Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kente Nguo ya Wafalme

Kente Nguo ya Wafalme

Kente Nguo ya Wafalme

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI GHANA

MIKONO ya mfumaji inasogea haraka-haraka juu ya kitambaa. Fundi huyo anaangalia kwa makini kitambaa chembamba kirefu cha rangi nyang’avu kilicho mbele yake, akifanya kazi kufuatana na mdundo wa kitanda cha mfumi. Anashikilia kamba katikati ya vidole vyake vya miguu; kamba hizo husogeza vijiti—ambavyo husogea juu na chini vikitenganisha na kuendesha nyuzi zenye urefu wa meta sita zinazoitwa mitande. * Mfumaji hutokeza mapambo kwa kufuma kwa uangalifu uzi mmoja-mmoja wa hariri wenye rangi nyangavu katikati ya nyuzi za mitande zilizotenganishwa.

Kitambaa kinachofumwa ni chenye upana wa sentimeta kumi tu. Lakini kina rangi mbalimbali nyangavu na mapambo tata. Fundi anatabasamu kwa furaha anapochunguza kazi yake—nguo halisi ya kente.

Ufundi wa Kale

Mafundi stadi wamekuwa wakifanya kazi ya kufuma kwa maelfu ya miaka. Sikuzote nyuzi za kitani, pamba, na hariri zimepatikana kwa wingi. Rangi mbalimbali zilitengenezwa kwa mizizi na majani ya mimea, na mfumaji aliweza kuzitumia kutengeneza nguo zenye mapambo sahili.

Wafumaji miongoni mwa watu wahamaji wa Afrika walibuni vitanda vya mfumi vilivyokuwa vidogo na rahisi kusafirisha. Vifaa hivyo vilitumiwa kufuma kitambaa chembamba chenye upana wa sentimeta 7.5 hadi 11.5. Kisha vitambaa hivyo vyembamba vilishonelewa pamoja ili kutengeneza kitambaa kimoja kikubwa kilichotumiwa kama vazi. Wanyama wa kubeba mizigo walivuka majangwa, mito, na safu za milima mirefu wakibeba vitanda hivyo vya mfumi. Vilisafirishwa na wafanyabiashara wa kale navyo viliwasaidia sana watu waliovitumia.

Tamaa ya Kitambaa

Wafalme na machifu wa Afrika Magharibi walitawala kwa karne nyingi ile nchi yenye madini nyingi ambayo wavumbuzi Wazungu waliiita Gold Coast. * Wafalme wa Waashanti na familia zao walitajirishwa sana kwa dhahabu nyingi iliyochimbwa huko. Wafalme hao na machifu wao wakuu walivalia vito vya dhahabu na nguo ya pekee ili kuonyesha utajiri, nguvu, na mamlaka zao mbele ya raia wao. Nguo ya pekee ambayo watawala hao walivalia ilikuja kuitwa kente. Huenda iliitwa hivyo kwa sababu ya ufumaji wake uliofanana na ufumaji wa kikapu. Wafumaji wa makabila mengine ya Gold Coast walifuma vitambaa vyembamba pia, lakini kwa wafalme Waashanti, nguo ya kente iliwakilisha sifa na cheo cha kifalme.

Wafumaji wa Gold Coast walitumia pamba iliyosokotwa nchini humo. Ni nyuzi za samawati tu zilizopatikana. Nyuzi hizo za samawati zilifumwa katika nguo nyeupe ya pamba ili kutokeza mapambo ya mistari na miraba kwenye nguo za wenyeji wa huko.

Watu wa kawaida hawakuruhusiwa kuvaa nguo ya kifalme ya kente iliyofumwa kwa njia bora kabisa. Vikundi vya wafumaji stadi wa kifalme vilianzishwa ili kutengeneza nguo bora za hali ya juu. Mbinu ya kufuma nguo hizo ilifichwa kabisa isijulikane. Wafumaji wengine wote walikatazwa kufuma mapambo yaliyokuwa ya mfalme na nyumba yake pekee. Mfalme alikuwa na nguo nyingi sana, kila moja ilikuwa na mapambo yake ya kipekee. Kulingana na mapokeo, mfalme alivalia nguo tofauti kila alipotokea hadharani.

Kutafuta Nyuzi Zenye Rangi

Aina nyingine ya nguo ilianza kupatikana huko Gold Coast katika karne ya 16. Nguo hiyo mpya haikufumwa kwenye vitanda vya mfumi vya Afrika bali ilitengenezwa katika nchi za mbali na kuletwa na mabaharia wa kwanza Wazungu waliokuja kutafuta pembe za ndovu, dhahabu, na watumwa. Nguo hiyo ilikuwa na nyuzi zenye rangi nyingi nyangavu za kuvutia. Punde si punde, nguo hizo zenye rangi nyekundu, manjano, na kijani kibichi zikawa bidhaa muhimu za biashara. Watu wachache sana walikuwa na mali za kutosha kujipatia nguo hiyo ghali kutoka kwa wafanyabiashara Wazungu. Waashanti matajiri waliosafirisha dhahabu, pembe za ndovu, na watumwa kwenye majahazi yaliyokuwa yanangojea pwani ndio tu waliokuwa na mali za kutosha kujipatia nguo hiyo. Hata hivyo, wafalme wa Waashanti na machifu wao hawakutaka nguo hiyo.

Wafumaji walipopata nguo hiyo waliondoa kwa uangalifu nyuzi zenye rangi walizotaka na kutupa nguo iliyobaki. Nyuzi hizo zilifumwa tena na wafumaji wa mfalme. Nyuzi za rangi tofauti-tofauti zilipopatikana, ufundi na mapambo mapya yalibuniwa, na mafundi waliweza kuboresha sana ubunifu na ufumaji wao. Wafumaji stadi wa makabila mengine waliajiriwa na wafalme wa Waashanti, kwa hiyo nguo ya kente ikawa nguo bora isiyo na kifani.

Mapambo ya maumbo yaliyofanana na samaki, ndege, matunda, majani, machweo, pinde za mvua, na mambo mengine ya asili, yalifanyiza sanaa ya ufumaji iliyokuwa yenye mambo mengi madogo-madogo na iliyokuwa na maana mahususi. Nguo iliyokuwa na uzi wa dhahabu ilifananisha utajiri, nguo yenye uzi wa kijani kibichi ilifananisha kitu kipya, nyeusi ilifananisha huzuni, nyekundu ilifananisha hasira, na nguo ya fedha ilifananisha utakato na shangwe.

Wafumaji walifanya kazi kwa subira na bila haraka kwa miezi mingi ili kumaliza nguo moja tu wakijua kwamba nguo waliyotengeneza ingeonyesha stadi zao na ubunifu wao. Nguo hiyo bora ya kente ilikuwa ghali sana kwa hiyo ni watu wachache tu walioweza kuinunua.

Nguo ya Kente ya Siku Hizi

Muda si muda, mamlaka ya wafalme na machifu ilipunguka. Hakukuwa tena haja ya kubainisha watu wa ukoo wa mfalme na watu wa kawaida kwa mavazi yao. Wengi zaidi walitaka kuinunua nguo hiyo ilipoanza kutumiwa na watu wa kawaida. Ubora, ufumaji, na bei ya nguo ya kente ilipungua ilipofumwa chapuchapu kwa sababu wengi walitaka kuinunua.

Leo, ufumaji wa nguo ya kente hufanyizwa kwa nyuzi zisizo za asilia na vitu vingi, kama vile mifuko, tai, mishipi, kofia, na mavazi hutengenezwa kwa wingi kutokana na nguo hizo zisizo asilia. Wafumaji wengi wa siku hizi hawafumi nguo ya kente jinsi walivyoifuma zamani. Nguo bora za kale za kente zimehifadhiwa na kupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine katika jamaa mbalimbali. Naam, zama zile za kufuma nguo bora ya kente iliyoitwa nguo ya wafalme kwenye vitanda vidogo sahili vya mfumi zimepita.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Mitande ni nyuzi zinazoingizwa kutoka juu hadi chini katika kitanda cha mfumi. Nyuzi nyingine huingizwa katikati ya mitande.

^ fu. 9 Inayoitwa Ghana leo.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Vitanda vya mfumi vya kufuma nguo nyembamba si vizito na ni rahisi kusafirisha

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mfumaji hutumia miguu yake kuendesha vijiti