Tumia Dawa kwa Hekima
Tumia Dawa kwa Hekima
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI
DAKTARI wako anapokuagiza utumie dawa, bila shaka yeye hufanya hivyo akiwa na nia nzuri, akipendekeza dawa kupatana na uchunguzi wake, maarifa yake ya kitiba, na uzoefu. Hata hivyo, mgonjwa hapaswi kutarajia kwamba daktari ndiye mwenye daraka lote kuhusiana na afya yake. Mgonjwa ndiye anayewajibika kuhusiana na vitu anavyoingiza mwilini mwake.
Unapotumia dawa ambazo daktari amependekeza, fikiria miongozo ifuatayo inayofaa kutoka kwa daktari mmoja wa tiba:
● Dawa zote zina madhara fulani. Una haki ya kujua dawa ambazo daktari amependekeza na madhara yake. Daktari wako asipokueleza habari hizo, usisite kumuuliza. Mara nyingi manufaa za dawa zitazidi madhara. Lakini unapaswa kujulishwa habari hizo ili ufanye uamuzi wa busara.
● Dawa huathiri watu kwa njia tofauti. Daktari wako hawezi kutabiri kwa usahihi jinsi dawa fulani itakavyokuathiri. Ukihofu kwamba dawa imekuathiri kwa njia ambayo haikutarajiwa, mwone daktari.
● Uliza utatumia dawa hiyo kwa muda gani. Pia, chunguza iwapo dawa hiyo inaweza kukufanya uwe mraibu.
● Jihadhari usije ukaacha kutumia dawa bila kuambiwa na daktari, labda eti kwa sababu unahisi nafuu. Huenda hali yako itakuwa mbaya zaidi ukiacha kutumia dawa. Badala yake, mwone daktari kwanza.
● Sikuzote, tumia dawa kama ulivyoshauriwa na daktari.