Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Carthage—Jiji Lililokaribia Kuangusha Roma

Carthage—Jiji Lililokaribia Kuangusha Roma

Carthage—Jiji Lililokaribia Kuangusha Roma

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA

KWENYE pwani ya kaskazini ya Afrika, karibu na Tunis, jiji kuu la Tunisia, kuna magofu ya jiji la kale la Carthage. Hata mtalii akikosa kuyaona, haidhuru, kwani hakuna mambo mengi ya ajabu. Hata hivyo, hapo ndipo pana mabaki ya mojawapo ya majiji makuu ya kale—jiji ambalo lilikaribia kushinda milki ya Roma yenye nguvu. Kulingana na mwanahistoria Mroma Livy, “pambano hilo kati ya majiji yenye utajiri mwingi duniani liliwahangaisha sana wafalme na watu wengi,” kwani yalikuwa yanapigania utawala wa ulimwengu.

Mwanzo wa Jiji Hilo

Katika milenia ya pili K.W.K., Wafoinike waliishi kwenye eneo dogo kando ya Pwani ya Mediterania, kaskazini na kusini mwa Lebanoni ya sasa. Kwa sababu walikuwa mabaharia stadi, walikwenda magharibi kutafuta dhahabu, fedha, chuma, bati, na madini ya risasi. Walibadilishana vitu hivyo kwa mbao (kama vile mwerezi maarufu wa Lebanoni), nguo za rangi ya zambarau-nyekundu, marashi, divai, vikolezo, na bidhaa nyingine zilizotengenezwa. *

Wafoinike waliposafiri kuelekea magharibi, walianzisha makazi kwenye pwani za Afrika, Sicily, Sardinia, na kusini mwa Hispania—huenda hiyo ndiyo Tarshishi inayotajwa katika Biblia. (1 Wafalme 10:22; Ezekieli 27:2, 12) Kulingana na mapokeo, jiji la Carthage lilianzishwa mnamo mwaka wa 814 K.W. K., miaka 60 hivi kabla ya adui yake Roma, kuanzishwa. Mtaalamu wa mambo ya kale ya Afrika Kaskazini, Serge Lancel, asema hivi: “Kusitawishwa kwa Carthage, karibu na mwisho wa karne ya tisa W. K., kuliathiri kwa karne nyingi hali ya kisiasa na ya kitamaduni ya nchi zilizo magharibi ya Mediterania.”

Mwanzo wa Milki

Kama mwanahistoria François Decret anavyoeleza, Carthage ilianza kujenga milki kwenye rasi iliyofanana na “nanga kubwa iliyoingizwa baharini.” Kwa kutumia mafanikio ya Wafoinike wa kale, Carthage ilisitawisha biashara yake ikawa muungano mkubwa wa wafanyabiashara wenye choyo. Biashara hiyo ilihusisha hasa uingizaji wa metali katika jiji hilo. Ilidhibiti biashara kwa kutumia manowari zake na wanajeshi waliokodiwa.

Wenyeji wa Carthage hawakutosheka kamwe na mafanikio yao, hivyo walitafuta daima masoko mapya. Yadhaniwa kwamba, wapata mwaka wa 480 K.W.K., yule nahodha Himilco aliwasili Cornwall, eneo la Uingereza lenye madini mengi ya bati. Miaka 30 hivi baadaye, yasemekana kwamba Hanno, mshiriki wa mojawapo ya familia maarufu za Carthage, aliongoza safari ya meli 60, zilizobeba wanaume na wanawake 30,000, ili kuanzisha makoloni mapya. Huku akipita kwenye Mlango-Bahari wa Gibraltar na kusafiri kwenye pwani ya Afrika, huenda Hanno alifika kwenye Ghuba ya Guinea na hata kwenye ufuko wa Cameroon.

Kutokana na bidii hiyo na kutumia busara sana katika biashara, Carthage likawa jiji lenye ufanisi mwingi zaidi katika ulimwengu wa kale. Kitabu Carthage chasema hivi: “Kufikia mwanzo wa karne ya tatu [K.W.K.], ustadi wake wa kiufundi, manowari zake, na biashara yake . . . ilifanya jiji hilo liwe maarufu zaidi.” Mwanahistoria Mgiriki, Appian, alisema hivi kuhusu wenyeji wa Carthage: “Walilingana na Wagiriki kwa uwezo; walilingana na Waajemi kwa utajiri.”

Uvutano wa Baali

Japo walikuwa kila mahali magharibi mwa Mediterania, Wafoinike waliunganishwa na imani zao za kidini. Wenyeji wa Carthage walirithi dini ya Kikanaani kutoka kwa babu zao Wafoinike. Kwa karne nyingi, watu fulani wa Carthage walitumwa kila mwaka kwenda Tiro ili kutoa dhabihu kwenye hekalu la Melqart. Huko Carthage, mungu-mume aitwaye Baal-Hammon na mungu-mke aitwaye Tanit walikuwa miungu mikuu iliyoabudiwa. Jina Baal-Hammon lamaanisha “Bwana wa Brazier,” na Tanit amehusianishwa na Astarte.

Sehemu mbaya zaidi ya dini ya Carthage ilikuwa kutoa dhabihu za watoto. Diodorus Siculus aripoti kwamba mnamo mwaka wa 310 K.W.K., wakati jiji lilishambuliwa, wenyeji wa Carthage walidhabihu watoto 200 waliotoka katika familia maarufu ili kumtuliza Baal-Hammon. Kichapo The Encyclopedia of Religion chasema hivi: ‘Kumdhabihu mtoto asiye na hatia kwa niaba ya mtu mwingine lilikuwa tendo bora kabisa la kutuliza miungu. Huenda tendo hilo lilifanywa ili kuhakikisha hali njema ya familia na ya jumuiya vilevile.’

Mnamo mwaka wa 1921, wanaakiolojia waligundua eneo ambalo baadaye liliitwa Tofethi, kupatana na neno la Biblia linalotumiwa kwenye 2 Wafalme 23:10 na Yeremia 7:31. Wanaakiolojia walipochimba walipata matabaka ya madumu yaliyokuwa na majivu ya mizoga ya wanyama (waliotumiwa kama dhabihu za badala) na majivu ya maiti za watoto. Madumu hayo yalizikwa chini ya mabamba yaliyokuwa na maandishi ya nadhiri. Yakadiriwa kwamba eneo la Tofethi lina majivu ya watoto zaidi ya 20,000 waliotolewa kama dhabihu katika kipindi cha karne mbili tu. Leo, wachanganuzi fulani wa historia hudai kwamba eneo la Tofethi lilikuwa tu mahala pa kuwazika watoto waliokufa walipozaliwa au waliokufa wakiwa wachanga sana hivi kwamba hawakuweza kuzikwa kwenye makaburi makubwa ya kale. Hata hivyo, kama Lancel, aliyetajwa mwanzoni, asemavyo, ‘hatuwezi kukana kabisa kuwa wenyeji wa Carthage waliwadhabihu wanadamu.’

Mzozo Kuhusu Utawala

Milki ya Tiro ilipoanguka katika karne ya sita K.W. K., Carthage ilishika hatamu za uongozi juu ya Wafoinike wa magharibi. Lakini Carthage haikupata mamlaka bila kupingwa. Mapema kabla ya hapo, wafanyabiashara wa Carthage na Ugiriki walizozana ili kudhibiti maeneo ya bahari, na vita ikazuka wapata mwaka wa 550 K.W.K. Mnamo mwaka wa 535 K.W. K., wenyeji wa Carthage, wakisaidiwa na marafiki wao Waetruria, waliwafukuza Wagiriki kutoka kwenye kisiwa cha Korsika na kumiliki Sardinia. * Kutokana na hilo, pambano kati ya Carthage na Ugiriki la kung’ang’ania Sicily—kisiwa kilichokuwa muhimu sana—lilipamba moto.

Wakati huohuo, Roma ilianza kuonyesha uwezo wake. Mikataba kati ya Carthage na Roma iliimarisha haki za kibiashara za Carthage na kuwazuia Waroma wasiingie Sicily. Lakini Roma ilipomiliki rasi ya Italia, uvutano wa Carthage uliokuwa ukizidi karibu sana na Italia ulionwa kuwa tisho. Mwanahistoria Mgiriki, Polybius, wa karne ya pili K.W.K. alitaarifu hivi: “Waroma waliona . . . kwamba wenyeji wa Carthage wamemiliki Afrika, * sehemu kubwa ya Hispania, na visiwa vyote vilivyokuwa katika Bahari za Sardinia na Tyrrhenia. Iwapo wenyeji wa Carthage wangetwaa Sicily, wangekuwa majirani wasumbufu na hatari sana, kwani wangezingira Italia kutoka pande zote na kutisha maeneo yote ya nchi hiyo.” Kwa sababu ya faida za kibiashara, watu fulani katika Baraza Kuu la Roma walitaka sana kuzuia uvamizi huo wa Sicily.

Vita vya Punic

Mnamo mwaka wa 264 K.W.K., mgogoro uliotokea huko Sicily uliwapa Waroma kisingizio cha kuingilia kati. Roma ilivunja mkataba fulani kwa kutuma majeshi, na kuzusha Vita ya Kwanza ya Punic. Vita hiyo, iliyokuwa mfululizo wa baadhi ya mapambano makubwa ya kale ya wanajeshi wa majini, iliendelea kwa zaidi ya miaka 20. Hatimaye, mnamo mwaka wa 241 K.W.K., wenyeji wa Carthage walishindwa na wakalazimika kutoka Sicily. Pia, Roma iliwanyang’anya Korsika na Sardinia.

Ili kulipia hasara hizo, Hamilcar Barca, jenerali mmoja wa Carthage, alipanga kurudisha mamlaka ya Carthage kwa kusitawisha milki huko Hispania. “Carthage Mpya”—Cartagena—ilianzishwa kwenye pwani ya kusini-mashariki ya Hispania, na baada ya miaka michache, Carthage ilikuwa imetajirika tena kutokana na madini ya Hispania. Kama ilivyotarajiwa, ustawi huo ulitokeza mgogoro kati ya Carthage na Roma, na mnamo mwaka wa 218 K.W.K., vita ikazuka tena.

Kiongozi wa jeshi la Carthage alikuwa mwana mmoja wa Hamilcar, Hannibal, jina linalomaanisha “Aliyependelewa na Baali.” Hannibal alipoondoka Cartagena mnamo Mei 218 K.W.K., alianza safari ndefu sana kupitia Hispania na Gaul, akipita kwenye milima ya Alps pamoja na jeshi lake la Waafrika na Wahispania na tembo 40 hivi. Kwa kuwa walivamiwa ghafula, Waroma walishindwa vibaya. Mnamo Agosti 2, 216 K.W.K., kwenye pambano la Cannae—“mojawapo ya misiba mibaya zaidi ambayo jeshi la Roma liliwahi kupata”—jeshi la Hannibal liliua wanajeshi wa Roma waliokuwa mara mbili ya idadi ya jeshi lao. Waliua wanajeshi wa Roma wapatao 70,000 huku wanaume 6,000 tu kati yao ndio waliokufa.

Ilionekana ni kana kwamba Roma ingeshindwa! Lakini, bila kukata tamaa, Waroma waliendelea kusumbua majeshi ya Hannibal kwa miaka 13 iliyofuata. Roma ilipotuma jeshi kwenda Afrika, mataifa ambayo yalishirikiana na Carthage hapo awali yaliiacha ishindwe huko Hispania na Sicily. Hivyo, Carthage ililazimika kumwita tena Hannibal. Mwaka uliofuata, mnamo 202 K.W.K., Jenerali Mroma Scipio Africanus alishinda jeshi la Hannibal huko Zama, kusini-magharibi mwa Carthage. Jiji la Carthage lililazimika kusalimisha manowari zake, likazuiwa kuwa na jeshi lenye kujitegemea, na likatozwa fidia kubwa. Fidia hiyo ilipasa kulipwa kwa miaka 50. Baadaye Hannibal alikimbilia uhamishoni, na akajiua wapata mwaka wa 183 K.W.K.

“Delenda est Carthago!”

Amani ilileta ufanisi Carthage, hivi kwamba ikaamua kulipa fidia hiyo baada ya miaka kumi tu. Ustawi huo, na vilevile mabadiliko ya kisiasa, ulionwa kuwa hatari sana na maadui wa Carthage wasio na huruma. Kwa miaka miwili hivi hadi kifo chake, yule mtawala mzee Mroma Cato, alimalizia hotuba zake zote mbele ya Baraza Kuu kwa kusema hivi: “Delenda est Carthago!,” yaani, “Ni lazima Carthage liharibiwe!”

Hatimaye, mnamo mwaka wa 150 K.W.K., ilisemekana kwamba mkataba fulani umevunjwa na Waroma wakapata kisingizio walichotaka. Vita ikatangazwa. Iliitwa “vita ya kufagia kabisa.” Kwa miaka mitatu, Waroma walizingira ngome ya jiji hilo yenye urefu wa kilometa 30. Sehemu fulani ya ngome hiyo ilikuwa na kimo cha meta 12. Hatimaye, mnamo mwaka wa 146 K.W.K., ufa ukafanyizwa. Wanajeshi wa Roma, walipoingia kupitia vijia vyembamba walitupiwa vitu, nao walipigana vita vikali bila silaha. Wanaakiolojia walithibitisha rekodi hiyo ya kale walipogundua mifupa ya wanadamu iliyofunikwa kwa mawe yaliyotapakaa, jambo linaloogopesha sana.

Baada ya siku sita za taabu, raia 50,000 wenye njaa ambao walikuwa wamekimbilia Byrsa—ngome ya mlimani—walisalimu amri. Wengine walijifungia katika hekalu la Eshmun kisha wakalichoma kwa kuwa hawakutaka kunyongwa au kufanywa watumwa. Waroma waliteketeza masalio ya jiji. Jiji la Carthage liliharibiwa na kulaaniwa rasmi, na watu hawangeweza kuishi humo tena.

Hivyo, katika muda wa miaka 120, Roma iliharibu kabisa miradi ya ubeberu ya Carthage. Mwanahistoria Arnold Toynbee alisema hivi: “Suala kuu la Vita ya Hannibal lilikuwa iwapo serikali mpya ya ulimwengu yenye uvutano wa Ugiriki ingekuwa Milki ya Carthage au Milki ya Roma.” Kichapo Encyclopædia Universalis chasema hivi: “Iwapo Hannibal angeshinda, hapana shaka angejenga milki kubwa ulimwenguni pote sawa na ile ya Aleksanda.” Kama ilivyokuwa, Vita vya Punic vilianzisha ubeberu wa Roma, ambao ulifanya Roma itawale ulimwengu.

“Roma ya Afrika”

Ilionekana kwamba Carthage ilikuwa imefikia mwisho wake kabisa. Lakini, karne moja tu baadaye, Yulio Kaisari aliamua kuanzisha koloni huko. Ili kumtukuza, koloni hiyo iliitwa Colonia Julia Carthago. Wahandisi wa Roma walisogeza udongo upatao meta mchemraba 100,000. Walifanya sehemu ya juu ya Byrsa kuwa jukwaa kubwa tambarare na kuondoa magofu yote. Mahekalu na majengo ya umma yenye madoido yalijengwa kwenye eneo hilo. Muda ulipopita, Carthage likawa ‘mojawapo ya majiji yenye ufanisi mwingi katika milki ya Roma.’ Lilikuwa jiji la pili kwa ukubwa katika eneo la Magharibi, baada ya Roma. Ukumbi wa maonyesho, viwanja duara vya maonyesho, mabafu makubwa ya maji moto, mfereji wenye urefu wa kilometa 132, na kiwanja cha sarakasi ambacho kingeweza kutoshea watazamaji 60,000 kilijengwa ili kutosheleza mahitaji ya wakazi 300,000 wa jiji hilo.

Ukristo ulifika Carthage yapata katikati ya karne ya pili W.K. na ukasitawi haraka. Yule mwanatheolojia maarufu na mtetea-imani Tertullian, alizaliwa huko Carthage wapata mwaka wa 155 W.K. Kutokana na maandishi yake, Kilatini kikawa lugha rasmi ya makanisa ya Magharibi. Cyprian, askofu wa Carthage wa karne ya tatu, aliyeunda mfumo wa vyeo vya makasisi vya madaraja saba, alikufa kama mfia-dini katika jiji hilo mnamo mwaka wa 258 W.K. Mtu mwingine kutoka Afrika ya Kaskazini, Augustine (354-430 W.K.), aliyetajwa kuwa mtu mwenye akili nyingi zaidi katika Ukristo wa kale, alihusika sana katika kuchanganya mafundisho ya kanisa na falsafa za Kigiriki. Uvutano wa kanisa hilo la Afrika Kaskazini ulikuwa mwingi sana hivi kwamba kasisi mmoja alisema hivi: “Ni wewe, Ee Afrika, unayeendeleza harakati za imani yetu kwa bidii nyingi sana. Unachoamua hukubaliwa na Roma na kufuatwa na wakuu wa ulimwengu.”

Hata hivyo, Carthage ingefikia mwisho wake. Kwa mara nyingine tena, mambo yaliyopata jiji hilo yalihusiana na mambo yaliyoipata Roma. Milki ya Roma ilipofifia, ndivyo na Carthage. Mnamo mwaka wa 439 W.K., jiji hilo lilitekwa na kuporwa na Wavandali. Wabyzantium walipoteka jiji hilo karne moja baadaye, jiji hilo liliponea kuharibiwa kwa muda mfupi. Lakini halikuweza kuwazuia Waarabu walioshambulia Afrika Kaskazini. Mnamo mwaka wa 698 W.K., jiji hilo lilitekwa, na baada ya hapo, mawe yake yalitumiwa kujenga jiji la Tunis. Katika karne zilizofuata, mawe ya marumaru na matale ambayo hapo zamani yaliremba jiji hilo la Roma, yaliporwa na kupelekwa hadi nchi nyingine ili kujenga makanisa makuu ya Genoa na Pisa nchini Italia, na yawezekana pia Canterbury, nchini Uingereza. Carthage liliacha kuwa jiji la kale lenye utajiri na uwezo mwingi zaidi, liliacha kuwa milki iliyokaribia kutawala ulimwengu. Hatimaye, jiji la Carthage likawa rundo la magofu lisilo na maana.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Jina Mfoinike latokana na neno la Kigiriki Phoinix, linalomaanisha “zambarau-nyekundu” na pia “mti wa mtende.” Neno la Kilatini Poenus lilifanyizwa kutokana na neno hilo, nalo limetokeza kivumishi “Punic,” linalomaanisha “mwenyeji wa Carthage.”

^ fu. 16 Kutokana na uhusiano wa karibu kati ya wenyeji wa Carthage na Waetruria, ambao ulidumu kwa karne kadhaa, Aristotle alisema kwamba ilikuwa kana kwamba mataifa hayo mawili yalikuwa taifa moja. Kwa habari zaidi kuhusu Waetruria, ona toleo la Amkeni! la Novemba 8, 1997, ukurasa 24-27.

^ fu. 17 “Wenyeji wa Carthage waliliita eneo linalozunguka Carthage, Afrika. Baadaye jina hilo lilirejezea maeneo yote yaliyojulikana ya bara hilo. Waroma waliendelea kutumia jina hilo walipofanya eneo hilo kuwa mkoa wao.”—Dictionnaire de l’Antiquité—Mythologie, littérature, civilisation.

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

ROMA

BAHARI YA MEDITERANIA

CARTHAGE (magofu)

[Picha katika ukurasa wa 14]

Mabaki ya mabafu ya Roma ya maji moto

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kusafirisha mierezi ya Lebanoni kwa meli za Wafoinike

[Hisani]

Musée du Louvre, Paris

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mapambo ya vioo yalivaliwa ili yalete bahati njema

[Hisani]

Musée du Louvre, Paris

[Picha katika ukurasa wa 16]

Wenyeji wa Carthage waliweka vinyago vya mazishi makaburini ili kufukuza roho waovu

[Hisani]

Musée du Louvre, Paris

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mauaji ya watoto yalikuwa sehemu ya ibada ya Wakanaani iliyorithiwa na wenyeji wa Carthage. Bamba hili laonyesha kaburi la mtoto aliyetolewa kama dhabihu

[Picha katika ukurasa wa 17]

Magofu ya jiji la Carthage, lililoharibiwa na Waroma mwaka wa 146 K.W.K.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Hannibal anatajwa kuwa mmojawapo wa wapangaji wakuu zaidi wa mikakati ya vita waliopata kuishi

[Hisani]

Alinari/Art Resource, NY