahusisha kubadili maumbile ya mimea—kubadili umbo la chembe zake za urithi.

Harakati za Kubadili Maumbile ya Mimea

Uchunguzi wa chembe za urithi umetokeza taaluma mpya inayoitwa biotekinolojia. Kama jina hilo linavyodokeza, taaluma hiyo huchanganya biolojia na tekinolojia ya kisasa kupitia mbinu kama vile kubadili chembe za urithi za vitu vilivyo hai (genetic engineering). Baadhi ya yale yanayoitwa makampuni mapya ya biotekinolojia, hukazia mno kilimo na yanajitahidi sana kupata idhini maalumu ya kutokeza mbegu zinazozaa sana, zinazokinza magonjwa, ukame, baridi kali, na zinazopunguza matumizi ya kemikali hatari. Ingenufaisha sana kama miradi hiyo ingeweza kutimizwa. Lakini watu fulani wana wasiwasi kuhusu mazao yaliyobadilishwa maumbile.

Kitabu Genetic Engineering, Food, and Our Environment chasema kwamba “mbinu ya kutokeza mimea ya jamii mbalimbali ina mipaka ya kiasili.” “Ua la waridi laweza kuchavushwa na ua jingine la waridi, lakini ua la waridi haliwezi kamwe kuchavushwa na kiazi. . . . Kwa upande mwingine, kubadili maumbile kwa kawaida huhusisha kuchukua chembe za urithi za jamii moja na kuzitia katika jamii nyingine kwa madhumuni ya kutokeza tabia fulani za pekee. Kwa mfano, huenda hilo likamaanisha kuchukua chembe ya urithi kutoka kwa samaki wa aktiki ambayo inaweza kutokeza kemikali isiyoganda, na kuitia katika kiazi ama stroberi ili ziweze kustahimili baridi kali. Sasa mimea inaweza kutiwa chembe za bakteria, virusi, wadudu, wanyama au hata za wanadamu.” * Hivyo basi, biotekinolojia inawaruhusu wanadamu kuvuka mipaka ya kiasili inayobainisha chembe za urithi za jamii mbalimbali.

Sawa na harakati za kuboresha uzalishaji, zile zinazoitwa na watu fulani harakati za kubadili maumbile hutokeza chembe za urithi za aina moja tu—watu wengine wanasema hali hiyo ni mbaya hata zaidi kwa sababu wataalamu wa chembe za urithi wanaweza kutokeza kiumbe kwa chembe bila kujamiiana au kupitia ukuzaji wa tishu. Mbinu hizo hutokeza viumbe wanaofanana kabisa au viumbe pacha. Kwa hiyo, wengi wangali wanahangaishwa na kudidimia kwa ukuzaji wa aina mbalimbali za mimea. Hata hivyo, mimea iliyobadilishwa maumbile imezusha masuala mapya, kama vile athari za mimea hiyo kwa wanadamu na mazingira. “Tunaingia hima-hima bila kufikiri katika muhula mpya wa biotekinolojia ya kilimo tukiwa na matumaini makubwa, bila kujizuia sana, na bila kujua matokeo yake,” akasema mwandishi wa sayansi Jeremy Rifkin. *

Kwa upande mwingine, kuweza kubadilisha maumbile ya chembe za urithi ni hatua inayoweza kunufaisha sana. Hivyo basi, makampuni yanashindana kupata idhini maalumu ya kutokeza mbegu mpya na mimea mingine iliyobadilishwa maumbile. Kwa sasa, mimea inaendelea kutoweka kwa kasi sana. Kama ilivyotajwa awali, serikali na mashirika fulani ya kibinafsi yameanzisha hifadhi za mbegu ili kuzuia msiba. Je, hifadhi hizo zitawezesha vizazi vijavyo viwe na mbegu mbalimbali za kupanda na kuvuna?

Hifadhi za Mbegu —Je, Zitazuia Mimea Kutoweka?

Bustani ya Royal Botanic Gardens huko Kew, Uingereza, imeanzisha ule unaosifiwa kuwa “mojawapo ya miradi mikubwa zaidi ya kimataifa ya kuhifadhi”—Mradi wa Hifadhi ya Mbegu za Milenia. Malengo makuu ya mradi huo ni (1) kukusanya na kuhifadhi asilimia 10, yaani zaidi ya jamii 24,000 za mimea yenye mbegu ulimwenguni kufikia mwaka wa 2010 na (2) kabla ya hapo, kukusanya na kuhifadhi mbegu za mimea ya kienyeji katika Muungano wa Uingereza. Nchi nyingine zimeanzisha pia hifadhi za mbegu ambazo huitwa nyakati nyingine, hifadhi za chembe za urithi.

Mwanabiolojia John Tuxill anasema kwamba angalau asilimia 90 ya mamilioni ya mbegu zinazotunzwa katika hifadhi hizo ni za mimea muhimu inayotokeza bidhaa na chakula, kama vile ngano, mchele, mahindi, mtama, viazi, vitunguu, vitunguu saumu, miwa, pamba, maharagwe ya soya, na maharagwe mengineyo, na kadhalika. Lakini mbegu ni vitu vilivyo hai ambavyo hudumu tu maadamu havijanyauka. Basi je, hifadhi za mbegu zinaweza kutegemewa?

Matatizo Yanayokumba Hifadhi Hizo

Utunzaji wa hifadhi za mbegu unagharimu pesa nyingi—Tuxill asema kwamba kila mwaka unagharimu jumla ya dola milioni 300 za Marekani. Hata hivyo, yeye asema kwamba huenda hata kiasi hicho hakitoshi, kwa kuwa “ni asilimia 13 tu ya mbegu zilizohifadhiwa zilizo kwenye mabohari yanayotunzwa ifaavyo na yanayoweza kutunza mbegu kwa muda mrefu.” Kwa kuwa mbegu zisizohifadhiwa ifaavyo hazidumu, ni lazima zipandwe mapema ili mbegu zitakazovunwa ziweze kuhifadhiwa; la sivyo, mbegu hizo huharibika. Bila shaka kuhifadhi mbegu ni kazi kubwa sana. Mabohari yaliyopo hayawezi kutosheleza uhitaji huo wala hakuna pesa za kutosha kuyadumisha.

Kitabu Seeds of Change—The Living Treasure chaeleza kwamba Maabara ya Kitaifa ya Kuhifadhi Mbegu huko Colorado, Marekani, “imekumbwa na matatizo mengi, kutia ndani ukosefu wa nguvu za umeme, friji zilizoharibika, na upungufu wa wafanyakazi na hivyo marundo makubwa ya mbegu yameachwa kiholelaholela bila kupangwa kulingana na jamii.” Hifadhi za mbegu huathiriwa pia na misukosuko ya kisiasa, kuzorota kwa uchumi, na misiba ya asili.

Kuhifadhi mbegu kwa muda mrefu hutokeza matatizo mengine pia. Katika mazingira ya asili, mimea inaweza kustahimili hali mbalimbali kwa kadiri fulani, na hivyo huweza kukinza magonjwa na hali nyingine ngumu. Lakini mbegu zikihifadhiwa katika mabohari kwa muda fulani, huenda zikashindwa kukinza magonjwa. Hata hivyo, mbegu za mimea mingi zinazohifadhiwa ifaavyo zinaweza kudumu kwa karne nyingi kabla ya kupandwa. Licha ya vizuizi hivyo na magumu mengine, ujenzi wa hifadhi za mbegu unaonyesha wasiwasi mkubwa uliopo kuhusu kutoweka kwa mazao.

Bila shaka, njia bora ya kuzuia mimea kutoweka ni kulinda mazingira ya asili na kupanda mazao mbalimbali. Lakini ili kufanya hivyo, asema Tuxill, tunahitaji “kusitawisha usawaziko mpya kati ya mahitaji ya wanadamu na ya mazingira ya asili.” Lakini je, ni jambo la akili kutarajia kwamba wanadamu “watasitawisha usawaziko mpya” kati yao na mazingira ya asili huku wakijikakamua sana kuboresha viwanda na uchumi? Na kama tulivyoona, hata kilimo kimeathiriwa na biashara kubwa zinazotegemea tekinolojia ili kupata faida kubwa. Lazima kuwe na suluhisho jingine.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Bado kuna ubishi mkali kuhusu jinsi vyakula vilivyobadilishwa maumbile vinavyoweza kuathiri mazingira, afya ya wanadamu na ya wanyama. Kuchanganya chembe za urithi za viumbe wa jamii tofauti kabisa kumewafanya wengine watilie shaka uhalali wa jambo hilo.—Ona Amkeni!, Aprili 22, 2000, ukurasa wa 25-27.

^ fu. 14 Gazeti la New Scientist laripoti kwamba viazi-sukari vya Ulaya “vilivyobadilishwa maumbile ili vikinze dawa moja ya kuua magugu, vimekuwa na chembe zisizotarajiwa za kukinza dawa nyingine.” Chembe hizo za ajabu zilitokea wakati viazi-sukari vilipochavushwa bila mpango na aina nyingine ya kiazi-sukari kilichobadilishwa maumbile ili kikinze dawa tofauti ya kuua magugu. Baadhi ya wanasayansi wanahofu kwamba kuenea kwa mimea ambayo inakinza dawa za kuua magugu kwaweza kutokeza magugu sugu ambayo hayawezi kuangamizwa kwa dawa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Je, Mkulima Yumo Taabani?

“Tangu mwaka wa 1950, idadi ya watu walioajiriwa katika sekta ya kilimo imepungua sana katika nchi zote zilizositawi kiviwanda. Idadi hiyo imepungua kwa zaidi ya asilimia 80 katika nchi nyingine,” lasema jarida la World Watch. Kwa mfano, idadi ya wafungwa nchini Marekani ni kubwa kuliko idadi ya wakulima. Mbona wengi wanaacha ukulima?

Sababu kuu ni upungufu wa mapato, madeni mengi, ufukara, na ongezeko katika utumizi wa mashine mbalimbali za kilimo. Mnamo mwaka wa 1910, wakulima nchini Marekani walipokea senti 40 hivi kwa kila dola iliyotumiwa kununua chakula, lakini kufikia mwaka wa 1997, mapato ya wakulima yalikuwa yamepungua kufikia senti 7 hivi. Mkulima wa ngano, lasema jarida la World Watch, “hupata senti 6 hivi tu kutoka kwa kila mkate unaonunuliwa.” Hilo lamaanisha kwamba wateja humlipa mkulima wa ngano kiasi kama kile wanacholipa kwa ajili ya karatasi ya kufungia mkate. Katika nchi zinazositawi, hali ya wakulima ni mbaya hata zaidi. Mkulima nchini Australia au Ulaya anaweza kuomba mkopo kutoka kwa benki ili kukabiliana na wakati mgumu; huenda mkulima wa Afrika Magharibi asiweze kupanda zao hilo tena. Huenda hata akashindwa kukabiliana na hali hiyo ngumu.

[Picha katika ukurasa wa 7]

“Ukuzaji wa mimea ya aina moja ulioanzishwa katika ‘Harakati za Kuboresha Uzalishaji’ umeathiri sana ukuzaji wa mimea ya aina mbalimbali na hifadhi ya chakula ulimwenguni pote.”—Dakt. Mae-Wan Ho

[Hisani]

Mandhari ya nyuma: U.S. Department of Agriculture

Centro Internacional de Mejoramiento de Maíz y Trigo (CIMMYT)

[Picha katika ukurasa wa 8]

Hifadhi ya Mbegu za Milenia, huko Uingereza, inahifadhi mbegu za mimea muhimu

[Hisani]

© Trustees of Royal Botanic Gardens, Kew