Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mti Unaoamka Mapema

Mti Unaoamka Mapema

Mti Unaoamka Mapema

MWISHONI mwa Januari au mapema katika Februari, vilima vingi vyenye mfululizo wa ngazi pana vya Israel hubadilika kwa njia ya kuvutia. Baada ya kuwa katika hali ya kutotenda katika majira ya baridi kali, milozi huamka na kuchanua maua. Kwa kuwa kwa kawaida mlozi hutangulia kuchanua maua kabla ya miti mingine, mti huo huonekana waziwazi. Maua yake meupe na ya waridi hurembesha mandhari wakati wa baridi kali. Jambo hilo hutukumbusha maneno ya Solomoni kwenye Mhubiri 12:5. Hapo Solomoni analinganisha mvi za uzee na ‘mlozi unaochanua maua.’

Kwa kuwa mlozi huchanua maua mapema, kwa kufaa neno la Kiebrania la mlozi humaanisha kihalisi “anayeamka.” Hivyo, mti huo umetumiwa katika Biblia katika mifano kadhaa yenye kuchochea sana. Kwa mfano, nabii Yeremia aliona tawi la mlozi katika njozi. Liliwakilisha nini? Yehova alimwambia hivi: “Niko macho kulitekeleza neno langu.” (Yeremia 1:11, 12, BHN) Kwa wazi, Yehova hachoki, wala halali. Lakini maneno yake yalikazia tamaa yake ya kumaliza kazi yake.—Isaya 40:28.

Karne nyingi kabla ya siku za Yeremia, fimbo ya mlozi iliyochanua maua ilitumiwa kumtambulisha yule ambaye Yehova alikuwa amemteua kuwa kuhani wa cheo cha juu. Fimbo ya kila mojawapo ya makabila 12 ya Israeli iliwekwa mbele ya Yehova katika hema la kukutania. Asubuhi iliyofuata fimbo ya mlozi ya Aroni haikuwa tu imechanua maua kimuujiza bali pia ilikuwa imezaa malozi mabivu! Fimbo hiyo ya mlozi iliwekwa ndani ya sanduku la agano kwa muda fulani itumike kama ishara kwa taifa hilo kwamba wasinung’unike tena dhidi ya wawakilishi walioteuliwa na Yehova.—Hesabu 16:1-3, 10; 17:1-10; Waebrania 9:4.

Yehova alitaka kinara cha taa cha dhahabu chenye matawi saba, kilichoangaza Mahali Patakatifu pa tabenakulo, kiwe na mapambo yenye umbo la maua maridadi ya mlozi. Kulingana na maelezo ambayo Musa alirekodi, “vikombe vitatu, vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi vilikuwa katika tawi moja, tovu na ua; na vikombe vitatu, vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, katika tawi la pili, tovu na ua; yalikuwa ni vivyo hivyo yale matawi sita yaliyokuwa katika hicho kinara. Katika kinara mlikuwa na vikombe vinne, vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, matovu yake na maua yake.”—Kutoka 37:19, 20.

Ijapo Biblia hutaja mlozi mara chache, inatueleza juu ya maua yake meupe maridadi na jinsi mti huo unavyoamka mapema. Zaidi ya yote, mti huo unaopendeza sana, hutukumbusha kwamba Yehova hatapumzika hadi atimize kusudi lake.—Isaya 55:11.