Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mabuu Yanayotumiwa Katika Matibabu

Mabuu Yanayotumiwa Katika Matibabu

Mabuu Yanayotumiwa Katika Matibabu

Ijapokuwa wazo hilo halivutii wengi, “daktari- mpasuaji” stadi na aliye safi ameanza kutumiwa tena—buu la kawaida. Ripoti moja katika Jarida la Shirika la Kitiba la Marekani (JAMA) inasema kwamba madaktari huko Uingereza walifanya uchunguzi wa majaribio kwa wagonjwa 12 waliokuwa na vidonda miguuni. Sita walitibiwa kwa kutumia kemikali ya hydrogel na wengine sita, kwa kuwekewa mabuu yaliyo hai kwenye vidonda. *

“Vidonda vya wale wagonjwa sita waliotibiwa kwa kutumia mabuu viliacha kuenea baada ya siku 3,” lasema jarida la JAMA. Kati ya wale waliotibiwa kwa njia ya kawaida, “ni wawili tu ambao vidonda vyao havikuenea baada ya kutibiwa kwa mwezi 1; na wale wengine wanne walihitaji matibabu zaidi.” Kulingana na jarida la kitiba la Uingereza la The Lancet, mabuu yanapotumiwa katika tiba, “muda wa matibabu unapungua sana kuliko ilivyo katika matibabu ya kawaida” nayo “hugharimu kiasi kidogo ikilinganishwa na tiba ya hydrogel.”

Madaktari wanapotibu kidonda kinachooza kwa kutumia mabuu, wao huweka mabuu machanga yasiyo na viini kwenye kidonda hicho, lasema jarida la JAMA. (Bila shaka madaktari hutumia mabuu yasiyoweza kushambulia tishu ambazo hazijaambukizwa.) Kisha kidonda hicho hufunikwa kwa kitambaa laini cha nailoni chenye mashimo. Wao hutumia pia pamba ili kufyonza umajimaji usiohitajiwa wa tishu zilizokufa. Mabuu hayo yakishiba kupita kiasi, yanatolewa na kutupwa, mengine mapya hutiwa kwenye kidonda hadi kinapoacha kuenea. Baadaye, damu huingia kwenye tishu safi na kusaidia kufanyiza nyama mpya.

“Hakuna mgonjwa aliyekataa matibabu ya mabuu,” asema Michael Walker, daktari-mpasuaji wa mishipa. “Wafanyakazi wa hospitali ndio huudhiwa na aina hii ya tiba na wala si wagonjwa.” Mbali na Muungano wa Uingereza, Marekani na Kanada hutumia pia matibabu ya mabuu katika vituo fulani vya matibabu. Daktari mmoja mpasuaji aliyetajwa katika gazeti The Lancet alisema kwamba “kuna wagonjwa wengi huko Marekani wanaoomba matibabu ya mabuu lakini ni madaktari wachache sana walio tayari kuyatumia kuwatibu.”

Tiba ya mabuu iligunduliwa bila kutarajiwa. Kulingana na gazeti la Science World, “madaktari wanaotibu askari vitani, waliona kwamba vidonda vya askari vilivyoshambuliwa na mabuu vilipona upesi kuliko vidonda visivyokuwa na mabuu. Punde si punde matibabu ya mabuu yakagunduliwa.” Na sasa yanatumiwa katika mamia ya hospitali huko Marekani na Ulaya.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Matibabu hayo ni tofauti na yale ya kutumia mdudu anayeitwa ruba ili kufyonza damu. Ona gazeti la Mnara wa Mlinzi la Kiingereza la Juni 15, 1982, ukurasa wa 31.

[Picha katika ukurasa wa 22]

Baadhi ya mabuu yakiwa kwenye kidole (ukubwa halisi)

[Hisani]

Picture copyright SMTL, http://www.smtl.co.uk/

[Picha katika ukurasa wa 22]

Kabla

Baada

[Hisani]

Photos by R. Sherman, University of California, Irvine