Gurudumu Kubwa la Vienna Linalopendwa Sana
Gurudumu Kubwa la Vienna Linalopendwa Sana
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRIA
VILIMA vya Vienna vyenye misitu vyaonekana kule nyuma, huku jiji lenye kupendeza la Vienna likiwa mbele. Mandhari iko shwari kabisa hivi kwamba waweza kusikia muziki mtamu wa msowero wa Strauss. Kijana mmoja ameteua mandhari hiyo kwa kusudi maalumu, lakini sasa anajitahidi sana kutuliza moyo wake unaopigapiga anapomwomba mpenziwe wafunge ndoa. Wako meta 60 kutoka chini. Wamefikaje huko? Yeye si mgeni wa kwanza wala wa mwisho kufika kwa ajili ya pindi hiyo ya pekee kwenye Riesenrad, yaani, gurudumu kubwa la Vienna linalopendwa sana.
Gurudumu hilo kubwa, lililo kwenye bustani moja kubwa ya Vienna inayoitwa Prater, limekuwa jambo la pekee sana katika jiji hilo kwa zaidi ya miaka 100. Tangazo la kukaribisha watu, ambalo liko kwenye lango la bustani hiyo, lasema hivi: ‘Waijua Vienna iwapo tu umeiona ukiwa kwenye gurudumu kubwa.’ Ingawa gurudumu hilo limekuwepo kwa muda mrefu zaidi ya magurudumu mengine makubwa ya Ferris, limepitia hali ngumu. Gurudumu hilo kubwa la chuma cha pua lilitokeaje? Liliokokaje hali hizo ngumu?
Gurudumu la Kwanza la Ferris
Ili kujua historia ya gurudumu hilo kubwa, twahitaji kufikiria yaliyotukia katika karne ya 19 na wakati wa Mapinduzi ya Viwanda. Wakati huo, chuma cha pua kilitumiwa sana katika
ujenzi. Majengo ya chuma cha pua yenye miundo ya kustaajabisha yalijengwa katika majiji makuu mbalimbali ulimwenguni, kama vile jengo la Crystal Palace huko London lililojengwa kwa chuma cha pua na kioo, Palm House huko Vienna, na Mnara wa Eiffel huko Paris. Lakini jiji la Chicago ndilo lililojulikana sana kwa ujenzi wa aina hiyo, na huko ndiko mhandisi Mmarekani George Ferris alijenga gurudumu kubwa la kwanza wakati wa Maonyesho ya Ulimwengu ya 1893.Gurudumu la Ferris lenye kupendeza lilikuwa na kipenyo cha meta 76 na vigari 36. Kila kigari kilitoshea abiria 40. Watu walisafirishwa juu kwa dakika 20 ili kuona mandhari maridadi ya jiji la Chicago na maeneo ya karibu. Wageni wengi waliokwenda kwenye maonyesho hayo walivutiwa hasa na gurudumu hilo. Lakini baada ya muda, gurudumu la Ferris la Chicago lilichakaa, na baada ya kuhamishwa mara mbili, liliharibiwa mnamo mwaka wa 1906. Hata hivyo, watu wengine tayari walikuwa wameanza kufikiria kujenga gurudumu kubwa kwingineko.
Gurudumu Kubwa Lajengwa Vienna
Yaonekana Walter Basset, afisa mstaafu wa jeshi la majini la Uingereza aliyekuwa pia mhandisi, alipendezwa sana na gurudumu kubwa la Chicago. Mnamo mwaka wa 1894, alianza kuchora ramani ya gurudumu kubwa sana ambalo lingejengwa huko Earl’s Court, London. Baadaye, alijenga magurudumu mengine huko Blackpool, Uingereza, na Paris. Wakati huohuo, Gabor Steiner, msimamizi wa burudani huko Vienna, alikuwa akitafuta vivutio vipya. Siku moja mwakilishi wa Walter Basset alimpendekezea Steiner washirikiane kujenga gurudumu kubwa huko Vienna. Wanaume hao waliafikiana upesi na wakapata uwanja mzuri ili kujenga kivutio hicho kipya kilichobuniwa Uingereza. Lakini vipi kuhusu kupata kibali cha ujenzi?
Steiner alipopeleka ramani ya ujenzi kwa wasimamizi wa jiji, afisa mmoja alitazama ramani hiyo, kisha akamtazama Steiner, halafu akatazama ramani tena. Kisha akatikisa kichwa chake na kuuliza: “Bw. Mkurugenzi, je, kweli wafikiri kuwa utapata mtu atakayekuruhusu kujenga dude hili hatari na akubali kulaumiwa?” Steiner akasihi hivi: “Lakini magurudumu kama hayo yanapatikana Uingereza na Blackpool, na yanafanya kazi vizuri bila hitilafu yoyote!” Afisa akakataa katakata. Afisa huyo alijibu hivi: “Waingereza wanaweza kufanya watakavyo, lakini sitahatarisha uhai wangu.” Bila woga, Steiner alizidi kuomba idhini na hatimaye akapata kibali cha ujenzi.
Ujenzi wa gurudumu hilo kubwa la chuma cha pua ulivutia watu sana. Watu wenye udadisi walikusanyika kila siku kwenye eneo hilo la ujenzi kuzungumza juu ya maendeleo ya ujenzi huo. Baada ya miezi minane tu, ujenzi ulimalizika. Siku ya Juni 21, 1897, Bibi Horace Rumbold, mke wa balozi wa Uingereza huko Vienna, alipigilia msumari wa mwisho kwenye gurudumu hilo. Siku chache baadaye, gurudumu hilo kubwa lilianza kutumiwa na umma. Kama Steiner alivyosema baadaye: “Kila mtu alifurahi, na watu walifurika kwenye ofisi za kukatia tiketi.”
Historia ya Gurudumu Kubwa
Mwana-mfalme Francis Ferdinand, aliyepaswa kurithi ufalme wa Austria-Hungaria, alipenda kutazama jiji kuu la milki hiyo akiwa juu ya gurudumu hilo kubwa. Alipouawa mnamo Juni 1914 hilo liliathiri
pia hali ya gurudumu hilo kubwa. Kifo chake kilichochea Vita ya Kwanza ya Ulimwengu. Gurudumu hilo halikutumiwa tena na mteja huyo maarufu, wala watu hawakuruhusiwa tena kutumia gurudumu hilo kwa kuwa lilitumiwa na wanajeshi kama ulingo wa ulinzi. Watu waliruhusiwa tena kutumia gurudumu hilo mnamo Mei 1915. Wakati huo, nchi hiyo ilikumbwa na uhaba wa chuma na watu walielekeza macho yote kwenye gurudumu hilo kubwa. Lingebomolewa! Mnamo mwaka wa 1919, gurudumu hilo liliuzwa kwa mfanyabiashara mmoja wa Prague, aliyepaswa kulibomoa kwa muda wa miezi mitatu tu. Lakini kazi ya kubomoa gurudumu hilo tata ingegharimu pesa nyingi zaidi ya thamani ya chuma ambacho kilitumiwa kwa ujenzi. Basi, gurudumu hilo maarufu liliponea chupuchupu kubomolewa na likaendelea kuwaburudisha watu waliolipenda.Mabadiliko makubwa yalitokea huko Vienna kutokana na vita na pia kuanguka kwa ufalme wa Austria-Hungaria. Katika miaka ya 1930, uchumi ulizorota, na hali ya kisiasa ilisababisha wasiwasi. Steiner, ambaye hapo awali alikuwa maarufu sana, alilazimika kukimbia ili kujinusuru kwa sababu alikuwa wa asili ya Kiyahudi. Hata hivyo, katika miaka ya 1939 na 1940, gurudumu hilo kubwa lilipata wateja wengi sana. Ni kana kwamba Vita ya Pili ya Ulimwengu, ambayo ilikuwa ikiendelea, iliwafanya watu wapende sana anasa. Lakini mnamo Septemba 1944, habari zenye kuogofya zilisambaa jijini—gurudumu kubwa lilikuwa likiungua! Hitilafu ya umeme kwenye treni ya burudani iliyokuwa karibu, ilisababisha moto ambao ulienea kwenye gurudumu kubwa na ukaharibu vigari sita. Na bado matatizo mabaya zaidi yangetokea.
Mnamo mwezi wa Aprili 1945, wakati Vita ya Pili ya Ulimwengu ilipoelekea kumalizika, gurudumu liliungua tena. Wakati huo, vigari vyote 30 viliungua kabisa pamoja na mitambo ya kuendesha gurudumu hilo. Kiunzi cha chuma cha gurudumu kilichoungua ndicho tu kilichosalia. Hata hivyo, huo haukuwa mwisho wa gurudumu hilo. Huku nyumba nyingi zikiwa magofu baada ya vita, kiunzi cha gurudumu hilo kiliendelea kusimama, japo kilikuwa kimeharibika. Kwa mara nyingine tena ilionekana kwamba kubomoa gurudumu hilo kungegharimu pesa nyingi sana. Je, kulikuwa na suluhisho jingine?
Naam! Gurudumu hilo lilirekebishwa upya. Hata hivyo, kwa sababu ya usalama, nusu ya idadi ya vigari vilivyokuwepo awali ndivyo tu vilivyorekebishwa. Tangu Mei 1947 hadi leo, gurudumu hilo limeendelea kuzunguka, likiwapeleka abiria taratibu, juu na chini. Watu wanaoishi mbali kutoka Vienna wameona gurudumu hilo kubwa kupitia sinema kama The Third Man, ambayo ilikuwa na muziki mtamu uliochezwa kwa zitha.
Gurudumu kubwa la Vienna limedumu huku magurudumu makubwa yaliyojengwa kule Chicago, London, Blackpool, na Paris yamekuwa takataka. Gurudumu hilo linaonyesha jinsi watu walioishi baada ya vita walivyoanzisha maisha mapya kwa bidii na limekuwa alama ya Vienna. Ukitembelea Vienna, hapana shaka utapenda kuzunguka katika gurudumu hilo kubwa. Ukiwa huko, huenda utamwona mzee akiwaeleza wajukuu wake jinsi alivyojaribu kutuliza moyo wake uliokuwa ukipigapiga wakati Nyanya yao alipokubali kuolewa naye walipokuwa huko juu kwenye gurudumu hilo kubwa.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 19]
RIESENRAD (GURUDUMU KUBWA)
Lilijengwa mwaka wa 1897
Kimo: meta 64.75
Kipenyo cha gurudumu: meta 60.96
Uzani wa gurudumu: tani 245
Uzani wa kiunzi chote cha chuma: tani 430
Mwendo: kilometa 2.7 kwa saa
[Hisani]
Chanzo: The Vienna Giant Ferris Wheel, by Helmut Jahn and Peter Petritsch, 1989, page 39
[Picha katika ukurasa wa 21]
Jinsi mandhari ya kaskazini-mashariki mwa Vienna inavyoonekana kutoka kwenye gurudumu kubwa