Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jiji la Afrika Lenye Watu wa Mashariki na Magharibi

Jiji la Afrika Lenye Watu wa Mashariki na Magharibi

Jiji la Afrika Lenye Watu wa Mashariki na Magharibi

Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Afrika Kusini

INAFURAHISHA kama nini kutembea kwenye barabara za Durban! Utaona watu wengi, hasa vijana, wamevaa mavazi yenye mitindo ya Magharibi. Lakini, tazama pia wanawake wazee Wazulu ambao wamevalia nguo ndefu na vitambaa vyenye rangi nyangavu kichwani. Pia, kuna wanawake Wahindi ambao wamevalia sari au mavazi ya Wapunjabi. Unapokaribia pwani, yamkini utawaona wanaume kadhaa Wazulu wanaokokota riksho ambao wamevalia mavazi yenye madoido. Bila shaka, Durban lenye watu wa Mashariki na Magharibi ni jiji la kipekee la Afrika. Jiji hilo lenye kuvutia lilianzaje?

Jiji la Durban la Afrika Kusini limekaliwa kwa miaka mia mbili hivi. Wazungu wakoloni 40 hivi walihamia eneo hilo na kulifanya makao yao mwaka wa 1824. Wakati huo, ufalme wenye nguvu wa Wazulu ulikuwa unatawala kutoka kaskazini ya Durban na ulitawaliwa na Shaka, mfalme aliyekuwa shujaa wa vita. Miaka 20 baadaye, Durban na eneo la karibu la barani lilitekwa na Uingereza. Wakoloni hao wapya na Wazulu walipigana vita mara kadhaa katika karne ya 19.

Wakoloni Waingereza waligundua wakati uleule kwamba miwa ilisitawi sana katika sehemu za pwani. Walileta vibarua kwa mashamba yao ya miwa kutoka India, iliyokuwa koloni nyingine ya Uingereza wakati huo. Wahindi zaidi ya 150,000 walikuja Durban kati ya mwaka wa 1860 na 1911. Kwa hiyo, wale wakazi zaidi ya milioni tatu wanaoishi Durban leo wanatoka sehemu tatu tofauti za dunia—kuna wenyeji Wazulu, Wahindi kutoka India, na Wazungu kutoka Uingereza na Ulaya magharibi.

Jiji hilo lina mambo mengine yenye kupendeza. Kama unavyoweza kuona katika picha, kuna sehemu nyembamba ya ardhi yenye mwinuko mkali inayoitwa Bluff inayotenga bandari ya asili na Bahari ya Hindi. Ardhi hiyo yenye kuvutia ina urefu unaozidi meta 90 na mimea inasitawi juu yake. Kila siku meli kubwa huingia katika bandari hiyo iliyokingwa. Kitabu Discovery Guide to Southern Africa kinaeleza kwamba bandari ya Durban ni “bandari kubwa na yenye shughuli nyingi kushinda zote huku Afrika, na ni ya tisa kwa ukubwa ulimwenguni.” Watalii wanavutiwa na pwani bora ya Durban nao wanafurahia maji yake yenye uvuguvugu. Kuna mahali panapofaa pa kufanya mchezo wa kuteleza kwa ubao kwenye mawimbi, na wanaotaka kuogelea wanatulia wakijua kwamba kuna nyavu za kuzuia papa.

Wale wanaopenda Biblia wana sababu nyingine ya kupendezwa na jiji hilo. Wanafunzi wa Biblia, kama vile Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo, walianzisha ofisi ya tawi huko mwaka wa 1910. Kisha, mkusanyiko wa kwanza wa Wanafunzi wa Biblia huku Afrika ulifanywa Durban mnamo Aprili 1914. Watu 50 hivi walihudhuria, kukiwepo watu kutoka sehemu za mbali za Afrika Kusini. Waabudu wapya 16 walibatizwa kwenye mkusanyiko huo wa pekee. Baadhi ya wale waliohudhuria walikuwa Wakristo watiwa mafuta waliodumisha uaminifu hadi kifo. Mmojawapo alikuwa William W. Johnston, aliyekuwa msimamizi wa kwanza wa ofisi ya tawi katika Afrika.

Mashahidi wa Yehova wamekuwa na mikusanyiko mingine mingi huko Durban tangu mwaka wa 1914. Mnamo Desemba 2000, watu 14,848 walihudhuria mikusanyiko miwili ya “Watekelezaji wa Neno la Mungu” iliyofanywa jijini Durban, na wapya 278 wakabatizwa. Fikiria familia moja ya Wahindi iliyohudhuria. Miaka 10 iliyopita, Somashini alimsaidia baba yake, Alan, kupata kweli ya Biblia. Alan alijaribu kuacha ulevi na alikuwa akitafuta kusudi la maisha. Somashini, aliyekuwa na umri wa miaka mitatu tu, alimletea baba yake kitabu alichokuwa amepata katika nyumba ya jirani fulani. Mara moja Alan alipendezwa na kichwa chake, Amani na Usalama wa Kweli—Wewe Unaweza Kuupataje? Alifurahia yale aliyosoma, na akaanza kushirikiana na Mashahidi wa Yehova. Kweli ya Biblia ilimchochea Alan ahalalishe ndoa yake. Punde si punde, mkewe, Rani, alipendezwa na akaanza kuhudhuria mikutano ya Mashahidi wa Yehova vilevile. Wakati huo, Alan na Rani waliishi kwa wazazi wa Rani, ambao ni washiriki wa mojawapo ya makanisa ya Jumuiya ya Wakristo. Wazazi wa Rani walipinga imani yao mpya na kuwapa sharti la mwisho: “Ama mwache Mashahidi ama mwondoke nyumbani mwetu!”

Alan na Rani waliamua kuondoka ijapokuwa haikuwa rahisi kupata makao. Marafiki fulani miongoni mwa Mashahidi wa Yehova waliwasaidia kupata mahali pazuri pa kuishi. Alan na Rani walibatizwa mwaka wa 1992. Waliendelea kufanya maendeleo na leo Alan anatumikia akiwa mzee katika kutaniko la Kikristo.

Kuna zaidi ya makutaniko 50 ya Mashahidi wa Yehova jijini Durban. Makutaniko mengi yana washiriki Wazulu tu. Hata hivyo, makutaniko kadhaa yaliyo katikati ya jiji, yana washiriki Wazulu, Wahindi, na Wazungu. Ukihudhuria mojawapo ya mikutano yao, utaona mengi kuliko tu watu wa Mashariki na Magharibi. Huenda Shahidi yeyote ambaye amevalia vizuri atasimamia mkutano awe ni Mwafrika, Mhindi au Mzungu. Lakini jambo moja ni wazi: Kwa kutazama wasikilizaji utaona kwamba Biblia ina nguvu ya kuunganisha watu wa mataifa yote wawe na urafiki mchangamfu unaodumu.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Watu wa jamii zote huhudhuria mikutano ya kutaniko pamoja

[Picha katika ukurasa wa 26]

Alan, Rani, na watoto wao

[Picha katika ukurasa wa 26]

Jengo la baraza la mji huko Durban

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Picha: Courtesy Gonsul Pillay