Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vuli Ni Majira Yenye Kuvutia Sana

Vuli Ni Majira Yenye Kuvutia Sana

Vuli Ni Majira Yenye Kuvutia Sana

VULI ni majira ya pekee sana. Ni wakati ambapo, sehemu zenye tabia ya nchi ya wastani, huwa na anga lisilo na mawingu, jua huangaza mchana, na usiku huwa baridi. Wakati huo vilima vyenye misitu huwa na rangi mbalimbali za manjano, za machungwa, na nyekundu. Pindi hiyo misindano na mierezi isiyokauka majani huwa maridadi miongoni mwa miti inayopukutika majani ya rangi ya manjano na nyekundu.

Majira ya vuli huthaminiwa sana katika nchi za Mashariki kama vile Japani na Korea. Nchini Japani mara nyingi watu huenda ‘kuangalia rangi za vuli’—yaani, wanafanya tafrija katika majira ya vuli ili wapate fursa ya kufurahia umaridadi wa maumbile.

Mbuga nyingi za kitaifa nchini Korea huwa maridadi sana katika majira hayo. Kwa hiyo magazeti huwafahamisha watu kuhusu wakati bora zaidi wa kufurahia umaridadi wa majira ya vuli. Watu wengi hupenda kuzuru Soraksan, mojawapo ya mbuga maarufu za kitaifa nchini Korea. Kuna majabali ya matale na miamba mirefu yenye misindano iliyo karibu-karibu, ambayo yaonekana hupatikana sana katika mandhari ya nchi za Mashariki. Miti inayoitwa beech na maple ambayo huzingira majabali ya matale katika mbuga ya Soraksan, huwa na rangi nyekundu wakati wa vuli. Vilele vya majabali vinapoibuka katika ukungu wa asubuhi huvutia watu wanaoamka mapema alfajiri. Watazamaji hawawezi kamwe kusahau mandhari hiyo.

“Sikuzote mimi hufurahia kutembea milimani lakini hasa wakati wa vuli,” aeleza Park Ii-kyun, Mkorea mchangamfu aliye katika miaka yake ya 70. “Katika majira ya vuli ni kana kwamba Mungu hupaka vilima rangi nyingi sana—rangi ambazo hubadilika siku kwa siku, rangi ambazo humeremeta kunapokuwa na anga jangavu la vuli.” Mkewe, Kông-young, hufurahia kutazama majani ya vuli yakianguka kama vipepeo wa dhahabu.

Kwa Nini Majani Hubadilika Rangi?

Mtu mwenye udadisi huenda akataka kujua kwa nini majani yanabadilika rangi. Kwa nini jani hubadilika kuwa la manjano au jekundu?

Miongoni mwa njia ambazo miti hujitayarisha kwa ajili ya baridi kali ni rangi za vuli. Miti huanza kuacha kusambaza maji na madini kwenye majani kisilika katika majira ya vuli, siku zinapokuwa fupi. Kama tokeo kila jani hufanyiza tabaka linalozuia maji kupita chini ya kikonyo. Tabaka hilo linalofanyizwa na tishu kama ya mtonga—huzuia maji na madini kufika kwenye jani kutoka sehemu nyinginezo za mti na mwishowe jani huanguka.

Hali hiyo inapoendelea, rangi ya asili ya karotini huanza kubadili majani kuwa manjano au kuwa na rangi ya machungwa. Rangi hizo za asili kwa kawaida huwapo katika majira ya kiangazi, lakini huwa hazionekani kwa sababu ya rangi ya chanikiwiti iliyo katika majani. Kwa upande mwingine, rangi nyekundu, hutokana hasa na anthocyanin, rangi ya asili inayotokezwa na majani wakati wa vuli peke yake. Wakati wa vuli, chanikiwiti hutokomea, na rangi nyekundu na ya manjano ya asili huongezeka katika jani. Jani la mti wa poplar lisilo na chanikiwiti hubadilika na kuwa na rangi ya manjano nyangavu, lakini jani la mti wa maple huwa na rangi nyekundu nyangavu.

Majira ya Vuli Yenye Kuvutia

Watu wengi wanaopendezwa na maumbile wamegundua kwamba majira ya vuli hubadilika kila mwaka na ni tofauti katika sehemu mbalimbali. Inategemea hasa aina ya miti inayopukutika majani iliyo katika eneo fulani. Kwa mfano, miti mbalimbali ya maple huwa na rangi mbalimbali nyekundu zenye kuvutia sana. Aina mbalimbali ya miti hiyo hukua kiasili katika nchi za Mashariki, na mara nyingi hupandwa katika bustani.

Jambo jingine muhimu ni tabia ya nchi. Kiasi cha anthocyanin kinachotokezwa na majani hutegemea hasa hali ya hewa. Majani hutokeza kiasi kikubwa zaidi cha anthocyanin siku zisizo na mawingu na zenye jua, na kunapokuwa na baridi usiku. Kwa kawaida tabia ya nchi katika Mashariki ya Mbali huwa hivyo wakati wa vuli. Japani na Korea ni nchi zenye milima-milima. Vilima vingi nchini humo huwa na misitu yenye miti mbalimbali inayopukutika majani, na hivyo watalii hufurahia kuona rangi zenye kuvutia wakati wa vuli.

Ukuzi Mpya Wenye Kupendeza

Mpukutiko wa majani ni muhimu na ni maridadi pia. Miti huhifadhi maji na nishati wakati wa majira ya baridi kali kwa kupukutisha majani yake. Miti huondoa pia kemikali hatari ambazo hurundamana kwenye majani wakati wa kiangazi.

Mabilioni ya majani yanayoanguka ardhini huenda wapi? Hubadilishwa na wadudu, kuvu, nyungunyungu, na wanyama wengine wanaoishi ardhini kuwa mbolea, ambayo inarutubisha udongo. Kwa hiyo baada ya kung’aa, majani hayo yaliyopukutika huwa mbolea inayosaidia mimea kusitawi tena katika majira ya masika! Je, kuna utaratibu mwingine wowote unaopendeza kuliko ukuzi huo mpya? Tunapotua na kustaajabia maumbile hayo, huenda tukaona ni kana kwamba ‘miti yote ya kondeni inapiga makofi’ na kumsifu Muumba kimyakimya.—Isaya 55:12; Zaburi 148:7-9.