Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mapambo ya italia Kazi Bora ya Sanaa

Mapambo ya italia Kazi Bora ya Sanaa

Mapambo ya italia Kazi Bora ya Sanaa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

Tumewasili Torre del Greco kwenye Ghuba ya Naples ili kutazama jinsi mapambo fulani, yanayopatikana hasa katika sehemu hii ya Italia, yanavyotengenezwa kwa mkono. Mapambo hayo yanaitwa “cameo” nayo hutengenezwa kwa kauri. Tumepanga kutembelea karakana moja ambayo hutengeneza mapambo hayo. Hata hivyo, labda ungependa kujua kwanza mapambo hayo ni nini na jinsi yalivyoanza kutengenezwa.

MAPAMBO hayo hutengenezwa kwa kuchonga picha kwenye vito, mawe magumu, au kauri. Vito aina ya ageti, onyx, sardoniki, na aina mbalimbali za kauri zinafaa hasa kwa kutengeneza mapambo hayo kwa kuwa zina tabaka zenye rangi mbalimbali zinazowezesha msanii kutokeza picha ndogo zenye kupendeza.

Mapambo hayo yalipendwa sana katika siku za milki ya Uajemi na milki ya Ugiriki na Roma kwa kuwa mengi yaliyotengenezwa wakati huo kwa mawe magumu au vito yamedumu hadi leo. Mapambo yanayotengenezwa kwa kauri si ya kale sana. Mapambo yaliyotengenezwa kwa sehemu ya ndani ya kauri yenye rangi maridadi yalichongwa huko Ufaransa, Ujerumani na Flanders katika karne ya 14 na 15. Yaelekea watu wenye kupenda vitu vya hali ya juu kwenye jumba la kifalme la Ufaransa walipendezwa na vitu vilivyotengenezwa kwa kauri. Watu waliokwenda safari za uvumbuzi waliingiza vitu vingi vigeni vya kipekee huko Ulaya kama vile, magamba ya kobe wakubwa, pembe za nyangumi, vito aina ya jade, kaharabu, na kauri ngeni. Kwa sababu hiyo watu wengi walianza kupendezwa na vitu vya asili, na wasanii stadi, watengenezaji vito, na wachongaji walichochewa kubuni vitu vipya. Yawezekana ni katika karne ya 16 ndipo ilipotambuliwa kwamba kauri za konokono aina ya Cassidae na Cypraeidae ndizo hasa zinafaa kwa kutengeneza mapambo hayo.

Katika karne ya 18 watu walianza kupendezwa tena na sanaa ya kale, na mapambo yaliyotengenezwa kwa kauri yalipendwa sana wakati huo, ijapokuwa watu fulani waliyadharau na kuyaona kuwa vito bandia kwa kuwa thamani ya kauri ilikuwa ndogo kuliko ya vito. Siku hizi mapambo hayo hutengenezwa katika miji miwili tu. Mmoja ni Idar-Oberstein, Ujerumani, ambapo mapambo hayo hutengenezwa hasa kwa vito vya agati vinavyochongwa kwa mashine, na ule mwingine ni Torre del Greco, Italia, ambapo mapambo ya kauri hutengenezwa kwa mkono.

Basi, kwa kuwa sasa tunajua mambo machache kuhusu mapambo hayo, twende tuone jinsi mapambo ya kauri yanavyotengenezwa siku hizi.

Katika Karakana

Karakana tunayotaka kutembelea iko kwenye barabara nyembamba katikati ya mji wa Torre del Greco. Meza ya fundi imejaa vyombo vya kazi na mapambo yanayoendelea kutengenezwa. Tunastaajabishwa kuuona uzuri wa picha anayochonga—picha tata ya maisha matulivu ya mashambani.

Kauri hizo hutoka Visiwa vya Bahamas na vilevile sehemu mbalimbali za Karibea na baharini huko Afrika Mashariki. Aina mbalimbali za kauri hutumiwa kutengeneza mapambo yenye rangi tofauti-tofauti. Kwa mfano, kauri aina ya Cassis madagascariensis (kwa kawaida inaitwa kauri ya sardoniki), hutumiwa kutengeneza mapambo yenye michoro myeupe yaliyochongwa kwenye mandhari ya nyuma yenye rangi ya kahawia; na kauri aina ya Cypraecassis rufa (kauri ya kalkedoni) hutumiwa kutengeneza mapambo yenye rangi za nyekundu-kahawia zilizofifia na zilizokoza. Mapambo yenye rangi zinazotofautiana sana ndiyo yenye thamani kubwa.

Kwanza kauri hukatwa kwa kutumia mashine yenye wembe wa duara unaopunguzwa joto kwa maji. Kwa kawaida mapambo yatakayotengenezwa huwa yenye umbo la yai au mviringo. Maumbo hayo huchorwa kwenye uso wa ndani wa sehemu ya kauri hiyo, na baadaye sehemu hiyo hukatwa katika vipande kadhaa vidogo. Kwa kawaida, kauri moja yatosha kutengeneza pambo moja kubwa na mapambo mawili madogo. Wasanii stadi pekee ndio wanaojua jinsi ya kukata kauri za aina mbalimbali vizuri. Kwa mfano, ikiwa kipande fulani kina matuta matatu, huenda ikafaa picha yenye vitu vitatu ichongwe kwenye kipande hicho. Baada ya kukata vipande hivyo, kila kipande hunolewa kwenye gurudumu la kunoa hadi kiwe na umbo linalotakikana. Kisha, ili kurahisisha kazi, kipande hicho hushikamanishwa na fimbo fupi ya mbao, na upande wa nje wenye mikwaruzo hulainishwa hadi uwe na unene unaofaa. Wakati huo ndipo msanii anapoangalia umbo la kipande hicho na kuamua picha atakayochonga. Yeye huchora picha hiyo kwenye kipande hicho na kuanza kuchonga.

Kekee ya stima hutumiwa kuchonga picha isiyo kamili. Halafu, msanii huanza kuchonga kwa mkono akitumia vyombo vikali sana vyenye ukubwa mbalimbali. Picha inapasa kutokezwa kwa usahihi kwenye tabaka lenye rangi iliyokoza. Kwa kuchonga hadi vina mbalimbali, msanii stadi anaweza kuchonga picha ya shela zinazopitisha mwanga. Matokeo ni picha maridadi sana kwenye mandhari ya nyuma yenye rangi iliyokoza!

Inawezekana kuchonga picha nyingi mbalimbali. Huenda umeona picha inayopendwa sana ya upande mmoja wa uso wa mwanamke mwenye madaha. Picha ndogo sana za upande mmoja wa kitu au mtu au picha za maua huchongwa kwenye pete na vipuli. Mapambo makubwa, yenye urefu wa sentimeta 7.5, hutumiwa kutengeneza pini inayofungwa juu ya nguo, au mikufu. Mapambo hayo yanaweza kuwa na picha zinazoonyesha mambo mengi, kama vile mandhari, maisha ya mashambani au maisha ya wakati wa milki ya Ugiriki na Roma. Mapambo makubwa kabisa yanaweza kuwa yenye urefu wa sentimeta 20, nayo yanaweza kuwekwa kwenye fremu au kuwekwa kwenye nguzo. Thamani yake inategemea hasa ustadi na uangalifu wa msanii, wala si ukubwa wake wala thamani ya fremu au nguzo tu. Baadhi ya mapambo hayo ni kazi bora ya sanaa.

Haitawezekana kamwe kutengeneza mapambo hayo ya kauri kwa mashine, wala mapambo mawili hayawezi kufanana kabisa kwa kuwa ni lazima msanii achunguze hali ya pekee ya kila kauri na kuichonga kwa kupatana na hali hiyo. Kwa kweli hayo ni mapambo maridadi ya kipekee—kazi bora ya sanaa ndogo sana.

[Picha katika ukurasa wa 16]

MAPAMBO YANAVYOTENGENEZWA

Kauri ambazo hutumiwa kutengeneza mapambo

Sehemu itakayotumiwa inakatwa

Picha inachorwa kwenye kipande cha kauri kilichokatwa

Kipande cha kauri kinakatwa kiwe chenye ukubwa unaotakikana

Baada ya kutengeneza kipande kiwe na umbo analotaka, msanii anafanya kazi kwenye meza yake

[Picha katika ukurasa wa 17]

Gemma Augustea, pambo lililotengenezwa kati ya mwaka wa 10 W.K. na 20 W.K. Ukubwa wa pambo hilo ni sentimeta 19 kwa sentimeta 23

[Hisani]

Erich Lessing/Art Resource, NY