Jumba la Makumbusho la Uingereza Larekebishwa
Jumba la Makumbusho la Uingereza Larekebishwa
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA
Kila mwaka, wageni milioni sita hivi hutembelea Jumba la Makumbusho la Uingereza huko London. Mwaka mmoja hivi uliopita, nafasi ya jumba hilo iliongezwa kwa asilimia 40. Hilo liliwezekanaje?
Maktaba ya Jumba la Makumbusho la Uingereza na Jumba lenyewe la Makumbusho lilifunguliwa kwa watu wote mwaka wa 1759. Jengo hilo lilimalizwa kujengwa mwaka wa 1852. Lakini katika 1997, maktaba hiyo, inayoitwa Maktaba ya Uingereza, ilihamishwa kwenye jengo jingine karibu na hapo, pamoja na vitabu milioni 12 na makumi ya maelfu ya hati na nishani. Hivyo, nafasi ya Jumba la Makumbusho la Uingereza iliongezeka wakati ua wa katikati ambao ulikuwa umefungwa kwa karibu miaka 150 ulipofunguliwa kwa watu wote!
Sehemu iliyovutia watu sana katika ua huo, unaoitwa Ua Mkubwa, ni kile Chumba cha Kusoma chenye dari la kuba. Tangu kilipoanza kutumiwa mwaka wa 1857, Chumba cha Kusoma kimependwa na watafiti kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni. Mohandas Gandhi, Charles Darwin, na Karl Marx ni baadhi ya watu maarufu ambao wametumia chumba hicho cha maktaba hiyo maarufu. Hii ndiyo mara ya kwanza ambapo watu wote wameruhusiwa kutembelea chumba hicho. Vitabu 25,000 vya jumba hilo la makumbusho vimo katika chumba hicho.
Dari la kuba la chumba hicho maarufu limerekebishwa. Sasa ule Ua Mkubwa na kile Chumba cha Kusoma kimefunikwa kwa dari maridadi lenye uzito wa tani 800. Dari hilo limetengenezwa kwa kiunzi cha chuma chenye vipande 3,312 vya vioo vyenye umbo la pembe tatu. Ukubwa wa kila kipande ulipimwa kwa usahihi kwa kompyuta.
Katika Chumba cha Kusoma, unaweza kupata habari nyingi sana zilizomo katika Jumba hilo la Makumbusho la Uingereza kupitia kompyuta. Gazeti la The Times la London lilisema kuwa majengo hayo yaliyorekebishwa yanapendeza sana. Wageni pia hukubaliana na wazo hilo kwa uchangamfu!
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Katikati juu na chini: Copyright The British Museum; nyingine zote: Copyright Nigel Young/The British Museum