Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Misitu ya Mvua

Nchini India, ilijulikana kwamba misitu ya mvua ilipatikana tu katika jimbo la kusini la Kerala. Hata hivyo, hivi majuzi mwanamazingira Saumyadeep Dutta aligundua eneo lenye msitu wa mvua lenye ukubwa wa kilometa 500 za mraba linalounganisha majimbo ya kaskazini-mashariki ya Assam na Arunachal Pradesh, laripoti gazeti la Down to Earth la New Delhi. Wanyama-pori wa aina nyingi huishi katika msitu huo—‘jamii 32 za mamalia na jamii 260 za ndege, kutia ndani jamii zisizopatikana sana kama vile ndovu, simba-milia na chui, kakakuona wa China, dubu aina ya sloth, mbawala aina ya sambar, sokwe aina ya hoolock, kwale, hondohondo, na aina fulani ya bata.’ Hata hivyo, kwa kuwa miti mingi hutumiwa sana ulimwenguni pote, misitu mingi ya mvua iko karibu kuangamizwa, lasema gazeti Down to Earth. Wataalamu fulani wa mambo ya asili wanahofu kwamba miti yote hiyo ikikatwa, maeneo yenye misitu ya mvua yatabadilishwa kuwa mashamba.

Mngurumo wa Simba-Milia

Kwa nini mngurumo wa simba-milia huwamaliza nguvu wanyama na watu fulani? Wanasayansi wa Taasisi ya Fauna ya Uchunguzi wa Mawasiliano huko North Carolina, Marekani, ‘wamethibitisha kwamba simba-milia hutokeza sauti ya chini sana, mngurumo wa chini sana hivi kwamba hauwezi kusikiwa na wanadamu,’ laripoti gazeti The Sunday Telegraph la London. Wanadamu wanaweza tu kusikia sauti zenye frikwensi ya zaidi ya hezi 20. Lakini, simba-milia ‘hutokeza mingurumo ya chini sana ya hezi zisizozidi 18 na kuiunganisha na mngurumo tunaoweza kusikia. Kulingana na Elizabeth von Muggenthaler, msimamizi wa taasisi hiyo, tokeo huwa kwamba wanadamu wanaweza kuhisi mngurumo wa simba-milia ambao unawamaliza nguvu kwa muda,’ laeleza gazeti hilo. Hata watu ambao wamewazoeza simba-milia kwa muda mrefu wametambua jambo hilo.

Kulainisha Nyama kwa Kutumia Vitu Vinavyolipuka

Kwa kawaida, wapishi hulainisha nyama kwa kuipiga-piga kwa nyundo ya mapishi au kwa kuongeza unga wenye vimeng’enya vya kulainisha nyama. Hata hivyo, watafiti huko Maryland, Marekani, wamefanya majaribio ya kulainisha nyama kwa kutumia mawimbi ya mshtuo, laripoti gazeti la New Scientist. Watafiti hao huweka nyama juu ya bamba la chuma, chini ya pipa la plastiki lililojazwa maji. Kisha wanawasha robo moja hivi ya msokoto wa baruti ndani ya pipa hilo. Ripoti hiyo yasema hivi: “Maji hupitisha wimbi la mshtuo linalolainisha nyama, lakini pipa hilo hulipuliwa kabisa.” Licha ya kulainisha nyama, mbinu hiyo huua bakteria, kama vile E. coli, zinazoweza kusababisha ugonjwa wa tumbo. Hata hivyo, kama anavyosema Randy Huffman wa Taasisi ya Nyama ya Marekani: “Tatizo hasa ni kutumia mbinu hiyo katika maisha ya kila siku.”

Meli Hueneza Magonjwa

Gazeti la The Daily Telegraph la London lasema hivi: “Maji yanayofanya meli iwe thabiti yanaeneza magonjwa ulimwenguni pote, na kuhatirisha wanadamu, wanyama na mimea.” Maji hayo hufanya meli iwe thabiti na kisha humwagwa baharini au bandarini. Nchini Marekani, watafiti wa Kituo cha Utafiti wa Mazingira cha Smithsonian huko Maryland waligundua kwamba maji hayo yanayobebwa na meli au vyombo vingine vya baharini huwa na bakteria na virusi vingi sana. Mimea iliyokuwa ndani ya maji hayo katika meli 15 zilizochunguzwa kwenye Ghuba ya Chesapeake, ilikuwa na bakteria inayosababisha ugonjwa wa kipindupindu. Kama ilivyotarajiwa, lita moja ya maji hayo ilikuwa na bakteria zipatazo milioni 830 na virusi milioni 7,400—mara sita hadi nane ya idadi ya viumbe wengine.

Vitu Vingi Mno vya Kuchezea

Gazeti la The Sunday Times la London laripoti hivi: “Kulingana na uchunguzi mpya, watoto wanapoteza uwezo wa kucheza vizuri kwa sababu wanapewa vitu vingi mno vya kuchezea.” Sababu moja ya uchunguzi huo ni kwamba watu huko Uingereza wanahangaikia jinsi “wazazi wanavyobadilisha kabisa maisha ya utotoni kwa kuwaachia watoto wao vitu vya kuchezea, kompyuta na televisheni badala ya kuwa pamoja nao.” Baada ya kuwachunguza watoto 3,000 wenye umri wa miaka mitatu hadi mitano, Profesa Kathy Sylva wa Chuo Kikuu cha Oxford alikata shauri hivi: “Wanapokuwa na vitu vingi vya kuchezea hawawezi kukaza fikira, na watoto wasipokaza fikira hawajifunzi kucheza vizuri.”

Kushuka Moyo Kazini

Gazeti The Guardian la London laripoti hivi: ‘Kuhangaika, kuchoka sana na kushuka moyo kumeongezeka sana kazini.’ Kwa mujibu wa Shirika la Wafanyakazi Ulimwenguni la UM, wafanyakazi 3 kati ya kila wafanyakazi 10 katika Muungano wa Uingereza wana matatizo ya akili, na mfanyakazi 1 kati ya kila wafanyakazi 10 nchini Marekani ameshuka moyo sana. Asilimia 7 hivi ya watu wanaostaafu mapema nchini Ujerumani ni wale walioshuka moyo. Zaidi ya nusu ya wafanyakazi nchini Finland wana dalili za mikazo. Nchini Poland, mahangaiko yanayosababishwa na idadi kubwa ya watu wanaokosa kazi yaliongezeka kwa asilimia 50 mnamo mwaka wa 1999, ilhali visa vya kujiua viliongezeka pia. Ripoti hiyo yaonyesha kwamba watu wengi sana watashuka moyo kwa sababu ya tekinolojia mpya zinazoendelea kutumiwa na mbinu mpya za usimamizi kazini. Na yaonya kwamba “kufikia mwaka wa 2020, saa za kazi zitapotea bure hasa kwa sababu ya mikazo na magonjwa ya akili wala si kwa sababu ya aksidenti za barabarani, UKIMWI na ujeuri.”

Hasara Inayoongezeka ya Uhalifu

Gazeti The Independent la London laripoti hivi: “Uhalifu katika Uingereza na Wales unagharimu jamii dola bilioni 85 za Marekani kila mwaka.” Idadi hiyo iliyofafanuliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani kuwa ni ya kadiri, ni asilimia 6.7 ya mapato ya jumla ya nchi hiyo. Mauaji na mauaji ya bila kukusudia ndiyo matendo ya uhalifu yanayosababisha hasara kubwa. Kwa wastani, kila mojawapo ya matendo hayo husababisha hasara ya zaidi ya dola milioni 1.4 nchini humo, ilhali kila mojawapo ya matendo mengine mabaya ya uhalifu wa kutumia jeuri husababisha hasara ya dola 27,000 kwa wastani. Upunjaji na udanganyifu husababisha robo moja hivi ya hasara ya jumla. Kiasi hicho hakihusishi “gharama zinazotumiwa kujilinda na uhalifu, hasara kwa familia za wahasiriwa, fedha zilizotumiwa na Serikali kuzuia uhalifu, . . . au gharama ya madai ya bima,” laongezea gazeti hilo.

Magugu Ni Bora Kuliko Dawa za Kuua Wadudu-Waharibifu

Wakulima wa Afrika Mashariki wanatumia magugu badala ya dawa za kuua wadudu-waharibifu ili kuboresha mazao yao ya mahindi, laripoti gazeti la New Scientist. Vitu viwili viharibifu huangamiza sana mazao ya mahindi ya wakulima wa Afrika Mashariki. Cha kwanza ni Striga, mmea unaoharibu mazao ya mahindi yenye thamani ya dola bilioni 10 za Marekani kila mwaka. Mtafiti wa Kenya Ziadin Khan aligundua kwamba wakati gugu linaloitwa desmodium linapopandwa kati ya safu za mahindi, mmea huo wa Striga haukui. Kitu cha pili kiharibifu ni mabuu ya mdudu aina ya stem borer. Kwa miaka mingi, mdudu huyo ameharibu theluthi moja ya zao la mahindi. Hata hivyo, Khan amegundua kwamba wadudu hao hupenda kula gugu fulani la kienyeji liitwalo napier. Wakulima huzuia mahindi yasishambuliwe na wadudu hao kwa kupanda gugu hilo katika mashamba yao. Umajimaji fulani unaonata kutoka kwenye nyasi hiyo huyanasa na kuyaua mabuu. Khan asema hivi: “Ni bora kuliko dawa za kuua wadudu-waharibifu, na haigharimu pesa nyingi. Imeongeza mazao ya hapa kwa asilimia 60 hadi 70.”

Udanganyifu wa Mwanaakiolojia

Mmojawapo wa wanaakiolojia bora nchini Japani ambaye amesifiwa kuwa mchimbaji bora sana kutokana na uvumbuzi wake unaoonekana kuwa wa kustaajabisha, amerekodiwa akidanganya. Shirika linalochapisha gazeti la Mainichi Shimbun lilitega kamera ya video ambayo ilimrekodi huyo mwanaakiolojia akivizika vitu vya kale vilivyotengenezwa kwa mawe kwenye eneo ambalo lingechimbwa. Alifanya hivyo kabla ya kikosi cha wachimbaji kufika. Kwa kuwa hangeweza kukana uthibitisho huo, mwanaakiolojia huyo alikubali kuwa alivizika vitu alivyokuwa amekusanya. Sasa, kazi yake yote ya uvumbuzi ya miaka 30 inachunguzwa tena kwa makini. Kutokana na hilo, wachapishaji watalazimika kusahihisha vitabu vya marejeo vya akiolojia na vitabu vinavyotumiwa shuleni.

Aksidenti Zinazowapata Watoto

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa katika nchi 26 na Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF), aksidenti ndiyo kisababishi kikuu cha vifo vya watoto katika mataifa yenye ufanisi mwingi ulimwenguni. Gazeti la Mainichi Daily News la Japani laripoti hivi: “Majeraha yalisababisha asilimia 40 hivi ya vifo vya watoto walio na umri wa kati ya mwaka 1 hadi 14 katika nchi zilizochunguzwa,” hivyo watoto 20,000 walikufa kila mwaka. Mambo yanayoongeza uwezekano wa watoto kujeruhiwa yatia ndani umaskini, kulelewa na mzazi mmoja, familia kubwa, na wazazi wanaotumia dawa za kulevya. Shirika hilo la UNICEF liliwahimiza watu watilie maanani “vitu vinavyolinda uhai vilivyothibitishwa: helmeti, viwango vya mwendo wa magari katika maeneo yenye watu wengi sana, viti vya usalama vya watoto ndani ya magari, mikanda ya viti, vifuniko vinavyozuia watoto kutumia dawa, vigundua-moshi vya nyumba, na viwango vya usalama kwenye viwanja vya michezo.”