Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Safu ya Milima ya Rocky Iliyofanyizwa Karibuni Zaidi

Safu ya Milima ya Rocky Iliyofanyizwa Karibuni Zaidi

Safu ya Milima ya Rocky Iliyofanyizwa Karibuni Zaidi

HUKU tukiwa tumechoka sana, tuliwasha stovu yetu na tukaanza kutayarisha kiamsha-kinywa. Kwa siku tano, tulikuwa tumesafiri kilometa zipatazo 5,000 kwa gari, toka New York hadi Wyoming. Tulipokuwa tukila kiamsha-kinywa, tulitazama mandhari.

Jua liling’aa na hewa ilikuwa safi na yenye kuburudisha. Hatukuwa tumewahi kufurahia tafrija kama hii—mandhari ilivutia! Tulikuwa tunakula karibu na ufuko wa Ziwa Jackson katika Mbuga ya Kitaifa ya Wanyama ya Grand Teton. Mbele yetu kulikuwa mandhari nzuri ya milima mirefu. Hiyo ndiyo ilituvutia zaidi kati ya mambo yote tuliyoona katika safari yetu ya kilometa 16,000 magharibi mwa Marekani. Tulijua kwamba endapo tungepata fursa ya kurudi, hapana shaka tungerudi.

Mlima wa Grand Teton una kimo cha meta 4,200 hivi, na milima mingine katika safu hiyo ina kimo cha zaidi ya meta 3,700. Japo milima hiyo ni mirefu, kuna milima mirefu zaidi. Huenda hata ukakosa kuona Safu ya Milima ya Teton unaposafiri kwa gari, ikitegemea umetokea upande gani. Ukitokea upande wa magharibi, utaona tu kwamba ardhi imeinuka kidogo—na hiyo si ajabu! Hata hivyo, ukitokea upande wa mashariki, utaona kwamba milima hiyo imeinuka kwa urefu wa kilometa moja na nusu juu ya bonde lililo chini. Pasina shaka, milima hiyo huvutia.

Twarudi Tena

Baada ya kutamani sana kurudi kwa miaka mingi, hatimaye tulifanya hivyo. Wakati huu tulisafiri kwa ndege hadi Jackson Hole, Wyoming, kisha tukasafiri kwa gari kaskazini hadi kwenye safu ya milima ya Teton. Jiunge nasi tunapoanza safari yetu kwenye Ziwa Jenny lenye barafu linalofanana na kito. Ziwa hilo liko chini ya milima mirefu zaidi ya safu hiyo.

Ngozi yetu yawashawasha tunapopigwa na hewa baridi ya asubuhi. Japo jua halijachomoza, hatuko peke yetu. Watu wengine wameamka na wameanza kukurukakara. Wapiga-picha fulani wanataka kupiga picha wakati milima inapomulikwa na miale ya macheo ya jua ya rangi ya waridi na ya kidhahabu. Ghafula bin vuu, twasimama tuli. Mbawala-jike mkubwa amesimama mbele yetu! Anakauka, yu chonjo kabisa kwani mtoto wake anajilisha yapata meta tisa tu kutoka tulipo. Twachukua kamera zetu taratibu. Bila kuvuta pumzi, twalenga shabaha na kupiga picha. Sasa twaweza kupumua tena; huo ndio mwanzo tu wa siku yetu kwenye Ziwa Jenny.

Twajiunga na kikundi cha wasafiri katika mashua na punde si punde twafika chini ya kijia chenye urefu wa kilometa moja na nusu kinachopanda juu kwenda kwenye Mwinuko wa Inspiration. Mara tunaposhuka mashua, twapigwa na hewa baridi ya msitu. Tunapoendelea kupanda kijia hicho, hatulioni ziwa sana. Twaanza kusikia mvumo wa maporomoko ya maji yaliyo mbali. Huku tukihemahema, twatoka msituni na kupumzika kwenye mwamba fulani. Twafurahia nuru nyangavu ya asubuhi na kuvuta hewa baridi ya milimani. Ziwa Jenny, lililo na rangi ya yakuti-samawi, liko chini. Ziwa hilo limezingirwa na miti ambayo iko juu ya kilima kinachoonekana. Ni kana kwamba liliundwa na fundi stadi wa vito.

Juu yetu kuna vilele virefu vya milima vinavyoitwa Kundi la Cathedral. Katika miaka ya 1930, Dakt. Fryxell, mtaalamu wa mambo ya asili aliyechunguza safu hiyo ya milima, aliandika hivi: “Huku vikiwa vimeinuka juu ya vilele vingine vyote, vikiwa na ncha kali [vilele hivyo] vyaelekeza maoni na mawazo ya mtu juu zaidi.” Twastaajabishwa na kuvutiwa sana na fahari ya Mwinuko wa Inspiration. Tayari twahisi kwamba jitihada zetu zimefanikiwa. Lakini kuna zaidi.

Kwa kushangaza, kijia kinakuwa tambarare na kinapinda chini ya Korongo la Cascade. Kuna majabali yaliyo juu yetu, na vijito vinatiririka kwenye majabali hayo. Twajiuliza hivi, ‘Ni nguvu gani zilizofanyiza mandhari hii?’ Kwa ghafula, mtoto mwenye shauku anatufikia. Hawezi kuzuia shauku yake. Huku akihemahema, atuambia hivi: ‘Tumemwona kongoni wa aina fulani! Harakisheni, mwaweza kumwona pia!’

Twaacha kufikiria jinsi milima hiyo ilivyofanyizwa. Twachukua kamera, na kujitayarisha kumpiga picha mmojawapo wa wanyama wenye kupendeza zaidi wanaotangatanga katika mbuga hiyo. Msichana huyo anatupeleka mahala tunapoweza kuona vizuri. Wakiwa wamenyamaza, washiriki wengine wa familia yake wanatuonyesha mahala mnyama alipo. Twamwona mnyama huyo aina ya kongoni penye kinamasi karibu na mto. Huku tukitazama kwa kustaajabu na kuinua kamera zetu, twafurahi kwamba tulifika hapo wakati barabara.

Jiolojia na Mabamba ya Dunia

Kukiwa na mengi ya kuona, ni rahisi sana kusahau kuuliza kuhusu historia ya mandhari hiyo yenye kuvutia. Hata hivyo, mbuga hiyo hujitahidi sana kuwaelimisha watu kwa kuchapa vijitabu na kupanga makundi ya watu watembezwe na wasimamizi wa misitu.

Tulielezwa kwamba ingawa ardhi tunayokanyaga yaonekana kuwa imara, kwa njia fulani ni kama ziwa lililoganda wakati wa masika, yaani, si imara kama inavyodhaniwa! Wanajiolojia wameamini ile nadharia kwamba uso wa dunia umefanyizwa kwa mabamba na kwamba mabamba hayo yanasonga huku yakiwa juu ya miamba mingi iliyoyeyuka. Jambo la kupendeza katika nadharia hiyo ni kwamba wakati mabamba hayo yanapogongana, safu za milima zaweza kuibuka.

Kwa habari ya Safu ya Milima ya Teton, yaonekana kwamba bamba moja liliinua bamba jingine, kama mtaimbo. Kisha mlima ukaibuka. Wanajiolojia husema kuwa mlima huo hufanyizwa kunapokuwa na nyufa miambani. Wanasema kwamba Safu ya Milima ya Teton ilifanyizwa hivi majuzi, inapolinganishwa na mandhari nyingine za kijiolojia. Hivyo kijitabu cha mbuga hiyo hutaja safu hiyo kuwa “safu iliyofanyizwa karibuni zaidi na yenye kuvutia zaidi katika Milima ya Rocky.”

Vilifanyizwa kwa Maji na Barafu

Majibu hayo yalitupendeza, lakini yalizusha maswali mengine. Tulifikiria kuhusu matembezi yetu kwenye Ziwa Jenny. Miamba hiyo ilichongwaje? Pia, vipi kuhusu kile kilima kinachozingira ziwa hilo, chenye miti mingi sana? Wanajiolojia walijibuje maswali hayo? Vitu hivyo vyote vilifanyizwa kwa maji. Kulingana na nadharia, yasemekana kwamba wakati fulani hapo zamani, barafu ilichonga makorongo ya Safu ya Milima ya Teton. Kilima hicho kilicho kando ya ziwa kilifanyizwa kwa barafu iliyokuwa ikisonga. Kilima hicho kilizuia udongo wenye rutuba pamoja na kiasi fulani cha barafu hiyo ambayo sasa imeyeyuka.

Huenda nadharia hiyo ikaeleza ni kwa nini kuna mimea mingi kando ya ziwa hilo, hasa inapolinganishwa na eneo la changarawe tupu na nyanda zenye vichaka zilizo karibu. Huku tukiwa tumestaajabu sana, tulimwomba msimamizi huyo wa misitu atueleze zaidi. Alieleza kwamba utendaji mwingine ndio ulifanyiza vilele vilivyochongoka vya milima hiyo. Alitaja utendaji huo kuwa kazi ya barafu ya kutenganisha miamba. Maji huingia katika nyufa miambani. Yanapoganda yanapanuka. Nguvu hizo hutenganisha miamba na kuacha mchongo. Tulimshukuru sana kwa maelezo yake na upendezi wake kwa milima hiyo.

Wanyama

Mbali na mandhari zenye kupendeza, eneo hilo lina wanyama wengi pia. Hilo lilifanya safari yetu kwenye mto maarufu uitwao Mto Snake kuwa yenye kupendeza zaidi. Tulipokuwa tukitazama mandhari hiyo, tuliona furukombe na tai wanaoitwa bald wakipaa angani na kuingia mtoni ili kuwakamata samaki. Mtu aliyetutembeza kwa mashua, ambaye ni mwanabiolojia aliyehitimu, alitueleza jambo la kushangaza. Japo tai huyo ndiye mkubwa na mwenye kuvutia zaidi, furukombe ndiye bingwa wa kuvua samaki. Alituambia kwamba aliona tai wakiwanyang’anya furukombe samaki. Na kwa hakika, tuliona mmoja wa tai hao akimnyemelea furukombe mchanga. Furukombe alimwachilia samaki na kutoroka.

Tulifurahi sana kuwaona wanyama katika makao yao ya asili. Makao ya Kitaifa ya Kongoni wa Elk yako karibu na hapo, na wengi wa kongoni hao huhamia kwenye Mbuga ya Kitaifa ya Wanyama ya Grand Teton wakati wa kiangazi. Tulisimamisha gari mara nyingi ili kutazama vikundi vya kongoni hao wakisonga polepole huku wakila. Nyakati nyingine, tulisimama barazani kwenye hoteli yetu ili kuwaona kongoni wakila kwa utulivu penye miti iliyokuwa karibu na maji. Wakati wa usiku, ni kana kwamba wanyama hao walikuwa wakiwatumbuiza watu waliokusanyika ili kuwatazama wakila. Japo tulikuwa tumechoka, tulikaa ili kuona mandhari ambayo sisi wenyeji wa jiji huona mara haba—anga jeusi hivi lenye nyota zinazometameta.

Siku yetu ya mwisho ilifurahisha sana. Tulihofu na kustaajabu sana tulipopita kwa gari kati ya kundi la nyati waitwao bison. Wanyama hao wakubwa walio shaghalabaghala walijaa pande zote za barabara. Hatukutaka kuondoka! Lakini wakati wa kuondoka ulikuwa umewadia.

Tulipoketi ndani ya ndege tukisubiri kusafiri, tulifikiria safari yetu. Tulifurahia mambo tuliyokuwa tumeona kifupi—milima, hewa ya milimani, na wanyama. Ilisisimua kama nini kuweza kutosheleza hamu yetu ya muda mrefu ya kutembelea tena Safu ya Milima ya Teton! Kwelikweli, safu ya Milima ya Rocky iliyofanyizwa karibuni zaidi inapendeza sana.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 19]

Madokezo kwa Wageni

Jipe muda ili uzoee hewa hiyo yenye oksijeni kidogo. Bonde liko meta 1,800 juu ya usawa wa bahari. Huenda watalii fulani kutoka sehemu tambarare wakaathiriwa kwa sababu ya kuwa kwenye eneo lenye milima-milima, kama kwa kuumwa na kichwa au kukasirika upesi. Huenda itakuwa vema kwa wazee-wazee, hasa walio na magonjwa ya moyo au ya kupumua, kupata ushauri wa daktari kabla ya kufunga safari hiyo.

Jitayarishe vema kabla ya kuanza matembezi hayo. Kumbuka kwamba maji humalizika haraka mwilini mtu anapokuwa kwenye maeneo yenye milima mirefu na yenye ukame. Beba maji mengi.

Mbuga hiyo ni nyika, na ina wanyama wengi wakubwa, wenye kupendeza, lakini walio hatari. Watalii fulani hupenda kuwakaribia wanyama sana, lakini wanyama wanaweza kushambulia ghafula. Sikiliza na ufuate mashauri ya wasimamizi wa misitu kuhusu namna ya kushughulika na wanyama-pori katika mazingira yao. Maneno ya wasimamizi hao wa misitu hayatakupendeza tu bali pia yatakulinda.

[Ramani katika ukurasa wa 17]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MBUGA YA KITAIFA YA WANYAMA YA GRAND TETON

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mlima Moran, Safu ya Milima ya Teton

[Picha katika ukurasa wa 17]

Korongo la Upper Cascade

[Picha katika ukurasa wa 18]

Nyati aina ya “bison”

[Picha katika ukurasa wa 18]

Tai aina ya “bald”

[Picha katika ukurasa wa 18]

Machweo ya jua kwenye Safu ya Milima ya Teton

[Picha katika ukurasa wa 18]

Aina ya kongoni dume