Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mfumo Tata wa Viumbe

Mfumo Tata wa Viumbe

Mfumo Tata wa Viumbe

“Unamna-namna wa viumbe hutulinda. Maisha zetu na kazi zetu huutegemea.”—Shirika La Mazingira La Umoja Wa Mataifa

KUNA viumbe vingi na vya aina nyingi duniani. Usemi “aina mbalimbali za viumbe” humaanisha aina zote za viumbe zilizomo ulimwenguni. Aina hizo zatia ndani bakteria ndogo sana, miti mikubwa ya sequoia, minyoo, na tai.

Viumbe vyote duniani hufanyiza mfumo mkubwa sana wa kutegemeana, unaotia ndani vitu visivyo na uhai. Viumbe hutegemea vitu visivyo na uhai kama vile angahewa la dunia, bahari, maji yasiyo na chumvi, miamba, na udongo. Wanadamu ni sehemu muhimu ya jumuiya hiyo ya viumbe.

Aina mbalimbali za viumbe hutia ndani bakteria zote na viini vinginevyo. Aina nyingi za viumbe hivyo huwezesha utendaji muhimu wa kemikali ambao huendeleza uhai duniani. Aina mbalimbali za viumbe, yaani, mfumo wa viumbe, hutia ndani pia mimea ambayo hutengeneza oksijeni kupitia usanidimwanga. Mimea hiyo hufyonza nishati ya jua na kuihifadhi kama sukari. Viumbe vingi hupata nishati hasa kupitia sukari.

Unamna-namna Unaotoweka

Kwa kusikitisha, ijapokuwa kuna viumbe vingi vyenye kuvutia na vya aina mbalimbali, watafiti fulani wanasema kwamba wanadamu wanaangamiza aina za viumbe haraka sana. Kwa njia zipi?

Uharibifu wa makao. Hiki ndicho kisababishi kikuu cha kuangamia kwa viumbe. Uharibifu wa makao huhusisha ukataji wa miti ili kupata mbao na kupata maeneo ya malisho, kuchimba migodi, na ujenzi wa mabwawa na barabara mahala palipokuwa na misitu zamani. Maeneo yanapopungua, viumbe hupoteza vitu vinavyohitaji ili kuendelea kuwepo. Mazingira ya asili yanaangamizwa na kutenganishwa. Wanyama hukosa njia ya kuhamia maeneo mengine. Chembe mbalimbali za urithi hupungua. Viumbe haviwezi kupona vinapokabili magonjwa na hali nyingine ngumu. Hivyo, pole kwa pole aina moja baada ya nyingine hufa.

Aina fulani za viumbe zinapoangamia, aina nyingine pia zaweza kuangamia kwani sehemu moja ya mfumo wa viumbe inapoangamizwa sehemu nyingine zaweza kuathiriwa. Aina zinazotegemewa zinapoangamia—kama vile zile zinazochavusha—jambo hilo laweza kuathiri aina nyingine nyingi za viumbe.

Aina ngeni za viumbe. Wanadamu wanapoingiza aina ngeni katika mazingira, aina hiyo yaweza kuchukua makao ya aina nyingine zilizokuwepo awali. Aina hizo ngeni zaweza pia kubadili mazingira kiasi cha kwamba aina zilizokuwepo hulazimika kuhama, au zaweza kuleta magonjwa yasiyoweza kukingwa na aina zilizokuwepo. Hasa kwenye visiwa, mahala ambapo aina za viumbe zimeishi zikiwa peke yake kwa muda mrefu na hazijapata kushirikiana na aina mpya, huenda aina zilizokuwepo zikashindwa kubadilika kulingana na hali hiyo mpya na hivyo kuangamia.

Mfano mzuri wa jambo hilo ni mwani “mharibifu” unaoitwa Caulerpa taxifolia. Mmea huo unaangamiza aina nyingine zinazopatikana katika Bahari ya Mediterania. Baada ya kuletwa kimakosa kwenye pwani ya Monaco, mmea huo sasa umeanza kuenea chini ya bahari. Mmea huo una sumu, na haijulikani iwapo kuna mmea mwingine unaoweza kuuangamiza. “Huu waweza kuwa mwanzo wa msiba mkubwa wa mazingira,” asema Alexandre Meinesz, profesa wa mambo ya bahari kwenye Chuo Kikuu cha Nice, Ufaransa.

Uwindaji unaopita kiasi. Jambo hili limeangamiza aina kadhaa za viumbe. Mfano mmoja ni wa njiwa anayeitwa passenger. Mapema katika karne ya 19, huyo ndiye ndege aliyepatikana sana huko Amerika Kaskazini. Njiwa hao walipohamia eneo jingine—wakiwa katika makundi-makundi ya njiwa bilioni moja au zaidi—walifanya anga liwe jeusi kwa siku nyingi. Hata hivyo, kufikia mwisho wa karne ya 19, njiwa huyo alikuwa amewindwa sana hivi kwamba alikuwa karibu kuangamia. Kisha, mnamo Septemba 1914, njiwa wa mwisho kabisa wa aina ya passenger alikufa katika bustani moja ya wanyama huko Cincinnati. Vivyo hivyo, nyati wa Marekani wa zile Nyanda Kubwa aliwindwa sana hivi kwamba alikuwa karibu kuangamia.

▪ Ongezeko la idadi ya watu. Katikati ya karne ya 19, idadi ya watu duniani ilikuwa bilioni moja. Baada ya karne moja na nusu, watu bilioni tano waliongezeka. Hivyo wanadamu wameanza kujiuliza iwapo wanakabili hatari ya kumaliza mali asili. Kila mwaka, idadi ya watu inapoongezeka, aina mbalimbali za viumbe huzidi kuangamia haraka.

▪ Hatari ya kuongezeka kwa joto la dunia. Kwa mujibu wa Kamati ya Serikali Mbalimbali kuhusu Badiliko la Tabia ya Nchi, yamkini halijoto itaongezeka kwa nyuzi 3.5 Selsiasi katika karne hii. Huenda hilo ni ongezeko la haraka sana hivi kwamba aina fulani za viumbe zitaangamia. Kulingana na watafiti, yamkini kisababishi kimoja cha kuangamia kwa miamba ya matumbawe (ambayo hutegemeza sana aina mbalimbali za viumbe baharini) ni kuongezeka kwa joto la maji.

Wanasayansi husema kwamba usawa wa maji baharini ukiongezeka kwa meta moja, huenda sehemu kubwa ya maeneo ya pwani yenye umajimaji, ambayo ni makao ya aina mbalimbali za viumbe, yataharibiwa. Wanasayansi wengine huamini kwamba huenda ongezeko la joto la dunia linaathiri mabamba ya barafu ya Greenland na Antaktiki. Barafu hiyo ikiyeyuka, huenda msiba ukatokea katika mazingira.

Kuangamia Haraka

Aina za viumbe zinaangamia haraka kadiri gani? Majibu kwa swali hilo si sahihi kabisa. Wanasayansi wangali hawajui aina nyingi zinazoangamia. Kwanza, ni lazima wajue idadi ya aina zilizopo. Kulingana na John Harte, mwanasayansi wa ekolojia kwenye Chuo Kikuu cha California, Berkeley, “kuna aina milioni moja na nusu hivi za viumbe duniani zinazojulikana, lakini twajua kwamba kuna aina nyingi ambazo hazijatambuliwa, na huenda jumla ya idadi hiyo ni kati ya milioni 5 na milioni 15.” Wengine hukadiria kwamba kuna aina milioni 50 au zaidi. Kulingana na mwanasayansi Anthony C. Janetos, haiwezekani kujua idadi kamili kwani “aina nyingi za viumbe zitaangamia hata kabla hazijatambuliwa na kuainishwa.”

Bado wanasayansi wa kisasa hawajaelewa utaratibu tata unaowezesha viumbe vipatane vizuri na mazingira. Iwapo wanadamu hawajui idadi ya aina zilizopo, wataelewaje ule mfumo tata wa viumbe na jinsi unavyoathiriwa wakati aina mbalimbali zinapoangamia? Watajuaje jinsi kuangamia kwa aina za viumbe kunavyoathiri mfumo unaotegemeza uhai duniani?

Wanasayansi wanapojaribu kukadiria kiwango cha kuangamia kwa aina za viumbe, japo makadirio yao hutofautiana, kwa kawaida yanavunja moyo sana. Mwandishi mmoja alisema hivi: “Asilimia 50 hivi ya mimea na wanyama ulimwenguni watakabili hatari ya kuangamia katika miaka mia moja ijayo.” Utabiri huu wa Harte unahuzunisha hata zaidi: “Wanabiolojia wanakadiria kwamba ukataji wa miti katika maeneo ya tropiki utaangamiza nusu au zaidi ya nusu ya aina za viumbe zilizopo duniani katika miaka 75 ijayo.”

Kwa kutegemea makadirio ya mwanasayansi Stuart Pimm wa Chuo Kikuu cha Tennessee, gazeti la National Geographic lilisema kwamba “asilimia 11 ya ndege, au aina 1,100 kati ya aina zipatazo 10,000 zilizopo ulimwenguni, ziko karibu kuangamia; kuna wasiwasi kwamba aina nyingi kati ya hizo 1,100 hazitakuwapo mwishoni mwa [karne ya 21].” Gazeti hilohilo lilisema hivi: “Hivi majuzi, wataalamu maarufu wa elimu ya mimea waliripoti kwamba mmea mmoja kati ya kila mimea minane uko karibu kuangamia. Pimm asema hivi: ‘Si aina zinazopatikana visiwani au katika misitu ya mvua tu, wala si ndege wala wanyama wakubwa wenye kuvutia tu. Kila kitu kimo hatarini na jambo hilo linatukia kila mahala. . . . Aina za viumbe zinaangamia haraka kotekote ulimwenguni.’”

Je, Twahitaji Aina Zote Hizo?

Je, kuna haja ya kuhangaikia kuangamia kwa aina mbalimbali za viumbe? Je, kweli twahitaji aina tofauti-tofauti za viumbe? Wataalamu wengi wanaoheshimiwa husisitiza kwamba twahitaji aina hizo. Aina za viumbe duniani huwaandalia wanadamu chakula, kemikali muhimu, na bidhaa na huduma nyinginezo. Pia, fikiria kuhusu faida zinazoweza kutokana na aina ambazo hazijagunduliwa. Kwa mfano, imekadiriwa kwamba dawa 120 kati ya dawa 150 kuu ambazo madaktari huwapendekezea watu nchini Marekani, hutengenezwa kwa mali asili. Hivyo, aina za mimea zinapoangamia, wanadamu hupoteza njia ya kuvumbua dawa na kemikali mpya. Bwana Ghillean Prance, mkurugenzi wa Bustani za Kew huko London, alisema hivi: ‘Kila mara aina moja ya kiumbe inapoangamia, tunapoteza kitu ambacho tungetumia siku za baadaye. Tunapoteza dawa inayoweza kutibu UKIMWI, au zao linaloweza kukinza virusi. Hivyo, ni lazima tukomeshe uharibifu wa viumbe, si kwa faida ya dunia tu bali kwa ajili ya . . . mahitaji na matumizi yetu.’

Pia, twahitaji mazingira yanayoweza kudumisha uhai wa viumbe vyote. Mazingira yasiyo na kasoro hutimiza kazi muhimu kama vile kutengeneza oksijeni, kusafisha maji, kuondoa vichafuzi, na kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Wadudu huchavusha mimea. Vyura, samaki, na ndege huangamiza wadudu waharibifu; kome na viumbe vingine vinavyoishi majini husafisha maji; mimea na vijidudu hutengeneza udongo. Huduma hizo hutokeza faida kubwa sana za kiuchumi. Kulingana na kadirio la kiwango cha chini lililofanywa kupatana na bei za 1995, aina mbalimbali za viumbe ulimwenguni pote huleta faida ya dola bilioni 3,000 za Marekani kila mwaka.

Hata hivyo, japo tunategemea sana aina mbalimbali za viumbe, yaonekana kwamba wanadamu wanakabili tatizo kubwa linalohatarisha ule mfumo tata wa viumbe. Sasa, wakati ambapo twaanza kuelewa umuhimu wa aina mbalimbali za viumbe, wanadamu wanaangamiza aina nyingi kuliko wakati mwingine wowote! Hata hivyo, je, wanadamu wanaweza kutatua tatizo hilo? Unamna-namna wa viumbe duniani utapatwa na nini wakati ujao?

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

Uhai Una Thamani Gani?

Huenda mazungumzo kuhusu umuhimu wa kuwa na aina mbalimbali za viumbe yakaelekea kuonyesha kwamba twapaswa kujali viumbe vingine iwapo tu vinatufaidi. Wengine wanaonelea kwamba hayo ni mawazo yasiyofaa. Mtaalamu wa elimu ya visukuku Niles Eldredge alionyesha thamani ya uhai kwa kusema hivi: “Sisi wanadamu huthamini pia viumbe katika mazingira yetu—aina za viumbe vinavyovutia, maeneo ya pori yenye kupendeza—kwa sababu ya thamani yake muhimu. Kitu fulani ndani yetu hutambua kwamba tuna uhusiano fulani na mazingira hayo ya asili na kwamba twapata utulivu na furaha tunapokuwa katika mazingira hayo inapowezekana.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Orodha ya Viumbe Vilivyomo Hatarini

Orodha ya viumbe vilivyomo hatarini (“Red List”) huchapishwa na Shirika la Kimataifa la Kuhifadhi Viumbe na Mali Asili. Shirika hilo huchunguza hali ya aina za viumbe zilizomo hatarini. Baadhi ya aina za viumbe zilizomo hatarini zilizoorodheshwa kwenye orodha ya mwaka wa 2000 zimeonyeshwa kwenye ukurasa huu:

Ndege aina ya wandering albatross (Diomedea exulans)

Hiyo ni mojawapo ya aina 16 za ndege wa albatross ambazo zasemekana zinahatarishwa ulimwenguni pote. Yasemekana kwamba idadi kubwa ya ndege hao huzama wanaponaswa kwenye ndoana zenye vyambo. Ndoana hizo huvutwa na mashua za wavuvi.

[Hisani]

Photo by Tony Palliser

Tumbili aina ya douc langur mwenye miguu myekundu (Pygathrix nemaeus)

Tumbili huyo wa Asia anayependeza hupatikana sehemu ya kusini katika eneo la katikati ya Vietnam na katika sehemu kadhaa za Laos. Anahatarishwa na uharibifu wa makao na uwindaji. Mnyama huyo huwindwa kwa ajili ya chakula na viungo vyake vya mwili vinavyotumiwa kutengeneza dawa za kienyeji.

[Hisani]

Tumbili kwenye ukurasa wa 7 na 32: Photo by Bill Konstant

Konokono wa Korsika (Helix ceratina)

Konokono huyo aliyehatarishwa sana huishi kwenye eneo la hekta saba tu katika vitongoji vya Ajaccio, kwenye pwani ya kusini-magharibi ya Korsika. Huenda konokono huyo akahatarishwa kwa sababu kuna mradi wa kujenga uwanja wa ndege na barabara zinazoelekea ufukoni.

[Hisani]

Photo by G. Falkner

Ua la golden pagoda (Mimetes chrysanthus)

Ua hilo maridadi liligunduliwa mwaka wa 1987 katika Rasi ya Magharibi huko Afrika Kusini. Mioto inayotokea mara nyingi, na aina ngeni za mimea zinazoenea mahala ambapo ua hilo lapatikana huendelea kulihatarisha.

[Hisani]

Photo by Craig Hilton-Taylor

Taa wa maji safi (Pristis microdon)

Samaki huyo aliye hatarini hupatikana katika bahari

ya Hindi na ya Pasifiki Magharibi, na pia katika ghuba,

hori, na mito iliyo karibu. Samaki huyo huvuliwa sana

na idadi yake imepungua sana. Wamo hatari pia

kwa sababu ya kuzorota kwa makao yao.

[Hisani]

Photo courtesy of Sun International Resorts, Inc.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Kuangamizwa kwa Viumbe Vingi vya Baharini

Mali asili za baharini, ambazo wakati mmoja zilionekana kuwa haziwezi kumalizika, zimepungua. Mtaalamu wa elimu ya visukuku Niles Eldredge, alifafanua jinsi viumbe vya baharini huvuliwa kupita kiasi alipoandika hivi katika gazeti la Natural History: “Tekinolojia ya kisasa imewezesha kazi ya kuvua viumbe vya baharini iwe rahisi sana hivi kwamba maeneo makubwa ya chini ya bahari yanabaki tupu kama vile misitu inavyokuwa wakati miti yote inapokatwa. Hata hivyo, tekinolojia hiyo huangamiza sana viumbe vingi. Kasa na sili wa baharini, na aina nyingi za samaki na wanyama wasioweza kuuzwa, hufa kila mara wavuvi wanapovuta nyavu zao au wanapotumia chombo cha kukokota wavu.”

Gazeti la National Geographic likizungumzia “hasara ya kuvua uduvi,” lilieleza kwamba “kwenye Ghuba ya Mexico [kando ya Texas, Marekani] huenda ratili nyingi za viumbe vya baharini—hasa samaki wachanga—huangamizwa ili kuvua ratili moja tu ya uduvi.” Samaki na chaza hao wasiotakikana husemwa kuwa wamenaswa bila kukusudia. Mwanabiolojia mmoja wa serikali alieleza hivi kwa huzuni: “Kwa wastani, kwa kila kiumbe kinachokusudiwa kuvuliwa, viumbe vinne huangamizwa.” Aina nyingi za viumbe vya baharini zilizomo hatarini huangamia kwa njia hiyo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

Viumbe vya Msituni Ambavyo Havijagunduliwa

Kuna viumbe vingi misituni, kutia ndani aina ambazo hazijagunduliwa na mwanadamu. Mwanasayansi wa ekolojia John Harte alisema hivi: “Misitu ya mvua ya tropiki hupatikana kwenye eneo la dunia lisilozidi asilimia mbili na ndiyo makao ya angalau asilimia 50 au hata labda asilimia 90 ya aina zote za viumbe duniani. Idadi hiyo ya juu imetokezwa kwa sababu inadhaniwa kuwa idadi kubwa ya aina za viumbe ambazo hazijagunduliwa ni za tropiki kwani wanabiolojia wamechunguza maeneo madogo tu ya tropiki yaliyotengana. Hata hivyo, sehemu nyingine pia hazijachunguzwa kwa makini, na bila shaka kuna aina nyingi zisizojulikana na wanasayansi zinazopatikana humo. Sehemu hizo zatia ndani misitu iliyo kwenye maeneo yenye tabia nchi ya wastani, kama vile misitu iliyo katika sehemu zenye unyevu za Kaskazini-Magharibi mwa Pasifiki huko Marekani.”

Ni nani ajuaye mambo ambayo mwanadamu atagundua iwapo atachunguza viumbe vya msituni ambavyo havijagunduliwa?

[Picha katika ukurasa wa 5]

Njiwa aitwaye “passenger,” sasa ameangamia

[Hisani]

U.S. Fish & Wildlife Service, Washington, D.C./Luther C. Goldman