“Lori” Ndogo za Mwili Wako
“Lori” Ndogo za Mwili Wako
SIKU tano zilizopita chembe hiyo ilikuwa na kiini. Lakini baada ya kipindi cha kukomaa na kuongezeka sana ikajibana kwa nguvu, na kuondosha kiini chake. Ikawa chembe nyekundu ya damu ambayo haijakomaa, iliyo tayari kuingia katika damu yako. Baada ya siku mbili hadi siku nne kutoka sasa, itakuwa chembe nyekundu ya damu iliyokomaa kabisa.
Chembe hiyo ndogo inafanana sana na lori. Chombo chake cha kubebea ni hemoglobini, yaani, protini inayosafirisha oksijeni (hewa). Imekadiriwa kwamba katika maisha yake ya miezi minne, “lori” hiyo itasafiri kilometa 250 hivi kotekote mwilini mwako. Kuna mishipa midogo sana ya damu bilioni kumi mwilini mwako, hiyo ikiwekwa pamoja ingekuwa na urefu wa kutosha kuzunguka dunia mara mbili. Trilioni kadhaa za chembe nyekundu za damu huhitajika ili kusafirisha oksijeni hadi sehemu zote za mwili.
“Lori” hiyo ndogo husafiri daima katika mishipa yako ya damu. Mwendo wake unategemea hali mbalimbali. Chembe hiyo inaweza kusafiri kwa kasi kufikia sentimeta 120 hivi kwa sekunde inaposafiri kwenye “barabara kuu,” yaani, ule mshipa mkuu unaoanzia moyoni unaoitwa aorta. Chembe hiyo inapoingia kwenye “barabara ndogo” za mwili, inapunguza mwendo hatua kwa hatua kufikia milimeta 0.3 kwa sekunde inaposafiri katika ile mishipa midogo kabisa.
Mahali Chembe za Damu Zinapotengenezwa
Chembe nyingi za damu hutengenezwa katika uboho wa mtu mzima mwenye afya. Kila siku, uboho wako hutengeneza chembe nyekundu za damu bilioni moja, chembe nyeupe za damu milioni 400, na vigandisha-damu bilioni moja kwa kila kilogramu ya uzito wako. Chembe hizo huchukua mahali pa zile chembe ambazo hufa kila siku. Katika mwili wa mtu mzima mwenye afya, mamilioni ya chembe nyekundu za damu huharibika kila sekunde na nyingine huchukua mahali pake.
Sasa, ili chembe hiyo nyekundu isiyokomaa iingie katika mkondo wa damu, hiyo hukaribia ukuta wa nje wa mishipa midogo ya damu katika uboho, hujipenyeza kupitia kitundu kidogo, na kuingia katika damu. Kwa muda wa siku tatu zaidi, itaendelea kutengeneza hemoglobini. Lakini hatimaye, itakapokuwa chembe nyekundu iliyokomaa, itaacha utendaji huo.
Mzunguko wa Damu wa Aorta na wa Mapafu
Katika karne ya 17, madaktari waligundua kwamba kuna mizunguko miwili ya damu. Katika mzunguko unaohusisha aorta, “lori” ndogo hizo, yaani, chembe nyekundu, huanza safari moyoni na kusafiri hadi sehemu zote mwilini. Chembe hizo hupelekea mwili oksijeni, na kuondoa takataka inayoitwa kaboni dayoksaidi. Kisha chembe nyekundu hurudi moyoni. Katika mzunguko unaohusisha mapafu, “lori” hizo husafiri hadi kwenye mapafu. Zinaacha kaboni dayoksaidi mapafuni na kuchukua oksijeni. Kwa hiyo, mzunguko huo hupeleka hewa mwilini.
Chembe Nyekundu Zinapopungua
Mara kwa mara idadi ya chembe nyekundu hupungua isivyo kawaida. Madaktari huita hali hiyo upungufu wa damu. Hali hiyo inaweza kusababishwa na mambo mbalimbali kama vile (1) kasoro katika utengenezaji wa chembe nyekundu, au chembe hizo zisipokomaa ifaavyo, (2) kuharibika kwa chembe nyingi isivyo kawaida, au (3) kutokwa damu nyingi. Upungufu wa damu unaweza kusababishwa vilevile na uvimbe wa aina mbalimbali.
Matatizo yanaweza kutokea wakati madini ya chuma yanapopungua katika damu, au wakati madini yanapokuwa mengi mno. Kiasi kidogo cha madini ya chuma katika damu huzuia chembe nyekundu zisikomae ifaavyo. Kwa hiyo, chembe zinakuwa ndogo na zenye rangi hafifu. Mara nyingi, hali hiyo hutibiwa kwa kuongeza madini ya chuma mwilini. Nyakati nyingine kiasi cha madini ya chuma katika damu huzidi. Hali hiyo inaweza kutokea wakati ambapo chembe nyekundu zenye kasoro hupasuka na kuachilia madini za chuma kuenea mwilini. Polepole, viungo vyote mwilini vinatiwa sumu. Hali inakuwa hatari moyo unapotiwa sumu. Karibu wagonjwa wote wanaougua hali hiyo hupatwa na ugonjwa wa moyo wenye kudumu.
Tungehitaji kuandika vitabu vingi ili kueleza kazi yote ambayo chembe nyekundu za damu zinafanya mwilini mwako. Hata hivyo, maajabu ya chembe za damu ambayo tumeeleza kwa sehemu tu, yatukuza hekima ya Yule aliyebuni na kuumba uhai. Mwabudu mmoja wa kale wa Muumba mkuu mwenye hekima alisema hivi: “Kwa njia yake tuna uhai na twaenda na kuwako.”—Matendo 17:28.